Bombardier iliyonaswa Canada yawagonganisha Lissu, Dk. Slaa

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema Dkt Wilbroad Slaa

ALIYEKUWA Mbunge wa Karatu na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, ameibuka na kudai kwamba kampuni ya ujenzi inayotajwa kuishikilia ndege ya Tanzania aina ya Bombardier Q400-Dash 8, ilikwishatuhumiwa kwa uzembe bungeni.

Kampuni ya Stirling Civil Engineering Ltd, ndiyo, kwa mujibu wa maelezo ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, imeishikilia ndege hiyo iliyonunuliwa na Tanzania nchini Canada. Uamuzi huo wa kuishikilia unatajwa kuwa ni utekelezaji wa matakwa ya Mahakam a ya Kimataifa ya Usuluhishi, kuiwezesha  kampuni hiyo kulipwa deni lake la dhidi ya serikali ya Tanzania la dola za Marekani milioni 38.7 ambazo ni takriban shilingi bilioni 87.

Msingi wa deni hilo ni kuvunjwa kwa mkataba wa kati ya serikali na kampuni hiyo wa ujenzi wa barabara kutoka eneo la Wazo Hill jijini Dar es Salaam hadi Bagamoyo, mkoani Pwani.

Akizungumzia kadhia hiyo Dk. Slaa alisema pamoja na hali hiyo, kampuni  ya ujenzi ya Stirling si “nadhifu” katika kazi zake na hata wabunge walikwishailalamikia bungeni mwaka 2005, akisisitiza kuwa, yeye ni kati ya wabunge waliopata kuilalamikia kampuni hiyo.

Katika mawasiliano yake na gazeti hili, Dk. Slaa aliyepata kuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema kwenye uchaguzi mkuu wa 2010 alisema; “Siamini kama serikali huwa inavunja mikataba ovyo. Kauli hiyo ni vema ikathibitishwa kwa ushahidi na hasa kuonyesha ni vipengele vipi vya mkataba vimevunjwa au sheria ipi imekiukwa. Si vema kutoa kauli za jumla jumla bila uthibitisho.

Kauli hiyo ya Slaa inapingana na madai ya Lissu ya hivi karibuni kwamba mkataba kati ya serikali na kampuni hiyo ulivunjwa ovyo, kinyume cha utaratibu na ndio maana, kampuni hiyo imekwenda kushitaki katika Mahakama ya Kimataifa na kushinda kesi.

Slaa anaeleza zaidi; “Kama ni suala la kushikiliwa Bombardier ninachokumbuka ni kuwa kampuni husika ilishindwa kumaliza ujenzi wa barabara hiyo (Wazo Hill hadi Bagamoyo) katika muda uliotajwa  ndani ya mkataba.”

Alieleza kwamba hata sehemu ambayo kampuni hiyo ilikamilisha kipande cha ujenzi wa barabara, basi, ujenzi huo ulikuwa chini ya kiwango na pale kampuni hiyo ilipopewa muda kurekebisha udhaifu huo ilishindwa kufanya hivyo.

“Bungeni tulipiga sana kelele kuhusu ucheleweshaji huo na kazi isiyoridhisha. Nilikuwa Mbunge wa Karatu wakati huo na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na kumbukumbu ziko kwenye hansard, tatizo watu hawapendi kufanya utafiti,” alisema Slaa.

Akizungumzia suala la Tanzania kushindwa kesi kwenye Mahakama ya Kimataifa, Dk. Slaa alisema; “..hiyo haina maana ya kuwa kampuni hiyo ilikuwa “absolutely” na haki. Mahakama zinategemea zimeelekea wapi hasa hizi za biashara ya kimataifa ambazo kimsingi zinalinda maslahi ya nchi zao. Hili nililizungumzia sana bungeni hasa kutokana na uzoefu wangu katika Bunge la ACP/EU – Joint Assembly ambalo nilikuwa nikiwalisha Bunge la Tanzania mwaka 1996 hadi 2000 .Tuliitaka serikali yetu ichukue hatua bahati mbaya haikuchukua hatua.”

Madai ya Lissu

Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chadema Tundu Lissu

Agosti 18, mwaka huu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema Tundu Lissu katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alifichua suala hilo la ndege ya Tanzania kuzuiwa na kampuni hiyo ya ujenzi ya Stirling.

Katika mkutano wake huo Lissu alisema ndege hiyo imeshindwa kuletwa nchini Julai mwaka huu kama ilivyopangwa kutokana na kuzuiwa nchini Canada kwa kuwa serikali inadaiwa fidia na kampuni hiyo.

Akifafanua alisema kutowasili kwa ndege hiyo kama ilivyopangwa licha ya kukamilika kutengenezwa nchini Canada kunatokana na uamuzi wa aliyekuwa waziri wa ujenzi, kwa wakati huo, kuvunja mkataba kati ya serikali na kampuni hiyo bila kufuata utaratibu na kisha kampuni hiyo kufungua kesi Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi.

Kampuni hiyo ilifungua kesi hiyo mwaka 2009 ikidai kukiukwa kwa mkataba na ilipofika Juni 2010 mahakama hiyo ya kimataifa ilitoa tuzo ya ushindi kwa kampouni hiyo ikiitaka serikali ya Tanzania ilipe fidia ya dola za Marekani milioni 25, na deni hilo likiwekewa riba ya asilimia nane.

Lissu aliwaambia waandishi wa habari aliokuatana nao kwamba serikali ilikataa kulipa fidia hiyo hadi Juni 30 mwaka huu wakati mahakama ya kimataifa ilipotoa kibali kwa kampuni hiyo kukamata mali zote za Tanzania zitakazokuwa katika nchi za Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ubelgiji, Uganda na Canada.

Athari kwa uchumi

Kama uamuzi huo utatekelezwa kwa kulipa fedha hizo kwa mdai huyo, ni dhahiri kwamba bajeti iliyoipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaathirika, kwa kuwa fedha hizo hazikuwa zimetengwa kwa ajili ya malipo hayo bali shughuli nyingine za kijamii na hata ulipaji madeni mengine, yakiwamo ya ndani.

Baadhi ya watumishi waandamizi serikalini waliozungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yao gazetini wamedai kuwa shughuli za baadhi ya wizara au idara za serikali zitaathirika moja kwa moja wakihofia hata baadhi ya miradi ya maendeleo kuweza kuathirika pia.

“Ndege ya Bombadier ni sehemu ya alama za Rais Magufuli tangu aingie madarakani, yeye ndiye amenunua ndege hizo na hii kampuni ‘imemshika pabaya’. Kwa vyovyote vile ni lazima fedha hizo zitalipwa iwe kwa awamu ama vyovyote kama uamuzi wa mahakama hautatenguliwa. Magufuli hawezi kukubali kuona alama ya uongozi wake (ununuzi wa bombardier) inavurugwa,” alisema mmoja wa viongozi waandamizi serikalini.

Mmoja wa wakurugenzi wa halmashauri nchini katika mazungumzo yake na gazeti hili alieleza kwamba kati ya mafungu ya kibajeti yanayoweza kuathiriwa na deni hilo kama litapaswa kulipwa ni pamoja na mafungu ya “matumizi mengine” maarufu kama OC na hata baadhi ya miradi isiyotoa matokeo ya haraka “kisiasa”.

Msimamo wa serikali

Tayari serikali kupitia kwa naibu msemaji wake mkuu, Zamaradi Kawawa, imekwishazungumzia suala hili na licha ya kukiri kuzuiwa kwa ndege hiyo, ilisisitiza kwamba ufumbuzi wa kadhia hiyo unasakwa.

Akizungumza na waandishi wa habari siku moja mara baada ya Lissu kuzungumzia suala hilo katika mkutano wake na waandishi wa habari, Zamaradi alisema serikali inatafuta suluhu ya suala hilo lakini kwa upande mwingine, aliwalaumu baadhi ya wanasiasa kwa kushirikiana na kampuni ya Stirling ili kampuni hiyo ifanikiwe kukamata mali za Tanzania.

Hata hivyo, licha ya kuwalaumu wanasiasa, Zamaradi hakutaja majina ya wanasiasa hao.

Tayari Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ambaye ndiye aliyekuwa mwanasiasa wa kwanza kumuuliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kuhusu ahadi ya serikali ya kuileta ndege ya bombardier mwezi uliopita kushindwa kutekelezeka, amezungumzia hali hiyo ya serikali kutuhumu wanasiasa wa upinzani kuhujumu taifa, akisema kazi ya wanasiasa hao wa upinzani ni “kuinyoosha” serikali pale inapokosea kiasi cha kuhatarisha masilahi ya umma.

12 thoughts on “Bombardier iliyonaswa Canada yawagonganisha Lissu, Dk. Slaa”

 1. Anonymous says:

  Ni dhahili kuwa Dr. Slaa amefilisika kifikita na sasa hana tofauti kabisa na wasomi wengine ambao wameamua kuipaka mafuta serikali kwa mgongo wa chupa pasina kujua kuwa ukweli daima ujitenga na uongo! Bila shaka mikataba yenye afya kwa taifa inakipengere na taratibu za kuvunja au kuisitisha ikiwa upande fulani haulidhishwi na utekelezaji wa mkataba husika!! Si dhani kama taratibu zikifuatwa kwa usahihi bila hisia binafsi taifa lingeingia hasara ktk uvunjaji wa mikataba husika!! Ni wazi kuwa taratibu na sheria hazikufuatwa na maana tumepigwa faini!

 2. majid says:

  Ni dhahili kuwa Dr. Slaa amefilisika kifikita na sasa hana tofauti kabisa na wasomi wengine ambao wameamua kuipaka mafuta serikali kwa mgongo wa chupa pasina kujua kuwa ukweli daima ujitenga na uongo! Bila shaka mikataba yenye afya kwa taifa inakipengere na taratibu za kuvunja au kuisitisha ikiwa upande fulani haulidhishwi na utekelezaji wa mkataba husika!! Si dhani kama taratibu zikifuatwa kwa usahihi bila hisia binafsi taifa lingeingia hasara ktk uvunjaji wa mikataba husika!! Ni wazi kuwa taratibu na sheria hazikufuatwa na maana tumepigwa faini!

 3. Anonymous says:

  Kazi bado zito hataserikari ina makosa kutotoa tarifa mapenkkku

 4. Emmanuel marato says:

  Bado kazi zito

 5. Massanda O'Mtima Massanda says:

  “Mdharau mwiba guu huota tende”! Labda tujiulize, kama serikali haikuridhishwa na utendaji wa mkandarasi huyu, je, ilifuata taratibu za kusitisha mkataba wake? Na kama ilifuata taratibu stahiki, kwa nini haikutetea uamuzi wake mahakamani? Na kama ilijitetea, je, kwa nini haikuchukua hatua zaidi baada ya hukumu hiyo ya ama kukata rufaa au kulipa faini hiyo kwa wakati?

 6. Anonymous says:

  Huyu bwana Slaa msimshangae ameacha upadiri kwa hiyo washamjua udhaifu wake ndio maana wanamtumia na Slaa kwa wairaq alizaliwa polini mama wake akiwa anatafuta kuni.Haaaaaaaaaaaaaaaa.

  1. Mwakatuma says:

   Acha ujinga wewe, sasa kuzaliwa porini mama akiwa anaokota kuni kuna mahusiano gani na hiyo maada?. Tatizo uelewa wako ni mdogo kwani DR. Slaa kaisaidia nn serkali hapo? Mbona kaeleza kuwa kuna wakati walishauri serkali juu ya hiyo mikataba lakini haikutekeleza. Tatizo lenu mnataka kila anayeshauri serkali atumie lugha za mapovu kama huyo Lissu.

 7. Ben Barka says:

  Kwanini Tundu asioneshe nyaraka (documentary evidences) ili kuthibitisha anachodai? Kama hawezi basi angalao atuambie alipata wapi habari hizo? SOURCE

  1. Anonymous says:

   WE UMEONA SERIKALI YAKO IMEGOMA ? kawaambia wagome awape document ila wamekiri sasa hunazihitaji au unataka karatasi cha kuchambia huna maji chooni kwenu

 8. benzene says:

  Hahaaaa watanzania bwana….mnapenda klaumu kila kitu hata kama hamna mnachojua…..kama bunge liliidhinisha kuwa mkndarasi kashi dwa, serikali inatakiwa kufanyaje? Dr Slaa yuko smart siku zote.

 9. ako says:

  Ben unahitaji ushahidi gani kutoka kwa Lisu. Waziri amakwishakiri kukamatwa kwa ndege hiyo. Kama Zito au Lisu wasingelisema hilo basi watanzania wasingelijua linaloendelea. Katika Maslahi ya nchi tusitetee viongozi wasiotimiza wajibu wao. Yanayotokea katika swala la ndege hii ni muendelezo wa matatizo mengi yanayohusu mikata yetu na makampuni ya kimataifa. Tusiwalaumeu wanaofichua uchafu. Ili rais asikwazwe na matatizo ya aina hii ni vizuri serikali yake ipitie mikataba yote ambayo serikali iliingia na wawekezaji wanje ili kabla utawala wake vinginevyo atakuwa anatatua matatizo ya viongozi waliopita. kuwalaumu viongozi wa upinzani ni kujaribu kufich udhaifu wa baadhi ya viongozi serikalini. Zito na Lisu wameliweka swala hili wazi kwa watanzania. Lakini tujue kuwa swala hili limeshaandikwa kwenye baadhi ya magazeti ya nje. Au wanalaumiwa kwa kuwa ilitakiwa kuwa siri? watanzania tusijue udhaifu na uzembe wa viongozi wetu? Badala ya kutatua tatizo,tunawashambulia na kuwatishia watoa siri. ama kweli hutujifunzi.

 10. migoely ndaro says:

  Comment:iyo ndege tafadhali na omba mh raisi magufuli ije hizo ni kodi zetu,uzembe wa uyo waziri alie katisha mikataba kizembe na wananchi tunaendelea kuumia kweli sitoitena kura yangu kwa serkali hii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *