Michezo
Baada ya usingizi wa miaka 76, vijana kuiamsha Yanga?
Mwandishi Wetu
Toleo la 218
21 Dec 2011
  • Ndoto za saccos, benki, harambee zaibuliwa Jangwani

KLABU ya Yanga, Desemba 18, mwaka huu, ilifanya kongamano  la vijana wa klabu hiyo, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa kuadhimisha miaka 50 ya iliyokuwa Tanganyika.

Swali kubwa na muhimu, kwa nini Yanga na hasa kupitia kwa vijana wake ijielekeze moja kwa moja katika maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika?

Hili ni swali muhimu linalohitaji majibu kwa Watanzania wote, hasa vijana ambao historia ya harakati za kudai huru hawaifahamu vema.

Lakini kabla ya majibu, ni vema tukaelewana kuhusu mchakato wa harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika. Harakati hizo zilihusisha juhudi, mbinu na ubunifu wa hali ya juu, tena katika uratibu wa siri.

Yanga, kwa kiasi kikubwa ni sehemu ya harakati hizo na kimsingi, baadhi ya vikao vya siri wakati wote wa harakati za kutafuta Uhuru wa Tanganyika, vilikuwa vikifanyika katika baadhi ya majengo ya Klabu ya Yanga.

Kutokana na kumbukumbu hiyo muhimu kihistoria, Yanga ilikuwa na kila sababu ya kuendeleza maadhimisho ya miaka 50 ya iliyokuwa Tanganyika kwa njia ya kipekee. Njia hiyo ni kuwakutanisha vijana wa klabu hiyo kongwe, yenye umri wa miaka 76 sasa, ikiwa imezaliwa Februari 12, mwaka 1935.

Malengo ya kongamano

Kwanza, miongoni mwa malengo ya kongamano hilo la Desemba 18, ni  kumshukuru Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, kwa niaba ya Watanzania wote, kwa kuenzi juhudi zilizoihusisha Yanga na wanaharakati wengine kudai Uhuru, hadi leo hii kufikia kumbukumbu ya miaka 50 nchi ikiwa na amani.

Lakini kubwa zaidi, kongamano hilo limelenga kuhakikisha vijana wa Yanga, ambao ni sehemu ya kundi kubwa la vijana wa Tanzania, kutambua na kuheshimu mchango wa klabu hiyo katika harakati za kutafuta Uhuru wa Tanganyika.

Harakati zilizoongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Mazao ya harakati hizo ni pamoja na Tanganyika kuwa huru na baadaye kuungana na Zanzibar, kuunda Jamhuri ya Muungano, kwa kuwahusisha raia wa Zanzibar chini ya Abeid Amani Karume.

Mbali na hayo, kongamano pia lililenga kuwezesha  kujitathimini na kuangalia mchango wa vijana kwa klabu ya Yanga na taifa kwa ujumla, miaka 50 ya Uhuru.

Vijana wa Yanga kwa pamoja wanasema moja ya changamoto zinazowabili ni kubuni namna bora ya kutumikia klabu yao na nchi kwa ujumla.

Wanaamini, kupitia risala yao iliyosomwa kwenye kongamano hilo na Cyprian Musiba kwamba, nguvu ya maendeleo, amani, umoja na mshikamano klabu ya Yanga iko mikononi mwa vijana, lakini pia nguvu ya vurugu katika klabu hiyo nayo iko mikononi mwa vijana.

Katika kutambua umuhimu huo, vijana wa Yanga kupitia kongamano lao wamejadiliana na hatimaye kupanga mikakati kuhakikisha Yanga inabaki salama lakini ikiwa na rekodi bora ya soka na kiuchumi, Afrika na dunia kwa ujumla.

Vijana walikumbushana kuelekeza zaidi nguvu zao katika kuiinua klabu hiyo na si kushiriki kuchochea na kufanikisha vurugu ambazo kimsingi, zinaandaliwa na watu wenye malengo binafsi, ikiwa ni pamoja na uroho wa madaraka.

Kupitia kongamano hilo vijana wa Yanga walifiakiana na uongozi wa klabu yao kupitia kwa Mwenyekiti wake, Lloyd Nchunga, kwamba klabu yao iwe na malengo ya kujiendesha kwa kujitegemea.

Kuanzishwa SACCOS Yanga

Ili kuweza kujitegemea, vijana walishauri uongozi wa Yanga kupitia kwa Nchunga, kuanzisha Saccos ya Yanga ili baadaye, mafanikio yake yaweza kutumika kama chachu ya kuanzisha Benki ya Yanga, itakayotoa huduma kama benki nyingine.

Hiyo ni hatua kubwa katika kubuni namna klabu hiyo kongwe inavyoweza kujitegemea, jambo ambalo halikuwahi kufanyika kwa miaka 76 sasa.

Maana ya Saccos hiyo ni kwamba iwapo itafanikiwa, vijana wa Yanga watafaidika kwa njia nyingi, ikiwamo kupata ajira klabuni, kuweza kukopeshwa kwa kadiri ya masharti nafuu yatakayowekwa.

Faida nyingine ni kufanikisha kwa ufanisi zaidi michakato wa kusajili wachezaji na hata makocha wenye viwango vya juu zaidi duniani, ikiwa ni pamoja na kumpata kocha mwenye daraja A, anayetambuliwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Mkakati wa kumiliki kiwanja bora

Pia kupitia kongamano hilo, vijana wa Yanga walishauri viongozi wa klabu kuwa na mikakati ya kuwa na uwanja wake wenye ubora wa kimataifa ambao utakuwa unatumika katika mechi zake za ligi na klabu kujipatia mapato kirahisi kuliko ilivyo sasa.

Kwa sasa Yanga ina uwanja usio wa kiwango bora na matokeo yake, wachezaji  wamekuwa wakiumia kutokana na nyasi kuwa za kiwango duni. Yanga pia imekuwa ikipata hasara kwa kulazimika kutumia fedha nyingi kukodi uwanja wa mazoezi, jambo linalotajwa kuwa ni aibu.

Pia imependekezwa na vijana hao kuwa uongozi utafute utaratibu wa kukodisha sehemu ya chini ya jengo lake la makao makuu kuwe na mashine za kutolea fedha, maarufu kama ATM za benki mbalimbali ili klabu hiyo inufaike zaidi na jengo lake.

Vijana hao pia wameshauri Yanga itumie vizuri idadi kubwa ya wanachama na wapenzi wake, ikiwa ni pamoja na kuendesha harambee kwa ajili ya kufanikisha mipango ya maendeleo ya klabu.

Viongozi wa Yanga kupitia mabalozi wa Tanzania walioko nje ya nchi ambao ni wanachama na mashabiki wa klabu, wameshauriwa kufanya mawasiliano na mabalozi  hao ili kutafuta wafadhili ijengwe shule ya michezo kuanzia chekechea hadi chuo kikuu.

Lakini pia Yanga iendeleze utaratibu wa zamani wa kuwa na klabu rafiki kama zile za Zanzibar, Ivory Coast na Afrika Kusini na hata nje ya nchi ili iwe rahisi kupeleka wachezaji wao kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na kujenga uhusiano mzuri na klabu hizo rafiki.

Yanga na wanachama wapya

Uongozi wa klabu hiyo umeshauriwa na vijana hao kuongeza wanachama mikoani na hata nje ya Tanzania. kupitia kongamano hilo la vijana, imeshauriwa klabu iwe na vyombo vyake vya habari kama televisheni, radio na magazeti, kama moja ya ufumbuzi wa tatizo la ajira lakini pia kufikisha taarifa za Yanga kwa uhakika zaidi mbele ya umma.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Toa maoni yako

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.