Balozi wa China awatangulia wabunge kuhusu bajeti

BALOZI wa China nchini Tanzania, Dk. Lu Youqing, amewatangulia wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hususan wanaotarajiwa kukosoa bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018, akisema ni bajeti nzuri.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais – Ikulu jijini Dar es Salaam leo, Juni 9, 2017, Balozi Youqing ameahidi kusaidiana na Serikali ya Tanzania katika masuala ya maendeleo, hususan uwekezaji sambamba na ujenzi wa miundombinu.

Taarifa ya Ikulu inaeleza kwamba balozi huyo ameielezea bajeti hiyo iliyowasilishwa bungeni mjini Dodoma Juni 8, mwaka huu, kuwa “imeakisi dhamira ya kuongoza kasi ya maendeleo katika sekta mbalimbali.

Katika mazungumzo yake na Rais Dk. John Magufuli yaliyofanyika leo, Ikulu, balozi huyo ameeleza kwamba bajeti hiyo inasukuma kasi zaidi katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali sambamba na ujenzi wa viwanda.

Ameeleza kwamba Tanzaniai itaendelea kuwa kipaumbele cha nchi ya China katika uwekezaji na zaidi ya hapo, ataendelea kushawishi raia wa China kuwekeza nchini.

Balozi huyo anakuwa wa kwanza miongoni mwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini kujitokeza wazi wazi kusifu bajeti ya serikali katika bajeti hii ya pili ya serikali ya awamu ya tano.

Amewatangulia wabunge ambao wataanza rasmi kuwasilisha maoni yao kwa njia ya mjadala kuanzia Jumatatu, Juni 12, mwaka huu.

Kwa kuzingatia taratibu za uwasilishaji bajeti bungeni, inatarajiwa kwamba siku ya Jumatatu, Kamati ya Bajeti ya Bunge itawasilisha maoni yake ikifuatiwa na Maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni chini ya Waziri Kivuli wa Wizara ya Fedha na Mipango, kisha wabunge watapata nafasi ya kuendeleza mjadala huo ambao kwa sehemu kubwa unaweza ukawa na mwelekeo wa kuunga mkono bajeti hiyo.

Uwezekano huo wa kuunga mkono bajeti hiyo unatokana na ukweli kwamba wabunge wengi hasa wa chama tawala – Chama cha Mapinduzi – CCM kumshangilia mara kwa mara Waziri wa Fedha Dk. Philip Mpango alipowasilisha bajeti hiyo bungeni, shangwe zinazotajwa kuashiria kuunga mkono bajeti hiyo.

One thought on “Balozi wa China awatangulia wabunge kuhusu bajeti”

  1. body says:

    China ijitoe kwenye mambo ya ndani ya nchi. Ipo hapa kutetea maslahi yake. Toka lini nchi za nje zinaingilia mambo ya ndani ya nchi.

    Comflict of Interest. Amekujaje hata kusikilizwa. Hatuna Wasomi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *