KUMETOKEA vioja ndani ya Bunge, nalo limeingiliwa na abrakadabra! Ndiyo, imani za kishirikina zimeingia bungeni. Wakati huu wa Bunge kujadili Bajeti tumeshuhudia Bunge likitumia sehemu ya muda, nguvu na rasilimali zetu katika kufuatilia uvumi wa kishirikina.
Tumekwenda mbali, tunaambiwa Bunge letu tukufu linachunguza uvumi huo! Hiki ni kioja kwa namna yake, maana kama jambo ni la uvumi iweje lichunguzwe. Kwamba tumefika mahali tunatumia muda na fedha zetu kuchunguza uvumi! Hivi ushahidi na vielelezo vya uvumi vinapatikanaje?
Kama jambo ni la uvumi, basi kawaida ya anayehusishwa na uvumi ni kuukanusha vikali uvumi huo. Tulitaraji Bunge, mara baada ya kuanza kuenea kwa uvumi huo lingekanusha vikali baada ya kujiridhisha kuwa ni uvumi tu. Tena ni uvumi wenye kuhusiana na imani za kishirikina. Imani za kishirikina zimechangia sana kurudisha nyuma maendeleo yetu. Tuna mifano ya mauaji ya akina mama wazee na malbino yanayochangiwa na imani hizo. Bunge liwe mfano wa kupiga vita imani hizo.
Ni ajabu, na pengine ni mambo ya aibu hata mbele ya wahisani wanaochangia Bajeti yetu wanaposikia, kuwa katika karne hii ya Sayansi na Teknolojia, Bunge la nchi linatumia muda wake na rasilimali zake kufuatilia na hata kuchunguza masuala ya imani za kishirikina.
Ili kulinda heshima ya Bunge letu na nchi yetu, jambo hili lingeangaliwa kisayansi na kiteknolojia zaidi ili nasi twende na wakati. Kama inadaiwa kuna mbunge ameingia bungeni usiku na kuweka vitu kwenye viti vya wabunge, basi kuna ya msingi ya kuangalia, kujiuliza na kuyapatia majibu kabla ya kuchukua hatua nyingine.
Haya yafuatayo tunaweza kabisa kuanza nayo kuyaangalia kabla ya kulifanya jambo hili kuwa ni kitu kikubwa kinachotuchukulia muda na fedha zetu; Sote tunaelewa, kuwa Jengo la Bunge ni mahali pa kazi kama ilivyo mahali pengine. Walipa kodi wa nchi hii wamechangia jengo la Bunge lijengwe na liwe ni mahali pa kazi zenye lengo la kumsaidia Mtanzania na kulinda maslahi ya umma wa Watanzania. Kila sehemu ya kazi ina taratibu zake.
Tuna imani kuna waliopewa dhamana ya kuruhusu na kuzuia wageni kuingia ndani ya jengo hilo katika wakati wa kazi na baada ya kazi. Lakini kikubwa, huwezi kuingia ndani ya jengo la Bunge bila kufunguliwa mlango na mwenye dhamana ya kushika funguo za mlango huo. Na kwa nini mbunge aliyeingia humo aingie usiku badala ya wakati wa kazi? Tunaambiwa hakuingia peke yake, je aliingia na nani?
Kilichotokea hapa ni ukiukwaji wa taratibu za kazi. Tuaambiwa aliyehusika anajulikana lakini jina halitajwi. Huku hakusaidii kupunguza uvumi, kunaongeza uvumi na kutupotezea wakati wa kujadili mambo ya kimsingi ya taifa letu. Jengo la Bunge ni la kisasa na la gharama kubwa. Tunaambiwa kamera za kurekodi matukio ndani ya jengo hilo hazikufanya kazi isipokuwa moja tu. Je, ni nani anayehusika na kuhakikisha kamera hizo zinafanya kazi?
Maswali yanayoulizwa hapa na mengineyo yana wahusika wa kuyajibu. Bunge litusaidie kupata majibu ya maswali haya ya msingi ili tupunguze hofu ya kutokea kwa madhara makubwa huko twendako. Maana, tunachokiona hapa ni uzembe wa baadhi ya watendaji katika Jengo hilo la Bunge. Leo kaingizwa Mheshimiwa Mbunge usiku, hatujui kesho ataingizwa nani. Inahusu usalama wa Jengo la Bunge kwa maana ya usalama wa Wabunge wetu. Tuko katika karne ambayo, mbali ya mambo mengine, tunapambana na ugaidi. Kamera za ndani na nje ya ukumbi wa Bunge si za mapambo. Zimewekwa ili kuchangia katika shughuli za usalama. Wahusika wanafanya nini?
Naam. Ni wakati sasa wa Bunge kukemea vikali imani za kishirikina na hasa zinapofika na kuingia ndani ya Bunge. Huko nyuma tumesikia habari za popobawa na kadhalika. Haya ni mambo ya abrakadabra, kama ninavyoyaita siku zote. Hayana maana yoyote. Ni kama vile mbinu ya wajanja fulani kututaka tutoke kwenye mstari wa kujadili mambo ya msingi yenye kuhusu hali yetu ya sasa na mustakabali wa nchi. Tusikubali kutoka kirahisi kwenye mstari wa kujadili ya maana na ya msingi kwa taifa. Na hapa nitarudi kwenye kujadili yenye kumhusu Mtanzania wa kawaida kuhusiana na Bajeti ya mwaka huu.
Jumatatu ya juma hili nilisimama kituo kimoja cha mafuta mjini Iringa. Usiku ulikuwa unakaribia. Mbele yangu nilimwona mama aliyeshika galoni ndogo. Ni galoni tupu ya ujazo wa lita tano. Alisimama sehemu ya kuuzia mafuta ya taa. Nilisogea, nilimsalimia. Akaniambia anamsubiri kijana wa kumpimia mafuta ya taa. Anaitwa Mama Mwajuma.
Mara akatokea kijana anayehusika. Anaitwa Bakari. Mama Mwajuma alinunua mafuta ya taa ya shilingi 200! Bei ya lita moja ya mafuta ya taa kwa siku hiyo ilikuwa ni shilingi 1450. Kwa shilingi 200 hupati hata robo lita. Mama yule alipimiwa nukta kadhaa za mafuta. Ndiyo, alipimiwa matone kadhaa ya mafuta ya taa.
Na kama ilivyo jina lenyewe la mafuta, Mama Mwajuma alikwenda kununua mafuta ya kuwashia koroboi. Hakuwa na uwezo wa kununua lita moja ya mafuta ya taa, ni bei ya juu sana. Bakari, kijana mwuza mafuta aliniambia; kuwa zamani kipimo cha kuanzia ilikuwa ni mafuta ya shilingi 500. Kwamba mpaka mwaka jana lita moja ilikuwa ni shilingi 900. Bakari alizidi kunielimisha, kuwa kutokana na kuelewa unyonge na hali ngumu za watu wengi, wameamua kuwasaidia hata wenye kutaka mafuta ya taa ya shilingi 200.
” Tutafanye kaka, si unaona mama huyu hali yake.Nikimkatalia mafuta ya shilingi 200 atakwenda kulala giza. Ni bora nimpe hayo matone ya mafuta akajaze kibatari chake”.
Naam. Tunachoongelea hapa si uvumi. Ni hali halisi. Bei za mafuta zimepanda sana, hivyo ugumu wa maisha umezidi kwa Watanzania wengi zaidi. Bei ya nishati ya umeme nayo ni ya juu sana. Leo kwenye miji yetu kuna Watanzania wanaotumia vibatari. Hawamudu tena kulipia gharama za umeme.
Tufahamu, kuwa kwenye hospitali na zahanati zetu kuna wagonjwa wanaolala chini kwa kukosa vitanda. Kuna wagonjwa wanaokosa dawa. Katika nchi yetu hii, achilia mbali vijijini, mijini kuna barabara za mitaa zenye mashimo kama mahandaki. Tuna shule vijijini na mijini ambako wanafunzi wanakaa chini na wengine kukosa walimu. Haya yanatokea katika nchi yetu hii.
Kwa nini wagonjwa wetu walale chini na wakose dawa? Kwa nini watoto wetu wakae chini madarasani na kukosa walimu? Fedha zinakwenda wapi? Haya na mengineyo ndio maswali tunayopaswa kujiuliza na kujiumiza vichwa. Haya si mambo ya uvumi. Haya si mambo ya abrakadabla. Ni hali halisi. Hatuhitaji tume kuchunguza. Tunahitaji kuchukua hatua. Sasa.
Toa maoni yako