Michezo
Ustaarabu umetushinda, tuweke na makato ya vyoo
Chesi Mpilipili
Toleo la 203
14 Sep 2011

NILIVUTA karatasi na kalamu na kuanza kuandaa makala ya kupinga uamuzi wa Serikali wa kuufunga Uwanja wa Taifa kwa mechi za Ligi Kuu yetu mara tu baada ya kusikia taarifa hiyo ikitangazwa kwenye kipindi cha michezo cha moja ya vituo vyetu vya redio.

Hoja iliyokuwa kichwani mwangu ilikuwa ni ile ya kutaka kufahamu sababu za Serikali kukurupuka na kufunga uwanja huo siku tatu kabla ya kuanza kwa mechi za Ligi Kuu ambapo baadhi ya timu zilikuwa zimeishakubaliwa kuutumia uwanja huo kama uwanja wao wa nyumbani.

Hata hivyo, nilishindwa kuendelea kuandaa makala yangu hiyo baada ya kusikia sababu zilizosababisha Serikali kuchukua uamuzi wa ghafla wa kuufunga uwanja huo kwa mechi za Ligi.

Imeelezwa kuwa Serikali iliamua kufunga uwanja huo kutokana na uharibifu mkubwa uliofanywa na wahuni wachache (sio mashabiki wa mpira!) wakati wa mchezo wa Ngao ya hisani kati ya timu mbili kubwa nchini, Yanga na Simba uliokuwa umefanyika siku mbili kabla ya uamuzi wa Serikali kuufunga uwanja huo.

Serikali imesema kuwa uharibifu huo mkubwa ulijumlisha kuvunjwa kwa masinki ya kunawia mikono na yale ya chooni na pia viti vya kukalia kwenye majukwaa.

Ni wazi kuwa hapa hatuhitaji kutumia sana ‘intelijensia’ kuweza kufahamu ni mashabiki wa timu gani siku ile walikuwa na sababu ya kufanya uhuni ama ushamba ule!

Ndio, waliofanya ushamba huu ndio wale wale ambao mtu mzima na akili zake na ana familia inayomtegemea anakojolea ndani ya chupa ya maji na kisha kuirusha chupa hiyo kwa mashabiki wenzake walio chini yake kwenye jukwaa!

Serikali ilifafanua pia kuhusu gharama kubwa za kuendesha uwanja huo hasa unapotumika kwa mechi za timu zisizokuwa na mashabiki wengi na hivyo kuingiza mapato madogo yasiyokidhi gharama kubwa za kuutunza uwanja ambao ni moja ya viwanja bora kabisa barani Afrika.

Kwa mujibu wa maelezo kutoka serikalini, Uwanja ule sasa ungetumika kwa mechi za kimataifa tu zinazohusu timu ya taifa na zile zinazohusu timu za Yanga na Simba zitakazocheza na wapinzani wao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika na ile ya Kombe la washindi ambayo timu hizo ndio wawakilishi wetu.

Hata hivyo, siku moja tu baada ya tamko la serikali la kufungia uwanja huo, TFF ilipeleka maombi kwa serikali iziruhusu Yanga na Simba kutumia uwanja huo katika michezo yao miwili ya Ligi Kuu kwa kile kilichoelezwa kuwa wingi wa mashabiki wa timu hizo ungehakikisha mapato makubwa yanayokidhi gharama kubwa za matunzo ya uwanja huo.

Hii kidogo inashangaza. Serikali iliamua kuufunga uwanja huo kutokana na uharibifu mkubwa uliofanywa na mashabiki wachache baada ya mchezo wa Ngao ya Hisani kati ya Yanga na Simba lakini papo hapo TFF ikatuma maombi kutaka wale wale waliosababisha uwanja ule kufungwa wautumie kwa ajili ya mechi zao mbili za Ligi Kuu!

Kwa maana nyingine ni kuwa TFF ilikuwa inaziombea Yanga na Simba ambao mashabiki wao ndio waliosababisha uwanja huo kufungwa kutokana na uharibifu mkubwa uliofanyika baada ya mechi yao ya Ngao ya Hisani kutumia uwanja huo kwa mechi zao mbili za Ligi Kuu na hivyo kuwepo na uwezekano wa kuwepo uharibifu mara mbili zaidi ya ule uliosababisha uwanja kufungwa!

Nasema hivi kwa sababu katika taarifa yao TFF hawatuambii jinsi ambavyo watahakikisha kuwa mashabiki wa timu hizo hawafanyi uharibifu kwenye uwanja huo kama walivyofanya kwenye mechi yao ya Ngao ya Hisani na kusababisha Uwanja kufungwa siku tatu kabla ya Ligi kuanza.

Wanachotuambia ni jinsi tu mashabiki wengi wa timu hizo watalavyoingiza mapato makubwa na hivyo kukidhi gharama kubwa za kuendesha uwanja huo, basi. Ama kweli Mpira Pesa.

Nijuavyo mimi makato kwa ajili ya gharama za uwanja yanayokatwa baada ya mechi ni kwa ajili ya kulipia maji, umeme na ukarabati mdogo mdogo wa sehemu zinazoharibika kila baada ya mechi. Hayajumlishi kufidia ushamba wa kuvunja viti na masinki wa choo unaofanywa na wahuni wachache!

Nilidhani kama TFF ina nia ya kweli ya kupeleka mpira mikoani basi wangengeziomba timu hizo kucheza mechi zake mbili za Ligi kwenye Uwanja mwingine mkubwa wa Kirumba Mwanza ambako hakuna viti vya plastiki ambavyo washamba wachache wanaweza ‘kuvionea’ na kuvivunja bali watazamaji wanakalia zege gumu lenye umri wa zaidi ya miaka 30 sasa!

Kama TFF wanang’ang’ania Yanga na Simba kucheza kwenye Uwanja wa taifa basi angalau watuhakikishie kwanza usalama wa Uwanja wetu uliotugharimu mamilioni ya fedha kuujenga. Watueleze hatua watakazochukua ili kuhakikisha kuwa viti na vyoo vya Uwanja wetu haviharibiwi na pale vitapoharibiwa timu zinazohusika zitavilipiaje.

Ninaamini pia kuwa kuna kila sababu sasa ya kuweka makato maalumu kwenye mapato ya timu zote zitakazotumia uwanja huo kwa ajili ya mechi zao. Makato haya yawe mbali na yale makato ya kawaida ya gharama za uwanja ambayo tayari yana majukumu yake.

Hapa nina maana kuwa kuanzishwe utaratibu ambapo kama Yanga na Simba zinacheza basi baada ya mechi uongozi wa Uwanja kwa kushirikiana vyombo vinavyohusika wanapitia amali zote za uwanja zilizofanyiwa uharibifu, wanazipigia mahesabu na gharama yake inagawanywa kwa timu mbili zilizocheza mechi na kisha kukatwa kwenye mapato ya mechi zinazofuata za timu hizo.

Ninaamini kuwa angalau kwa njia si tu kwamba tutakuwa angalau tumedhibiti uharibifu wa uwanja wetu kwa kiasi fulani bali hata timu zetu nazo zitapaswa kuwachukulia hatua mashabiki wake wanaofahamika kuwa ni mahodari wakuvunja vyoo ili kukwepa adha ya kukatwa mapato yao!

Wanajulikana. Katika moja ya mechi kubwa zilizochezwa uwanjani humo nilipata kwenda maliwatoni wakati wa mapumziko na kukuta vyoo vyote vimejaa na watu wanasubiriana lakini mhuni mmoja akawa anajisaidia haja ndogo kwenye masinki ya kunawia mikono huku walionekana kuwa ni rafiki zake wakimuangalia na kucheka tu!

Kwa kuwa kila Mtanzania anapaswa kuwa mlinzi wa mwenzie nikamuuliza mheshimiwa yule alikuwa anafikiri anafanya nini vile. Jibu lake likawa “kwani Vipi!” huku yeye na wenzake wakiniangalia kama nilikuwa nataka kuanzisha lolote.

Kwa vile wote walikuwa na vifua vipana kuliko changu, nikaamua kubaki na amani yangu. Na meno yangu.

Ni wazi pia kuna umuhimu wa ile ‘screen’ kubwa ya uwanjani pale kuanza kazi na kamera zake kuwekwa hadi kwenye vyoo ili pale msimamizi wa kamera zile anapoona mshamba fulani anavunja masinki yetu anaunganisha moja kwa moja kwenye screen kubwa kiwanjani ili aonekane tumzomee kisha achukuliwe hatua zinazostahili!

Tukifanya haya na kuendelea kufunza watu wetu ustaarabu angalau tunaweza tukawa na uhakika wa Uwanja wetu uliotugharimu mabilioni ya vijisenti ili kuujenga kudumu kwa miaka 100 ijayo.

 

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Chesi Mpilipili
chesimpilipili@gmail.com

Toa maoni yako