Arumeru Vijijini wasonga mbele mradi wa viwanja

Arusha
Shamba la kahawa la Burka
Shamba la kahawa la Burka

KAMATI ya Fedha na Uchumi ya Halmashauri ya Arusha Vijijini imeridhia kupitishwa kwa mradi mkubwa wa kugawa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa mji mpya katika eneo la Lakilaki, nje kidogo ya mji wa Arusha.

Uamuzi huo umekuja baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa mradi huo ulikuwa shakani kutokana na tofauti za kimtazamo kati ya Mbunge wa Jimbo hilo, Goodluck ole Medeye, kwa upande mmoja na madiwani, watumishi wa halmashauri kwa upande mwingine.

Wasiwasi juu ya kusuasua kwa mradi huo unatokana na hatua ya halmashauri hiyo kukopa takriban Sh. bilioni 8.6, katika Benki ya Biashara Afrika (Commercial Bank of Africa) ili kulipa fidia kwa kampuni iliyokuwa ikimiliki shamba  hilo.

Ni mkopo huo wa fedha ambao tayari halmashauri inatakiwa kuanza kulipa riba yake ndiyo ulioanza kuwatia hofu baadhi ya watumishi na madiwani kuwa iwapo mradi huo ungekwamishwa, basi halmashauri hiyo ingejitia kitanzi.

Mradi huo wa Lakilaki unaweza kutoa viwanja 400 na ni mwendelezo wa Halmashauri hiyo ya Arusha Vijijini kujenga miji mipya ya kisasa kwa kupima viwanja katika maeneo yaliyokuwa mashamba ya walowezi yanayozunguka mji wa Arusha. Tayari halmashauri hiyo imegawa viwanja katika mashamba ya Burka na Gomba Estate, baada ya wamiliki wake kulipwa fidia.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana mwishoni mwa wiki kutoka ndani ya halmashauri hiyo zilieleza kuwa kikao cha kuridhia mradi huo wenye thamani ya mabilioni ya fedha kilifanyika katika ukumbi wa halmashauri, Januari 17, mwaka huu.

Kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Simon ole Saning’o, kilihuduriwa na wajumbe wote wa kamati pamoja na Mbunge Medeye, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi.

Taarifa za ndani zinadai kuwa kulikuwa na mvutano mkali baina ya Medeye na wajumbe wa kamati hiyo ambao wote waliunga mkono hatua ya kupitishwa kwa mradi huo.

“Pamoja na Medeye kujenga hoja kadhaa ikiwamo ile ya kutoshirikishwa kama mbunge  wakati mradi ukibuniwa, wajumbe karibu wote walimpinga na kupendekeza kuwa mradi uendelee na vinginevyo halmashauri ingejikuta matatizoni,” alieleza mtoa taarifa wetu.

Mbunge huyo  anadaiwa kupinga mpango huo ambao anadai kuwa hauna manufaa kwa wananchi wa kawaida wa jimbo lake na anapendelea mipango ya kugawa ardhi iwalenge watu wa kipato cha chini na pia Serikali iwape hatimiliki za kimila kwa mujibu wa sheria mpya za ardhi.

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha Vijijini, Simon ole Saning’o, alikiri kufanyika kwa kikao hicho cha kamati na kuongeza kuwa kwa sasa maazimio hayo bado ni siri ya halmashauri.

“Kanuni zetu haziruhusu kuzungumzia suala fulani mahususi kama hili hadi hapo maazimio yatakapoletwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kitakachokutana Januari 27, ambako tunatarajia kuyawasilisha kwa majadiliano zaidi,” alisema Saning’o.

Mwenyekiti huyo alikanusha pia kuwapo kwa tofauti kati ya madiwani na mbunge wao na kuongeza kuwa, kuna baadhi ya mambo yanakuzwa na watu wenye malengo mabaya na maendeleo ya halmashauri yao.

“Hakuna tofauti kati ya madiwani na mbunge hata kidogo, kuna watu wanazusha mambo tu na nia yao ni kuzorotesha shughuli za maendeleo ya halmashauri yetu ila sisi tumewapuuza tu,” alisema.

Wakati  kukiwa na dalili njema kuwa sasa mradi huo utafanyika, wiki moja iliyopita Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi, Mkoa wa Arusha iliwaita na ‘kuwafunda’ madiwani na viongozi wa chama hicho Wilaya ya Arumeru, kwa lengo la kujaribu kumaliza mgogoro unaotishia utekelezaji wa miradi kadhaa ya maendeleo ya wananchi katika wilaya hiyo.

Taarifa ambazo Raia Mwema ilizipata mwishoni mwa wiki zinaeleza kuwa kikao hicho kilifanyika katika ofisi za CCM Mkoa wa Arusha, mwanzoni mwa wiki iliyopita na kwamba, wajumbe wa kamati ya siasa wakioongozwa na Mwenyekiti wake, Onesmo Nangole, walizungumza na madiwani pamoja na viongozi wa chama wa wilaya hiyo ya Arumeru.

Arumeru, kichama na Serikali inatambuliwa kama wilaya moja lakini ina halmashauri mbili ya Arusha Vijijini na Halmashauri ya Meru pamoja na majimbo mawili ya uchaguzi, ambayo ni Arumeru Magharibi na Arumeru Mashariki.

Kikao hicho kilihudhuriwa na madiwani zaidi ya 10 pamoja na viongozi wa juu wa chama hicho ngazi ya wilaya. Pamoja na mambo mengine, kikao kilijadili usimamiaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika wilaya hiyo.

Pamoja na kufanyika kwa kikao hicho, kumekuwapo na taarifa zinazoenea kwa kasi zikidai kwamba, Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye, yuko katika maelewano duni na baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Arusha Vijijini kutokana na mwenendo wa mradi huo wa kugawa viwanja katika shamba hilo la Lakilaki.

Hatua hiyo inaelezwa kuleta msuguano wa chini kwa chini baina ya mbunge huyo na madiwani ambao tayari wamepitisha uamuzi wa kugawa viwanja katika shamba hilo lenye ekari zaidi ya 1,000 katika vikao vya Baraza vilivyofanyika mwaka 2011.

Mazingira hayo ndiyo chanzo cha Kamati ya Siasa ya CCM, Mkoa wa Arusha kuchukua hatua za kuitisha kikao kwa lengo la “kusafisha hali hewa na kuwafunda” madiwani na viongozi wa chama kuwa wanapswa kuvunja makundi yao na kushirikiana kutekeleza ilani ya chama hicho kabla ya mwaka 2015.

“Kilikuwa kikao cha kidiplomasia tofauti na vikao vingine vya chama vilivyozoeleka siku hizo ambavyo hutawaliwa na fitina na mizengwe, tulielezwa umuhimu wa kuwa pamoja ili kutekeleza miradi ya maendeleo na pia kuongeza mshikamano katika chama,” kilieleza chanzo chetu kutoka ndani ya kikao hicho.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa viongiozi wa CCM ngazi ya mkoa walichukua hatua hiyo ya kuwakutanisha madiwani, mbunge na viongozi wa CCM ili kurudisha umoja na mshikamano na pia kutoa onyo kwao kutokana na kuwapo kwa hali ya kuimarika kisiasa kwa chama cha upinzani cha CHADEMA, katika maeneo mengi ya Wilaya ya Arumeru.

“Mwenyekiti Nangole aliwaonya kuwa mchezo wa makundi wanaouendeleza ndiyo utakuwa mauti yao katika uchaguzi wa mwaka 2015 iwapo hatakuwa pamoja na kushikamana kwa kufanya kazi pamoja,” alieleza zaidi mtoa taarifa wetu.

Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda, alilithibitisha gazeti hili Raia Mwema kufanyika kwa kikao hicho cha na kuongeza kuwa, vikao vya aina hiyo ni vya kawaida ndani ya CCM.

“Tulikutana kwa lengo la kujadili masuala ya maendeleo ya wananchi wa Wilaya ya Arumeru kama utekelezaji wa ilani ya uchaguzi, uhai wa chama na kukumbushana wajibu na majukumu yetu,” alisema Chatanda.

Hata hivyo, katika kile kinachotafsiriwa kama viongozi wa CCM mkoa walikuwa ‘wanampigia mbuzi gitaa’ muda mfupi baada ya kikao hicho cha kamati ya siasa, baadhi ya viongozi walifanya kikao kingine kikiwahusisha viongozi na watu mashuhuri katika wilaya hiyo katika klabu maarufu ya The Big Y, iliyopo eneo la Sekei wilayani humo kupanga mkakati wa kuwaengeua baadhi ya viongozi wa CCM ngazi ya wilaya.

Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa kiongozi mmoja mwenye madaraka makubwa wilayani humo (jina linahifadhiwa kwa sasa) ndiye aliyeitisha mkutano huo na kwamba na mambo mengine, alijaribu kuwaeleza viongozi hao hali ya kupwaya kwa uongozi wa chama ngazi ya wilaya.

“Aliyeitisha kikao aliwaeleza wajumbe waliohudhuria kuwa iko haja ya kufanya mabadiliko ndani ya uongozi wa CCM ngazi ya wilaya kuwa na mwenyekiti ambaye ana ushawishi wa kisiasa na atakayesaidia kuimarisha chama kwa kuwaunganisha watu na hivyo, CCM kuwa katika nafasi nzuri ya kushinda Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015,” kilizidi kueleza chanzo chetu.

Anayetajwa kutaka kumrithi mwenyekiti aliyeko madarakani kwa sasa ni mfanyabiashara maarufu mjini Arusha (jina linahifadhiwa), ambaye pia aliwahi kuwa mtumishi katika vyombo vya ulinzi na usalama katika miaka 1980 na kustaafu kwa hiari.

Kwa mujibu taarifa hizo mfanyabiashara huyo ndiye anayeungwa mkono na na kundi hilo na tayari  mkakati wa maandalizi ya “kumuuza” kwa wanachama wa CCM Wilaya ya Arumeru yameanza na yataratibiwa na kamati maalumu ya watu wanne, iliyoundwa katika kikao hicho.

Katika kikao hicho pia walikubaliana kuunda mtandao imara kichama utakaowezesha kushinda katika uchaguzi wa nafasi mbalimbali ndani ya CCM ambao unatarajiwa kuanzia ngazi ya mashina kuanzia Aprili, mwaka huu, katika nafasi zote katika chama na jumuiya zake.

Add new comment

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.