Bajeti kuongeza uzalishaji mazao

HATUA ya serikali kupunguza ushuru wa mazao kutoka asilimia tano ya thamani ya mauzo hadi asilimia tatu kwa mazao ya biashara na asilimia mbili kwa mazao ya chakula huenda ikaongeza uzalishaji wa mazao hayo.

Matumaini hayo yameelezwa na wadau mbalimbali wa kilimo kanda ya Ziwa katika mahojiano maalum na Raia Mwema, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza – NCU (1984) Ltd, Enock Masele, ni miongoni mwa wadau wa kilimo wanaoamini uzalishaji wa mazao utaongezeka na kukuza uchumi wa wakulima.

“Hapa sasa kikubwa tunachoomba ni mvua za kutosha maana ninaamini hatua hiyo ya serikali itahamasisha wananchi wengi kukazania kilimo cha mazao ya biashara na chakula kama pamba, kahawa, mahindi na mpunga,” amesema Masele.

Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, James Bwire, amesema hatua hiyo ya serikali inalenga kuinua uchumi wa wakulina na kuongeza ajira katika sekta ya kilimo nchini.

“Ninatoa wito kwa wananchi kuongeza bidii katika shughuli za kilimo na kuiunga mkono serikali katika juhudi za kuleta maendeleo ya taifa letu,” amesema Bwire.

Nao Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rorya, Samwel Kiboye maarufu kwa jina la Namba Tatu na mkazi wa wilaya ya Tarime mkoani Mara, Peter Wangwe maarufu kwa jina la Keba, wamepongeza hatua hiyo ya serikali.

“Ninaipongeza serikali kwani uamuzi wa kushusha ushuru wa mazao utawapatia wakulima nafuu ya uzalishaji na kuinua kipato chao,” amesema Kiboye.

“Serikali ikitekeleza hatua hiyo itakuwa imefungua mlango wa kuwainua wakulima kiuchumi, lakini pia kuongeza uzalishaji wa mazao ambao pia utakidhi mahitaji ya viwanda nchini,” amesema Wangwe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *