Bravo Malinzi, tuchongee mzinga tuline asali

PAUL Makonda, Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam ndiyo habari ya mjini wakati huu ambao Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ ametoa wimbo mpya.

Si kawaida Diamond Platnumz kutoa wimbo ikamezwa na kitu kingine. Mara zote alizotoa nyimbo zilibamba kuanzia vituo vya habari, mitandao ya kijamii hadi mitaani. Nyimbo zake hubamba kila kona.

Nani anayejua kama Diamond Platnumz katoa wimbo mpya wiki iliyopita? Ni watu wachache sana wanaojua.

Kama taarifa za Makonda 'zilivyomeza' kusikika, nyimbo mpya ya Diamond Platnumz ndivyo hivyo hivyo ilivyomeza kusikika kwa matokeo ya Kidato cha nne yaliyotoka mwishoni mwa wiki iliyopita na Dar es Salaam kuwa miongoni mwa mikoa iliyofanya vibaya matokeo hayo.

Licha Makonda kumeza kila kijiwe hivi sasa na yeye kutajwa tajwa mara nyingi kwenye vinywa, amemeza hadi taarifa za soka ambazo zenyewe ni ngumu kumezeka. Taarifa za soka hazimezwi kirahisi, lakini Makonda amezimeza.

Timu ya soka ya taifa vijana, ‘Serengeti Boys’ imefuzu kushiriki michuano ya Mataifa Afrika, itakayofanyika baadaye nchini Gabon.

Kama ilivyo watu wachache waliojua Diamond Platnumz katoa wimbo mpya ndiyo hata kwenye Serengeti Boys ni watu wachache wanajua taarifa ya timu hii.

Serengeti Boys imepata nafasi hiyo baada ya kushinda rufaa yake dhidi ya Congo Brazzaville ambao walimchezesha mchezaji kijeba katika hatua za kufuzu.

Ni hatua nzuri kwa mashabiki wa soka nchini kushuhudia kikosi hicho kikiwa sehemu ya timu zitakazoshiriki michuano hiyo ya vijana inayotazamwa na mawakala wengi duniani.

Kando ya stori za Makonda kutikisa jiji, wakati huu mashabiki wa soka Tanzania muda mwingi walitaka kusikia stori za mafanikio ya soka ambazo zimekuwa adimu kusikika zikipenya kwenye ngoma za masikio yao.

Linapokuja suala la nchi kufuzu kama nchi ni lazima tuungane pamoja kupongezana na kujiuliza kwanini hivi sasa tumefuzu na kwanini wakati mwingine tulishindwa kufuzu.

Haya ndiyo maswali muhimu ya kujiuliza tunapokuwa katikati ya furaha yetu. Kufuzu kwa Serengeti Boys hakutakiwi kuwa mwanzo wa migogoro na kutugawa Watanzania na kuleta makundi baina yetu sisi wenyewe.

Safari ya Serengeti Boys kwenda Gabon haitakiwi kuishia kwenye timu hiyo ya chini ya miaka 17 na ikae muda mrefu ndiyo ije kufuzu tena. Kufuzu kwa timu hii kunatakiwa kuwe mwanzo mzuri kwa timu nyingine kufuzu kwenye michuano mbalimbali.

Licha ya mafanikio yote ya Serengeti Boys, lakini tusiishie kujisifu na mafanikio haya badala yake tutumie kama mwanzo wetu wa kufuzu tena na tena.

Mpira wetu hauna misingi sahihi ya soka inayoweza kutufanya tubweteke na hatua hii ya Serengeti Boys na tujione tumeshamaliza kila kitu.

Tujipongeze kidogo kisha tuutafakari mpira wetu ambao umekuwa na sintofahamu nyingi zaidi.

Kama hatuwezi kujitafakari ni wazi tutakwenda Gabon kutembea, tutarudi na kufuzu kwetu tena itakuwa ndoto.

Licha ya matatizo yote ya Rais wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kushindwa kuungoza vyema mpira wetu kama kiongozi mkuu, lakini kwenye hili la Serengeti Boys anahitaji kupongezwa. Ameacha alama yake TFF.

Malinzi anatakiwa kuchukua changamoto anazokutana nazo kuujenga mpira na kuwa faida kwa taifa kama hivi Serengeti Boys ilivyofuzu. Asizichukue changamoto kuona anakosolewa sana kuliko kusifiwa.

Wadau hawataacha kukosoa wakiona kuna matatizo pahala. Yanapokuja mafanikio kama hivi ni lazima watu wampongeze na waungane naye pamoja.

Moja ya watu walionishangaza ndani ya TFF ni Mwenyekiti wa Hadhi na Sheria ya Wanachama, Eliud Mvela ambaye katika uchaguzi wa soka Mkoa wa Kilimanjaro alizungumza maneno aliyoyajua yeye mwenyewe.

Mvela aliuambia umma kuwa “nashangaa wakati huu timu ya taifa vijana imefuzu michuano, kila mtu yuko kimya na hakuna anayeona mafanikio ya Malinzi.

Aliongeza: “Kwa hiki kilichofanyika itoshe kuona Malinzi ni mtu sahihi katika maendeleo ya soka. Nimeshangaa kutoona taarifa nyingi za timu yetu (Serengeti Boys) kufuzu kwenye vyombo vya habari, lakini taarifa nyingi za kukosea kwa TFF ndizo zinazosikika,” alisema Mvela.

Mvela amezungumza nini hapa? Aliyemuelewa aniambie! Au kwa fikira zake anajua wanaoikosoa TFF ndiyo maadui wa Malinzi? Kama anajua hivyo basi ni wazi hatufai kuwepo hata pale TFF.

Muda tulionao hautakiwi kuwa wa kupigana vijembe kwa mtu huyu kumpiga vijembe mtu mwingine.

Mvela hakutakiwa kusimama mbele ya hadhira na kuzungumza aliyoyaamua kuyazungumza.

Wakosoaji si maadui kama anavyodhani. Wakosoaji ndiyo wanaoleta changamoto ambazo wakati huu tunakaa pamoja na kujisifu mafanikio ya Serengeti Boys.

Kama Mvela anashangaa watu kuwa kimya na mafanikio ya Serengeti Boys, awatafutie watu kitu cha kusema au kuandika.

Maana aina ya maneno yale inaonyesha wazi kuna baadhi ya wadau anaamini wana kinyongo na Malinzi, kitu ambacho sikipi nafasi kukiamini.

Muda wa kunyoosheana vidole umeshapita, huu ni muda wa kujitazama wapi tulikosea na wapi tukaze nati ili tuzidi kupata mafanikio zaidi ya haya, lakini tukikaa kumsikiliza Mvela ni wazi tutaendelea kuwa hapa tulipo kwa miaka mingi tu.

Uwekezaji wa soka la vijana ndiyo inayotakiwa kugeuka stori zetu kuu katika vijiwe vyetu vya soka si vinginevyo.

Mazungumzo mazuri ndiyo yanayojenga kwenye kila sehemu inayohitaji mafanikio, kama wakosoaji wanaokosoa wanaonekana wana shida na Malinzi, tukiri hapa Serengeti Boys imefuzu kwa bahati na hakuna mpira wowote ule wa maana.

Wakosoaji hawana shida na Malinzi, wana shida na mpira unavyoendeshwa ambao sasa Serengeti Boys wameshatuchongea mzinga ni kazi ya Malinzi kuwa na mipango thabiti ili baadaye tuline asali 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *