Makala
Baada ya Dk. Ulimboka, vipi kuhusu Dk. Mkopi?
Godfrey Dilunga
Toleo la 250
18 Jul 2012

MSHAIRI wa kale, ambaye ni mzaliwa wa Roma, Italia na gwiji wa fasihi ya kilatini, Publius Ovidius Naso, maarufu kama Ovid, alipata kusema; “kwa ujumla, daktari bora zaidi kuliko wote (duniani) ni muda.

Publius aliyezaliwa Machi 20, mwaka 43 (kabla ya kristo) akikadiriwa kuishi kwa miaka kati ya 58 na 60, yuko sahihi hadi leo hii.

Ni kweli, licha ya mgomo wa baadhi ya madaktari wetu hapa nchini, Publius bado anaendelea kuwa sahihi. Dhana hii ya Publius inanisukuma kujadili kadhia ya madaktari nchini na hatua zilizochukuliwa na maofisa wa serikali.

Katika kadhia hii, ukiondoa mgomo wa baadhi ya madaktari na kupigwa kwa Dk. Steven Ulimboka (Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari), kuna suala la kufikishwa mahakamani kwa Dk. Namala Mkopi (Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari-MAT).

Kwanza nikiri suala la Dk. Mkopi linapaswa kujadiliwa bila kuingilia uhuru wa Mahakama, kwa sababu amekwishakufikishwa mahakamani.

Kwa maana hiyo, nitajadili hatua iliyochukuliwa na vyombo vya dola kabla ya kufikishwa kwa Dk. Mkopi mahakamani. Yaani nitajadili au kuhoji usahihi wa sababu zilizowashawishi maofisa wa serikali kupanga kumkamata ili kumfikisha kortini Dk. Mkopi.

Kimsingi, katika hatua hiyo ya kumkamata Dk. Mkopi kuna maswali mengi ya kujiuliza kwa kuhusisha maofisa wa serikali kwa upande mmoja, lakini pia kwa kuwatazama madaktari wenzake kwa upande mwingine.

Tujiulize maswali haya tukikumbuka ujumbe wa mshairi, Publius kwamba; daktari bora zaidi duniani ni muda.

Kuhusu swali namba moja

Swali hili la kwanza ni kuhusu uamuzi wa vyombo vya dola kumkamata na kumshitaki Dk. Namala Mkopi. Katika swali hili la kwanza hoja mbalimbali zinajitokeza.

Kwa mfano, muundo wa Chama cha Madaktari (MAT) ukoje? Ukijiuliza swali hilo utabaini muundo unamtaja mwenyekiti, katibu na kamati ya utendaji.

Maana yake, chochote kinachohusu MAT hakiwezi kuwa uamuzi wa mwenyekiti na katika mazingira maalumu inaingia akilini zaidi kumhusisha katibu kuliko mwenyekiti, kwa sababu katibu ndiye mtendaji mkuu.

Hivyo basi, kwa kuzingatia muundo huo ni kwa nini amekamatwa mwenyekiti badala ya katibu? Tangu mwanzo, kwa kuzingatia ripoti za vyombo vya habari, matamko kuhusu madaktari na mgomo hayakutolewa na mwenyekiti pekee, bali yalimhusu katibu na kamati tendaji ya MAT kwa ujumla. Tafakari je, ni kwa nini akamatwe mwenyekiti?

Bila shaka, uamuzi sahihi kwa kuzingatia mtazamo wa serikali ulipaswa kuwa ni ama kuishitaki kamati tendaji yote ya MAT au katibu wa MAT pekee au wote kwa ujumla. Kumshitaki Dk. Mkopi pekee ni kumuonea.

Kumkamata Dk. Mkopi ni kosa kwa maofisa wa serikali. Ni uthibitisho wa kile kinachoitwa “uchovu” wa kuchambua mambo katika usahihi. Uchovu unaowakabili maofisa wengi serikalini hivi sasa. Uchovu wa namna hii, Rais (mstaafu) Benjamin Mkapa aliwahi kusema ni uvivu wa kufikiri.

Agizo lolote kuhusu taasisi yoyote (tena agizo la maandishi), likiwamo lile la kutangaza kusitisha mgomo linapaswa kuandikwa kwenda kwa katibu wa taasisi husika na sababu ipo wazi kwamba, katibu ndiye mtendaji na si mwenyekiti.

Kama taasisi inatuhumiwa, maana yake ‘fikra’ zinazounda tuhuma hizo zinaamini katika utendaji “usiofaa” wa taasisi husika.

Kama ni hivyo, ni dhahiri aliyepaswa kufikishwa mahakamani si Mwenyekiti Dk. Mkopi, bali ni ama katibu pekee au mwenyekiti na katibu kwa pamoja au kamati yote ya utendaji ya MAT. Swali hili la kwanza linatuonyesha ombwe la fikra miongoni mwa maofisa wa serikali.

Kuhusu swali namba mbili

Swali la pili ni je, vyombo vya dola vimetafiti nini kuhusu Dk. Mkopi? Wanadai alishiriki, kupitia MAT, kuhamasisha mgomo na hata kushindwa kuuzuia. Je, ni mazingira gani yanawashawishi (dola) kuamini hivyo?

Zipo taarifa za kina miongoni mwa madaktari kwamba Dk. Mkopi hakuwa akishiriki mgomo wa madaktari licha ya wenzake kushiriki mgomo huo.

Nimezungumza na walio karibu na Dk. Mkopi, ambao wamekuwa wakifuatilia kwa karibu suala hili la mgomo wa madaktari. Wanathibitisha Dk. Mkopi hakushiriki mgomo kwa kugoma, bali alishiriki kusaidia kufuta mgomo.

Unaweza kujiuliza, ni kwa nini hakushiriki mgomo? Sababu zipo, na kati ya sababu hizo pengine ni aina ya wagonjwa aliokuwa akiwatibu na ambao bado anawatibu. Lakini pia sababu nyingine pengine ni utashi wa moyo wake.

Dk. Mkopi amekuwa akitibu watoto wadogo wenye magonjwa ya kansa. Madaktari wenzake wanasema moyo wake ulikuwa “mzito” kuwagomea watoto wale wenye kansa pale Hospitali ta Taifa Muhimbili.

Katika hili, baadhi ya madaktari wenzake walianza kumwandama kwamba akiwa kama mwenyekiti wa MAT anawasaliti, lakini yeye hakujali hilo. Kwake, kipaumbele kilikuwa kutibu watoto wenye magonjwa ya kansa.

Dk. Mkopi, aliyepata kuwa mwanafunzi Shule ya Msingi Mapambano, Sinza jijini Dar es Salaam na shule za sekondari Tambaza na Azania (Dar es Salaam) kwa ajili ya kidato cha kwanza hadi nne, na cha tano hadi sita, wito wa kidaktari haukumshawishi kuwakimbia watoto waliokuwa wanaugua kansa.

Aliwatibu watoto ambao alikuwa akijua ni taifa la kesho na kama angewakimbia basi angekuwa na “cha kujibu” mbele ya Mwenyezi Mungu.

Katika mazingira haya tujiulize; je, huyu anaweza kushawishi mgomo kiasi cha kumshitaki yeye binafsi badala ya taasisi (MAT)? Kama alivyoeleza Mshairi, Publius muda utatoa majibu.

Bado ni dhahiri, dola imeshindwa kutafiti suala hili. Bila shaka ni uthibitisho wa uvivu wa kufikiri na kupambanua mambo ndani ya mfumo wa kiutendai serikalini.

Kama kungekuwa na fikra zilizojitosheleza na kwa kuzingatia nafasi ya Dk. Mkopi wakati wote wa mgomo, huyu angepaswa kushitakiwa pamoja na katibu wake, au kamati yote ya utendaji ya MAT.

Kuhusu swali la namba tatu

Tuliona umati wa madaktari waliofurika mara baada ya Dk. Steven Ulimboka kufikishwa Muhimbili kwa ajili ya matibabu baada ya kutekwa na kuteswa.

Siungi mkono Dk. Ulimboka kupigwa na kuteswa kama ambavyo siungi mkono kwa yeyote kufanyiwa vitendo hivyo, ndani ya nchi inayodaiwa kuwa ya amani na utulivu.

Lakini nilifurahishwa na mshikamano na umoja miongoni mwa madaktari. Kwa uzito ule ule, nilitarajia madaktari watajitokeza pale Dk. Mkopi alipofikishwa kortini.

Ni kweli madaktari walijitokeza pale Mahakama ya Kisutu, lakini si kwa uzito ule wa Dk. Ulimboka. Je, hii inatoa tafsiri gani?

Tafsiri zinaweza kuwa nyingi. Kwa mfano, inawezekana tangu awali madaktari hawakuwa na imani na Dk. Mkopi, pengine kwa kuwa alikuwa akitibu watoto wenye kansa muda wote wa mgomo (hakugoma).

Lakini pia inawezekana baadhi ya madaktari hawakufika pale (Mahakama ya Kisutu) kwa sababu ya majukumu mengine au dharura binafsi. Lakini pia inawezekana wengine waliona ni bora amekamatwa licha ya ‘wema’ wake wa kutogoma. Serikali ilipaswa kutafiti mazingira haya.

Kuhusu swali namba nne

Swali namba nne linahusu nafasi ya Dk. Mkopi baada ya kurejea kutoka Ikulu kulikofanyika mazungumzo kati ya MAT na Jumuiya ya Madaktari kwa upande mmoja na Rais Jakaya Kikwete, kwa upande mwingine.

Baada ya kurejea kutoka Ikulu, Dk. Mkopi alikutana na madaktari. Kwa namna ya kipekee, licha ya kuwapo hisia kwamba jopo madaktari lililotoka Ikulu limetumwa kuzima mgomo, ni Dk. Mkopi kwa sehemu kubwa ndiye aliyewashawishi wenzake kurejea kazini (angalau kwa wiki kadhaa).

Kwa maana nyingine, ni Dk. Mkopi aliyewashawishi baadhi ya madaktari kurejesha imani yao kwa matumaini kuwa madai yao yatafanyiwa kazi baada ya wenzao kukutana na Rais.

Mtu wa namna hii aliyerejesha matumaini kwa kiwango hicho tena katika mazingira magumu ya kutiliwa shaka na wenzake, hawezi kuhamasisha mgomo. Badala yake, mtu wa namna hii ataendelea kutafuta suluhu.

Inawezekana hata ndani ya taasisi (MAT) Dk. Mkopi alikuwa akiwashawishi wenzake watafute suluhu. Vyombo vya dola vilipaswa kutafiti nafasi ya Dk. Mkopi ndani ya MAT kabla ya kumchukulia hatua yeye binafsi. Bila shaka, muda utatueleza kama alivyosema Mshairi Publius.

Kuhusu swali namna tano

Swali namba tano linahusu kitendo cha jumla cha kumshitaki Dk. Mkopi, kwa nafasi yake kama mwenyekiti.

Kwa sababu kushitakiwa kwake kumehusishwa na nafasi yake MAT. Bila shaka, wahusika wengine kama nilivyoeleza awali walipaswa kuwa ama ni yeye (Dk. Mkopi) na katibu wake au wote wawili pamoja na kamati tendaji ya MAT.

Kwa bahati mbaya aliyeshitakiwa ni Dk. Mkopi ambaye kama wale watoto wadogo wenye kuugua kansa wataitwa kuhojiwa au wazazi wao, bila shaka watakumbuka Dk. Mkopi aliwahi kuwatibu wakati wa mgomo na kwa hiyo, Dk. Mkopi hakugoma.

Watoto hao au wazazi wao watakuwa wanasikitika kila wanaposikia daktari aliyepata kuwatibu ndiye ameshitakiwa kuchochea mgomo. Mazingira haya yalipaswa kufanyiwa utafiti na vyombo vya dola.

Kwa hali ilivyo, maudhui ya swali hili la tano katika makala hii linatuletea ujumbe kwamba; Dk. Mkopi kwa sasa anateswa kisaikolijia.

Kwa bahati mbaya, wengi tunaumizwa na mateso aliyopata Dk. Ulimboka lakini hatujali maumivu ya kisaikolojia anayokumbana nayo Dk. Mkopi. Maumivu ambayo, pengine wengine wanaoyatambua ni wale watoto aliokuwa akiwatibu kansa pale Muhimbili. Wito wangu ni kwamba, maofisa wa serikali watatafiti suala hili kwa umakini.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Godfrey Dilunga
gdilunga@raiamwema.co.tz
+255-787643151

Toa maoni yako