BAADHI ya viongozi wa CCM ‘wamevaa’ mantiki ya maelezo ya aliyekuwa Rais wa Kenya, Daniel Arap Moi.
Oktoba 22, mwaka 1978, Rais Moi alihutubia mkutano wa hadhara, mjini Nyeri, Mkoa wa Kati na kusisitiza kile kilichoitwa “mtu mmoja, kazi moja.”
Dhana hiyo ya mtu mmoja, kazi moja ni tofauti na mwenendo wetu nchini ambako mtu anakuwa diwani, mbunge na mkuu wa mkoa kwa wakati mmoja.
Moi alihoji akisema: “Iwapo wewe ni mwalimu na wakati huo huo ni diwani, ukitakiwa ukafanye kazi za udiwani siku tatu (mfululizo) wakati wote huo watoto watafundishwa na nani?”
Moi hakuishia hapo, akawashutumu viongozi waandamizi akisema: “Wamekuwa wakiacha makoti yao yakining’inia katika viti vyao ofisini kama ishara ya kuonyesha wako karibu, lakini kumbe yuko maili 20 akifanya magendo.”
Mfano huu wa Moi na hasa mantiki ya kuning’iniza makoti ofisini na kukimbilia kwenye magendo, ni sawa na kinachoendelea CCM.
Tofauti ndogo iliyopo ni kwamba, baadhi ya viongozi wa CCM wamebakisha mwili ofisini badala ya makoti, lakini fikra, maarifa na utashi vipo kwingine.
Wenzao wa Kenya walining’iniza makoti wakiwa kwenye magendo, wao (baadhi nchini) wamejiegesha tu kwenye viti ofisini; huku maarifa na utashi vikilenga manufaa binafsi kisiasa au kibiashara.
Lakini wakati wengine wamejiegesha ofisini, baadhi yao pia wamekimbia ofisini kama Kenya. Wanasahau kuwa wako nje ya ofisi na huko huko kwenye ‘magendo’ wanazozana. Wanazozana nje ya ofisi katika harakati za magendo hadi kuwagutusha waliobaki ofisini.
Sasa katika uwanja wa magendo, fulani anaamini mwenzake anamdhulumu au kumhujumu. Hili si suala la kupuuza. Tutajadili siku nyingine.
Mjadala wa leo ni tofauti ingawa unahusu CCM. Nimewahi kuijadili CCM na umuhimu wa kufanya hivyo haujafikia tamati kwa sababu hiki ni chama tawala.
Lakini leo ‘nimuombe’ Profesa wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Palamagamba Kabudi kuwakumbusha wana-CCM kile alichokisema Rashidi Kawawa, mwaka 1978.
Enzi hizo, akiwa mwandishi wa habari, Desemba 23, 1978, Palamagamba Kabudi alitumwa na mhariri wake wa Gazeti la Mzalendo, kuripoti mahafali ya makada wa CCM, Chuo cha Kivukoni, Dar es Salaam.
Ilikuwa takriban miezi mitano hivi baaada ya kuanzishwa CCM. Katika mahafali yale, mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Shughuli za CCM, Rashidi Kawawa, cheo ambacho kimefutwa ilhali ni muhimu.
Katika shughuli hiyo, Kawawa ilibidi ajibu sehemu ya risala ya wahitimu. Ukurasa wa mbele wa gazeti la Mzalendo siku iliyofuata, Desemba 24, mwaka 1978 lililokuwa likiuzwa senti 70, habari yenye jina la Palamagamba Kabudi ilieleza kwa kina mantiki ya kuboresha CCM.
Kabudi aliandika kuwa viongozi wa CCM na wananchi kwa ujumla walitakiwa kuhakikisha vikao vya shina vinafanyika mara kwa mara.
Lakini si kufanyika tu, bali pia vihudhuriwe na wanachama wote ili kuimarisha zaidi uhai wa chama hicho, kuanzia ngazi ya chini.
Kwa mujibu wa habari hiyo, Kawawa alishauri akisema: “Itakuwa vema kama kila shina litakuwa na orodha ya watu wanaohudhuria vikao vya shina na asiyehudhuria vikao aitwe kuelimishwa kuhusu umuhimu wake.”
Alisisitiza kuwa vikao hivyo vina wadhifa sawa na vikao vya ngazi ya wilaya au mkoa na hata Taifa kwa sababu hapo ndipo unapoanzia uhai wa chama.
Habari ilieleza Kawawa alikuwa akijibu risala ya wahitimu ambao katika mafunzo kwa vitendo, waligundua udhaifu wa matawi na mashina. Kwamba, udhaifu shina na matawi husababisha chama legelege.
Kawawa alisema ili kuhakikisha mikutano ya shina inaheshimika, lazima viongozi waheshimu vikao kwa kuhudhuria ili kutoa mfano mzuri kwa wananchi wa kawaida.
Ilinibidi nifanye upekuzi wa matukio kuhusu CCM ili kujua kwa nini chama hicho kwa sasa kipo katika ‘malumbano’ baina ya viongozi wake wakuu.
Kimsingi, baada ya upekuzi wangu wa matukio mbalimbali ya CCM enzi hizo kikiwa chama halisi cha kizalendo nimetafakari kwa kujiuliza.
Je, chama hicho bado kinaamini kuwa uhai wake ni shina? Je, ni chama chenye wingi wa wanachama wa dhati au wanachama wanaoingia ili kupata uongozi tu?
Je, bado chama hicho kina mashina yenye dira na chimbuko la mijadala ya kisiasa na kimaendeleo? Lakini kubwa zaidi; je, viongozi wakuu wa CCM wanashiriki katika mikutano ya shina wanakoishi? Kama hawashiriki kwa nini? Je ni kwa sababu wao ni ‘wakubwa’, ni vigogo wa kitaifa?
Je, mfumo wa kupokea maoni kutoka shina moja hadi jingine, shina na tawi, tawi kwa tawi umekufa au bado una nguvu?
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete amepata kuhudhuria mkutano wowote wa shina la CCM ‘anakoishi’?
Vipi kuhusu Mzee Pius Msekwa, Yusuf Makamba au John Chiligati? Wanajadiliana na wana-CCM wenzao kwenye shina wanakoishi au wao ni watu wa ofisini Lumumba?
Wanashiriki mijadala ya chama ngazi ya shina na wananchi au wanachama wa kawaida? Kama hawashiriki, mfumo wa shina unaelekeza adhabu gani kwao? Je, kushiriki au kutoshiriki vikao vya shina kunaimarisha CCM?
Je, kama kiongozi yeyote wa kitaifa hashiriki vikao vya shina mtaani anakoishi, kuna utaratibu gani bora zaidi kwake kukutana na wanachama wa kawaida kujua wanachofikiri?
Haya ndiyo maswali niliyoibua baada ya kusoma wiki iliyopita habari iliyoandikwa na Palamagamba Kabudi, akinukuu alichokisema Mzee Kawawa, mwaka 1978.
Shina ndiyo chombo mtetezi nambari moja wa chama. Shina ndiyo lenye taarifa za wakazi wanaotaraji kuwa wagombea uongozi.
Shina si chombo cha kuimarisha nyakati za uchaguzi pekee. Utetezi wa chama si shughuli ya Mkuu wa Kitendo cha Propaganda pekee, ofisi ndogo za CCM Lumumba Dar es Salaam.
Leo hii viongozi wanunuzi wa kura wanaamini hawana sababu ya kushiriki shughuli za kisiasa kwenye shina la chama na wengine wanashindwa hata kuhudhuria vikao vya Bunge, itakuwa vikao vya shina la CCM?
Tafakari, ni wabunge wangapi wa CCM wanaohudhuria vikao vya shina na kuwaheshimu, kuwasilikiza na kushauriana na viongozi au wanachama wenzao?
Viongozi wakuu wa CCM hawaamini tena katika siasa za shina, wamewekeza katika nguvu ya fedha. Lakini pia hata kwenye maeneo ambayo viongozi wa CCM wanakutana katika vikao vya shina, uzito wa vikao husika umehujumiwa.
Katika maelezo yake, mwaka 1978, Mzee Kawawa anasema ni muhimu viongozi wakuu kuhudhuria mikutano kwenye shina wanakoishi.
Kwa kuzingatia mtazamo huo wa Kawawa, tafakari ni kwa nini CCM ishindwe kuweka masharti kuwa moja ya vigezo kuwania uongozi ni mahudhurio na ushiriki katika vikao vya shina?
Kwa ujumla ukitafuta majibu ya maswali hayo yote utabaini kuwa kama CCM ingekuwa ikitekeleza na kuheshimu vikao au shughuli za shina kama enzi za mwanzo wa uhai wake, kingekuwa chama chenye mfumo bora zaidi Afrika katika kujiratibu.
Lakini hali ni kinyume chake. Mfumo bora wa kutambua na kuvipa uzito vikao vya shina umeshindwa kusimamiwa na kutetewa.
Badala yake, umeibuka mfumo wa kuunda mitandao ya kusaka fedha na kisha uongozi. Kazi moja, mtu mmoja, CCM inaugua laana ya kutelekeza nguzo za uhai wake.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika
Toa maoni yako