Makala
Siku Field Marshal John Okello ‘alipotimuliwa’ Zanzibar
Ahmed Rajab
Toleo la 227
22 Feb 2012

YAFUATAYO ni masimulizi mafupi ya kipindi kifupi cha Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari, 1964 yaliyoipindua serikali ya ubia ya chama cha Zanzibar Nationalist (maarufu Hizbu) na kile cha Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP). Tunaangazia nini hasa kilitokea usiku wa Jumamosi Januari 11, yaliyojiri siku ya pili yake na mwezi mzima wa Januari, mwaka 1964 .

Tumeyakusanya masimulizi haya baada ya kuzungumza na walioshiriki katika Mapinduzi hayo ambao baadaye walisaidia kudhibiti madaraka na kuunda taasisi zilizoziba pengo la Serikali iliyopinduliwa ya Waziri Mkuu, Muhammed Shamte Hamadi.

Usiku wa manane wa Januari 11, makada wapatao 200 wa Umoja wa Vijana wa Afro-Shirazi (Afro-Shirazi Youth League) walielekea kwenye kambi ya polisi ya Ziwani, nje kidogo ya mji huko Unguja.

Wakiongozwa na Yusuf Himid wapinduzi hao hawakukabiliwa na upinzani walipofika Ziwani ila waliikuta ghala ya silaha iko wazi na wakazinyakua silaha na kukimbia nazo hadi kwenye uwanja ulio nje ya jengo la Raha Leo.

Hapo ndipo palipokuwa makao makuu ya Mapinduzi kwa siku chache na ndipo wapinduzi walikokuwa wakipewa silaha. Studio za redio ya Serikali pia zilikuwa hapo.

Moja ya sababu zilizoyafanya Mapinduzi yafanikiwe haraka ni uamuzi wa viongozi wa Serikali iliyopinduliwa — Sheikh Muhammed Shamte na Sheikh Ali Muhsin Barwani — kuwataka wafuasi wao wasitumie nguvu kuyapinga. 

Hivyo, mbali na mapigano yaliyozuka saa za asubuhi ya Jumapili Januari 12, mbele ya Steshini ya Polisi Malindi, hapajazuka mapigano Unguja kati ya waliopindua na waliopinduliwa. Pemba nako pia hakukuwa na upinzani ijapokuwa kisiwa hicho kilikuwa ngome ya vyama vya ZNP na ZPPP.

Wengi wa wapiganaji waliokuwa kwenye Stesheni ya Polisi ya Malindi walikuwa wakuu wa polisi Wakiingereza. Wakipigana na makada wa Umma Party ambao ndio pia waliouteka uwanja wa ndege, bandari pamoja na kituo cha mawasiliano ya nje cha Cable & Wireless, kilichokuwa kwenye jengo ambalo sasa ni Hoteli ya Serena Mji Mkongwe.

Kwa hakika, kinyume cha baadhi ya watu walivyoandika hapakutokea mauaji ya kimbari.  Aliyeanzisha uvumi huo alikuwa John Okello aliyeandika kwenye kitabu chake kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar kwamba watu zaidi ya elfu kumi waliuliwa. Okello aliongeza kwamba aliamrishwa na Yesu Kristo kuwakomboa ‘Waafrika’ wa Zanzibar kutoka kwa ‘wageni’.

Tutamrejelea Okello na wengine waliokuwa Raha Leo baadaye. Kwanza tukumbushe kwamba mkesha wa Januari 12, mwaka 1964, Zanzibar haikuwa na jeshi.  Kulikuwa polisi waliokuwa wakiongozwa na Waingereza. Wengi wa askari polisi walikuwa raia wa Tanganyika. Serikali iliyopinduliwa ilikataa kuandikiana mkataba wa kijeshi na Uingereza kwa sababu ikihisi mkataba kama huo utaonekana kuwa wa kikoloni.

Hatuwezi kusema ni nani hasa aliyepiga risasi ya mwanzo au ya mwisho katika Mapinduzi. Naitoshe tusemapo kwamba kwa vile hakukuwa na upinzani, Serikali iliyokuwa madarakani iliporomoka kama ‘nyumba ya karata’.

Tuwarejelee sasa waliokuwa Raha Leo, makao makuu ya Mapinduzi kwa siku chache. Kwanza tumuangalie Okello ambaye sauti yake ndiyo iliyokuwa ikivuma kwenye Redio Zanzibar.

Hatuna uhakika nani alimpeleka Okello Raha Leo.  Wengine wanasema ni Yusuf Himidi. Wengine wanasema ni Seif Bakari aliyetoa rai atumiwe kutoa matangazo kwenye redio kwa vile sauti yake ilikuwa na lafudhi ngeni ya kutisha.

Uhakika tulio nao ni kwamba Okello alipotokea Raha Leo na mabastola yake, Aboud Jumbe alishtuka na akauliza: “Nani huyu? Katokea wapi?”

Kijana huyo aliyekuwa na umri wa miaka 27 hakujulikana kabla ya Mapinduzi. Alikuwa mtu asiyejua kuandika wala kusoma na akili zake zikimtosha mwenyewe. Hakuwa na sifa za uongozi na wala hakushiriki katika vuguvugu lolote la kisiasa.

Akijibandika cheo cha kijeshi cha Field Marshall ni yeye aliyetangaza kwamba serikali ya ZNP/ZPPP imepinduliwa. 

Kwa hakika, kazi hiyo ya kutangaza kufanikiwa kwa Mapinduzi kwanza alipewa Ramadhan Haji, mmoja wa wapinduzi. Lakini alikataa. Jina la Okello lisingelisikika lau Ramadhan Haji angekubali kutangaza kwamba Serikali imepinduliwa na  kwamba wapinduzi waliidhibiti nchi.

Waliokuwa wakiongoza mambo Raha Leo tangu Mapinduzi yaanze, hadi Jumatatu Januari 13, walikuwa Aboud Jumbe, mmoja wa viongozi wa chama cha Afro-Shirazi (ASP), Thabit Kombo (Katibu Mkuu wa ASP) na Badawi Qullatein wa Umma Party. Muda wote huo, Sheikh Abeid Amani Karume (kiongozi wa ASP), Abdulrahman Babu (mwenyekiti wa Umma Party) na Abdalla Kassim Hanga (ASP) walikuwa Dar es Salaam.

Mnamo siku hizo hizo liliundwa Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri lililokuwa na mamlaka kamili ya kuiendesha Zanzibar. Mabaraza hayo mawili yalikuwa taasisi kuu za Serikali ya kimapinduzi ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Na sio ile iitwayo ‘Kamati ya Watu Kumi na Nne’ ambayo baadhi ya watu wanasema kuwa ndiyo iliyoandaa Mapinduzi.

Okello akipenda kujigamba kwamba ndiye aliyeyapanga na kuyaongoza Mapinduzi. Alikuwa akitoa matamshi ya kushtusha na ya ajabu-ajabu kwenye Redio Zanzibar. Kwa mfano, siku moja alidai kwamba alipwe mshahara mkubwa zaidi ya aliokuwa akilipwa Rais Karume. Siku nyingine akasema kwamba kasri zote alizokuwa akitumia sultani kupumzikia apewe yeye.

Kuna siku aliyotoa hukumu kwamba mzee mmoja wa zaidi ya miaka 60 afungwe kwa miaka 99. Alisema kama huyo bwana atakufa gerezani basi mwanawe afungwe ili kuendeleza kifungo na mwanawe akifa basi mjukuu wake afungwe mpaka itimie miaka 99.   

Nyakati nyingine aliwaonya watu wazitie moto familia zao na wao wenyewe mpaka wafe ‘kabla ya majeshi yangu kuja.’ Alikuwa akitoa vitisho visivyowahi kamwe kusikika Zanzibar.

Kuna siku alitangaza kwamba wakazi wa eneo moja ambako alikuwa apite, wajipange foleni barabarani wakiwa wamevaa chupi tu.

Okello alikuwa ni adha, kitisho, kichekesho na fedheha kwa Zanzibar. Viongozi wapya wa nchi walichoka naye na wakaamua kumchukulia hatua.   Salim Rashid, mmoja wa viongozi wa Umma Party aliyekuwa katibu wa Baraza la Mapinduzi anasema kwamba, kwanza alilizungumza suala la Okello na Sheikh Karume. Halafu akalizungumza na Brigadia Yusuf Himid na mwisho yeye, Yusuf Himid na Kanali Ali Mahfoudh wakalitafutia dawa.

Ilisadifu kuwa siku moja Okello alisafiri kwenda Dar es Salaam akifuatana na Jaha Ubwa, aliyekuwa katibu wake. Walipokuwa wanatarajiwa kurudi Zanzibar, Karume, Yusuf Himid, Salim Rashid na Ali Mahfoudh walikwenda uwanja wa ndege kumsubiri.

Siku hiyo anaikumbuka vizuri Luteni Hashil Seif aliyekuwa ofisa wa zamu kwenye kambi ya jeshi huko Migombani karibu na uwanja wa ndege. Alipigiwa simu akitakiwa aende kwa haraka uwanja wa ndege.  Hakuambiwa anaitiwa nini.

Alipofika ndipo alipoambiwa kwamba kuna ndege ya Shirika la Ndege la Afrika ya Mashariki iliyokuwa inakuja kutoka Dar es Salaam ndani yake wakiwemo pia Okello na Jaha Ubwa. Akaelezwa kwamba awaruhusu abiria wote pamoja na Ubwa washuke, lakini amzuie Okello asishuke. Halafu amwambie rubani ampeleke Okello Kenya.

Hashil naye akampigia simu komredi mwenzake Luteni Amour Dugheshina kumwita aende uwanja wa ndege amsaidie. Maluteni wote wawili walikuwa na bunduki za aina ya ‘machine gun’.

Ndege ilipotua walipanda ndani ya ndege, wakampokonya silaha Okello na  kutekeleza amri waliopewa. Rubani wa ndege alikasirika sana. ‘Uso wake ulighadhibika, utafikiri mnyama aliyekosewa risasi,’ alieleza Hashil.  

Lakini rubani hakuwa na la kufanya ila kuiwasha ndege na kuelekea Kenya. 

Huku nyuma Salim Rashid akampigia simu Oginga Odinga, Makamu wa Rais wa Kenya, kumuarifu kwamba wamemfukuza Okello na ‘wanamrejesha’ Kenya. Alifanya hivyo kwa makosa kwa sababu kutokana na jina lake akifikiri kuwa Okello ni Mjaluo kutoka Kenya.

Kumbe alikuwa mtu wa kabila la  Acholi aliyezaliwa Uganda na alikwenda Unguja kabla ya kuhamia Pemba ambako alikuwa mwashi, mtiaji rangi nyumba na mpasuaji mawe.

Swali la kujiuliza hapa ni; je, iwapo kweli Okello alikuwa ‘kiongozi mpendwa wa Mapinduzi’ ilikuwaje wafuasi wake na wanamapinduzi wenzake wasimtetee alipoadhiriwa uwanja wa ndege na kufukuzwa nchini? Ilikuwaje akafukuzwa kwa urahisi hivyo?

Kuna uzushi mwingi kuhusu kipindi hiki kifupi cha historia ya Zanzibar. Kwa mfano, kuna filamu ya kubuni ya Wataliana inayoonyesha maiti chungu nzima za watu waliopigwa risasi. Filamu hiyo ilikuwa na lengo moja tu; kuonyesha ‘ukatili na unyama wa Waafrika.’ 

Hakuna ithibati  yoyote kwamba watu waliouawa katika siku za mwanzo za Mapinduzi walifika elfu kumi. Ukweli ni kwamba jumla ya watu waliouawa siku hizo haipindukii 200, katika sehemu za mjini hawazidi 25.

Uzushi mwingine ni kwamba walipelekwa Watanganyika, Zanzibar wakiwa na silaha kwenda kupindua. Na si kweli kwamba Mapinduzi yalikuwa na msisitizo wa kikabila. Katika kipindi cha mwanzo cha Mapinduzi msisitizo ulikuwa wa kitabaka.  Nyimbo zilizokuwa zikiimbwa kwenye Redio Zanzibar zikiwazungumzia ‘wakwezi na wakulima’ na wafanyakazi kwa jumla na si makabila.

Mapinduzi ya Zanzibar yalianzisha taasisi mpya za utawala zikiwa pamoja na Baraza la Mapinduzi, Baraza la Mawaziri na ofisi ya Rais. Taasisi hizo zilikuwa zifanye kazi kwa muda wa mwaka mmoja tu kwa vile ilikwishaamuliwa kwamba Januari 1965 pafanywe uchaguzi wa kulichagua Bunge la Katiba, lililokuwa litunge Katiba ya kudumu ya Zanzibar.

Baraza la Mapinduzi la Zanzibar pamoja na Serikali mpya zilianza kwa ubia baina ya chama cha ASP na Umma Party. Ingawa wanachama wa ASP ndio waliofanya Mapinduzi waliutambua mchango wa wafuasi wa Umma Party na hasa mchango wa makada wao waliopata mafunzo ya kijeshi nchini Cuba.

Vijana hao wa Umma walizitia wasiwasi serikali za Marekani na Uingereza na kuzifanya ziamini kuwa utawala mpya wa Zanzibar ulikuwa wa ‘kikomunisti’.  Dhana hiyo ndiyo iliyosababisha kuchukuliwa hatua ya kuyachimba na kuyagandamiza Mapinduzi ya Zanzibar yaliyodumu kutoka Januari 12, hadi 26 Aprili, mwaka 1964.

 

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Ahmed Rajab
ahmed@ahmedrajab.com

Maoni ya Wasomaji

Kwa mara nyengine tena, napenda kuchukuwa fursa hii adhimu kukushukuru sana sana kwa kuandika kitu ambacho kimetufungua macho wengi maana kilikuwa na utata mkubwa juu ya dikteta John Okelo, Idadi ya watu waliokufa siku ya Mapinduzi na ile filamu maarufu ya ki-Taliana inayoonesha jinsi ya watu walivyouliwa.
 
Nakupongeza tena kwa makala yako nzuri sana na usiwache kutufungua macho zaidi

Nadhani kuna jambo linalojificha juu ya Okello,na maelezo ya mwandishi ni kama ya kumzushia vile;lazima alikuwa na u-special fulani ktk mapinduzi hayo na ndio maana akapwewa jukumu muhimu hivyo!

Mbona mwandishi unapoteza ukweli mimi sikumbuki Mapinduzi ila tumesoma na kusikia kuwa kuna watu wengi wamepoteza maisha kwenye mapinduzi ya zanzibar na wewe unasema kuwa watu hawazidi zaidi ya 200.je hiyo 200 uniona ndogo
 

Estimations between around at least 3000 up to 13,000. Kwa hivo nami nadhani idadi ya 200 si ukweli. Check references in Shivji, 2008, Pan-Africanism or Pragmatism, p.2 or Abdul Sheriff, 2001,Race and Class in the Politics of Zanzibar. In: Africa Spectrum, Jg. 36, 3, 2001, p.314

Tatizo la simulizi zako ni kile kitendo cha kuwaonyesha Watanzania bara kama watu wabaya sana.                    Kama serikali ilikuwa ya Sultan na alisaidiwa na mwingereza askari walitokaje Tanganyika kwasababu wakati huo mwingereza alishaondoka.
Pili, Unasema kitendo cha Okello kurudishwa Kenya kilikuwa dhalili na kwamba wanamapinduzi wenzake hawakumpenda! Fair enough! Je, kilikuwa dhalili kuliko kilichompata Abeid Aman Karume?
Tatu, Wakati unasimamia mapinduzi halali, wapo wenzako wanaosema ni jitihada za Nyerere kueneza imani ya kikristo. Hawa hawatambui mapinduzi na utawajua kwa aina ya nywele zao. Swali ni kuwa, Je kulikuwa na ushiriki wa Nyerere? na Je mapinduzi ni halali ?

Ustadhi Makala yako imekaa kama hadithi kuliko ukweli,mengi tumeyasikia kuhusu Okello na nafasi yake katika mapinduzi ya Zanzibar.Lakini katika makala yako unajaribu kutufanya tuamini ya kua John Okello hakua lolote na si chochote.Sasa nataka nikuulize maswali yafuatayo.Kama kweli hakua lolote na si chochote?Nini kimekusukuma kuandika makala hii?Kwanini alipata umaarufu na kuweza kuheshimiwa na kuogopwa na viongozi wa juu akiwemo Karume "mwenyewe mtu asie jua kusoma wala kuandika na hakili zake zilimtosha mwenyewe"Kwa mujibu wa makala yako?Alipata ujasiri wapi kutoa matamko uliyoyahorodhesha katika makala yako?Kwanini waliamua kumfukuza na alipotelea wapi?Ustadhi usijaribu kupotosha historia,hata kama mtu alikua na mapungufu kiasi gani tujadili mapungufu na nafasi yake katika histori ya mapinduzi,na sio kujaribu kufuta historia yake.Ahsante kwa hadithi.

Hii naona wana ASP kama wanajaribu kuficha uchafu na ubaya wao na wanajaribu kuwa cover ndugu zao wa bara na kina mchonga meno, nani asiyetambua ukweli iliyotokea na mauwaji wa kikati zilizofanywa na hao wanojitia wana mapinduzi, halafu wanajitia kuita mapinduzi ya halali, kuna halali hapo ?????? baada ya kupinduwa serikali ya halali iliyochaguliwa na wananchi. na hioo uuwaji ya ma elfu kutakuwa na uhalali hapo, wanafikiri Mwenyenzi Mungu hayupo na wala hana habari, kwa Mwenyenzi Mungu malipo dunia na akhera yapo, wataweza kuwadanganya binadamu dunia lakini kamwe hawatoweza kumdanganya Mwenyenzi Mungu.

kwa mujibu wa muandishi MAPINDUZI YALIKUWA HALALI na yalifanywa na na WAZNZ WENYEWE ................kweli ikidhihiri uongo hujitenga
 

......hapa inahitajika kupata wasifu sahihi wa Okello, je yeye ni nani, alizaliwa wapi, alikuwa mwnajeshi kweli au alikuwa mkwezi na mkulima, ilikuwaje atoke Kenya/Uganda na awe kinara na mwasisi wa mapinduzi? je alikuwa mamruki/alikodiwa?

Makala  inaikataa filamu bila ya kuthibitisha kitaalamu kwa wasomaji wake ukweli  juu ya  ubunifu wa hiyo  filamu maarufu ya Ki-taliana inayoonyesha mauwaji ya wananchi Zanzibar mwaka huo wa 1964 na hii ya watu wasiopindukia 200 na katika sehemu za mjini hawazidi 25 katika siku za mwanzo za mapinduzi. Makala isitufiche warithi wa nchi hii tunahitaji kuelewa.
Ukiiangalia filamu ya kitaliano inaelezea mauwaji kati ya January 18 na 20, 1964.  Inamaana baada ya January 12, 1964 mauwaji yaliendelea. Nchi zilizo makini na utendaji wake na kusimamia sera na haki zake ingelikanusha filamu hii na kuwatafuta na kuwashitaki wahusika waliobuni ubunifu huu. Ama serikali zikolikizo au ndio hewala bwana au ukweli upo juu ya filamu hii.
Nimaoni yangu.

Wanzanzibara wanamatatizo ambayo yanasababishwa na dini iloletwa na Waarabu na pia tatizo lingine la kujiona kuwa wao ni Waarabu zaidi ya Waafrika.
Hapa mwandishi anaonesha kama Mapinduzi yote yalifanywa na Wanzíbari bila kuhusisha Tanganyika, maana yake ni kuwa wao ndo walokuwa wenyewe wenye nia ya dhati ya Mapinduzi lakini ukiona wanamhusisha Nyerere na Tanganyika watasema alifanya ili kueneza Ukristo Zanzibar. Hii ni dhambi ambayo inawatafuna Wazenji na ni kama kukimbia kivuli chao wenyewe. Yaani ikisemwa kama kuna Watanganyika itaambiwa kwa kuwa ilikuwa kueneza Ukristo Zenji.
Mwandishi anamuonesha John Okello kama mtu mjinga,mbaya na asiye na weledi wowote, swali ni je ilikuwaje hao wenye akili na usomi kumchagua yeye John Okello awe kiongozi wa Mapinduzi???
Je kama alivyouliza mchangiaji hapo juu, kuwa kama kitendo cha kumrudisha John Okello kwao kinaonesha hakuwa anapendwa na wanamapinduzi sasa je kitendo cha kumuua Karume kwa risasi kinaonesha wanamapinduzi walimpenda pia???
Hapa mwandishi hataki hata kuonesha kama John Okelo alikuwa ana mchango wowote kufanikisha mapinduzi Zanzibar, sijui kwanini labda kwa kua John Okelo nio Mkristo au kwa kua alikuwa Mweusi (Jaluo/Acholi) hana damu za kiarabu?? Je ni kweli hana mchango wa wa kuandaa vijana kufanikisha mapinduzi?? Hii ni aibu na chuki dhidi ya watu wengine kwa lamba dini yao au rangi ya ngozi yao kutotambua hata mchango wao mdogo katika kazi waloifanya.
Mwandishi anasema askari walikuwa polisi kutoka Tanganyika, anasema viongozi wa mapinduzi walikuwa Dar-es salaam (Tanganyika), pia kasahau kusema kua Karume alipewa askari kutoka Tanganyika kuimarisha ulinzi baada ya mapinduzi, lakini hataki kuonesha kama Tanganyika ilikuwa na nia ya ukweli kufanya mapinduzi Zanzibar. Nafikri Nyerere angekua na asili ya Kiarabu au angelikuwa Mwisilamu labda mwandishi angesema historia tofauti na alivyoandika leo hii.
Nataka nikufunde kidogo mwandishi wa habari hii ya Mapinduzi Zanzibar.
Jina Zanzibar ni kwa lugha ya Kiajemi ikimaanisha ni Pwani ya watu weusi (Coast of black people). Hao wahamiaji wa Kiajemi na Kiarabu ambao leo kunawafanya Wanzanzibar kujinasibisha nao walikuta babu zetu weusi katika visiwa hivyo, Waarabu waliweka matabaka kwa kuangalia rangi za ngozi zao na asili zao, ndio mana Wanamapinduzi waliiondoa serikali ya Ki-Oman katika Zanzibar. Leo hii kizazi hiki kinataka kurudi huko huko badala ya kufikri kuungana na kutengeza nchi moja ya Tanzania. Eti sisi Waislamu wao Wakristo, eti sisi waarabu wao Waafrika, ndio ujinga huu, twataka nchi yetu hatutaki muungano. Jina la kikoloni ndilo twang'ang'ania bila haya.
Nafikri kwa leo niishie hapa, labda wakati mwingine nitakuja "NIKIPATA NAULI".
 

huja kimoja cha maama ulichosema. Uislamu ni tatizo lako!

Ahmed rajab,
una matatizo makubwa sana wewe. Simulizi zako zinajaribu kujenga hisia za kujenga Jamhuri ndani ya Jamhuri. Haya ni yanayoanza kushamiri zanzibar sasa. upotoshaji mwingi.
Suala la Okello Liko wazi. Tatizo lake ni kutovumilia uwoga wa Wazanzibari wetu hasa viongozi. Baada ya kuona kutokujiamini kwingi kwa viongozi wetu hivyo akatangaza kuwa Karume awe Waziri Mkuu na yeye Rais wa Zanzibar. Tatizo likaanzia hapo.....
2.Okello alikua sponsored na Mwl. Nyerere, Oginga Odinga, Owino(aliyetumwa kumfuata Uganda akiwa msaidizi binafsi wa General Titto Okello)  na Chief Odemba Kagose. Mkutano wa kumleta Okello kwenye mapinduzi ulifanyika kwa Chifu Odemba usiku wa manane na Oginga aliondoka alfajiri kurudi Kenya. usisahau Oginga alitusaidia ktk logistics ili kumzuia Kenyatta kuingilia na kuchukua Zanzibar kuwa mali yake binafsi. Pemba makao yake ya kuishi na Unguja kisiwa rasmi cha Utalii duniani. KARIRI HII.
Wengi wa viongozi waandamizi wa serikali ya mapinduzi walikua Dar siku za Mapinduzi. macruiter wengi toka Bara walifanya kazi  siku ya mapinduzi. Tusidanganyane kwa sababu kikazi kikubwa cha leo kimenyimwa historia ya kweli. Usichangie upuuzi huu.
Muungano wa Tanzania si wa kushtukiza au bahati mbaya.
Prof. Msukwa Theodore
Thesalonike.

Nimesoma kwa uangalifu makala Yao. Lakini Ina uproots haji mkubwa sana. Hivi karibuni nimesoma makala ya mchambuzi we historia anayeitwa William Shao. Nimesoma na hats vitabu kadhaa Khufu jambo Hilo. Kulingana na tote yaliyoandikwa na waandishi wengine ambayo hayajapingwa na ambayo yana mantiki, makala Yao Ina lengo mona kubwa. Na lengo hilo ni kupotosha ukweli aw historia ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hao uliowahoji ndio wale wale wasiotaka ukweli ujulikane.

Simulizi hii haisemi kweli ya dhaili, kuna baadhi inapotosha ukweli, sijui lengo la mwandishi ni kuficha nini, kusema watu walikufa wengi au watu waliua wenzao? Eneo la mwnanyamala kule dar es salaa katika mtaa wa mchangani, kuna mzee aliyepigana katika kufanya haya mapinduzi, anasema kwa mkono wake anakumbuka alikata vichwa 7kwa panga na kuua kabisa. Baadaye alipewa bunduki ambayo aliitumia kwa kuua, mwishoni alifukuzwa na serikali ndipo akaenda kupanda majahazi hadi bagamoyo ambapo alitembea na wenzake 4 hadi jangwani kabla hajmpata mwanamke wa kikwele alikwenda kumficha  na kisha kuoana. mzee huyu anaitwa Mussa Ramadhan Chapa.
Pili mwandishi atwambie bwana Okello alikuwa na nafasi gani ktk serikali mpya, atwambie pia kwa nafasi ipi alitumia kwenda kutoa matangazo hayo kwenye radio na tatu atwambie ni kwa uwezo upi alipewa katibu wa kutembea nae ,yaani ndg Jaha Ubwa. Tunasubiri

Mwandishi anapenda kuandika makala za uwongo zisitao na kina fanya utafiti kujua Okello alikuwa kuwepo zenji na kwa jukumu gani na nani aliyemfukuza zenji safari yake ya mwisho ilikuwa ikulu na ndiyo waliompeleka kenya

Toa maoni yako