Makala
Askofu Kilaini: Kikwete ameelemewa na mafisadi
Aristariko Konga
Toleo la 007
12 Dec 2007

ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Method ius Kilaini, anasema baadhi ya viongozi wa serikali wanapokea pesa kutoka kwa wawekezaji wa nje, na hivyo kumfanya Rais Jakaya Kikwete awe na wakati mgumu katika kuongoza vita dhidi ya ufisadi wa kimataifa. Askofu Kilaini aliiambia Raia Mwema katika mahojiano maalum, yaliyofanyika wiki iliyopita, kwenye ofisi yake iliyoko katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam.

Alisema kwamba anamwonea huruma Rais Kikwete kwa kuwa lengo lake jema, la kupambana na rushwa kubwa au ufisadi wa kimataifa, linahujumiwa na baadhi ya viongozi walioko chini yake, wenye dhamana za kusaini mikataba na wawekezaji

wa nje, ambao hupewa pesa nyingi ili kuwapendelea wageni hao. Alisema kwamba wawekezaji hao wa kigeni huja nchini na pesa nyingi kwa lengo la kuwekeza, lakini huwa na malengo mengine zaidi na hivyo kuwahonga pesa baadhi ya viongozi walioko madarakani, ili walinde maslahi yao.

“Wanakuja na vitu vyao na mapesa mengi sana. Sasa wanapofika hapa wanayatumia mapesa haya kuwapa viongozi walioko madarakani.

Viongozi wa aina hii, ambao ndio walipaswa kumsaidia Rais Kikwete, ndio hao hao wanakuwa wa kwanza kumkwamisha. “Hao ndio wanaofanya dhamira nzuri ya Rais Kikwete, ya kupambana na rushwa hii kubwa, iwe ngumu kuitekeleza. Inabakia tu kusikia kelele za rushwa kwenye mahakama zetu hizi ndogo, ikiwahusu watu wadogo…Hii haitoshi,” anasema. Kilaini anasema kwamba, ufisadi huu wa kimataifa (rushwa kubwa) unalindwa sana na viongozi hao waliohongwa, kiasi kwamba mtu akijaribu kulinda maslahi ya taifa, hushurutishwa na wakubwa wake kwamba anapaswa kunyamaza.

“Ufisadi wa kimataifa, ambao ndio unaolisumbua taifa hivi sasa, unalindwa sana na walioko madarakani. Mtu akijaribu kuingilia kati anaambiwa ‘nyamaza’ na walioko juu yake. “Kwa hiyo serikali yetu ina kazi kubwa sana, na hasa Rais wetu Kikwete, ambaye ameonyesha moyo wa kutaka kupambana na tatizo hilo…

Ana kazi kubwa kwa sababu kuna watu wanashirikiana na wawekezaji hawa wa nje ili kujinufaisha wao. Ni kazi ngumu sana kwake. Mafanikio yako mbali sana nasi.” Askofu anasema kwamba vita dhidi ya ufisadi wa kimataifa inakuwa ngumu sana kwa sababu mikataba yenyewe ina usiri mkubwa, kiasi kwamba hata wale ambao wanatarajiwa kuwa wa kwanza kuupiga vita, wanajikuta hawana taarifa mapema kutokana na mazingira ya kificho.

“Wale ambao wanapaswa kuwa wa kwanza kupiga vita suala hili, na wenye dhamana hiyo, wanashindwa kupata taarifa na hata wanapokuja kuzipata, wanakuwa wamechelewa sana na mambo yamekwisha kufanyika na kuleta athari.

“Kutokana na usiri huu, kazi ya kupigana vita na ufisadi inakuwa ngumu sana. Hapa ndipo dhamira ya Rais Kikwete inakuwa vigumu kutekelezeka.

Hata hivyo, Askofu Kilaini anasema suala la ufisadi wa kimataifa halikujitokeza wakati wa utawala wa Rais Kikwete, bali lilianza kujitokeza wakati wa utawala wa Awamu ya Tatu, wakati Rais Benjamin Mkapa alipofungua zaidi milango ya uwekezaji wa nje.

Mara kadhaa wabunge wamekuwa wakilalamika ndani ya Bunge, kwamba mikataba hiyo ingekuwa inawekwa wazi mbele yao, lakini upande wa serikali umekuwa ukipinga dhana hiyo kwa madai kuwa mambo mengi ni ya siri baina ya wale wanaoingia kwenye makubaliano ya mkataba.

Katika hotuba yake ya kwanza bungeni, Rais Kikwete alionyesha kuguswa na mikataba mbalimbali na hivi karibuni amebainisha kwa kusema kwamba mikataba aliyoizungumzia wakati ule ilikuwa ni ile kati ya serikali na makampuni ya madini na tayari amechukua hatua kwa kuunda tume ya serikali na baadaye kamati ya kupitia upya mikataba ya madini. Hata hivyo, Mkapa alipoingia madarakani kwa ‘gia ya Mr Clean’ aliunda Tume ya Kero za Rushwa mara tu alipoingia madarakani, tume iliyoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba, lakini matokeo ya tume hiyo ya kihistoria hayajaonyesha kuzaa matunda yaliyokusudiwa.

Badala yake imekuja kubainika kwamba kipindi cha utawala wa awamu ya tatu kilisheheni rushwa kubwa kubwa ambayo imeliingiza taifa katika matatizo makubwa. Kabla hata ya kuanza kwa kipindi cha pili cha utawala wake, Mkapa alijiingiza katika biashara akiihusisha familia yake na baadaye mawaziri wake na mfano maarufu ni ule wa kujihusisha kwake na ununuzi wa mradi mkubwa wa mkaa wa mawe wa Kiwira.

Mkapa kupitia kampuni yake ya ANBEM Limited alianzisha kampuni (kabla ya kujitoa) iitwayo TANPOWER kwa kushirikiana na kampuni ya Waziri wake, Daniel Yona, kampuni iliyonunua hisa za mradi wa Kiwira, mauziano ambayo yamezua gumzo kubwa hasa ikizingatiwa kwamba kwa wakati huo wote walikuwa madarakani kama Rais na Waziri wa Nishati na Madini.

Hivi karibuni, wanasiasa wa kambi ya upinzani na zaidi Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa, waliibua kile kilichoitwa ‘orodha ya mafisadi’ ambayo pamoja na mapungufu yake, iliibua mjadala mkubwa katika siasa za Tanzania kiasi cha kuwachanganya viongozi na watendaji wa serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Tuhuma hizo, mbali ya kutaja majina ya baadhi ya watu, ziliibua hoja kadhaa ambazo baadhi zimejibiwa na baadhi hadi leo hazijatolewa maelezo, angalau ya kubabaisha. Baadhi ya mawaziri na watendaji walitishia kwenda mahakamani lakini hadi sasa hakuna taarifa rasmi za kufunguliwa kesi mahakamani.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi

Toa maoni yako