Cameroon yatawazwa mabingwa wapya Afrika

Goli la ushindi la dakika za mwisho lamaliza miaka 15 ya Cameroon kusubiri ubingwa wa Afrika.

BAADA ya Misri kupata bao la kuongoza katika dakika ya 22 ya mchezo, Cameroon ilipambana na kufanikiwa kutoka kifua mbele kwa ushindi wa mabao 2-1 katika pambano kali la fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Vincent Aboubakar alikwamisha bao la ushindi dakika mbili kabla ya kipenga cha mwisho, kwa kubetua mpira juu ya mlinzi Ali Gabr na kuujaza kimiani.

Nicolaus Nkoulou ndiye aliyefunga bao la kusawazisha kwa Cameroon, kwa kichwa katika dakika ya 60 ya mchezo.

Bao hilo la kusawazisha lilifuatia lile la kuongoza la kiungo wa Arsenal ya Uingereza Mohamed Elneny aliyefunga katika dakika ya 22 kwa bao zuri.

Wachezaji na mashabiki wa Cameroon walishangilia kwa nguvu baada ya bao la ushindi la Aboubakar, ambalo liliashiria kurudi kwa wafalme hao katika kilele cha soka la Afrika, baada ya kusubiri kwa miaka 15.

Ushindi wao wa jana unaifanya nchi hiyo kuwa ya pili kwa mafanikio barani humo nyuma ya Misri – na ni mara ya kwanza kuifunga Misri katika fainali ya michuano hiyo baada ya kushindwa kufanya hivyo mara tatu.

Mshambuliaji wa Besiktas ya Uturuki Aboubakar alikimbilia kwa mashabiki wa Cameroon katika uwanja wa Stade de l'Amitie huko Libreville kushangilia, huku akifuatwa na wachezaji wenzake na benchi la ufundi la timu yake.

Cameroon ambayo haikuwa inapewa nafasi kubwa kufika mbali katika michuano ya mwaka huu lakini iliwashangaza wengi kwa kufanikiwa kufika fainali na kuishinda Misri ambayo ilikuwa inapewa nafasi kubwa kushinda taji hilo kwa kufunga bao katika dakika za mwisho.

Wachezaji, maafisa wa Cameroon wakishangilia bao la ushindi la Vincent Aboubakar.

Pamoja na kukumbwa na matatizo mengi kabla ya michuano hiyo, ikiwemo kujitoa kwa wachezaji muhimu kama Joel Matip na Eric Chuopo-Moting, kocha Hugo Broos alifanikiwa kuunda kikosi cha vijana na kupata matunda yake kwa kuwa ni timu yenye kucheza kwa nguvu na yenye uwezo wa kubadilika kulingana na mazingira.

Misri maarufu kwa jina la The Pharaohs – ilikuwa inawania ubingwa huo kwa mara ya nane baada kuwa nje ya mashindano hayo kwa miaka saba – ilianza vizuri na bao la Elneny lilimaliza kazi nzuri ya timu.

Kiungo huyo wa Arsenal alianza move hiyo na kuimaliza, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mohamed Salah ndani ya eneo la kumi na nane na kupiga shuti lililomshinda Fabrice Ondoa.

Kipindi cha pili Misri iliruhusu Cameroon kumiliki mpira, kosa ambalo watabaki kujutia.

Mshambuliaji Benjamin Moukandjo wa Cameroon alimimina krosi nzuri, na Nkoulou aliizidi nguvu safu ya ulinzi ya Misri na kupiga shuti lililomshinda Essam El Hadary na kujaa wavuni.

Baada ya bao hilo la kusawazisha, mpira ulikuwa mzuri zaidi, huku Cameroon ikiongozwa na uzuri wa washambuliaji Christian Bassogog na Jacques Zoua, iliwalazimisha Misri kurudi nyuma kujilinda na kuwafanya waanze kutumia mipira mirefu kwenda kwa Salah na Ramadan Sobhi.

Uchovu uliingia kwa wachezaji wa Misri na mwishowe Cameroon walipata kile walichokuwa wanatafuta kwa kuzidisha mashambulizi dhidi ya safu ya ulinzi ya Misri.

Aboubakar alimiliki mpira uliotokana na pasi ndefu kwa kifua chake nje kidogo ya kumi na nane na kuuinua juu ya mlinzi Gabr, kabla ya kumpita na kupiga shuti lililojaa wavuni kwa mguu wake wa kulia.

Misri – ikiwa na mchezaji mwenye uzoefu na mwenye uzoefu zaidi katika mashindano hayo – El Hadary, walibaki wameshtushwa baada ya kuweza kumiliki mpira vizuri katika kipindi cha kwanza.

Misri ilikuwa ikitegemea safu nzuri ya ulinzi ikiongozwa na Ahmed Hegazy, Gabr na mchezaji wa Hull City Ahmed Elmohamady. Pia walikuwa na wachezaji hodari kwa Elneny na Salah.

Misri waliweza kufanya sehemu yao katika mchezo huo wa fainali, lakini ni nguvu na uhimili wa Cameroon ambayo ndiyo ilitoa burudani murua katika mchezo huo.

Kocha wa Ubelgiji Broos alidhihirisha umoja uliopo katika timu yake, kwa kushangilia ubingwa wa kwanza wa Mataifa ya Afrika.

“Nimefurahishwa na wachezaji,” alisema. “Hili sio kundi la wachezaji wa mpira, ni kundi la marafiki.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *