Makala
CCM, CHADEMA hapatatosha Arumeru Mashariki
Paul Sarwatt
Toleo la 226
15 Feb 2012
Mandhari ya wilaya ya Arumeru
  • Bosi wa AICC atajwa kubeba mikoba CCM
  • Wa CHADEMA aitisha kikao kujipanga
  • Ni mbio za kujaza nafasi aliyoacha Sumari
  • Yatabiriwa utakuwa mpambano wa haja

SIKU chache baada ya Tume ya Uchaguzi (NEC) kutangaza tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, wanasiasa kutoka vyama mbalimbali wameanza harakati za kuwania jimbo hilo.

Uchaguzi huo mdogo utafanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo, Jeremiah Sumari, aliyefariki dunia Januari 19 mwaka huu na kuzikwa Januari 21 kijijini kwake wilayani humo.

Wiki iliyopita Tume ya Uchaguzi ilitangaza Aprili Mosi, kuwa ndiyo siku ya kufanyika kwa uchaguzi huo, na kampeni zake zitaanza Machi nane na kumalizika Machi 31.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva, wapiga kura wa jimbo hilo watapaswa kutunza vitambulisho vyao vya kupigia kura kwa kuwa tume haitarajii kuandikisha wapiga kura wapya, na badala yake watatumia daftari la kudumu la wapiga kura.

Aidha, katika taarifa hiyo, Mwenyekiti huyo wa NEC alieleza kuwa tume hiyo pia haitaongeza vituo vipya vya kupigia kura na badala yake vituo vitakavyotumika ni vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Wakati NEC ikitangaza taratibu hizo, mgombea wa kwanza kujitokeza hadharani kutaka kurithi nafasi ya Sumari ni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Joshua Samwel Nassari (26) ambaye alitangaza rasmi nia yake ya kuwania jimbo hilo Jumamosi iliyopita.

Nassari ambaye alishindwa na Sumari kwa kura chache katika uchaguzi wa mwaka 2010 alitangaza nia yake katika hafla fupi ya kuchangisha fedha kwa ajili ya uchaguzi huo iliyofanyika katika hoteli ya kitalii ya Kibo mjini Arusha.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, pamoja na wapenzi, wanachama na wakazi wa Jimbo la Arumeru Mashariki wanaoishi mjini Arusha.

Katika uchaguzi uliopita mgombea huyo kijana alipata kura 27,000 wakati Sumari ambaye alishinda na kuwa Mbunge wa jimbo alipata kura 32,000.

Akizungumza katika hafla hiyo Nassari alieleza kuwa lengo la kutangaza nia ya kutaka kuwania nafasi hiyo kwanza ni kuomba ridhaa ya chama chake ili apitishwe kupeperusha bendera ya chama hicho.

Alisema kama mzaliwa wa jimbo hilo anataka kutumia haki yake kitatiba kuwania nafasi hiyo ili apate fursa ya kuwawakilisha wananchi wa Arumeru Mashariki katika Bunge la Jamhuri.

“Mwaka 2010 niligombea ikiwa muda mfupi tu baada ya mimi kuhitimu masomo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuleta changamoto kubwa katika uchaguzi huo na rekodi zangu zinajieleza kwa kura nilizopata,” alisema. “Kwa sasa nimejipanga sana nikiwa na mtaji wa kura zaidi ya 27,000 na vyama vingine hasa CCM, hawana tena nafasi ya kupenya katika jimbo hili, nina imani kama tutaungana viongozi, wanachama na mashabiki wa CHADEMA tutashinda kwa urahisi,” alisema.

Alisema kilichomsukuma kuingia katika mbio za kuwania kiti hicho kwanza ni kutoridhika na matokeo ya uchaguzi uliopita akisema anahisi kuwa matokeo yake hayakuwa sahihi hasa katika hatua za mwisho za majumuisho ya kura kutoka vituo vyote.

Alisema matokeo ya kura walizokusanya mawakala wa chama chake yalionyesha kuwa alipata kura 29,000 lakini baadaye wasimamizi wa uchaguzi katika jimbo walitangaza kuwa amepta kura 21,000 na leo katika tovuti ya tume ya uchaguzi yanaonyesha kuwa alipata kura 27,000.

“Ni mkanganyiko huo ndiyo ulionipa nguvu mpya ya kutaka kugombea tena nikiamini bado nina deni kubwa kwa wananchi wa Arumeru Mashariki ambao kwa wakati ule walijenga imani kubwa juu yangu na mimi ninawaahidi kuwa sitawaangusha, ” alisema.

Alisema iwapo atashinda nafasi hiyo tayari ameaandaa mipango madhubuti ya maendeleo katika sekta muhimu kama afya, maji, elimu na miundombinu kwa kuwa wabunge karibu wote waliopita hawakuwahi kutilia mkazo masuala hayo muhimu.

“Ni ukweli mchungu lakini lazima niuseme kuwa jimbo letu pamoja na kuzungukwa na rasilimali nyingi, wabunge waliotangulia ambao walikuwa kutoka chama tawala cha CCM hawakuelekeza nguvu zao katika kutumia rasilimali hizo kutatua matatizo ya msingi ya wananchi wa Jimbo la Arumeru Mashariki. Mimi nataka kuchukua mwelekeo tofauti,” alisema.

Aliongeza: “ Kwa mfano, upande wa barabara, jimbo lote lina kilomita tano za barabara ya lami ambayo ni kutoka eneo la Kilala hadi hospitali ya Nkoaranga na baadhi ya kata za pembezoni barabara ni mbaya sana na kuna maeneo hayafikiki kabisa kwa barabara.”

Alisema hali hiyo imezorotesha shughuli za kiuchumi katika jimbo hilo hasa mazao ya wakulima kufika sokoni kwa wakati na wagonjwa kufikishwa katika vituo vya afya na hospitali.

“Jimbo la Arumeru Mashariki lina matatizo mengi kama maji, afya na elimu, na mfumo wa utawala wa CCM umeshindwa kuwatengenezea fursa wananchi wa Arumeru Mashariki na matatizo hayo yote yanatokana na mfumo huo wa utawala wa viongozi wa CCM,” alisema.

Ingawa hadi mwanzoni mwa wiki hakuna mgombea mwingine kutoka CHADEMA aliyetengaza nia ya kuwania jimbo hilo taarifa zilizopatikana kutoka vyanzo kadhaa zinadai kuwa mhadhiri wa kitivo cha sheria, Chuo Kikuu cha Makumira, Anna Mghwira, anataka kujitosa kuchukua fomu kupitia CHADEMA.

Ingawa mhadhiri huyo hakupatikana kuthibitisha taarifa hizo, watu wake wa karibu waliliambia Raia Mwema kuwa mhadhiri huyo alikuwa anajipanga kuingia katika mchakato wa kura za maoni na kuingia katika mbio za kuwania jimbo hilo.

Akizungumzia uchaguzi huo Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, alisema ana imani kuwa chama chake kitafanya vizuri kutokana na rekodi nzuri waliyonayo katika jimbo hilo.

Alisema wanasubiri mchakato wa kura za maoni ndani ya chama chao na baada ya mgombea atakayepeperusha bendera ya chama kufahamika, ndipo watakapokuwa katika nafasi nzuri ya kuweka mikakati ya kukabiliana na nguvu za wapinzani wao, hasa CCM.

“Lakini niweke wazi kuwa mazingira ya Arumeru ni tofauti kidogo na majimbo mengine ambayo tulifanya chaguzi ndogo na kushindwa kama Busanda, Biharamulo, Igunga na Mbeya Vijijini. Hivyo tutajipanga hapa na kuweka mkakati wa kuhakikisha dosari zilizosababisha sisi kushindwa hazijirudii tena,” alisema Mwigamba.

Wakati CHADEMA wakiwa tayari wameanza harakati za kuwania jimbo hilo, kwa upande wa CCM, hali bado ni kimya ingawa kuna taarifa zisizo rasmi kutoka ndani ya chama hicho kuwa baadhi ya makada wake wilayani humo wameshaanza harakati za kumrithi Sumari.

Majina ya makada wanaotajwa kuwania nafasi ya kupeperusha bendera ya chama hicho ni pamoja na la Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Elishilia Kaaya ambaye pia ni Mjumbe wa NEC ya CCM kupitia Mkoa wa Arusha.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa iwapo Kaaya atagombea atakumbana na upinzani kutoka kwa Sioyi Jeremiah Sumari ambaye ni mtoto wa marehemu Sumari, taarifa ambazo hata hivyo hazikuthibitishwa zinaeleza kuwa tayari mgombea huyo alichukua fomu Jumatatu mchana katika ofisi za CCM wilaya ya Arumeru.

Kada mwingine ni Elirehema Kaaya ambaye anaelezwa kuwa ni mtumishi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza na ambaye pia alipata kugombea nafasi hiyo katika uchaguzi wa mwaka 2010 ndani ya chama na alishindwa katika kura za maoni na Sumari.Mwingine ni Julius Sarakiya.

Katibu wa siasa na uenenzi wa chama hicho Loota Sanare aliimbia Raia Mwema kuwa zoezi la uchukuaji fomu ndani chama hicho lilitarajia kuanza Jumatatu ya Februari 13 hadi Februari 18 na baada ya wanachama wote kurudisha ndipo watakapojua idadi ya waliojitokeza.

“Kwa sasa ni mapema kujua majina ya wanachama wetu wanaotaka kuomba ridhaa ya chama, kwani zoezi la kuchukua fomu ndiyo kwanza limeanza, ila wito wangu kwa wana CCM hasa wa Jimbo la Arumeru Mashariki ni kwamba wajitokeze kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi hiyo ndani ya chama,” alisema.

Wachambuzi wa masuala ya siasa mkoani hapa wanatabiri kuwa uchaguzi huo mdogo utakuwa kati ya chaguzi ngumu hasa kwa vyama vya CCM na CHADEMA ambavyo ndivyo vyenye ushindani mkubwa wa kisiasa nchini na katika jimbo hilo.

 

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi

Toa maoni yako

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.