JUMANNE Desemba 8, 2009 saa moja na nusu usiku, familia ya Balozi Andrea Tibandebage ya Kihanga Karagwe, ilipata pigo la kuondokewa na msingi wa familia hiyo Mwalimu Flora Nyakato Tibadegage. Msiba huo mkubwa ambao mbali na kuitikisa familia ya Balozi Tibandebage, umetikisa pia Wilaya ya Karagwe na Mkoa wa Kagera.
Tuna majonzi makubwa, tunalia na kusikitika kwa kuondokewa na dada yetu, ndugu yetu, rafiki yetu, mwenzetu na mwalimu wetu. Kwa umri mdogo wa miaka 61, tulikuwa bado tunamhitaji, tunahitaji huduma yake, upendo wake na mchago wake katika familia, kijiji, wilaya, mkoa na taifa zima. Tulihitaji bado ushauri wake wa kiroho na mchango wake katika kulinda na kutetea maadili ya jamii.
Mazishi makubwa ya Mwalimu Flora, yaliyoongozwa na Maaskofu wawili wa Kanisa Katoliki, Askofu Protase Rugambwa wa Jimbo Katoliki la Kigoma na Askofu Almachius Rweyongeza wa Jimbo Katoliki la Kayanga wakishirikiana na umati mkubwa wa waumini, viongozi wa vyama siasa na serikali, ndugu, jamaa, marafiki, watawa na idadi kubwa ya mapadri ni ishara tosha kwamba marehemu alikuwa na mchango mkubwa katika jamii. Alikuwa mchamungu alilipenda taifa lake na alilipenda Kanisa Katoliki na kulitumikia.
Kijiji cha Kihanga, kimempoteza Mama mpenda maendeleo; Mwalimu aliyewapenda watoto, ambaye alijitolea kuwafundisha watoto katika saa za ziada bila malipo. Aliifanya kazi hii kwa uaminifu mkubwa kiasi cha kufikia hatua ya kukosana na wazazi maana watoto walitumia saa nyingi kusoma na kushindwa kurudi nyumbani mapema kuchota maji na kuchanja kuni. Wazazi walilalamika, lakini Mwalimu Flora, aliziba masikio. Aliendelea kufundisha na kuwashawishi walimu wengine kufanya hivyo. Wale walioshinda mtihani wa darasa la saba na kushindwa kuendelea kwa kutokuwa na uwezo wa kulipa karo, alijitolewa kuwalipia. Watoto wengi wa kijiji cha Kihanaga walinufaika kwa msaada wa Mwalimu Flora.
Wilaya ya Karagwe, imepata pigo la kuondokewa na Mama Mshauri, mzalendo na shupavu ambaye alikuwa tayari kupambana na yeyote ambaye angejaribu kuvuruga maendeleo ya elimu ya msingi wilayani. Alitetea haki za walimu na wanafunzi, alitetea haki na kusimamia ukweli, alikuwa mama mpenda maendeleo ambaye hata baada ya kustaafu kwa hiari mnamo mwaka 1998, aliendelea kushiriki kwenye shughuli mbali mbali za Wilaya, mfano kuwa mjumbe wa mfuko wa elimu wa wilaya na kazi nyingine nyingi alizozifanya kwa kujitolea.
Alikuwa na wito wa ualimu. Hakufanya kazi hiyo kama mradi wa kujipatia kipato, bali aliifanya kwa moyo wake wote. Matendo yake yalionyesha jinsi ualimu ulikuwa ni wito wake. Alipokuwa Mwalimu Mkuu, aligombana na walimu waliokuwa wazembe, alitoa taarifa wilayani hadi wizarani akiwalalamikia walimu ambao hawakufundisha; alipendekeza wakatwe mishahara yao. Hili lilisababisha asipendwe na baadhi ya walimu wenzake.
Lakini matunda yake ni kwamba kila shule aliyofundisha watoto wengi walifaulu kwa wingi kujiunga na kidato cha kwanza. Aliamini kwamba watoto wakijengewa mazingira mazuri na walimu wakiwa na nyenzo na moyo wa kujitolea kufundisha saa za ziada ni lazima watoto wafaulu. Alijijengea utamaduni wa kuanza kuwaandaa watoto wakiwa darasa la tano na kuhama nao kila darasa hadi darasa la saba. Kwa mfumo huu aliweza kuwafahamu vizuri watoto wote na kuwasaidia wenye uwezo mdogo.
Ipo mifano mingi ya madaktari, wanasheria na mainjinia waliopata msingi wa elimu kutoka kwa mwalimu Flora. Baadhi yao hawajapata habari za msiba huu, kwa tanzia hii tunapenda kuwajulisha kwamba Mwalimu wao, Mungu kampenda zaidi! Hatunaye tena!
Wadogo zake wanasema juu ya pengo kubwa la kuondokewa na dada yao: “Tulipata bahati ya kuwa na wazazi watatu: Baba, mama na dada yetu Mwalimu Flora… kwetu hakuwa dada bali mzazi. Hata tulipokuwa wadogo na yeye akiwa na umri mdogo alitujali sana na alifanya mambo mengi zaidi ya umri wake. Tunasikitika sana kumpoteza. Mama yetu mzazi ni marehemu, dada yetu alimtunza Baba yetu kwa niaba yetu sote. Kifo chake ni pigo kubwa – ni pengo lisilozibika”.
Mwalimu Flora, alikuwa na sifa nyingi ambazo watu wengi waliohojiwa wakati wa kuandaa tanzia hii walizitaja: Muwazi, mvumilivu, jasiri, mpenda maendeleo, mwalimu wa kweli, mwalimu wa viwango, mzazi mwenye upendo, mzalendo, mcha Mungu, mwenye moyo wa kusaidia masikini na wasiojiweza, mwadilifu. Alipenda kila mtoto apate elimu bora na aliwapatia misaada mbalimbali wale ambao hawakuwa na uwezo wa kulipia gharama za kupata elimu. Mbali na sifa hizi zote alikuwa na sifa ya ziada: Mkali kama pilipili, mwenye upendo kupindukia! Alikuwa mkali kwa kila mtu! Alikuwa mkali kwa wazazi wake, wadogo zake, watoto wake, wanafunzi wake, ndugu na jamaa, viongozi wake na jamii nzima iliyokuwa ikimzunguka.
Sifa ya ukali ilikuwa na sura mbili; chanya na hasi. Chanya kwa maana kwamba alikuwa mkali kwa kulenga mafanikio katika familia yake na katika jamii nzima kwa ujumla. Alikuwa mkali kwa kushindwa kuvumilia mambo ya ovyo; alipenda utaratibu, alipenda kufuata sheria, alipenda kufuata haki, alipenda uwajibikaji.
Watoto wake walitoa ushuhuda huu: “Mama alikuwa mkali sana- lakini alikuwa mama mwenye upendo mwingi kwetu sisi watoto wake na watu wengine, hakuvumilia upuuzi ”.
Kwa upande mwingine ukali wa Mwalimu Flora ulikuwa hasi, kwa maana ya msimamo wake wa kutaka kuwa mkamilifu na kutaka wale wote waliomzunguka kuwa wakamilifu, ulisababisha awe na maadui. Baadhi walimwogopa. Ndio maana Familia ya Balozi Tibandebage, inapenda kuomba msamaha kwa wale wote waliomchukia Mwalimu Flora, kwa ukali wake wamsamehe. Hakuwa na nia mbaya; yeye alikuwa na udhaifu chanya, udhaifu wa kutamani ukamilifu. Duniani hakuna mkamilifu, lakini kutamani ukamilifu si dhambi!
Mwalimu Flora, ana sifa nyingi, mfano alikuwa mwanariadha mashuhuri. Mwaka 1965, alikuwa mshindi wa kitaifa wa mbio za mita 100. Alikuwa mchezaji hodari wa mpira wa kikapu. Alithamini michezo na kuifundisha shuleni. Aliwashauri walimu wa kike na kiume kutumia michezo kama silaha ya kuwasaidia kubaki katika maadili mema. Baadhi ya marafiki zake walihojiwa wakati wa kuandaa tanzia hii walitoa ushuhuda jinsi ushauri wa kuipenda michezo kutoka kwa Mwalimu Flora, ulivyowasaidia katika maisha yao. Mbali na sifa hizo zote kuna zile zinazomfanya kuchomoza na kuonekana ana mchango wa pekee katika taifa.
Akiwa na umri wa miaka 25, aliamua kuomba uhamisho kutoka Morogoro kwenda kufundisha shule za vijijini Karagwe. Huu haukuwa uamuzi wa kawaida wakati watu walikuwa wakitamani kuishi mijini kama vile Dar es Salaam na kujiendeleza hadi nje ya nchi. Mwalimu Flora, alikuwa na nafasi kubwa ya kuishi mjini na kujiendeleza nje ya nchi maana baba yake alikuwa Balozi. Pamoja na nafasi aliyokuwa nayo, alifanya uamuzi wa kuishi na kufundisha vijijini. Amefanya kazi hii kwa furaha kubwa kwa maisha yake yote. Matunda ya uamuzi wake huo yanaonekana wazi katika vijiji vya Karagwe.
Lakini pia uamuzi wake wa kutokuolewa ili apate nafasi ya kuwatunza wazazi wake na kuwapatia wadogo zake nafasi ya kufanya kazi mbali na nyumbani ni jambo lisilo la kawaida. Ni sifa ambayo inawaendea watu wachache. Utamaduni wetu kwamba mtoto wa kike ni wa kuondoka nyumbani na kujenga familia nyingine nje unapoteza nguvu tunapopata mifano kama ya Mwalimu Flora. Tunaanza kuona ukweli kwamba hata wanawake wanaweza mambo mengi; wanaweza kutunza familia – wanaweza kuwa nguzo ya familia. Kasumba ya kuwathamini watoto wa kiume na kuwapuuza watoto wa kike inaanza kupungua!
Flora Tibandebage alizaliwa Januari 25, 1948 kijijini Kasheshe -Karagwe. Alipata elimu msingi katika Shule za Tabora, Nyakasana, Ihungo na Kashozi kati ya mwaka 1954-1961. Alikwenda Sekondari ya Rosary Collage Mwanza kati ya mwaka 1962-1965 na kuhitimu kidato cha nne. Alijiunga na Chuo cha Ualimu Chang’ombe Dar-es-Salaam mwaka 1966 na kuhitimu kama mwalimu wa daraja A mnamo mwaka 1967. Alianza ualimu mwaka 1968 katika shule ya msingi ya Mwembesongo mjini Morogoro. Baadhi ya shule za msingi alizowahi kufundisha ni Kayanga, Shule ya Wasichana Nyakasana, Rwambaizi, Kimiza na Maguge. Alistaafu kwa hiari mwaka 1998.
Mwalimu Flora aligundua kuwa ana uvimbe katika titi moja mwaka 2001 na baadaye ilithibitishwa kuwa alikuwa na saratani ya titi. Alipata matibabu katika hospitali ya Ocean Road Dar es Salaam, Mulago na Nakaselo Medical Centre ya Kampala, Uganda; lakini saratani iliendelea kusambaa mwilini. Sifa yake ya ushupavu ilijionyesha vizuri wakati akipambana na ugonjwa wa saratani.
Ugonjwa huu ulimtesa sana, lakini hakupenda kuwaonyesha watoto wake, ndugu, jamaa na marafiki kwamba alikuwa na mateso. Hakupenda kuwabebesha watu mzigo wa ugonjwa wake. Alitaka kuubeba mzigo wake mwenyewe. Aliamini atashinda, aliamini ataendelea kuishi, daima alikuwa na matumaini. Aliendelea kutoa huduma kwenye familia yake na katika jamii. Ijumaa, Desemba 4, 2009 alizidiwa, na Jumamosi alipelekwa hospitali ya Rubya-Bukoba, ambako alipatia matibabu, madaktari walijitahidi kuokoa maisha yake lakini kwa mapenzi ya Mungu Mwalimu Flora, aliaga dunia Jumanne, Desemba 8, 2009 saa moja na nusu usiku.
Mwalimu Flora ameacha watoto wawili na wajukuu watatu. Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya mpendwa wetu.
Toa maoni yako