PAMBANO la kukata na shoka kati ya Edward Lowassa na Chama cha Mapinduzi (CCM) limekuwa linaahirishwa kila wakati. Hili ni pambano ambalo kila linapotangazwa, Taifa husimama kwa muda na watu kuahirisha shughuli zao ili kulishuhudia.
Mwisho wa wiki iliyopita kulikuwa na dalili kuwa pambano hili lingefanyika. Edward Lowassa mwenyewe alipuliza kipenga huko Mto wa Mbu pale aliposema tatizo kubwa la CCM ni uongozi na udhaifu wa watendaji. Akasisitiza kuwa pamoja na madhaifu hayo, bado anaipenda CCM na hana mpango wa kuhama. Katibu Mkuu wa CCM Wilson Mukama akajibu haraka kuwa Lowassa anajidhalilisha kutamka maneno hayo nje ya vikao; na kwamba ni bora ashughulikie matatizo ya jimbo lake kuliko yale ya CCM.
Inafurahisha katika ulimwengu wa sasa kwamba bado tuna watu wanaoamini kuwa ukweli fulani unaweza kubadilika ukisemewa ndani ya vikao kuliko ukisemwa hadharani! Kwa hapa, Lowassa amefunga goli la kwanza katika dakika ya kwanza maana aliyemjibu ni mtendaji mkuu wa CCM na Lowassa amesema CCM ina shida ya uongozi na utendaji.
Kama kawaida yake, Nape Nnauye, Katibu Mwenezi (Mpiga debe mkuu) wa CCM akajitupa uwanjani kwa kuwahakikishia Watanzania kuwa kuna agenda nzito mezani Dodoma na kuwa vikao vikikamilika, mbivu na mbichi zitajulikana. Kama kawaida, habari kemkem za kuvuja toka ndani ya vikao zikaanikiza kuwa sasa basi, Edward Lowassa na CCM wamefikia mwisho.
Hadi naandika makala hii, hakuna dalili zozote za kufanyika kwa pambano hilo na agenda kuu iliyo mezani katika vkao hivyo ni semina juu ya katiba mpya. Haielekei kuwa CCM ina mpango wa karibuni wa kushughulikia suala la Edward Lowassa.
Pamoja na kuahirishwa mara kwa mara kwa pambano hili, mambo kadhaa ya msingi yanazidi kujitokeza. Kwanza, sasa ni wazi kuwa wote CCM na Edward Lowassa hawako salama. Wote wawili wanajuana udhaifu na kilichobaki ni suala la “anza wewe” kupiga, mimi nitajibu. Mvutano wa namna hii kimchezo ni dalili ya wapambanaji kulingana uwezo. Tuhame kwenye lugha ya picha, tuseme kwa uwazi zaidi.
CCM inakubali kuwa Edward Lowassa ni mchafu, hafai, ni gamba na amekichafua chama. Wilson Mukama alipata kazi aliyo nayo hivi sasa, kwa kuandika na kuthibitisha hivyo katika ripoti yake kwa chama bila kumung’unya maneno. Alisisitiza kuwa chama kimekosa mvuto na kupoteza kura nyingi kwa sababu ya kuwakumbatia mafisadi wa Richmond, Dowans na EPA. Hakuna analoweza kufanya Edward Lowassa mbele ya CCM kujisafisha na kuaminika tena.
Anao wafuasi wengi ndani ya chama lakini kwa kadri siku zinavyosonga mbele, ama wanakata tamaa na kujiunga na makundi mengine ya maslahi, au watawala wanawaondoa katika mfumo au kuwapa majukumu mapya kwa gharama ya kumkana Lowassa.
Hata kama watawala wanaongozwa na woga, lakini hatua zao zinaelekea kulipa. Iwe uteuzi wa mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na teuzi nyinginezo, sifa ya awali isiyo rasmi lakini inayozingatiwa na wanaoteua, ni kuwa mpinzani wa Edward Lowassa. Watu wamechunguzwa, wamelishwa viapo na kukaguliwa kama wana harufu ya Lowassa katika mavazi yao na nyendo zao. Woga ni adui mkubwa wa utawala bora!
Kwa kumtosa Edward Lowassa CCM inakubali na kujipambanua kuwa ni chafu. Si hoja imechafuliwa na nani bali kinachoonekana ni uchafu na kupoteza sura na urembo wake wa awali. Wana CCM wanaokimbia na kujiunga na vyama vingine, hawafanyi hivyo kumkimbia Lowassa, wanaikimbia CCM na uchafu wake.
Yanayoonekana hadharani na kuudhi wanachama wake wengi, ni machache sana kuliko yale anayoyajua Edward Lowassa. Yawezekana hii ndiyo sababu kubwa ya kigugumizi cha CCM kumchukulia hatua Edward Lowassa. Kubaki naye ni tatizo, kumfukuza ni tatizo, na akiondoka mwenyewe ni tatizo pia.
Je, nini kifanyike ili kuachana kwa Lowassa na CCM kuwe na heri kwa wote? CCM ikimfukuza atajibu mapigo yanayoumiza; akibaki ndani ya CCM hataaminika kwa yeyote na CCM nayo haitaaminika mbele ya umma. Akiondoka mwenyewe, CCM itamwita majina mabaya kama inavyofanya kwa wanaoondoka. Kimsingi kifo cha Lowassa ni nafuu kwa CCM na kifo cha CCM ni sherehe kwa Lowassa, namaanisha kifo cha kisiasa.
Wapo wanaosema Edward Lowassa sasa ashauriwe au aamue kustaafu siasa na kukaa nyumbani kwake kama wastaafu wenzake. Nimewasikia watu walio karibu na “wenye chama” wakidai CCM iko tayari kumwacha apumzike na kufaidi matunda ya “jasho” lake. Mmoja amekwenda mbele zaidi kwa kudai kuwa hati ya makubaliano (MoU) inaweza kuandaliwa na kusainiwa ili kulinda pande zote mbili. Niliposikia pendekezo hili nimeogopa sana na kuhisi hatuna uongozi kama unaweza kumwogopa mtu binafsi kiasi hicho!
Kwa upande wake Edward Lowassa, atakuwa mjinga kuingia katika mtego huo. Ni afadhali CCM na serikali yake wakasema mambo yote wanayoyajua kuhusu Lowassa, hata bila ya yeye kutaja anayoyajua kuhusu CCM na serikali yake. Ukweli wa CCM na serikali juu ya Lowassa ni afya na faida kwa Lowassa kuliko ukweli wa Lowassa kuhusu CCM na serikali yake.
Kwa vyovyote iwavyo, kuna jambo kubwa kati ya miamba hii yaani CCM na Lowassa, na kwa kadri muda unavyosonga mbele bila kutanzua jambo hilo, tunaweza kujikuta tunatafuta wapatanishi wa kimataifa.
Lakini pia wapo wanaodai, tena kwa nguvu kuwa Edward Lowassa aeleze anachojua hadharani (siyo kwenye vikao) ili Watanzania wamjue vizuri alivyo mchafu au msafi. Uamuzi wa yeye kujiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu aliufanya hadharani; na ripoti ya Richmond iliyomtuhumu ilisomwa hadharani.
Lowassa anapaswa achukue hatua hii, si kwa sababu anataka kugombea urais au ufalme wa kuongoza Taifa hili, bali kwa sababu Watanzania wana haki ya kujua ni nini kinachosababisha Taifa liteseke kwa mvutano huu wa muda mrefu. Lowassa aeleze ukweli ili kama anapelekwa mahakamani umma uwe unajua ni nini hasa kilitokea. Kama kuna walioshiriki naye katika ufisadi, tuwajue na kuhitimisha imani yetu kwao.
Iwe CCM awe Lowassa, wasipofanya haya niliyoshauri tutarajie moja kubwa. Kwamba kuwekana mateka kunakoendelea kwa muda mrefu kutakuwa na mwisho mbaya. Urafiki wao na kulindana kwa mgongo wa mali za umma hakuwezi kufichwa milele.
Hivi karibuni tumeshuhudia magwiji wa shirika letu la kijasusi wakiumbuana na kuanza kumwaga siri hadharani. Mmoja ametuhumu na kubainisha kwa nini mwenzake aliondolewa katika uongozi wa idara na Baba wa Taifa, mwingine naye akajibu hayo aliyojibu.
Mwingine akamtuhumu mwenzake kwa kuuza nchi na kupokea fedha za aibu, na yeye akajibu kwa kudai kuwa mtuhumu aliiba fedha ya serikali kwa kutumia “kivuli” cha hospitali. Wote sasa mikono imezama katika kisima cha siri nyingi, na mpaka wahitimishe mashindano ya kuumbuana tutajua hata ulemavu ulio ndani ya maungo yao. Walikuwa wapi siku zote? Sasa kila mmoja anahaha kutafuta jukwaa katika televisheni ili “kumpaka” mwenzake.
Mchezo huo ndio unaoelekea kuendekezwa kati ya Lowassa na CCM. Kama aliiba, Lowassa hakuiba fedha za Kikwete, Mukama, Nape wala Msekwa. Ni fedha yetu na tuna haki ya kujua nini kilitokea. Kama CCM ilifaidi wizi huo ilihali Lowassa ameachiwa mzigo peke yake, tunahitaji kujua pia kwa sababu vilivyoibwa na waliokimbia, na hata hivi alivyokutwa navyo Lowassa, vyote ni mali yetu.
CCM si shamba letu la mananasi ya Msata, na serikali siyo kioski chetu cha kuuza “unga” pale Magomeni. Hata kama ni balaa kwa Lowassa kuondoka, ni balaa zaidi kubaki na hasa kama kubaki na kuondoka vinafanyika kwa njia ya kulindana na kutunziana siri za ufisadi.
Maoni ya Wasomaji
Siri ya kulindana kati ya
Siri ya kulindana kati ya Lowassa na CCM(JK)? Naona ipo wala siyo siri tena, ila ni bomu linalongojea kulipuka wakati wowote katika uhai wa jammii ya kizazi hiki kilichopo.Kama yale mabomu ya Mbagala na Gongolamboto jijinni Dar-es-Salaam.
Ikumbukwe wazi kuwa Lowassa alishasema hakuna alilolifanya katika sakata ya Richmond ambalo Raisi JK halijui. na kwa bahati nzuri Ikulu ilikaa kimya hadi sasa kukataa au kukubali hoja ya Lowassa.NAPE ALIFUNGA MUDOMO. NEC auCC za Ccm ziliziba Masikio
Makatibu wakuu (wezi wakubwa) inasemekana walishamushahuri JK na ndipo akapata la Kumweleza Lowassa atulie( sampuli ya akina JAIRO yalabi) na ndiyo maana hata kesi ya Jairo ni Mzigo kwa JK.
Kamati ya Bunge chini ya DR H MWAKIEMBE ndiyo hasa kiini cha kulindana katika hili Laiti wangesema yote bila kuficha chochote ,Tanzania leo ingekuwa ni nchi ya mfano wa Kuigwa kwa kupambana na ufisadi.Kama fadhira ya ukimya wake Mwakiembe huyoooo anakwea vyeo kila leo na huenda akawa pendekezo la JK kuwa Raisi 2015.
Kweli woga ni sumu ya uongozi katika jamii.NAPE YAJADIRI HAYA TUELEZE WANA TANZANIA.
Lowasa kajiuzulu uwaziri mkuu
Lowasa kajiuzulu uwaziri mkuu ni mbunge tu,Lakini bila kuandika habari za Lowassa ni kukosa manunuzi ya magazeti n.k.Ni ukweli usiopindika kuwa Lowassa ana mvuto na wala hajikombi kwa Chama chake wala watawala.Uwoga wa wabaya wake walifikiri umaharufu wake utaondoka haraka,lakini kila kukicha anapanda chati.Kama ulivyosema Kubaki naye ni tatizo, kumfukuza ni tatizo, na akiondoka mwenyewe ni tatizo pia.Mimi nafikiri ni uoga wa baadhi ya watendaji wakuu katika serikali na chama wanaficha ukweli juu ya Mbunge huyo.