Makala
CCM yawatuhumu wanaohamia CHADEMA
Deus Bugaywa
Mwanza
Toleo la 239
16 May 2012
  • Kigogo asema wanahongwa
  • Wao wasema anaweweseka

WAKATI baadhi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mwanza wanakitaka kiweke mikakati ya kujiimarisha ili kiepuke wimbi linalokikumba la wanachama na viongozi kukimbia uongozi umesema kiko imara na hakiyumbishwi.

Baada ya madiwani wawili wilayani Sengerema na wafuasi wao kukihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo, na kuwapo taarifa kuwa wapo madiwani wengine na wananchama wao walioko mbioni kukihama, baadhi ya wanachama na viongozi wamekuwa wakikitaka chama chao kujifanyia marekebisho makubwa ili kukinusuru.

Hata hivyo, hofu hiyo ya wananchama inaonekana haijafika kwa viongozi wake mkoani hapa ambapo wanaamini kuwa wanachama na viongozi wake wanaohama chama hicho na kujiunga na upinzani wamenunuliwa.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina, ameliamia Raia Mwema kwamba chama chake kiko imara na hakiyumbishwi na wanachama ‘maslahi’ wanaokikimbia chama hicho kwa kuwa bado wana wanachama wengi waadilifu na hakiwezi kupoteza muda kuhangaika na wanachama wasio waaminifu.

“Chama kiko imara wanachama wetu waaminifu wasibabaike. Tuna taarifa kuwa hawa wanaohama wamehongwa mamilioni ya pesa  kila mmoja, sasa mtu wa namna hii ni mchuuzi si mtumishi wa chama hawezi kutumikia wananchi,” alisema.

Alisisitiza kuwa chama kinajengwa na wanachama waaaminifu na walio tayari kukitumikia katika hali zote na hao ndio walio wengi ndani ya CCM na kuwataka wanachama wake wasibabashwe na wimbi hilo la mpito.

“CCM ni chama kikubwa na imara, hakiwezi kubabaishwa na kuhama kwa mwanachama au diwani kujiunga upinzani, kwani wewe unajua tuna madiwani wangapi CCM sasa unafikiri tunaweza kubabaishwa na madiwani wawili au watatu kuhama, wako wengi waliohama na chama kimebaki imara” alisema.

Wakati mwenyekiti huyo wa CCM akitamba hivyo, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Lugata, Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Adrian Tizeba, amesema huko ni kuweweseka kwa chama hicho kwa sababu kimekuwa kama hakijitambui na kinafanya mambo kwa kukurupuka.

“Anaposema tuliohama CCM tumehongwa alikuwapo wakati tunapewa hizo pesa au ana ushahidi? Mimi nimetoka kwa hiari yangu na nimetaja sababu waziwazi kwenye mkutano wa hadhara. Kilichoniondoa huku ni kulea wizi uliokuwa unafanywa katika halmashauri yetu na sasa umeona ripoti ya CAG imewaumbua wanachukuliwa hatua” alisema.

Alisema kwa kuwa sasa amehama chama hicho hataki tena malumbano na wana CCM lakini jambo moja analoweza kusema ni kuwa wananchi wakumbuke kuwa Septemba Mwaka jana walijenga hoja ya kutaka baadhi ya watumishi katika halmashauri wasimamishwe kwa sababu ya ufujaji wa pesa za wananchi lakini chama kikaweka kifua kuwatetea.

“Katika mazingira hayo mimi kama mwakilishi wa wananchi ilikuwa ni vigumu kuendelea kufanya kazi namna hiyo, utajiitaje mwakilishi wa wananchi wakati hawana zahanati, shule, madawati wala maji na pesa zipo zinaliwa na wajanja wachache halafu watu wanawatetea, mimi ninapigania haki na maisha ya wananchi waishi kama binadamu,” alisisitiza.

Kwa upande wake aliyekuwa Diwani wa Kata ya Nyampulukano, Hamisi Magwao, alisema anamshangaa Mabina kuweweseka kwa wao kuondoka kwa kuwa anajua yeye ndiye kwa kiasi kikubwa alikuwa mfadhili wa chama hicho katika kata na wilaya kwa hiyo kuondoka kwake ni lazima chama kibabaike.

“Kwanza CHADEMA ni chama cha watu masikini, kitatoa wapi milioni 40 za kunipa, kama CCM ni mfumo wao huo wa kununua watu ni wao, CHADEMA hakuna ujinga wa namna hiyo, na huyo Mabina ananifahamu mimi vizuri na anajua kuwa mimi si mtu wa kuhongwa, anahangaika tu” alisema.

Alitaja sababu zilizomfanya aondoke katika chama hicho kuwa ni wizi mkubwa uliotamalaki katika halmashauri hiyo ya Sengerema huku chama kikiwa mstari wa mbele kuwakingia kifua waliokuwa wanatafuna mali ya umma.

 “Mimi nilitoka kwa ajili ya wizi. Leo Mungu amesadia hatua zinachukuliwa, sasa hivi huko hapakaliki na mimi udiwani wangu ulikuwa wa wananchi, haukuwa mali yangu mwenyewe. Nilikuwa hapo kwa ajili ya kutetea wananchi, nimefurahi kwa kuwa hatua zinachukuliwa. Ninao ushahidi wa kutosha wa wizi kwenye halmashauri yetu na hata Takukuru au Serikali wakitaka nikawe shahidi mimi niko tayari, nimejitolea kuwa shahidi” alisema Magwao.

Katibu wa CHADEMA wa Mkoa wa Mwanza, Wilson Mshumbushi, akijibu tuhuma zilizoelekezwa kwao na Mabina alisema kuwa anakisikitikia chama hicho kwa sababu ni viongozi wake wamefunikwa na wimbi la mabadiliko linalopita wakiwa usingizini na kwamba wakiamka wanaweza kujikuta wasikokutarajia.

“Watu waeamua kupanda meli isiyokuwa na matundu, wanatubu na wanataka kuwa na mabadiliko katika nchi yao, huko ni kuweweseka kwa CCM, watu wote wanajua sisi hatuna hata baiskeli hapa (Ofisi ya chama Mkoa) tunatembea kwa miguu, tungekuwa tunanunua watu hizo pesa tungepata wapi, na wanachama wengi tu wanakuja kwetu, pesa za kutosha watu wote hao tungepata wapi,” anahoji Mshumbusi.

Anasisitiza kuwa hata kama CHADEMA wangekuwa na uwezo wa pesa namna hiyo wasingeweza kufanya hivyo na badala yake pesa hizo wangeziwekeza katika maendeleo ya wananchi vijijini ili kuchochea maendeleo.

Wakati vyama hivyo vikilumbana namna hiyo kiongozi mmoja wa CCM na mjumbe wa kamati ya siasa ya Mkoa ameliamia gazeti hili kuwa ili chama chao kiweze kundokana na kimbunga kinachokikumba kwa sasa ni lazima kikubali kuyashughulikia matatizo halisi ya wananchi.

“Mimi nikwambie ukweli, watu sasa hivi kila mahali hawakisemi vizuri chama chetu, hili naamini hata wewe unajua, ukiwa kwenye mazungumzo yeyote unaona hasira za wananchi dhidi ya CCM, lakini bahati mbaya viongozi ni wabishi hawataki kuiona hali halisi na hili ndilo litakalotumaliza,” alisema kwa sharti la kutotajwa jina.

Alitoa mfano ya kuwa baada ya kushindwa uchaguzi mdogo wa Kata ya Kirumba badala ya kufanya tathmini ya kisayansi kwa nini wananchi wamewakataa, kuna baadhi ya wajumbe ndani ya kikao wakaanza kuleta habari za majungu na kujadili watu kuwa hao ndio sababu ya wao kushindwa.

Alisema diwani wa kata moja jijini hapa alijikuta katika wakati mgumu kwenye vikao hivyo kwa vile tu mke wake ambaye ni afisa wa polisi alituhumiwa na wana CCM kuwa alikuwa hawapendelei katika maamuzi yake wakati anajua mumewe ni diwani wa CCM.

“Unaona matatizo yetu? Badala ya kikao kile kuanza kujadili hoja za maana, watu wakaanza kujadili jinsi Polisi walivyokuwa hawatupi upendeleo, mtu unajiuliza katika utendaji wa kazi huyo mama afisa wa polisi yeye alitimiza wajibu wake kama kazi zake zinavyotaka yeye siyo mwasiasa, lakini kuna watu walitarajia upendeleo na kwa kuwa tulishindwa wanataka kuifanya hiyo nayo iwe agenda yetu, huku ni kupoteza mwelekeo,” alisema.

Baada ya madiwani hao kutangaza hadharani kuhama CCM taarifa kutoka wilayani Sengerema zinaeleza kuwa wako madiwani wengine wanne wanaotarajiwa kukihama chama hicho katika kipindi kifupi kijacho.

Hata hivyo, kumekuwa na juhudi kubwa inayofanywa na Mkoa kuwashawishi madiwani hao na wafuasi wao wasikihame chama na taarifa toka ndani ya chama hicho wilayani Sengerema zinasema upo wasiwasi mkubwa kwamba wanaweza kuhama hata kama wanapozungumza na viongozi wa CCM wanaonekana kama wamekubaliana.

Wiki jana Raia Mwema lilishuhudia sehemu ya mazungumzo ya diwani mmoja wa Sengerema (jina tunalihifadhi) na Magwao kuhusu mustakabali wa siasa wilayani Sengerema akionekana wazi kutoridhika na hali ya mambo yalivyo.

“Sisi tumetoka CCM kwa sababu tunataka kuwakomboa wananchi, wewe ndugu yangu (anamtaja jina) nakujua ni mtu makini na tumetoka mbali na wewe kwenye harakati zetu, hamia huku, ninajua huko una wakati mgumu, njoo kwenye mapambano ya kweli” alisikia Magwao akimshawishi diwani huyo.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi

Maoni ya Wasomaji

Huyo mabina hawezi kusimamia hicho Chama zaidi ya yeye kujificha na uovu wake aliokuwa ameufanya miaka ya nyuma.na kwa ufupi ametengeneza mtandao wa kidhuluma dhidi ya watu waadilifu huku akibebwa na watu waliojifanya wanamalaka yasiyo nguswa.

Toa maoni yako