2017 ndiyo hii, Azam mnaishi dunia ipi?

KATIKATI ya kilele cha sherehe za kuuaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka 2017, shabiki mmoja wa kukereketwa wa klabu ya Azam, alikurupuka kusikojulikana na kupaza sauti yake juu kwa kusema “Mwaka ndiyo huu umeisha na unakuja mwaka mwingine, vipi mbona timu yangu (Azam) siielewi?” alijisemea kwa uchungu shabiki huyu ambaye ni mnazi kwelikweli wa Azam.

Shabiki huyu hakuwa mbali na ukweli. Azam hawajielewi kweli. Kama wenyewe hawajielewi, unadhani tulioko nje tunawezaje kuwalewa? Shabiki huyu alimaanisha uendeshaji wa timu yake. Uendeshaji wa Azam unaleta maswali mengi yaliyokosa majibu.

Azam ni klabu iliyojitosheleza kwa asilimia kubwa tofauti na klabu nyingi zinazoshiriki Ligi Kuu Bara. Kwa sura ya kimaendeleo, Azam imeziacha mbali na kuweka uwiano mkubwa wa mbingu na ardhi baina yake na timu kongwe Simba na Yanga ambazo zina rasilimali watu ambao ni mashabiki.

Azam wana kila kitu ambacho klabu ya soka inatakiwa kuwa nacho. Uwanja wao wa Azam Complex Chamazi ni kielelezo tosha hiki unachokisoma mbele ya mboni zako.

Simba na Yanga wana mipango mingi kwenye makaratasi yaliyofungiwa kwenye shubaka za ofisini. Azam tayari wana uwanja unaotumika kwa michezo mbalimbali. Ninapoandika hii, ninamaanisha ni klabu ya kipekee kwa klabu za nyumbani.

Licha ya Azam kuwa na vitu vingi vizuri vinavyomvutia hamasa kila mmoja kutaka kuwa sehemu ya familia ya timu hiyo, lakini uendeshaji wao hauna tofauti na klabu nyingi ambazo wachezaji wake wanasotea mishahara.

Uanzilishi wa Azam ulikuja kubeba matumaini ya Watanzania wengi ambao waliamini ujio wao utakuja kuonyesha tofauti ya klabu nyingine na wao, huku kila mmoja akijipanga kusahau mafanikio ya klabu kongwe ambazo mafanikio yao makuu ni kupaka rangi majengo yao na kufungana kisha kwenda kuchekana kwenye vikao vya kahawa.

Lakini Azam mambo yamekuwa sivyo ilivyotarajiwa, kila unavyobadilika mwaka mmoja kwenda mwingine hawaonyeshi kufanya kile kilichootwa wa Watanzania wengi zaidi ya nao wamekuwa wakiishi maisha yaleyale ya kama ya timu nyingine. Azam inaishije kama Toto African na Ndanda FC?

Uwekezaji wao haukutakiwa kuwa na sura hii waliyonayo sasa, walitakiwa kuwa na sura ya kipekee na kuwa mfano wa kuigwa kwa timu nyingi za ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Hivi karibuni nao wameingia katika mkumbo wa fukuzafukuza makocha kama ambavyo tumekuwa tukishuhuduia kwenye timu kongwe. Ndani ya misimu yao tisa katika ushiriki wao wa Ligi Kuu Bara, wameshafukuza  makocha wanane.

Katikati ya wiki iliyopita, wakati dunia ikibakisha saa chache kuumaliza mwaka 2016 na kuusubiri mwaka 2017, Azam walimfukuza kocha wao Zeben Hernandez na benchi lake la ufundi kufuatia klabu kuwa na matokeo ya kusuasua.

Kuondoka kwa makocha hao kumeifanya timu itoe fedha nyingi kuwalipa  makocha hao wa Hispania waliovunjiwa mikataba. Tatizo la makocha hawa halikuanzia uwanjani walipokuwa wakikosa matokeo. Tatizo lilianzia kwa mtu aliyewaona na kutaka waletwe nchini. Kabla ya mikataba ya Hernandez na wenzake kuwekwa wino mwekundu, aliyewaleta alitakiwa awajibishwe.

Jografia ya mpira wetu ni ngumu kwa makocha wanaotoka Hispania ambao ni waumini wa soka la chini na lenye kasi kuja kufanikiwa. Aliyeamuru wakina Hernandez waje nchini hakulijua hili kabla na kusainisha hundi ya fedha na kuwatafuta waliko na kuwaleta? Huyu ndiyo anatakiwa kutujibu.

Makocha wengi wenye historia ya kufanya vyema katika mpira wetu ni wale wanaotoka nchi za Ulaya Mashariki. Nchi hizo hazina tofauti na mazingira ya Afrika. Inasemekana mchezo wa kwanza Hernandez kuishuhudia Azam ilikuwa ni msimu uliopita kwenye mchezo wa timu hiyo dhidi ya African Sports ya Tanga iliyoshuka daraja, Uwanja wa Mkwakwani.

Katika mchezo huo, Hernandez alipokaa jukwaani alimuuliza mkalimani wake “Ni vipi uwanja huu unachezewa michezo ya ligi?” alihoji Hernandez akishangaa uchakavu wa uwanja huo.

Asilimia kubwa ya viwanja vya Tanzania vina sura ya Mkwakwani. Ukienda Mbeya utakutana na Sokoine, ukienda Mtwara utakutana na Nangwanda Sijaona. Viwanja vingi vina sura ya Mkwakwani na havikwepeki. Viwanja yenye sehemu nzuri ya kuchezea (pitch) viko vichache sana na hata ukijipa kazi ya kuvihesabu kwa vidole havifiki 10.

Aliyewaleta makocha hawa hakulijua hili kabla? Huyu ajitokeze kutuomba radhi na kutujibu maswali yetu.

Ulitaraji kushuhudia maajabu gani kwa Hernandez na wenzake ambao walikuja Afrika kwa mara yao ya kwanza? Hiki kilichowatokea ilikuwa lazima kiwatokee tu.

Licha ya hivyo, moja ya mahojiano ya Raia Mwema na Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba, mwanzoni kabisa mwa ujio wa Hernandez ambaye hakufahamu kitu chochote kuhusu soka la Afrika, Kawemba alisema mikakati yao na makocha hao wa Hispania ni kutengeneza timu na baadaye ndio watakuja kuvuna matunda.

Kutoka pale Kawemba aliposema kauli hiyo mpaka Hernandez na wenzake wakielekea Kipawa kupanda ndege kurudi kwao, Azam imezidi kurudi nyuma.

Zaidi ya misimu mitatu ya hivi karibuni haijashika nafasi ya tatu kama wanayoshika sasa katika msimamo wa ligi, huku wakipitwa idadi kubwa ya pointi na timu za Simba, Yanga zilizo juu yake.

Mara nyingi nafasi yao inakuwa ya juu, huku wapinzani wao wakuu wakiwa Yanga na si timu nyingine. Lakini tangu ujio wa Hernandez na wapinzani wakuu wa Azam ni timu za Kagera Sugar na Ruvu Shooting.

Huyu ndiyo Hernandez aliyeifikisha hapa Azam. Makocha hawa wameivuruga timu. Waliondoa idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni ambao waliifanya Azam ishinde taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup 2015) na Hernandez kutamba anakuja na kizazi kipya.

Lakini baada ya muda, Hernandez na wenzie nao wameenda mtaani kuungana na wachezaji waliowaondoa. Kuna kitu kinashangaza hapa. Inawezekana vipi mabosi wa Azam wakubaliane na Hernandez kuachana na kundi kubwa la wachezaji wa nje kisha wasimuuunge mkono kwenye hali ngumu ya matokeo aliyokuwa nayo?

Kama mabosi wa Azam walimuunga mkono kuondoa wachezaji wa nje ilitakiwa waendelee kumuunga mkono katika suala la kukosekana kwa matokeo na mwishowe waone kocha alikuwa na maana gani kuwaacha wachezaji wa nje ndiyo waje kumhukumu. Maana kama kukosea walishakosea tangu mara kwanza walivyomleta nchini.

Hali ya fukuzafukuza makocha kila mara inawapa sura mbaya na inaonyesha wazi hawana wataalamu sahihi wa masuala ya ufundi ambao wana uhakika na kazi wanazofanya kwenye suala zima la upatikanaji wa makocha.

Ni wakati wa wahusika wa masuala ya ufundi wa klabu hiyo kuwa na malengo ya kutafuta makocha sahihi kuifundisha timu hiyo. Kumleta kocha huyu kisha kukaa nae muda mfupi na kumtimua na baadae kumleta mwingine kunaharibu sura nzima ya klabu na kuitia hasara.

Hali ya kutimua makocha na kuwaleta wengine kila wakati inaitia hasara klabu kwa kuvunja mikataba wakati watu wa masuala ya ufundi wangesumbua vichwa vyao kupata mtu sahihi ambaye ataitoa klabu katika suala la ‘timua timua’ mpaka mafanikio.

Azam haitakiwi kuishi hivi inavyoishi sasa, inatakiwa iwe ya mfano wa kuigwa na wengi. Kama hali ya mambo itaendelea hivi sitashangaa shabiki yule akijitokeza tena mwishoni mwaka huu na kupaza sauti yake juu akisema 2017 ndiyo hii inaisha, Azam mnaishi dunia ipi?


0746-594360

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *