Chuo chazoa ada bila usajili

Mkuu wa wilaya ya Arumeru Alexander Pastory Mnyeti akiwa anakula kiapo cha utiii mbele ya mkuu wa mkoa wa Arusha.

Mkuu wa wilaya ya Arumeru Alexander Pastory Mnyeti akiwa anakula kiapo cha utiii mbele ya mkuu wa mkoa wa Arusha.

WANAFUNZI zaidi ya 140 wa chuo binafsi cha Rians Institute of Professional  Studies kilichopo eneo la Usa-river wilayani Arumeru, Mkoa wa Arusha wamerudishwa nyumbani baada ya chuo kubainika kutosajiliwa.

Chuo hicho kilikuwa kikitoa kozi za ngazi ya cheti katika masomo ya ualimu wa awali kwa watoto wadogo (chekechea), uandishi wa habari, menejimenti ya huduma za hoteli na uongozaji watalii (tour guide).

Habari zilizopatikana kutoka chuoni hapo na kuthibitishwa na viongozi wa serikali wilayani Arumeru zinaeleza kuwa chuo hicho kilianzishwa mwaka 2013 na raia wa Kenya anayeishi Arusha, Esther Rian.

Tangu mwaka huo wa 2013 hadi mwaka huu, chuo hicho kiliendelea kudahili wanafunzi kwa kozi zilizotajwa bila ya kuwa na usajili wowote na wanafunzi wengi waliojiunga pia walikuwa hawana sifa zinazotakiwa.

“Huyo ama alitumia uhusiano wake na viongozi wa dini hasa wachungaji katika makanisa ya Kilokole kuwashawishi wanafunzi kujiunga na chuo chake akiwalaghai kuwa chuo hicho ni kwa ajili ya wanafunzi kutoka familia maskini,” anadai mmoja wa watumishi wa chuo hicho ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.

Mama huyo anadaiwa kutoza ada kati ya shilingi 350,000 hadi 1,050,000 kwa mwanafunzi mmoja kwa kuzingatia aina ya kozi anayosomea mhusika. Vile vile inadaiwa kwamba chuo hicho hakikuwa na walimu wenye ujuzi unaostahili.

Akizungumza na Raia Mwema, rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho, Isaya Isaack, alisema baada ya kugundua kuwa chuo hicho hakina usajili mapema mwanzoni mwa mwezi Septemba, walikwenda ofisi mbalimbali za serikali kulalamika.

“Tulikwenda kwa mkuu wa wilaya, tulikwenda kwa kamanda wa polisi wa wilaya (OCD) na pia uongozi wa serikali ya mtaa lakini kote huko hatukupata msaada wa maana,” alisema.

Aliongeza kuwa mwishoni mwa wiki hii wanafunzi wote walitangaziwa kuwa chuo kimefungwa na warudi nyumbani na polisi waliwaambia kuwa wafungue kesi ya madai dhidi ya mwenye chuo.

Naye katibu wa wanafunzi hao, Appolo Benjamin, alisema baada ya kugundua kuwa chuo hakina usajili, uongozi uliwaeleza kuwa wangehamishiwa chuo kingine cha King Solomon na baada ya kufanya utafiti waligundua kuwa nacho hakina usajili.

“Kuna wenzetu wamebaki kama 20 hivi kutokana na wazazi au walezi wao kuchelewa kuwatumia nauli za kurudi makwao na wengi ni wa mikoa ya mbali kama Tanga, Mwanza, Singida na mikoa mingine ya kanda ya magharibi na ziwa,” alisema katibu huyo.

Mkuu wa chuo hicho, Abubakar Hamza, alithibitisha chuo hicho kufanya shughuli za kitaaluma bila ya usajili kama sheria za nchi zinavyoelekeza.

 “Mimi nimeteuliwa mwanzoni mwa mwezi huu baada ya principal aliyekuwepo kujiuzulu. Ni ukweli pia chuo hakina usajili baada ya ule wa awali uliokuwa chini Veta kufutwa tangu mwaka 2014 kutokana na mmiliki kushindwa kutekeleza baadhi ya masharti,” alisema.

Mkuu huyo wa chuo aliongeza kuwa kutokana na hali iliyojitokeza hakukuwa na njia mbadala isipokuwa kukifunga chuo hicho kwa muda ili taratibu za usajili zianze kufanyika upya na baadaye waendelee kudahili wanafunzi.

“Kwa sasa mmiliki wa chuo ana matatizo ya kiafya amelazwa kwa muda katika Hospitali ya AICC na madaktari wamesema anahitaji kupumzika hivyo masuala mengine yataamuliwa pale atakapotoka hospitali,” alisema mkuu huyo wa chuo.

Raia Mwema lilifanya jitihada za kuwasiliana na uongozi wa Hospitali ya AICC kuhusu mmiliki huyo lakini hakukuwa na rekodi yoyote inayoonesha  kulikuwa na mgonjwa mwenye jina hilo kwa wiki nzima.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti, alithibitisha chuo hicho kukosa usajili. “Kama serikali tumemwagiza OCD amtafute mmiliki wa chuo haraka sana ili ajibu tuhuma za kuwa na chuo ambacho hakijasajiliwa na pia kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria kujibu tuhuma za kukusanya fedha kutoka kwa wanafunzi kwa njia za udanganyifu,” alisema DC Mnyeti.

Mwisho

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *