LEO safu hii ina hadithi fupi kuhusu uhuru na kujitegemea. Ni hadithi niliyotunga kuenzi nusu karne ya uhuru wa nchi za Afrika. Hadithi hii ni ya kutunga. Lakini endapo itatokea majina ya wahusika, maeneo na matukio yakafanana na hali halisi kokote kule barani kwetu basi ninakiri kwamba itakuwa imetokea tu bila kudhamiriwa (coincidence).
Siku moja wanyama waliokuwa utumwani walipewa uhuru kutoka kwa madhalimu waliokuwa wakiwamiliki na kuwatumikisha. Siku hiyo walifurahia mno na kwa kipindi cha juma zima walifanya karamu ya kula na kunywa na kushangilia. Wote walijiona wamoja na kwamba walikuwa sawa. Baada ya sherehe za uhuru wakadhamiria kuanza safari ndefu ya kurejea nyumbani kwao ili kule wakajitawale na kujitegemea.
Ilikuwapo meli kubwa ya kutosha kuwabeba wote ili kuwarejesha ng’ambo ya bahari ambako ndiko asili yao. Ilikuwa ni safari muhimu sana ambayo kwa hakika kila mnyama aliyekuwa na akili timamu alitamani kuifanya.
Lakini siku ya safari ikafika. Likatolewa tangazo la kuwataka wanyama wote kuingia melini. Ghafla wakatimka nguruwe kwa kasi zote na kuingia melini kwanza. Na kule wakaelekea kila pahala palipoonekana nyeti. Katika chumba cha nahodha wakajaa. Kule chumba cha injini wakajaa. Katika stoo ya melini wakajaa. Katika jiko la melini wakajaa. Katika chumba cha mawasiliano ya simu wakajaa. Katika jukwaa la kupigia muziki wakajaa. Katika chumba cha mitambo ya sinema wakajaa. Na katika chumba cha madaktari wakajaa. Nguruwe nguruwe kila pahala.
Wanyama wengine wakaanza kuuliza: “inakuwaje nguruwe wamejaa maeneo yote nyeti ya meli hadi chumba cha nahodha kana kwamba wao wanajua kila kitu ikiwamo kuendesha meli?” Nguruwe wakakaa kimya. Na kila walipoulizwa jambo wao wakazidi kukomaa pale walipo. Walipoambiwa haya basi washeni meli tuanze safari, wao wakawa wanaguna tu. Ikafika wakati nguruwe wakaona kelele za wanyama wengine ni karaha na kadhia kwao.
Wakaanza kujibu mashambulizi. “Hapa hatutoki. Tunajua mna wivu sana. Na bado.” Wanyama wakatumia kila njia ya ushawishi wa maneno lakini wakakwama. Ikafika pahala madhalimu wakawasogelea na kuwauliza: “Kulikoni, mbona meli haiondoki? Au mmeghairi safari ya kurudi kwenye ukombozi wenu?”
Wanyama wale wakawashitakia nguruwe kwa madhalimu: “Mkuu si mnawaona nguruwe wamegomea katika vitengo vyote nyeti, ikiwamo chumba cha nahodha na wanyama wanaojua unahodha wameshindwa kuingia mle ndo maana tumeshindwa.” Basi madhalimu wakawashauri wanyama wale kwamba waanzishe mfumo wa kukalia maeneo nyeti kwa zamu. Na kwamba madhali nguruwe walikwishawahi vitengo, basi ilikuwa hawana budi kumalizia vipindi vyao. Na kwamba baada ya zamu ya nguruwe basi ingelikuja zamu ya wanyama wengine kama nyani au sokwe ambao walikuwa na uwezo wa kuendesha meli. Lakini amkani si shwari tena. Kumbe madhalimu wale baada ya kuona wanyama wenyewe wanahadaika mara moja wakaanza mawasiliano na nguruwe. “Nguruweee, hakikisheni mnakomaa hapo hapo hata zamu yenu ikiisha; tutawalinda.” Nao nguruwe kusikia hivyo wakafurahi kweli kweli.
Lakini kipo kitu kimoja walichokisahau nguruwe wale. Kwamba kila mnyama alikuwa na faida na umuhimu wake kutokana na kipaji chake tofauti na wengine. Ilikuwa ni suala la wanyama wote kukaa pamoja na kufanya majadiliano ili kufikia makubaliano ni mnyama gani atoe mchango gani kwa kadiri ya kipaji chake na hatimaye safari ianze na wote wasafiri kwa starehe hadi katika ng’ambo ya ukombozi wao.
Kwa kifupi tu ni kwamba walichokihitaji nguruwe wale ilikuwa ni raha binafsi; hawakujua injini inawashwaje, hawakujua meli inaendeshwaje au kuongozwaje, hawakujua chakula kinapikwaje, hawakujua muziki unapigwaje, hawakujua sinema inawashwaje, hawakujua wagonjwa wanatibiwaje, hawakujua mawasiliano ya simu melini yanafanywaje. Matokeo yake maisha yakaanza kuwa magumu kwa wanyama wote, wakiwamo nguruwe wenyewe.
Mara nguruwe wale wakaanza kuguguna chochote kilichokuwa mbele yao. Wale waliokuwa katika chumba cha rubani wakaanza kuguguna usukani. Wakaguguna vikorombwezo vya kuongozea meli. Wakaguguna makochi. Mwisho, walipomaliza kuguguna kila kitu, wakaanza kuguguna meli yenyewe.
Waliokuwa stoo wakatafuna chakula chote kule. Walipokimaliza, wakaanza kuguguna vyombo. Vilipomalizika wakaanza kuguguna ukuta wa meli. Waliokuwa jikoni wakaanza kuguguna sufuria. Wakaguguna jiko. Wakaguguna vyombo na walipomaliza; wakaanza kuguguna meli yenyewe. Waliokuwa chumba cha madaktari wakaanza kuguguna dawa. Wakaguguna vifaa vya maabara. Wakaguguna mashuka. Wakaguguna magodoro. Walipomaliza, wakaanza kuguguna ukuta wa meli.
Waliokuwa chumba cha injini wakaanza kunywa mafuta yakaisha. Wakahamia katika vikorombwezo vya injini wakaguguna wakamaliza. Wakaguguna kila kigugunika na walipovimaliza vyote, wakahamia katika ukuta wa meli.
Muda wote nguruwe walipokuwa wakiguguna kila kilichokuwa chini yao wanyama wengine walikuwa wakiwasihi kuacha kufanya hivyo ili walau zamu ya nguruwe ya kukaa katika vitengo itakapomalizika, wanyama wengine wenye ujuzi wakiingia katika vitengo husika safari ianze rasmi.
Kadiri nguruwe walivyozidi kukaa katika vitengo vile bila ujuzi uliohitajika na huku njaa ikiongezeka, sambamba na hamu ya kuguguna, ndivyo walivyozidi kuwa wakali. Matokeo yake kila mnyama aliyehoji kulikoni, nguruwe walipata kisingizio cha kumtafuna na yeye.
Matokeo yake, badala ya wanyama kuendelea kukosoa, nao taratibu wakaacha: wakawa wabeuaji. Nao wakaanza kutafuna au kuguguna kilichokuwa mbele yao. Na wanyama wakubwa kama simba wakaona sasa ipo haja ya kuwatafuna wanyama wadogo walio jirani nao. Wanyama kama nyati ikabidi watafune manyoya ya nyani wakiyafananisha na nyasi. Wanyama wengine wakajiunga na nguruwe katika kushambulia ukuta wa meli. Panya na fuko wao kwa vile walikuwa wadogo kiumbile wakaanzia kuguguna sakafu ya meli.
Wakati huo huo nguruwe wale kwa vile walikwishatengeneza matumbo makubwa sana na kwa vile walichokijua kuliko kingine chochote ni kuguguna na kugugunisha wakaanza kurejea tena kwa madhalimu kuwaomba japo vigugunio. Na kwa vile walikwishaweka nadhiri nao kwamba wataendelea kukalia vitengo, wakawa wakiwadondoshea makombo ambayo nguruwe walikula kwa kujificha.
Mara meli ile ikaanza kuegemea upande na wakati huo maji yakawa yakiingia ndani kwa wingi. Madhalimu wakaingilia kati. Dhalimu mkuu akawaambia wanyama: “Tuliwaambia katu hamuwezi kujitawala nyie. Angalieni sasa si tu kwamba mmeshindwa kuwasha meli na kusafiri zenu, mmeshindwa hata namna ya kushauriana na kutumia vipaji vyenu ili mfanikiwe katika jambo dogo tu la kuwasha meli na kuondoka hapa pwani ya utumwani.” Dhalimu mkuu akameza fundo la mate kisha akaendelea:
“Angalia kwa mfano. Nguruwe yeye uwezo wake mkubwa ni kuzalisha samadi ya kutosha kwa ajili ya kupata gesi na nishati ya kutumia katika meli, akang’ang’ania katika vitengo asivyovimudu. Mwangalie sokwe, hodari wa kuendesha meli lakini kajibanza kule kwenye deka. Haya nyani ilibidi akwee katika mlingoti wa meli kupandisha bendera lakini angepita wapi? Mwangalie sungura na masikio yake hodari kweli kwa mawasiliano ya simu lakini yule kalaliwa na nguruwe anapumua kwa taabu. Nguruwe nguruwe kila pahala.
“Mwangalie kiboko yeye bingwa wa mambo ya stoo lakini hakupata pa kupenya kabakia mguu mmoja ndani ya meli mwingine nje. Mwangalie simba; yeye ndiye bingwa wa kuwasha na kuhudumia mitambo yote ya injini lakini alishindwa kabisa kushuka kule chumba cha injini.” Mara Dhalimu mkuu akatizama juu, kisha akashusha uso wake na kuendelea:
“Mwangalie nyoka pale, yeye ni daktari bingwa wa mabingwa lakini kakosa kabisa pa kujipenyeza kwa vile nguruwe wamekwishajaa mle dispensari. Mwangalie chui, ni bingwa wa kupika na kuhakikisha kila aliye katika meli anapata chakula. Lakini yuuule kwenye deki kule. Mwangalie tembo ni kiongozi mwenye busara sana na angeliwasaidia mno katika majadiliano kufikia mwafaka lakini yeye ndo hata hiyo meli yenyewe ameshindwa kupanda. Nguruwe nguruwe kila pahala! Mmeshindwa kutumia vipaji vyenu katika uhuru na sasa tunawarejesha utumwani tukawasimamie. Sasa itabidi mteremke katika meli ile mrejee nchi kavu kwa sababu kama mnavyoona inaweza kuzama muda wowote nanyi mkiwamo.”
Ndipo wanyama wale wakalia na kusaga meno kwa sababu tu eti waliponzwa na ulafi na ubinafsi wa nguruwe. Nguruwe nguruwe kila pahala, meli yawezaje kwenda?
Maoni ya Wasomaji
Hadithi FIKIRISHI kuhusu
Hadithi FIKIRISHI kuhusu viongozi wa Afrika.
Hivi,Afrika imelaaniwa? Napata taabu kulielewa hilo hasa kutokana na matukio ya viongozi wake!
Goodluck Ayoub.
Ayoub, mfano wa hadithi hii
Ayoub, mfano wa hadithi hii kwa maisha ya nchi ya mbayuwayu wenye domo kaya kutwa kucha imeniacha nawaza mengi. Safari kweli haijaanza, watu wanakazana kutafuna tu! Kaazi kwei kwei.
Hadithi tamu sana yenye
Hadithi tamu sana yenye ukweli.