Askofu Mkuu hana ubavu wa kunitumbua – Askofu Mokiwa

Askofu Dk. Valentino Mokiwa akitoa mahubiri katika moja ya ibada alizowahi kuongoza.

ASKOFU wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk. Valentino Mokiwa, amesisitiza kwamba bado ndiye askofu wa dayosisi hiyo, kinyume cha uamuzi wa awali wa kumfukuza uliotangazwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana – Tanzania, Dk. Jacob Chimeledya.

Kwa mujibu wa Dk. Mokiwa, ataendelea kubaki katika wadhifa huo hadi pale mamlaka za juu zitakapoamua vinginevyo kwa kuzingatia taratibu za kanisa hilo, ingawa pia hakufafanua mamlaka za juu ni zipi zaidi ya askofu huyo mkuu. 

Askofu Mokiwa alitoa msimamo wake huo leo asubuhi (Januari 10, 2017), jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari. Katika mazungumzo yake na waandishi hao wa habari, Dk. Mokiwa alisema anatambua kuwapo kwa washauri wa Askofu Mkuu ambao ni wanasheria na wengine ni wasomi wa ngazi ya uprofesa lakini akasema kwa bahati mbaya wamekuwa wakimshauri vibaya askofu huyo mkuu wa kanisa hilo lililosambaa nchi mbalimbali duniani.

“Kwa hiyo Dayosisi ya Dar es Salaam haina mgogoro, mimi ndiye askofu, mgogoro uliopo ni wa kutengenezwa.  Mgogoro unatengenezwa ili pasitawalike na wakubwa waingie ili waweze kushika hatamu hapa,” alisema na kuongeza; “Andikeni, chunguzeni sawa sawa, kanisa si uwanja wa siasa, kanisa ni taasisi ya kiroho, ni taasisi ya Mungu kwa hiyo ninawasihi msipotoshe lakini wekeni ukweli kama ambavyo Mungu amewapeni nafasi ya ninyi kuwa wajulishaji wa mambo mema katika jamii.”

Alifafanua zaidi kwa kueleza; “Narudia kusema maandiko matakatifu yananukuu kitabu cha Malaki sura 2:7, kwa maana yapasa midomo ya Kuhani ihifadhi maarifa, tena yawapasa watu kuitafuta sheria kinywani mwake kwa kuwa yeye ni mjumbe wa Bwana wa Majeshi.”

Alisema watu wamehangaika lakini basi yanayotoka katika kinywa cha Kuhani lazima kuhifadhi maarifa kwa kuwa watu watakuja kuitafuta sheria kinywani mwake, kwa kuwa yeye ingawa anafanana na watu wengine ni binadamu kama wengine lakini yeye jina lake ni mjumbe wa Bwana wa Majeshi.

Katika kusisitiza, Askofu Mokiwa ambaye amekuwa miongoni mwa viongozi wa dini walioko mstari wa mbele kukosoa mambo mbalimbali ya kijamii, alisema; “Ninayasema nitakayosema kwa moyo mweupe kwa  sababu sikuzaliwa na adui, sikupanga kuishi na maadui, nataka mwisho wa safari yangu katika maisha haya nikumbukwe kwa heshima na si mtu aliyejitengenezea maadui lakini siwezi kuzuia maadui.”

Akieleza kilichotokea hivi karibuni, Dk Mokiwa alisema: “Nilipokea barua kutoka kwa Askofu Mkuu ikinitaka, nitumie neno ikinitaka, mimi ni Askofu Senior (mwandamizi), askofu senior aliyetumika kwa ngazi yangu huagizwi sana lakini unaombwa kiungwana.

“Lakini pale nilikuwa napewa ‘matching orders’ kwamba tayarisha mkutano saa nne kamili siku ya Jumamosi nataka kukutana na halmshauri yako ya kudumu ya dayosisi siku ya Jumatano. Kama nilivyosema kikatiba ndio chombo kati ya Sinodi na Sinodi. Nataka kuwapa mrejesho, na mimi nikatekeleza, maana imeandikwa ni vizuri kutii mamlaka, na hii ni mamlaka yangu na mimi nikaipa ushirikiano kwa namna hiyo”

Akaendelea kujieleza akisema: “Askofu Mkuu alikuja na kikao kile kilianza saa nne (asubuhi) juu ya alama, mimi nikiwa ndiye mwenyekiti wa kikao kile kwa sababu ndio askofu mwenye dhamana wa dayosisi hii, na ile ikiwa ndio halmashauri ya kudumu ya dayosisi hii, kiti kile kisingeweza kukaliwa na mtu mwingine isipokuwa mimi mwenyewe.

“Kilichotushangaza askofu wangu mkuu alikuja kwa namna, kwanza, ni mara ya kwanza kukutana na halmashauri ya dayosisi. Alitushangaza kuja na ujio mkubwa sana wa askari polisi waliokuwa wamevaa sare, walihesabiwa huko nje wasiopungua 12. Lakini kuna ambao hawakuvaa sare hatujui kwa kuwa wanavaa kama wengine.

“Kinachomleta Askofu Mkuu ni kitu alichokiita kuja kuleta mrejesho lakini akaishia kusoma barua ya kusema ameniondoa kwenye madaraka, huduma au kazi ya Askofu.”

Tamko la kumng’oa

Jana, Januari 09, 2017, Askofu Mkuu Dk. Jacob Chimeledya alitangaza kumstaafisha kwa lazima Askofu Valentino Mokiwa, kwa sababu mbalimbali, zikiwamo tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka sambamba na mali za kanisa.

Askofu Mkuu Chimeledya alitangaza kumstaafisha rasmi Askofu Mokiwa tangu Januari 7, 2017, akisema si askofu tena wa Kanisa la Anglikana.

Hata hivyo, ingawa Askofu Mokiwa alitangazwa kustaafishwa lakini naye alitangaza kugoma kutii agizo hilo na leo hii, Januari 10, 2017 ametangaza kuendelea na wadhifa wake mbele ya waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam.

Nini asili ya Kanisa Anglikana?

Anglikana ni kanisa ndani ya madhehebu ya Ukristo na asili yake ni nchini Uingereza. Msingi wa kuibuka kwake ni karne ya 16 ambapo mfalme Henry VIII wa Uingereza, alilitenga kanisa la nchi hiyo kutoka katika Kanisa Katoliki.

Kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia, baada ya mfarakano huo, yalifanyika mabadiliko mbalimbali upande wa imani, ibada na sheria kuelekea Uprotestanti. Hata hivyo mwelekeo wa kikatoliki uliendelea kuwepo, na bado unatajwa kuwa  nguvu, hasa katika baadhi ya dayosisi.

Katika karne zilizofuata, kutokana na uenezi wa himaya ya Uingereza duniani, Anglikana ilienea katika nchi mbalimbali  na leo ni kanisa lenye wafuasi wengi hasa Afrika katika nchi za Nigeria na Uganda, idadi ya waumini wa kanisa hilo ikitajwa kuzidi milioni 80.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *