WIKI iliyopita nilijaribu kukionya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa makini na hizi tetesi kuhusu vigogo kadhaa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wanaotaka kumeguka kutoka chama chao na kujiunga upinzani.
Kwa wanaoamini katika mfumo unaoruhusu watu kutofautiana kimawazo, kukosoana na kushindana katika kutoa fikra bora zaidi ni lazima wanatambua umuhimu wa kuwa na vyama vya siasa vyenye nguvu na mwelekeo thabiti.
Wakati mawazo yangu ya wiki iliyopita yalisukumwa na umuhimu wa kukiona CHADEMA (na upinzani kwa ujumla) kikiimarika zaidi na kuwa chama bora zaidi – ili kikishika madaraka kiwe makini - leo ninajaribu kusisitiza umuhimu mkubwa zaidi wa kukisaidia CCM kuwa imara zaidi kikiwa madarakani na kitakapokuwa upinzani.
Wafuatiliaji wa majadiliano ya mambo ya siasa katika mitandao na maeneo mengine watakuwa wamebaini chuki ya wazi ya wachangiaji wengi tu dhidi ya chama tawala. Wapo wachangiaji ambao wangelipenda kukiona CCM kikifa na kusahaulika kama vile UNIP cha Zambia, KANU cha Kenya, MCP cha Malawi na vingine kadhaa.
Na zipo sababu kadhaa zinazoweza kuelezea chuki hii ikiwamo ya CCM kukaa sana madarakani kiasi cha kujenga mazoea na kubweteka. Mifano ya kuthibitisha tabia hii ya kubweteka ipo mingi. Unapowaona wagombea ubunge wa chama tawala wanaoshinda uchaguzi kwa hongo wanatelekeza kabisa majukumu yao na wanapolaumiwa na wapigakura wao wanajibu kwa jeuri: “Nilishinda kwa pesa zangu msinisumbue”, ujue hiyo ni jeuri ya kubweteka.
Unapowaona wagombea wa ngazi zote katika chama tawala wakiahidi mambo lukuki, ikiwamo pepo, wakati wakiomba kura na baadaye wakishinda wanageuka kuwabeza wapigakura wao kwa kusema: “maisha bora hayatawafuata vijiweni, lazima mjiajiri,” hiyo ni jeuri ya kubweteka.
Unapowasikia watawala wakiwaambia wananchi wao kwamba: “mpende msipende lazima serikali itanunua ndege ya rais hata kama itabidi muishi kwa kula nyasi,” basi ujue hiyo ni jeuri ya kubweteka. Unapowaona watawala wanaaza kujiuzia mali ya umma, kama ilivyokuwa kwa nyumba za serikali, bila kuzingatia kwa kina athari za uamuzi wao wa kibinafsi kwa taifa zima basi ujue hiyo ni jeuri ya kubweteka.
Unapowaona watawala wanashiriki katika wizi wa kuiibia nchi yao wenyewe kama ule wa EPA, Richmond, IPTL na Radar, basi ujue hiyo ni jeuri ya kubweteka. Unapowasikia watawala wakiwaambia wananchi kwamba “uhuru mnaotumia kuikosoa serikali unatolewa kwenu bure na chama kilicho madarakani,” wakati Katiba ya nchi inasema: “Mamlaka ya serikali itatoka kwa wananchi”, basi ujue hiyo ni jeuri ya kubweteka.
Unapowasikia watawala wakikazana eti kutafuta wawekezaji kutoka nje waje kuwekeza katika kilimo ili kuiokoa nchi na baa la njaa – katika mazingira ambayo serikali inajiingiza katika matumizi yasiyo na umuhimu, yakiwamo ya anasa – ujue hiyo ni jeuri ya kubweteka.
Unapowasikia watawala wakisema ardhi ya Arumeru inayogombewa na wananchi wa Arumeru “kwanza ilikuwa ya walowezi (settlers)’ na si ya wananchi”, basi ujue hiyo ni jeuri ya kubweteka.
Unapoona watawala wanatengeneza mfumo wa kugawana madaraka kama vile wawindaji wagawanavyo vipande vya mnyama kwa ajili ya kwenda kula, huku wakipuuza, kuadhibu na hata ‘kuwamaliza’ wazalendo wenye uwezo kwa vile tu wanatofautiana nao kimawazo, basi ujue hiyo ni jeuri ya kubweteka.
Unapoona watawala hawasumbuki sana kushughulikia matatizo ya msingi ya wananchi kwa kuamini tu kwamba: “watasema watachoka na kisha watalala”, basi ujue hiyo ni jeuri ya kubweteka. Na unapowaona watawala wanawaambia waandishi wa habari kwamba: “Huku Busanda wananchi wenyewe hawana hata luninga; hata huo umeme wenyewe hakuna; hata nyie waandishi mkiripoti umbeya wenu hawa wakulima huku watajulia wapi?” ujue ni jeuri ya kubweteka.
Unapowaona watawala wako tayari kuua raia ili tu kulinda, kutetea na kufurahisha wageni waliowapa rasilimali, maliasili na hata fursa kuu za uchumi kwa makubaliano yenye maslahi binafsi basi ujue hiyo ni jeuri ya kubweteka.
Na haya yote yana maelezo muhimu sana katika mwenendo wa matokeo ya chaguzi za miaka ya hivi karibuni ambazo zimekuwa zikikipunguzia CCM kura nyingi sana. Tokea mwaka 1995 ulipofanyika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi, CCM kiliongeza asilimia 10 ya kura zake kila uchaguzi uliofuata hadi kufikia asilimia 81 mwaka 2005. Baada ya hapo, na hasa baada ya ubwetekaji kuongezeka mara dufu kwa sababu ya ushindi wa Tsunami wa 2005, basi CCM kikatengeneza mazingira ya kushusha kura zake mara dufu pia. Badala ya kupungua kwa asilimia 10 kama zilivyokuwa zikiongezeka, zikapungua kwa asilimia 20.
Huu si ujumbe mzuri kwa CCM hata kidogo. Na kwa hesabu rahisi tu za kuangalia mantiki ni dhahiri kwamba upo uwezekano wa kura za CCM kushuka kutoka asilimia 61 ya mwaka 2010 hadi asilimia 41 mwaka 2015. Hii inatokana na ukweli kwamba wakati tokea uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi kura za CCM zilikuwa zikiongezeka kwa asilimia takriban 10 kila mwaka hadi kufikia asilimia 81, wakati wa kushuka zilishuka ghafla kwa asilimia 20. Kwa wanaCCM wajinga wanaosoma udadisi wangu wanaweza kujawa na upepo na kuanza kupanga namna ya kunishughulikia (kama ilivyo kawaida ya wabwetekaji).
Lakini wanaCCM makini (ambao najua wapo), watachukulia maudhui ya safu hii kama kengele inayowasaidia kuamka kutoka katika usingizi unaowafanya wapoteze imani ya wananchi kila kukicha. Kabla ya mwaka 2010 tuliandika na kujadili sana udhaifu na ubwetekaji wa CCM tukitarajia wangelijirekebisha. Lakini wanaCCM wajinga ‘walijibu mapigo’ kuwabeza waliokuwa wakiwaambia kwamba ‘Mfalme yu uchi’ au ‘wanakata mti walioukalia’.
Hivi karibuni wanaCCM walianzisha mjadala kuhusu masuala ya msingi sana kuhusu siasa za nchi hii. Zikasikika sauti kutoka ndani ya CCM zikisema umefika wakati wa kuruhusu mgombea binafsi. Zikasikika sauti zikisema umefika wakati wa kuhoji matokeo ya urais mahakamani. Zikasikika sauti kutoka CCM zikizungumza lugha ambayo si utamaduni wa chama tawala. Wapo waliohitimisha kwamba CCM sasa wanajiandaa kuwa wapinzani. Hili lilikuwa hitimisho rahisi sana.
Kwa wanaotafakari kwa kina watabaini kuwa endapo CCM kingekuwa kinajiandaa kuwa upinzani jinsi kilivyo, basi kingelikuwa upinzani dhaifu sana. Kwa hatua kiliyofikia, ikiwamo kuparaganyika, kitahitaji mabadiliko ya kimapinduzi, kama jina lake lilivyo, ili kirejeshe imani ya wananchi. Na hakiwezi kuanza kujiandaa kuwa upinzani huku kikiwa dhaifu kiasi hiki. Kinahitaji kianze sasa mageuzi ya kimapinduzi kabla ya uchaguzi wa 2015.
Baada ya mageuzi hatua ya pili ya kimapinduzi ni kuachia madaraka kwa hiari katika uchaguzi ujao kwa kugombea ubunge na udiwani tu bila kuweka mgombea urais. Lengo liwe kukaa pembeni kikiwa upinzani kwa ajili ya kujijenga upya.
Pili, CCM kiruhusu tafakuri ya kina kuhusu misingi yake ya awali na jinsi kinavyoweza kuitafsiri katika dunia ya leo na ikakisaidia kuwa na pa kusimamia. Itakibidi chama kiache tabia ya upopo wa kusema chenyewe ni mnyama na wakati huo huo ni ndege; kwamba mchana chenyewe ni cha kijamaa na usiku kinakuwa cha kibepari. Kisitake kuvizia kura ya kila mtu kwa hila, kiwe wazi kuhusu kinayoyasimamia hata kama yatakinyima kura. Tatu, CCM kiwaombe radhi wakulima na wafanyakazi ambao kiliwatelekeza na kukumbatia wenye fedha kuanzia miaka ya 1990 au la basi kitangaze wazi kwamba kimewatosa (wakulima na wafanyakazi) kwa sababu ya ufukara wao na sasa kinaamini sera za kutetea wenye fedha na ubepari.
Nne, CCM kirekebishe katiba yake na muundo wake ili uendane na mabadiliko makubwa kinayotarajia kuyafanya kukiwezesha kuaminika kwa wananchi na ikiwezekana kushinda tena chaguzi za miaka ya 2020 na kuendelea. Tano, CCM kiamue tu kwa makusudi kuchagua viongozi wapya kabisa katika ngazi zote na chaguzi hizi zifanyike bila mizengwe wala hongo ili watakaopatikana katika ngazi zote wawe ni chaguo la hakika la wanachama.
Sita, endapo kitatangaza kuirejea Siasa ya Ujamaa ambayo msingi wake mkuu ni wakulima na wafanyakazi basi CCM kitangaze wazi kwamba sasa kinarejesha rasilimali na mali za Watanzania ambazo viongozi wamejigawia ama kwa kisingizio cha kubinafsisha au kwa kujiuzia (kama ilivyokuwa kwa nyumba za umma) na kusababisha hasara na ufukara zaidi kwa wananchi wengi.
Saba, endapo kitaamua kuendelea na sera za ubepari basi kiweke wazi ili wakulima, wafanyakazi na fukara wengine watafute chama kinachofanana na hali zao na kinachoweza kutetea maslahi yao. Nane, CCM kitapaswa kuwaomba radhi viongozi wa vyama vyote makini vya upinzani, wanachama na wakosoaji wengine kwa rafu kilizowachezea tokea mfumo wa vyama vingi uanze, zikiwamo za kashfa, vipigo, vifungo na hata wizi wa kura. Tisa, CCM kitalazimika kuomba radhi kwa Watanzania kwa hila, hadaa na ubovu wa sera zilizowatia umasikini zaidi huku zikinufaisha wachache, wakiwamo wageni. Baada ya kumaliza hatua hizi CCM kitakuwa chama bora sana cha upinzani na wananchi wanaweza kuamua kukirejesha madarakani miaka ya usoni.
Maoni ya Wasomaji
Kwa hapa tulipofika, CCM
Kwa hapa tulipofika, CCM haifai kabisa kuwa hata chama cha upinzani! CCM ipumzike kwa amani!