Habari
Aliyemshuhudia Dk. Ulimboka alonga
Mwandishi Wetu
Toleo la 246
4 Jul 2012
Dkt. Ulimboka akiwa ICU
  • Ni rafiki yake aliyekuwanaye wakati akitekwa

TAKRIBAN wiki moja baada ya kutekwa, kuteswa na kuumizwa vibaya kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, mmoja wa marafiki zake, Dk. Deogratius Michael (36), aliyeshuhudia tukio la kutekwa amezungumza na Raia Mwema akisema taarifa za baadhi ya vyombo vya habari kwamba ametoweka si za kweli.

“Nasikia kuna redio moja wamesema kwamba mimi sionekani na kwamba nimetoweka. Ukweli ni kwamba nipo. Napatikana na nimekuwa nikiwasiliana na watu mbalimbali. Ushahidi wa hilo ni kama hivi sasa ninavyozungumza nanyi,” alisema Dk. Deo jana Jumatano katika mazungumzo na Raia Mwema.

“Ukiacha kufika Kituo cha Polisi Bunju, nilikwenda pia Kituo cha Polisi Oyesterbay na katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam (Central Police) ambako niliandikisha maelezo.

“Siyo tu kuwa baada ya tukio hilo nilikuwa nikipeleka taarifa Polisi, lakini pia mimi ndiye niliyekuwa kwenye gari la wagonjwa la kampuni ya AAR lililomleta Dk. Ulimboka hospitalini MOI na kwa siku zote nne, tangu tarehe 27 Juni nilikuwa hospitalini MOI nikiwa pia karibu na wanafamilia. Hata siku ya kumpeleka nje nilikuwa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere,” alisema.

Aliongeza Dk. Deo:  “Mimi ndiye niliyepata taarifa za kuumizwa kwa Dk. Ulimboka na ndiye niliyekwenda Kituo cha Polisi, Bunju alfajiri ile kumtambua baada ya kupigiwa simu na Polisi.

Kamanda Ahmed Msangi “ Na si kweli pia yanayozungumzwa kwamba Kamanda Ahmed Msangi alikuwa kati ya waliokuwa kwenye tukio. Dk. Ulimboka na mimi tunamfahamu. Alipokuja kumhoji Dk. Ulimboka MOI alimkumbuka kwa kuwa tulikuwa tukionana naye kila mara, si kuwa alikuwa kwenye tukio siku hiyo”.

Katika hatua nyingine taarifa za maendeleo ya Dk. Ulimboka zilizopatikana jana Jumatano zinasema alikuwa akiendelea vizuri na kwamba atahitaji kusafishwa figo kwa muda wa karibu wiki tatu mfululizo.

Lakini wakati hayo yakiendelea, taarifa ambazo gazeti hili limezipata zinaeleza kuwa mgomo wa madaktari nchini pamoja na tukio hilo la Dk. Steven Ulimboka, sasa umeingia katika sura mpya baada ya kikundi cha mtandao unaodaiwa kufanikisha ‘kumuingiza’ Rais Jakaya Kikwete madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2005, kudaiwa kuhusika kufadhili baadhi ya madaktari  kuchochea mgomo huo.

Pamoja na baadhi ya wanasiasa ndani ya CCM kuhusishwa, lakini pia wamo wanasiasa kutoka chama kimoja cha upinzani kinachotajwa kuwa nyuma ya shinikizo la kuendeleza mgomo huo wa madaktari.

Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa vya habari, lengo la ufadhili huo, ambao hata hivyo umekanushwa na Katibu wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Edwin Chitage, ni kile kinachodaiwa kuwa ni hatua ya kulipa kisasi kwa kuzingatia mwenendo wa siasa ndani ya CCM na ‘panga-pangua’ ya viongozi serikalini, pamoja na mikakati ya vyama pinzani kujenga chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali.

Taarifa hizo zilizopatikana zinabainisha kuwa pamoja na madaktari kushinikiza uboreshaji wa maslahi yao, sambamba na utoaji wa huduma bora za afya, siasa za visasi ndani na nje ya CCM, zimeendelea kudandia mgomo huo na kuanza kuwafanya baadhi ya madaktari kufikiri upya ushiriki wao katika mgomo huku kukianza kujitokeza wito wa kutaka kurejea katika meza ya majadiliano.

Kujitenga kwa baadhi ya madaktari dhidi ya mgomo huo wa sasa kunathibitishwa na taarifa rasmi iliyotolewa na  Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha.

Katika taarifa yake, Aligaesha anasema; “Kurugenzi ya Tiba hospitalini hapo huduma zimeendelea kutolewa kwa kiwango cha kati wagonjwa ni wachache wanaokuja kutibiwa.

“Kwa upande wa idara ya tiba, madaktari bingwa wote na registrar (wasajili) wote wamefika kazini na wanafanya kazi. Interns (madaktari waliohitimu lakini wapo chini ya ungalizi) 11 wamefanya kazi. Major ward round (ukaguzi wodini) zimefanyika. Kliniki zote za leo zimeendelea kufanya kazi pia cliniki za mchana zitafanyika.

Kuhusu idara ya watoto, anasema madaktari bingwa wote wapo na wanafanya kazi wapo wodini wanaona wagonjwa. Changamoto ni kwamba inabidi pia wafanye kliniki za wagonjwa wa nje na wanajitahidi kufanya hivyo.

“Idara ya magonjwa ya nje. Registrars na Daktari Bingwa wote wapo na wanafanya kazi.

“Idara ya magonjwa ya afya ya akili, Madaktari Bingwa wote wamefika kazini . Bada ya wagonjwa wote kupelekwa wodini, walionwa na madaktari. Wagonjwa katika kitengo hiki ni wengi ukilinganisha na idadi ya madaktari bingwa, lakini kliniki zimeendelea kufanyika kwa kiwango cha kati. Kiliniki ya wagonjwa wajidunga imefanyika.”

“Idara ya magonjwa ya dharura, Registrar wote wamesaini lakini wliofanya kazi ni wawili tu. Daktari Bingwa yupo na anafanya kazi. Idara ya mazoezi ya viungo, Wafanyakazi wote wapo na wanafanya kazi,” anaeleza ofisa huyo wa Muhimbili.

Kuhusu Kurugenzi ya Upasuaji anasema huduma za upasuaji zinafanyika lakini si sawa na jinsi zilivyokuwa zinafanyika kabla ya mgomo kwani wagonjwa ni wachache kwenye baadhi ya kliniki na baadhi ya kliniki wagonjwa wanakuwa wengi.

“Wagonjwa wa upasuaji walioko wodini wanaonwa japo ni wachache ukilinganisha na hali ilivyokuwa. Baadhi ya huduma za upasuaji (operations) zimefanyika ingawa wagonjwa ni wachache kwa vile idadi ya wagonjwa wanaokuja kliniki au waliolazwa kwa ajili ya upasuaji ni wachache.

Akizungumzia huduma za tiba shirikishi anaeleza: “Vipimo vya maabara na vile vya uchunguzi wa radiolojia vinaendelea kufanyika kama kawaida ingawa idadi ya vipimo vimepungua ukilinganisha na kabla ya mgomo. Idara ya famasia pia inafanya kazi kama kawaida. Idadi ya wagonjwa wanaoandikiwa dawa ilipungua ukilinganisha na kabla ya mgomo. Na katika kurugenzi ya uuguzi, huduma za uuguzi zimeendelea kutolewa kwa kiwango cha kawaida.

Kwa upande mwingine, taarifa kutoka Hospitali ya Rufaa Bugando zinaeleza kuwa hali ya huduma za tiba hospitalini hapo bado ni tete.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa hali hiyo imesababishwa na tukio la kufukuzwa madaktari 47 waliokuwa katika uangalizi wa mafunzo kwa vitendo (interns). Interns hao waliondolewa hospitalini hapo na kurejeshwa kwa mwajiri wao ambaye ni Wazara ya Afya.

Kwa mjibu wa Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk. Charles Majinge, eneo litakaloathirika kwa kiasi kikubwa baada ya kufukuzwa kwa madaktari hao ni mapokezi ambako madaktari walioko hao ndiyo walikuwa wakiwapokea wagonjwa kabla ya kuonwa na madaktari bingwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jana, Mkurugenzi huyo alisema kuwa hali ya hospitali hiyo haitaathirika kwa kuwa madaktari waliopo wanaweza kumudu kukabiliana na upungufu huo hasa kwa kuwa kasi ya wagonjwa kwenda kupata matibabu katika hospitali hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Maoni ya Wasomaji

Tunaomba mfatilie kwa makini swala hili ili kukomesha vitendo vya kikatili kama hivyo..inauma sana kwa kusoma baadhi ya vyanzo vya habari kama magazeti kua ni serikali yetu inahusika kwa swala kama hili kiukweli ni aibu kubwa sana kwa taifa...msilegeze uzi kwa kufuatilia hilo,,,,!
 

Toa maoni yako