KATIKA sehemu ya kwanza ya makala hii, wiki iliyopita, nilizungumzia maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa chama tawala CCM, na jinsi ambavyo maadhimisho hayo yalikosa mvuto wa hisia za wananchi, kwa sababu ya chama hicho kuwatosa wanyonge na kuwakumbatia matajiri wakiwamo mafisadi.
Nilisema kwamba mwasisi wake, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alikwishakukitahadharisha chama hicho juu ya ‘dhambi’ hiyo yapata miaka 25 iliyopita, lakini waliokiongoza hawakujali; kama ambavyo pia wanaokiongoza hivi sasa hawajali.
Nilisema kwamba licha ya CCM kusheheni maprofesa na wasomi wengi wa hadhi ya Phd, wameshindwa kukiokoa chama hicho kutoka katika hatari ya kupoteza dola.
Nilisema ya kuwa wasomi hao wameamua kujiunga na mitandao ya mafisadi ndani ya chama hicho ili waendelee kuneemeka kifedha, na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kutetea nafasi zao za uongozi.
Katika sehemu ya kwanza ya wiki iliyopita, niliishia katika kuuelezea mtazamo wangu kuhusu wasomi wa nchi masikini za Afrika (Tanzania ikiwamo), nikisema kwamba kwa muda mrefu nimekuwa sina imani nao.
Leo, napenda niundeleze kidogo mjadala kuhusu wasomi wetu katika kujaribu kuelezea ni kwa nini hawa waliomo ndani ya CCM wameshindwa kukinusuru chama hicho na anguko linalokinyemelea.
Kwa mtazamo wangu, wasomi wengi wa nchi masikini za Afrika, badala ya kutumia usomi wao kusaidia kuwakomboa masikini na kuchochea maendeleo ya nchi zao, wamejiunga na watawala na kuunda uswahiba wa kutafuna nchi.
Ninapolitafakari jambo hili, mfano wa haraka unaonijia kichwani mwangu ni wa Zimbabwe. Nilipata kuwa mwangalizi wa Jumuiya ya Madola wa uchaguzi wa Zimbabwe mara mbili (mwaka 1998 na 2000), na safari hizo mbili zilinipa fursa ya kuuelewa usaliti wa wasomi wa nchi hiyo kwa wananchi masikini wa Zimbabwe.
Angalau kipindi hicho ZANU PF ilikuwa na maprofesa zaidi ya kumi, baadhi wakiwa ni wabunge tu lakini wengine wakiwa ni mawaziri.
Hawa, akiwemo Profesa Jonathan Moyo, ungewatarajia kuwa wa kwanza kumfunga paka (Rais Robert Mugabe) kengele, lakini sivyo walivyofanya. Ubinafsi wao na kuyajali matumbo yao tu, uliwafanya kuwa vikaragosi wa hali ya juu wa Rais Mugabe ndani ya ZANU PF na ndani ya serikali ya chama hicho.
Kwa hakika, msomi kama Profesa Moyo aligeuka mwiba mchungu si tu kwa wananchi wa Zimbabwe, lakini pia kwa waandishi wa habari. Sheria zile zilizotia kitanzi uhuru wa vyombo vya habari vya nchi hiyo ni matunda ya msomi huyo.
Yeye na wasomi wenzake ndani ya ZANU PF walihakikisha wanamtetea Rais Mugabe kwa nguvu zao zote; licha ya kujua kwamba ‘lori’ linaloendeshwa na rais huyo linaelekea kuzimu!
Leo hii, kinachoendelea Zimbabwe kinaisikitisha dunia nzima. Kama katika Tanzania asilimia 50 ya watu wetu wanatumia chini ya dola moja kwa siku, na hivyo kuishi chini ya mstari wa umaskini, takwimu za Zimbabwe zinatisha zaidi.
Hiyo ni nchi ambayo asilimia 50 ya watu wake hawana hata hiyo nusu dola ya kutumia kwa siku. Hiyo ni nchi ambayo katika baadhi ya vijiji, wananchi wanaweza kupitisha siku bila kupata hata mlo mmoja.
Wakati huko nyuma nchi hiyo ilikuwa inaongoza Afrika kwa kuuza barani Ulaya nyama iliyosindikwa na wakati huko nyuma ilikuwa inaongoza kwa kuuza nafaka, Zimbabwe ya sasa haina hata kidogo cha kuuza nje ukiachilia mbali alimasi zinazouzwa kimagendo na Rais Mugabe na mkewe Grace Mugabe kupitia watu wa kati akiwemo waziri yule wa Thailand.
Kwa ufupi, Zimbabwe ya sasa ni muflisi; lakini bado Mugabe yupo madarakani pamoja na maprofesa wake ndani ya ZANU PF!
Hivi karibuni ZANU PF kilifanya mkutano wake mkuu huko Bulawayo ambako maprofesa hao, licha ya kushuhudia wenyewe kwa macho yao Mzee Mugabe akisinzia mara kwa mara mkutanoni kwa kudhoofu kiafya na uzee (miaka 87), bado waliridhia matakwa yake ya kugombea tena urais kwenye uchaguzi ujao. Hakuna aliyenyanyuka kumpinga.
Lakini Zimbabwe haikuamka tu asubuhi na kujikuta imefikia kiasi hiki cha uozo. Ni sera za Rais Robert Mugabe ambazo kidogo kidogo ziliifikisha hapo, sera ambazo maprofesa kibao ndani ya ZANU PF walijua wazi kwamba zinaipeleka nchi kuzimu, lakini hawakuzikemea kwa sababu ya kujali matumbo yao tu.
Na ili uelewe vizuri kwamba wasomi wa ZANU PF walikuwa wanaongozwa na ubinafsi tu, mwangalie Profesa Moyo wa sasa. Baada ya Rais Mugabe kumtosa nje ya baraza lake la mawaziri na nje ya ZANU PF, Profesa Moyo aligeuka kuwa mpinzani mkubwa wa Mugabe na mkosoaji wake mkubwa.
Lakini huyo huyo Profesa Moyo baada ya kufanikiwa kuwa mbunge kupitia chama kingine kwenye uchaguzi uliopita, akaanza tena kujipendekeza kwa Mugabe kwa kuandika makala magazetini za kumsifu mzee huyo. Hao ndio wasomi wa Afrika ambao mimi binafsi nimepoteza imani nao!
Ndugu zangu, nimechukua muda mrefu kuelezea hulka ya wasomi wa ZANU PF ya Zimbabwe, kwa sababu inafanana na hulka ya wasomi wetu ndani ya chama tawala CCM na ndani ya serikali yake.
Wasomi hao wamekataa ‘kufa kidogo’ ili kuiokoa CCM yao, na badala yake wameamua kukaa kimya huku mambo yakienda hovyo. Baadhi yao wameamua hata kujiunga na mitandao ya mafisadi ndani ya chama hicho ili kujitajirisha zaidi.
Wasomi hao walikuwapo ndani ya CCM wakati viwanda nchini vikiuzwa, kimoja baada ya kingine, kwa bei poa kiasi cha kuifanya sekta ya viwanda sasa ionekane kama vile haipo kabisa nchini. Kilichopo sasa ni nchi kugeuzwa soko la bidhaa hafifu; hususan za China.
Hali hii imewafanya maelfu kwa maelfu ya vijana wetu Tanzania wanaomaliza vyuo vikuu wakose ajira. Wataajiriwa wapi wakati viwanda nchini vimekwenda na maji?
Wasomi hawa pia walikuwapo ndani ya chama tawala CCM wakati pesa za EPA zikikwapuliwa BOT, lakini hawakukemea au kujitenga na ufisadi huo.
Walikuwapo pia wakati mikataba ya kifisadi kama ile ya IPTL, Richmond na ya madini, nk, ikisainiwa na walikuwapo pia hata wakati wakubwa serikalini wakijiuzia nyumba za serikali wenyewe kwa wenyewe kwa bei poa.
Walikuwepo, lakini hawakukemea. Hawakukemea si ndani ya mikutano mikubwa ya CCM na si ndani ya serikali ambako baadhi yao wanahudhuria vikao vya baraza la mawaziri.
Isitoshe, baadhi ya wasomi hao ni sehemu ya hao wanaoufanya uchaguzi Tanzania uonekane kama vile ni gulio. Wao pia ni sehemu ya hao waliokubuhu kwa kutoa rushwa wakati wa mchakato wa kura za maoni za kutafuta wagombea ubunge wa CCM.
Uovu huo nilioutaja ambao ulitokea wakati wasomi hao wamo ndani ya CCM, na ambao ni sehemu ndogo tu ya uovu mwingi uliotendeka na unaotendeka tangu mafisadi wakiteke chama hicho, ndio ambao umeifanya CCM ipoteze mvuto wake kwa wananchi wengi masikini wa Tanzania.
Na kinachowaponza wasomi hawa wa CCM wasikemee uovu huo, ni kilekile kinachowaponza wasomi wa Zimbabwe; yaani uroho wa kupindukia wa madaraka unaombatana na fursa kemkem za kutajirika haraka kwa njia za mikato.
Kwa hiyo, tunapoingalia CCM hii yenye umri wa miaka 35, tunakiangalia chama kinachochungulia kaburi, chama ambacho hata wasomi wake wameshindwa kukiokoa.
Viongozi wa chama hiki na wale wa serikali yake wanaishi dunia tofauti kabisa na ile wanayoishi Watanzania masikini wanaowaongoza.
Wakati dunia yao ni ya kutajirika na kutajirika zaidi, dunia ya wanaowaongoza ni ya kuwa masikini na masikini zaidi.
Zama za Nyerere viongozi walikuwa wanajaribu kuishi, angalau kidogo, maisha ya wananchi. Si sasa. Sasa kila upande na dunia yake.
Na kiasi dunia hizo mbili zinavyogongana, ndivyo pia siku za CCM kuwa chama tawala zinavyokaribia mwisho; maana itafika mahali wananchi watatumia vyema kura zao na kujiondoa kwenye ‘lori’ linalowapeleka kuzimu!
Inaendelea
Maoni ya Wasomaji
Thank you very much Mr
Thank you very much Mr.Mbwambo for your article which has added an understanding to my brain.