Chozi la kiboko wa Mto Katuma

Viboko Katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi wakiwa wanaathirika kutokana na upungufu wa maji katika Mto Katuma.

Hivi karibuni mwandishi wetu, FELIX MWAKYEMBE alikuwa mkoani Katavi kwa kazi za kihabari. Chozi la viboko wa Mto Katuma ni  mfululizo wa makala kuhusu mto huo uliopo mkoani humo.

MTO Katuma, kwa Hifadhi ya Taifa ya Katavi, ni sawa na ilivyo damu kwa binadamu. Kukosekana au kupungua maji kwenye mto huo ni sawa na mwili wa binadamu kupungukiwa au kuishiwa damu.

Hivi ndivyo watalaamu wa ikolojia ya hifadhi hiyo wanavyoelezea umuhimu wa mto huo kwa ustawi wa hifadhi hiyo iliyopo Kusini mwa Mji wa Mpanda mkoani Katavi.

Mwanaikolojia wa Hifadhi ya Katavi, Elisa Manase anasema kuwa kutokana na umuhimu wa mto huo kwa hifadhi hiyo, wanalazimika kupaza sauti ili jamii na taifa kwa ujumla watambue madhara yatokanayo na uharibifu wa mazingira unaofanyika kwenye mto huo.

Hifadhi ya Taifa ya Katavi ni muathirika mkuu inapotokea maji kwenye mto huo yakapungua au kukauka. Hali hiyo imeshuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni, hususani kipindi cha kiangazi ambapo huwepo maji machache yakiunda bwawa dogo eneo la Daraja la Sitalike, jirani na hifadhi hiyo.

Kupungua au kukauka kwa maji kwenye mto huo huathiri maisha ya viumbe hai wanaotegemea maji hayo. Miongoni mwa viumbe hao ni pamoja na viboko, mamba, nyati, samaki, mimea kwenye ardhi oyevu na wadudu.

Huchangia vifo vya viumbe hai hao, huathiri uwezo wao wa kuzaliana ambapo hupungua, hupungukiwa uwezo wa kukabiliana na mifumo ya kimazingira.

Wanyama hao huwa katika hatari zaidi ya kuuawa na majangiri kutokana na kudhoofikana hujitokezamigogoro ya wanadamu na wanyama kwanihulazimikakuingia kwenye makazi ya wanadamu kutafuta chakula.

Miongoni mwa wanyama wenye kuathirika zaidi na kukosekana kwa maji katika Mto Katuma ni viboko ambao wakati wa kiangazi hulazimika kujikusanya katika bwawa dogo linalokuwepo katika daraja la Sitalike.

Katika bwawa hilo dogo la maji, viboko takribani 1,000 huweza kujikusanya wakigombania maji machache yanayokuwepo.

Manase anabainisha kuwa mkusanyiko ule sio mzuri kwa afya za viboko hao kwani huwapunguzia uwezo wao wa kuzaliana, hufikia wakati huanza kulana wao kwa wao, vitoto huawa na huwa katika hatari ya kushambuliwa zaidi na magonjwa pamoja na binadamu.

Inaelezwa zaidi na wataalamu hao kuwa, kukosekana kwa maji katika mto huo huathiri mfumo wa maisha ya viumbe, ardhi oyevu hukauka na mzunguko wa lishe hupotea.

Shughuli za binadamu, hususani kilimo cha umwagiliaji kisicho endelevu, kinatajwa kuwa chanzo kikuu cha kasi ya kupungua maji kwenye mto huo. Wanaikolojia wanatahadharisha kuwa iwapo kilimo hicho hakitadhibitiwa, basi uwezekano ni mkubwa wa mto huo kukauka katika miaka michache ijayo.

Tafiti zinaonyesha kuwa takribani asilimia 70 ya upotevu wa maji husababishwa na miundombonu mibovu ya kilimo hicho cha umwagiliaji.

Shughuli zingine za binadamu zinazofanyika kwenye eneo la juu ya Bonde la Mto Katuma ni pamoja na uchimbaji wa madini ya dhahabu, ufugaji na uvunaji miti.

Kuendelea……….   

One thought on “Chozi la kiboko wa Mto Katuma”

  1. Erick Cleophas says:

    Zifanyike juhudi nyingine kunusuru maisha ya wanyama hao adimu, halafu suala la uhifadhi lisiendeshwe kisiasa linahitaji nguvu ya ziada wale wanaosababishamto huo kukosa maji waondolewe haraka sana eneo hilo. Pia serikali itafute mabozer y maji hata 1000 wamwage kenye mto huo hasa walipo wanyama hao hili kusubilia kudra za mwenyezi mungu kwenye mvua za masika. Jamani huku Rukwa uwa tunapata taarifa juwa kuna waganga wa jadi wana uwezo wa kunyeshesha mvua basi DC, RC, RSO, DSO, organize hiyo wapo watu wanaweza kufanya hivyo labda kwa sababu mnawaona siyo wa maana nao wamekaa kimya, hebu watambueni wanaweza kuleta neema. Huu ni mtizamo wangu watanzania wenzangu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *