Habari
Wakati madaktari wakigoma...
Bunge lajichafua upya kwa posho
Mwandishi Wetu
Toleo la 224
1 Feb 2012
Spika Makinda na Rais Kikwete
  • Kibali cha Rais Kikwete chazua utata
  • Makinda asema wamejilipa muda
  • Wazika mradi wa nyumba za NHC
  • Mmoja asema CCM watafuta kifo

HALI ya hewa kati ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande mmoja, wananchi na kada nyingine za kijamii, imechafuka upya baada ya wabunge kujiongezea posho mpya kutoka Sh. 70,000 hadi Sh. 200,000 kwa siku, ikibainika kuwa fedha hizo hazitoki katika hazina ya Serikali bali zinamegwa kutoka katika fungu la bajeti ya maendeleo ya Bunge, Raia Mwema, limeelezwa.

Uamuzi huo wa Bunge sasa unatajwa kuchafua zaidi hali ya hewa nchini hasa ikizingatiwa kuwa suala hilo tayari lilikwishazua mjadala mkubwa na kupingwa na sehemu kubwa ya jamii nchini lakini sasa licha ya hali hiyo pamoja na mgomo wa madaktari unaoendelea nchini kwa sababu za kimaslahi, Bunge kwa upande wake limeamua kusonga mbele.

Uchunguzi wa gazeti hili ambao umethibitishwa na maofisa kadhaa waandamizi wa Bunge walioko Dodoma kwa ajili ya mkutano wa Bunge ulioanza jana (Jumanne), unabainisha kuwa wabunge watamega fedha hizo kutoka katika fungu lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba zao mjini Dodoma (Bunge Village).

Mradi huo wa “Bunge Village” ulipaswa kutekelezwa kwa ubia kati ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Hata hivyo, ingawa wabunge wanaweza ‘kukomba’ fedha hizo ili kujilipa posho, kitendawili kimesalia baada ya kujilipa mwaka huu wa bajeti, hali itakuwaje katika mwaka ujao wa fedha?

Lakini wengi wanaamini Serikali itaongeza bajeti ya Bunge katika mwaka ujao wa kibajeti utakaoanza Julai Mosi mwaka huu, ili kukidhi ongezeko hilo jipya huku kukiwa na madai kwa sasa kwamba Serikali imegoma kutoa fedha za nyongeza kwa maelezo kuwa bajeti ilikwishakupangwa, hali inayoulazimu uongozi wa Bunge kupangua mipango yake ya kibajeti katika taasisi hiyo ambayo ni moja ya mihimili nchi.

“Serikali imegoma kutoa fedha za ziada kwa ajili ya kuwalipa posho hizo mpya. Wamegoma hadi sasa kuwasilisha bajeti ya ziada (supplimentary budget) kwa sababu tu ya ongezeko la posho na kwa hiyo, fedha hizo zitatoka kwenye fungu mojawapo la wabunge ambalo ni mradi wa Bunge Village,” vinaeleza vyanzo vyetu vya habari kutoka serikalini na ofisi ya Bunge.

Awali, vyanzo vyetu vya habari kutoka Ikulu vilibainisha kuwa Rais Jakaya Kikwete aligoma kutia saini ongezeko hilo sambamba na kuzongwa na ushauri kuwa afute posho hizo na gazeti hili katika moja ya matoleo yake yaliyopita liliripoti hivyo, lakini sasa vyanzo hivyo vinaeleza kuwa Rais alimweleza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa “memo” (taarifa fupi ya maadishi); mnaweza kuamua kuhusu suala hili kwa kuzingatia mazingira ya sasa nchini pamoja na mwongozo wa busara zenu.

“Memo ya Rais haikuwa na maana wanaweza kufanya hivyo kwa wakati huu au baadaye, isipokuwa ilikuwa ikiwapa nafasi ya kutafakari kwa kuzingatia mazingira halisi ya nchi kwa kuwa nao pia ni viongozi wa kitaifa...Rais hakutaka kubishana wala kutunishiana nao misuli, nia yake ni kwamba uamuzi huu waufikie wabunge wenyewe na kikwazo kisiwe kibali chake,” kinaeleza chanzo chetu cha habari kutoka Ikulu.

Lakini wakati chanzo hicho cha habari kikieleza hivyo kutoka Ikulu, bungeni mmoja wa viongozi waandamizi amelidokeza gazeti hili kuwa, Rais Kikwete hakutaka kutunishiana misuli na wabunge ili kutochafua zaidi hali ya hewa katika wakati ambao Waziri wake wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, anatarajiwa kuwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya usimamizi wa mchakato wa kuandika Katiba, sheria ambayo muswada wake ulikwishapitishwa na Bunge, Novemba mwaka jana na Rais mwenyewe kuutia saini katika mazingira ambayo pia aliruhusu wadau wengine kuendelea kutoa maoni ya marekebisho.

Taarifa za uhakika ni kwamba sheria hiyo itafanyiwa marekebisho lakini pia Rais Kikwete anatarajiwa kukutana na wabunge wa CCM kwa ajili ya kuwaeleza kile kinachotajwa kuwa; “sababu za marekebisho” ya sheria ya mchakato wa Katiba mpya, sheria ambayo ilipiganiwa mno na wabunge wa chama hicho ili ipite.

Hata hivyo, ingawa inaelezwa kuwa Rais alituma ‘memo’ hiyo kwa uongozi wa Bunge katika hali ya tahadhari lakini ni Spika Makinda, anayedaiwa kuwatangazia wabunge wakati wa kikao chao cha kupeana muhtasari wa masuala muhimu ya nchi Jumatatu, wiki hii, kuwa Rais amekubali nyongeza ya posho mpya.

Kutokana na kauli hiyo ya Spika, zimeibuka taarifa za kuwapo kwa mtafaruku kati ya Ikulu, Bunge na uongozi wa juu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho kupitia kwa Katibu wake wa Halmashauri Kuu-Idara ya Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kiliweka bayana kuwa nyongeza ya posho haistahili kwa sasa na kwamba wabunge watumie busara kufikia uamuzi wa suala hilo.

Fungu la posho mpya

Kutokana na kuidhinishwa kwa posho mpya kwa wabunge, wabunge sasa katika kipindi cha mkutano huu na mikutano mingine, wanatarajia kutumia takriban Sh. 14,137,200,000 (takriban bilioni 14.14).

Mchanganuo wa takwimu hizo ni kwamba; katika mkutano wa Bajeti utakaofanyika kuanzia Juni, mwaka huu, ambao ni mkutano mrefu zaidi wa Bunge, wabunge watahudhuria Bunge kwa kukaa kitako kwa siku 75, na posho ya kukaa kitako (sitting allowance) kwa siku moja kama watahudhuria wote itakuwa ni Sh. 71,400,000 na jumla kwa siku zote 75 ni hizo Sh. zaidi ya bilioni 14.

Bunge pia litakuwa na mikutano midogo (mifupi), ukiwamo huu ulioanza mwanzoni mwa wiki hii na katika mikutano hiyo midogo wabunge watatumia takriban siku 63 kwa ajili ya mikutano hiyo ambayo italipwa posho mpya ya Sh. 200,000 na jumla ya fedha zote zitakazolipwa inatarajiwa kuwa ni Sh. 4,498,200,000 (kwa siku Bunge kama wanahudhuria wabunge wote Bunge linatumia Sh. milioni 71.4 kwa posho).

Lakini pia wabunge hulipwa posho ya kukaa kitako wanapokuwa katika vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge ambazo mara kwa mara hutangulia mikutano ya Bunge. Katika kamati, taarifa za uhakika zinabainisha kuwa wabunge hutumia siku takriban 60 kwa ujumla na kwa hiyo kwa kuwa kwa siku wanatumia Sh milioni 71.4 za malipo ya posho, kwa siku hizo 60, watakuwa wakitumia Sh 4,284,000,000. Ni kutokana na mchanganuo huo, Bunge sasa litakuwa linatumia bajeti ya jumla ya Sh. 14,137,200,000 kwa posho tu.

Chanzo chetu cha habari kinaeleza; “Ili posho hii iongezwe kwenye posho ya ubunge ambayo hutolewa kila mwezi kila mbunge atalipwa zaidi ya Sh. 3,300,000 kwa mwezi. Posho ya ubunge itakuwa Sh 8,415,000 na ongezeko hilo litasababisha upungufu wa Sh 7,068,600,000.”

Hali ndani ya kikao cha muhtasari

Katika kikao chao cha muhtasari ambacho hutumika kuwapa taarifa wabunge kuhusu masuala mbalimbali yakiwamo ya usalama wa nchi na mengine muhimu, inaelezwa kuwa masuala hayo muhimu hayakupewa nafasi na badala yake, mjadala wa posho mpya ulitawala takriban muda wote.

“Ulikuwa mjadala mkali sana, mashambulizi maalumu yalifanywa dhidi ya wabunge wanaopinga ongezeko la posho hadharani, Kabwe Zitto na Januari Makamba walishambuliwa waziwazi na kwa kweli katika hili ni wabunge karibu wote walikubaliana nalo. Ukiwaondoa hao akina Zitto, hapakuwa na msimamo wa wabunge wa chama fulani kwamba wamepinga,” kilieleza chanzo chetu cha habari ndani ya mkutano huo.

Inaelezwa kuwa ni Zitto ndiye aliyehoji fedha hizo za ziada zinatoka wapi kwa ajili ya kuziba pengo hilo, akisisitiza busara itumike zaidi kwa sasa lakini anadaiwa kujibiwa na Spika Makinda kuwa, Bunge lina mamlaka ya kupangua bajeti yake na kusisitiza kuwa ni lazima posho mpya zilipwe hata kama kelele zitapigwa.

Jana Makinda aliwaambia waandishi wa habari kwamba walianza kujilkipa posho hizo siku nyingi na kwamba walifanya hivyo kwa kibali cha Rais.

Kutokana na hali hiyo, Raia Mwema limeelezwa kuwa mradi wa nyumba za wabunge ndiyo utakaomegwa fedha zake ambazo ni zaidi ya Sh bilioni tano, ili kulipa posho katika kipindi hiki cha kuelekea bajeti mpya ya Serikali, kuanzia Juni, baadaye mwaka huu.

Sheria mpya imefuatwa?
 
Kuna madai kuwa kwa sasa nyongeza ya posho kwa wabunge imetengenezewa sheria ya mwaka 2008, ambayo kabla ya uamuzi wa kuongeza posho kufanywa, sheria inataka iundwe tume kwa ajili ya kufanya mchanganuo. Ni kutokana na matakwa hayo ya kisheria, inaelezwa kuwa hakuna tume iliyoweza kuundwa kwa ajili ya kazi hiyo na kwamba ongezeko hilo bado lina utata kisheria.

“Hii sheria ilifanyiwa kazi na Spika aliyepita Samuel Sitta na nakumbuka kati ya wabunge waliogharimiwa kusafiri katika nchi nyingine kwa ajili ya kujifunza mwenendo wa suala hili ni pamoja na Kabwe Zitto, nakumbuka alikwenda Kenya na kwingine.

“Baadaye sheria ikatengenezwa kwamba kabla ya posho kupandishwa ni lazima kwanza iundwe kamati ya watu wenye heshima katika jamii, wanaweza kuwa viongozi hata wastaafu, lakini wenye uzoefu katika utumishi wa umma kama makatibu wakuu au yeyote. Hii kamati haijaundwa na kama imeundwa nani wajumbe wake?” kinahoji chanzo chetu cha habari.

Hayo yakiendelea, John Daniel anaripoti kwamba Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere, amesema anasikitishwa na kuumizwa na Bunge kuwa sehemu ya kuzungumzia matatizo badala ya kuyatafutia ufumbuzi.

Ameonya kuwa hali hiyo isipodhibitiwa mapema wananchi watachukia wabunge wote na akawataka wabunge wenzake kubadili mfumo na kutambua kuwa kazi yao sasa ni kutekeleza ahadi na kutatua kero za wananchi, si kupiga siasa, na kuwataka wanaotaka siasa wasubiri mwaka 2015.

 “Yapo mambo mengi sana yanayoniumiza kama kiongozi, lakini kubwa zaidi ni Bunge kugeuka kuwa sehemu ya kusemea matatizo na si sehemu ya kutafutia  utatuzi kero hizo. Bado watu wanafanya siasa mpaka bungeni, kuna itikadi, Serikali inatoa majibu rahisi rahisi, mfumo huo ni hatari, iko siku wananchi watachukia Bunge.

“Niwaonye wabunge wa CCM kuwa kadri wanavyoendelea kukumbatia siasa badala ya kutekeleza ahadi ndivyo wananchi wanavyozidi kuwachukia. Mimi sikuchaguliwa kwa sababu CHADEMA (Chama cha Demokrasia na Maendeleo) kina wanachama wengi pale Musoma, hapana. Wengi walionipiga kura ni wana CCM, walifanya hivyo kutokana na kuwachukia wabunge wao,”alisema Nyerere.

Alitaja tofauti kati yao na wabunge wa CCM kuwa ni kupigania mgawanyo wa keki ndogo ya Taifa, wao wakipigania udhibiti na ubadhilifu wa fedha za umma na ongezeko la ukusanyaji ili kushughulikia kero nyingi zaidi za wananchi.

“Sisi wabunge wa CHADEMA tunapigania keki ya Taifa iongezeke ili tuweze kutatua kero za Watanzania, tunapigania udhibiti wa wizi wa fedha serikalini na taasisi zake pamoja na kuongeza ukusanyaji lakini wenzetu wa CCM wanapigania tugawane hichohicho kidogo.

“ Tunataka mianya ya kuliwa fedha za umma ushughulikiwe na kuongeza ukusanyaji, hiyo ndiyo tofauti yetu kubwa inayotufanya hata wakati mwingine tutoke nje ya Bunge,”alisema.

Alisema yeye kama mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kila kikao wanachojadili kwa sehemu kubwa ni ubadhirifu wa fedha za umma huku taarifa ikitolewa kuwa nchi ni masikini.

“Sehemu kubwa ya mijadala yetu ni ubadhilifu, ukisikia watu wanavyotumia fedha vibaya huwezi kukubali tugawane keki ndogo wakati wengine wanaitafuna watakavyo kwa ujanjaunja tu,”alisema.

Akizungumzia posho za wabunge alisema kimsingi wao kama wabunge wa CHADEMA hawakatai posho wanachokataa ni ubaguzi kwa watumishi wengine pamoja na viwango visivyoendana na hali ya watanzania walio wengi.

“Hatuwezi kukubali wabunge wapewe posho kwa kufanya kazi yao huku nesi anayekesha na mgonjwa akikosa posho. Haiwezekani mwalimu akafundisha mwezi mzima bila kutegemea posho huku wengine kila wakikaa wanalipwa, daktari akijua kuna posho hata moyo wa kuwahudumia wagonjwa utaongezeka zaidi.

“Tunataka kila mtumishi wa umma apate posho, hichohicho kilichopo tugawane kidogokidogo kila mtu apate, je viongozi wetu wanapokwenda kuomba misaada nje wanaomba ili tugawane posho? Huo ndio msimamo wetu. Sasa watu wasitutafsiri vibaya tunachohitaji ni usawa katika suala la posho,hata kama ikiongezeka si tatizo lakini kwanza lazima tujiulize ongezeko hilo linaendana na hali halisi ya Watanzania, na je imezingatia makundi yote,” alihoji.

 

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Maoni ya Wasomaji

Kama rais hakuwa ameidhinisha kulipwa posho za makalio kwa wabunge ilikuwaje waziri mkuu na spika watoe taarifa? Huu ni ushahidi tosha kuwa rais wetu hana msimamo ni mwoga na muongo. Kama spika na waziri mkuu wamezua si awawajibishe haraka?

MUOGA KWELI USHAMSHTUKIA EHH!!!!

hawezi kuwawajibisha katika hili, ameyaacha mangapi makubwa, kama ilivyotajwa kuwa ni mwoga, muongo, hana msimamo, anafanana na mbayuwayu.

Hawezi...kuwawajibisha!
Kama kawaida yake...anakaa kimya kwanza ajue upepo unaelekea wapi...akiona makelele yako wapi na yeye ananyanyuka na kusema yuko upande huo wenye makelele!
Huwa hana uhakika afanye lipi!

INASIKITISHA SANA TENA SANA HILI TAIFA LINAKOELEKEA......ALIYESHIBA HAMJUI MWENYE NJAA....KIMSINGI LINALOPASWA KUPIGIWA KELELE KATIKA HILI SUALA NI MFUMO MBOVU ULIOPO WA NANI ANAYEPASWA KUIDHINISHA POSHO ZA WABUNGE.....INAONESHA WANAJADILI WAO WAJILIPE SHS. NGAPI NA WANAJIIDHINISHIA WAO WA HAO HAO...WHERE IS CHECK AND BALANCE?
MHESHIMIWA ZITO NA TAASISI ZISIZO ZA KISERIKALI-KAMA SHERIA IMEPINDISHWA MBONA HAUJAHOJI BUNGENI AU NGOs KWA  NINI HAMJACHUKUA HATUA ZA KISHERIA?
LAKINI SIKU ZAJA AMBAPO WATANZANIA TUTASEMA IMETOSHA........!
 

Hivi watanzania tutaendelea mpaka lini kuweka Bungeni watu ambao wamepooza Ubongo na wamefika mwisho wa kufikiri? Hebu angalia haya:
1. Mgomo wa madakitari
2. Wagonjwa wanaofia Hospitalini kwasababu ya mgomo wa madakitari
3. Hali duni ya maisha ya watanzania.
4. Mishahara duni ya wafanyakazi Tanzania
Alafu wabunge wetu wapo Bungeni wanajadili posho na ni wawakilishi wa hawa wananchi wanaotaabika.
Najua wabunge wengi wengi hawajui Kiingereza, lakini rais wakati anawaagiza Mr. Pinda na Spika wa Bunge mbona alitumia Kiswahili? Ina maana hata Kiswahili hawakukielewa! Kama ni hivyo hawa wawakilishi wetu huko Bungeni wanaelewa Lugha gani? Hebu wabunge wetu jaribu kutumia akili acheni kutumia Matope au sirika(instinct)
Ni hayo tu.
       Mzee Kikwete Mungu akusaidie ingawa serikali yako imejaa vilaza!

KIONGOZI AINA YA BENDERA HUFUATA UPEPO HAELEWEKI NA HAWEZI LETA UKOMBOZI 'wokovu' KTK JANGA ASILOLIJUA,,,,
YES MAN NI WA KUOMBEWA SAAANA NA ANAHITAJI DELIVERNCE YA UKWELI....
MUNGU MREHEMU NA UTUREHEMU NA KUIBARIKI TANZANIA AFRIKA NA WATU WAKE

Toa maoni yako

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.