Chuo cha Mipango Dodoma na mafanikio ya kitaaluma

MIPANGO ni kati ya nguzo kubwa katika maendeleo. Historia inatueleza kuwa hata nchi zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo zilifikia hali hiyo kutokana na kuwa na mipango mizuri.

Serikali ya awamu ya kwanza chini ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kwa kutambua umuhimu wa mipango katika maendeleo ilianzisha Chuo cha Maendeleo Vijijini (IRDP) Dodoma mwaka 1979.

Elimu ya mipango hutoa fursa kwa walengwa kushiriki katika mchakato wa maendeleo unaolenga katika ustawi wao na kufikia malengo ya maendeleo katika nchi.

Elimu ya mipango ni muhimu pia katika uibuaji wa vipaumbele vya serikali vya Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA) kama ilivyoainishwa kwenye mpango huo.

Elimu ya Mipango imesaidia pia kutoa mchango kwa ajili ya mchakato wa bajeti unaojumuisha uandaaji wa mpango na bajeti yenyewe kupitia wataalamu mahiri walioandaliwa na chuo hasa kwenye serikali za mitaa.

Pamoja na hayo elimu ya Mipango imesaidia kutatua mambo yanayokwamisha maendeleo ya vijijini kupitia tafiti mbalimbali zinazofanywa na wanazuoni hasa katika sekta ya uchumi, mazingira, pamoja na kusaidia kuzishirikisha jamii kutambua masuala muhimu na fursa za  maendeleo kupitia mbinu mbalimbali ikiwemo uwezeshaji.

Mkuu wa chuo hicho Constantine Lifuliro, anasema kihistoria IRDP  kilianzishwa chini ya sheria namba nane ya mwaka 1980 kama kituo muhimu cha taifa cha kutoa mafunzo, kufanya utafiti, na kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu na kitaaluma katika mipango ya maendeleo vijijini.

Chuo hiki kilianza kama sehemu ya ya utekelezaji wa azma ya serikali ya kuimarisha mfumo wa madaraka mikoani ulioanzishwa mwaka 1972. Nia kuu ilikuwa ni kukuza na kuimarisha utaalamu wa upangaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo hususan vijijini.

Uanzishaji wa Chuo cha Mipango Dodoma ni matokeo ya tathmini ya mfumo wa madaraka mikoani uliofanywa na wataalamu mabingwa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwa msaada wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mipango ya Maendeleo (UNDP) na Shirika la Kilimo Duniani (FAO) uliobaini watumishi wengi kushindwa kumudu kazi zao kutokana na kukosa taaluma ya upangaji na usimamizi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo hivyo kushindwa kufikia malengo yaliyowekwa.

IRDP ni kitovu madhubuti cha utaalamu na taaluma katika kutoa mafunzo ya mipango ya maendeleo kwa wadau wa maendeleo ili kupunguza umasikini na kuleta maendeleo endelevu.

Lifuliro anasema chuo chake kililenga pia kuwezesha mchakato wa upangaji na uongozi wa maendeleo nchini kwa kutoa mafunzo, kufanya tafiti na kutoa huduma za ushauri na uelekezi wenye ubora wa hali ya juu kwa lengo la kuziba pengo lililopo la ufahamu na utaalamu kati ya watendaji na wadau mbalimbali wa mipango ya maendeleo.

Ili kufikia lengo hilo chuo kilipewa jukumu la kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi katika  nyanja zote za mipango ya maendeleo vijijini, kufanya utafiti katika mada mbalimbali zinazolenga maendeleo katika jamii, kukusanya takwimu na taarifa zote muhimu za mipango ya maendeleo hususan vijijini na kutoa ushauri na uelekezi katika mipango ya maendeleo.

Mafanikio ya Chuo cha Mipango yanaonekana wazi katika taaluma kama vile  kuongeza idadi ya programu za mafunzo ya muda mrefu kutoka programu  mbili hadi kufikia 10.

Programu zilizopanuliwa na kuongeza wigo wa utoaji elimu ya mipango ni kama vile, cheti katika Mipango ya Maendeleo Vijijini, stashahada katika Mipango ya Maendeleo, shahada ya kwanza katika Mipango ya  Maendeleo ya Mikoa pamoja na shahada ya kwanza katika Mipango na Usimamizi wa Mazingira.

Programu nyingine zilizoongezwa ni shahada ya kwanza katika Mafunzo ya Idadi ya Watu na Mipango ya Maendeleo, shahada ya kwanza katika Maendeleo ya Kifedha na Mipango ya  Uwekezaji, stashahada ya uzamili katika Mipango ya Maendeleo ya Mikoa.

Nyingine ni stashahada ya uzamili katika Mipango ya Mazingira, stashahada ya uzamili katika Mipango na Usimamizi wa Miradi pamoja na stashahada ya uzamili katika Utawala na Maendeleo Endelevu.

Kuhusu mitaala Lifuliro anasema mafunzo kwa programu zote imetayarishwa kwa Competence Based Education and Training Systems ambayo ni bora na inaendana na wakati.

Mafanikio mengine ni ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaojiunga na kuhitimu mafunzo mbalimbali, kukuza uwezo wa rasilimali watu kwa kuendeleza wafanyakazi kitaaluma na kitaalamu, kukamilika kwa ujenzi wa majengo, kuongeza ushirikiano na wabia wa maendeleo hivyo kupata ufadhili kwa miradi na kuanzisha Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza.

"Ili kuhakikisha wanafunzi wetu wanakomaa vya kutosha wanapata nafasi ya kufanya mafunzo kwa vitendo wakati wa mihula ya masomo ikiendelea. Katika mafunzo hayo wanashirikiana na wanajamii kutengeneza andiko linaloelezea hali ya kiuchumi na kijamii katika kijiji,  kata,  au wilaya wanayofanyia mafunzo hayo.

Hatua nyingine ya kimaendeleo iliyofikiwa na chuo ni ongezeko la idadi ya wanafunzi kutoka 22 mwaka 1979 akiwamo mwanamke mmoja tu kilipoanzishwa hadi kufikia 3842 mwaka wa masomo 2011/2012.

Ushauri, Uelekezi, Utafiti na Machapisho

Ili kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi za kitaalamu kuhusu mipango, IRDP kilianzisha kitengo kinachoratibu shughuli za utafiti na utoaji ushauri unaofanywa na wahadhiri ama peke yao au kwa kushirikiana na wataalamu wengine nje ya chuo.

Lengo kuu la kitengo hicho ni kuwezesha chuo kushirikiana na taasisi nyingine kuendesha tafiti, kutoa ushauri na kuandaa machapisho yanayohusu maendeleo vijijini.

Chuo kimefanikiwa kufikia malengo yake ya kuratibu na kusimamia utekelezaji wa sera ya tafiti chuoni na kukiwezesha kuwa na makala za kufundishia pamoja na takwimu zinazofaa kwa mipango ya maendeleo, kusaidia kubuni na kuwezesha wanajumuiya kuibua tafiti zinazofaa chuoni kwa upande wa wahadhiri na wanafunzi.

Mkuu huyo wa chuo anasema kama taasisi ya elimu hawakubaki nyuma katika kuwaendeleza watumishi wa IRDP ili kuwajengea uwezo zaidi wa kutoa taaluma iliyo bora zaidi na unaoendana na wakati kulingana na mabadiliko ya dunia ya mara kwa mara.

Anasema wamejiwekea utaratibu wa kuwaendeleza watumishi kupata mafunzo ya muda mrefu kama vile masomo ya shahada ya uzamivu, shahada ya uzamili, shahada ya kwanza, stashahada na astashahada katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Upanuzi wa Chuo

Kuhusu upanuzi wa chuo kukidhi haja ya idadi ya sasa Lifulilo anafafanua kuwa wamefanikiwa kupanuka kwa kukamilisha ujenzi wa majengo mbalimbali likiwamo bweni la Sumaye, maktaba, uzio kuzunguka chuo, jengo la kwanza la taaluma, jengo la ukumbi wa mikutano  na jengo la pili la taaluma lenye ghorofa saba ambalo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwaka huu.

Jengo hilo la ghorofa saba litakuwa na kumbi za mihadhara nne, vyumba vya madarasa nane, chumba cha kompyuta, ofisi za wahadhiri 50, maktaba ndogo mbili na vyumba vya  mikutano vitatu.

IRDP kimesogeza pia elimu karibu na wadau kwa kuanzisha kituo cha mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza  ili kutimiza malengo ya uanzishwaji wake wa kuanzisha vituo vya mafunzo vya kanda ili kuwasogezea wananchi huduma karibu.

Elimu ya Habari na Mawasiliano

Chuo cha Mipango Dodoma kimepiga hatua katika Elimu ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kufundisha wanafunzi wote wanaodahiliwa katika kozi mbalimbali masomo hayo pamoja na kuwa na maabara za kompyuta tatu zenye jumla ya kompyuta 150 zilizounganishwa kwenye mtandao wa mawasiliano ili kuwawezesha wanafunzi kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu TEHAMA na mengineyo.

Ushirikiano wa Chuo na Wizara, Taasisi na Asasi Mbalimbali

IRDP kinashirikiana  na taasisi na asasi mbalimbali za ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kama vile Ofisi ya Rais Tume ya Mipango, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Nyingine ni Wizara ya Fedha, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Chuo Kikuu cha  Ardhi, Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana, Volunteer Service Organization (VSO), Japan Overseas Cooperation Volunteers (JOCV), Korea International Cooperation Agency (KOICA), Netherlands University Federation for International Cooperation (NUFFIC), Management for Development Foundation (MDF), Netherlands Initiative for Capacity Development in Higher Education (NICHE), Ubalozi wa Uholanzi, Ubalozi wa Ireland, Galillee International  Institute of Management na Chuo Kikuu cha Wageningen.

Pamoja na mafanikio makubwa yaliyofikiwa, pia zipo changamoto kadhaa zinazokikabili chuo hicho kama vile ongezeko kubwa la wahitaji wa mafunzo yanayotolewa na chuo huku wakikosa uwezo wa kukidhi matakwa ya jamii kutokana na ufinyu wa miundo mbinu na rasilimali watu.

Matarajio

Malengo ya baadaye ya chuo cha Mipango Dodoma ni pamoja na kuendelea kuwa kituo madhubuti cha kutoa mafunzo, utafiti, ushauri na kufikisha mipango ya maendeleo kwa jamii ndani na nje ya nchi na kuwa na uwezo wa kutoa mafunzo katika nyanja zote za Mipango ya Maendeleo ili kukidhi mahitaji ya wadau wa maendeleo.

Lengo jingine ni kuanzisha vituo zaidi vya kanda vya mafunzo na habari, kutoa mafunzo hadi kufikia kiwango cha shahada za uzamivu pamoja na kuongeza kasi ya kukamilisha ujenzi wa miundo mbinu ili kuwezesha utoaji wa huduma na majukumu ya Chuo kwa ufanisi pia ni malengo muhimu kwa IRDP.

Katika mwaka wa masomo 2012/2013 Chuo kinatarajia kuanzisha kozi  mpya za shahada ya kwanza katika  Mipango na Usimamizi wa Rasilimali watu pamoja na shahada ya kwanza katika Maendeleo ya Miji na Usimamizi wa Mazingira.>

One thought on “Chuo cha Mipango Dodoma na mafanikio ya kitaaluma”

  1. Godfrey Cyprian says:

     

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *