Ahsanteni kwa 2016, mambo mapya 2017

HILI ni gazeti la mwisho la Raia Mwema kutolewa kwa mwaka 2016, labda tu kama litatokea tukio lisilotarajiwa litakalolazimu kwamba tuingie mtamboni na kuchapa toleo lingine.

Kwa vyovyote vile, mwaka 2016 ulikuwa na changamoto zake za tofauti na miaka mingine yote iliyopita. Tunataraji kwamba mwaka ujao wa 2017 nao utaibuka na mengine ambayo hatukuwa tumeyataraji sasa.

Hata hivyo, wakati tukiwashukuru wasomaji wetu watiifu kwa kuendelea kutuunga mkono tangu tumeingia sokoni takribani miaka kumi iliyopita, tumebaini kwamba kiu yenu ya habari imezidi kuwa kubwa kuliko wakati mwingine wowote kwenye historia ya binadamu.

Vyombo vingi vya asili vya habari (magazeti, redio na televisheni), vimepata changamoto kubwa kwenye miaka ya karibuni kutokana na kuibuka kwa kasi kwa mitandao ya kijamii.

Tumeona kwamba wasomaji wetu sasa kuna wakati mnapata habari mapema kabla hata magazeti yetu hayajatoka mitaani. Wakati mwingine, mnapata habari ambazo mnatamani kuziamini wakati huohuo lakini hamuwezi kupata uhakika hadi magazeti yaseme kesho yake.

Kwa kutambua hilo, sisi katika Raia Mwema tumejipanga katika kuhakikisha kwamba tunatii kiu mbili za wasomaji wetu kwa mpigo; kiu hizo ni ile ya kupata habari wakati huohuo tukio linapotokea na pia kuwafanyia uchambuzi wa habari husika kwa haraka hiyohiyo–isipokuwa kwa uhakika zaidi.

Tunataraji kwamba kwa hatua yetu hii ya kuwafikia wasomaji wetu kwa haraka –kupitia simu zenu za mikononi na mitandao ya kijamii, Raia Mwema litaendelea kubaki kuwa gazeti lenu pendwa.

Kwenye toleo hili na kwenye matoleo yetu mengine yafuatayo, tutaendelea kutoa maelezo kuhusu ni namna gani ninyi wasomaji wetu mtapata taarifa hizi popote pale mlipo, ali mradi mna simu, kompyuta au kifaa chochote kinachowezesha kupatikana kwa taarifa kuhusu habari muhimu.

Wakati tukiwatakia Heri ya Mwaka Mpya wa 2017 unaotarajiwa kuanza wiki ijayo, tunazidi kuwasisitizia wapenzi wasomaji wetu kwamba gazeti hili litabaki kuwa lenu kwa maana ya kuripoti yale mambo ambayo mnapenda kuyasoma.

Sote tunatazama mbele tukiamini kwamba mwaka ujao wa 2017 utakuwa wa faida kwa kila mmoja wetu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *