Makala
Maruhani hawakupindua Zanzibar
Ahmed Rajab
Toleo la 233
4 Apr 2012

SINA tabia ya kusutana, kubishana au hata kujibizana na wasomaji wa makala zangu wenye kutoa maoni tofauti na yangu. Ninaamini kwamba kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yoyote ayatakayo hasa pale maoni hayo yanapokuwa ni ya ufafanuzi au uchanganuzi wa matukio ya kihistoria.

Kufanya ufafanuzi lakini ni tofauti na kuuelezea ukweli hasa ule ukweli wenye kuhusika na tendo ama vitendo fulani.

Nimekuwa nikisubiri kwa shauku kubwa hitimisho la makala za mwandishi mwenzangu wa Raia MwemaJoseph Mihangwa kumhusu John Okello.  Mfululizo huo wake wa makala zake kuhusu Okello na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ulikuwa ni majibu ya maandiko yangu juu ya mada ya Okello. Kwenye sahafu (safu) ya leo nataka kuyajibu baadhi ya yaliyomo kwenye majibu yake.

Kuna baadhi ya Wazanzibari wanaoona kwamba hakuna faida yoyote kujadili yaliyopita hasa sasa wakati wa mchakato wa Katiba mpya. Lakini wanakosea kwani tunaposonga mbele ni lazima tujue si tu hapa tulipo lakini pia tulikotoka. La sivyo tutajikuta tunajikwaa kila tunapopiga hatua.

Kuna tatizo kubwa kumtathmini Okello na dhima yake katika Mapinduzi ya Zanzibar. Sababu yake ni kuwako kwa simulizi zenye kukinzana kuyahusu Mapinduzi hayo na walioshiriki kwenye matukio yaliyoanzia Januari 12, mwaka 1964.

Migongano ya simulizi hizo yanamfanya mtu afikirie kwamba labda mapinduzi hayo yalifanywa na maruhani na kisha ndipo wanaadamu nao wakaingia. Ndio maana wengine chambilecho Sheikh Thabit Kombo, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Afro-Shirazi Party (ASP), wanaifikiria historia ya Zanzibar yote kuwa ni uongo mtupu. 

Lazima niseme hapa kwamba baadhi ya wanaotoa simulizi mbadala huwa hawana nia njema na Zanzibar. Simulizi zao huupotosha ukweli ili ziweze kuwa na mishiko. Mihangwa si miongoni mwao.  Yeye ni mwandishi mahiri mwenye kuandika baada ya kuridhika kuwa amefanya uchunguzi wa kina kuhusu mada inayohusika.

Nimekuwa nikiyafuatilia maandishi yake kuhusu Zanzibar kwa muda mrefu na kwa maoni yangu huyu ni mwandishi mwenye kutupenda laisa kiasi sisi wazawa wa Zanzibar. 

Lakini kwa vile yeye si mzaliwa wa Zanzibar na wala hajakuwako Visiwani (hasa Unguja) wakati wa Mapinduzi kwa kiwango kikubwa amekuwa akiwategemea wengine kwa masimulizi yake.  Pingine hao ndio waliompotosha.

Sitothubutu kusema kwamba ubara wake umeugubika utaalamu wake kwa sababu hakuteleza kuyaeleza ya Zanzibar tu kama alivyomuelezea Othman Sharif kuwa alikuwa Mkomunisti wakati bwana huyo akijulikana kwa chuki zake dhidi ya wenye siasa za mrengo wa kushoto.

Mihangwa ameteleza kwa mengine pia.  Kwa mfano, amemuelezea Idi Amin kuwa ni Mlangi, mtu wa kabila la Lango, ilhali tunajua kwamba alikuwa Mnubi wa kabila la Kakwa.

Tukiliacha hili la Okello, ambalo hakika Mihangwa halielewi, maandishi yake mengine kuhusu Zanzibar hayakirihishi kama ya wenzake wengi wa Bara. Mara kadha wa kadha kabla ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa huko Zanzibar alikuwa akiwavua nguo watawala wa Visiwani kwa kufuata kisiri siri sera za kibaguzi zilizopitishwa na Mkutano Mkuu wa ASP mwaka 1973 kule Pemba.

Kwa kiwango Fulani Mihangwa amesaidia kuwaelimisha Wabara wenzake kuhusu mgongano wa maneno na vitendo vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Juu ya hayo lazima tumkumbushe Mihangwa kwamba Che Guevara, mzawa wa Argentina, hakwenda Cuba kama mfanyakazi mhamiaji kama alivyokuwa Okello.   Che alikuwa msomi aliyeshirikiana na akina Fidel Castro, Raul Castro, Camilo Cianfuegos na Wacuba wengine waliokuwa uhamishoni kwenda Cuba kwa dhamira thabiti ya kufanya Mapinduzi ya kuikomboa nchi hiyo kutokana na udikteta wa Batista.

Wala Che hakuwahi kujaribu kudai na kupora haki ya kutawala na uongozi kama alivyofanya Okello  Zanzibar. Wacuba walimtunuku Che nyadhifa za uongozi  kwenye serikali yao mpya kwa ridhaa yao na kwa heshima kubwa. Walimfanyia hayo kwa vile walitambua mchango wake adhimu kwenye Mapinduzi yao.

Kiashiria kingine cha mapenzi ya Wacuba kwa Che ni pale Wacuba walipokwenda Bolivia alikouawa Che na kulisaka kaburi lake na kisha kuirejesha Cuba maiti yake kwa mazishi ya kitaifa.  Kumfananisha Che na Okello ni kumtukana Che bila ya kiasi.

Okello alionyesha chuki kubwa kwa Wazanzibari na kujisifu kwa kuwaua wengi mbali na kujaribu kupora hatamu za utawala kutoka viongozi wa ASP. Ukweli ni kwamba Okello anafaa kulinganishwa na jamaa yake Joseph Kony wa Lords Resistance Army ya kule Uganda na sio kumweka pamoja na Major Ernesto ‘Che’ Guevara.

Laiti Okello angalikuwa hai basi yakini angelijiunga na LRA kwani ni muumini wa dini ya Ukristo uchwara wa kuendesha mauaji ya kikatili sawa na mhalifu Kony.

Okello mwenyewe alizidi kuipotosha historia pale alipolalama kuwa Waafrika wa Zanzibar wamemfukuza baada ya yeye kwenda Visiwani kuwasaidia kuwashinda Waarabu waliokuwa wakiwachinja. Hapo ndipo tatizo linapoanza na hicho ndicho kielelezo au kiashirio cha uzushi unaobatizwa kuwa ‘historia ya nyumbani’.

Kwenye makala yake ya mwisho juu ya kadhia ya Okello, Mihangwa amemalizia kwa kuibua maswali muhimu kuhusu uhasama mkubwa uliojitokeza upande wa baadhi ya wakuu wa ASP dhidi ya Makomredi, yaani wafuasi wa Abdulrahman Babu na chama cha Umma Party.

Hii ni mada nzito lakini lazima tuigusie. Hali ya kutoaminiana kati ya Makomredi na wakereketwa wa ASP imekuwepo wakati wote chini kwa chini tangu kilipoundwa chama cha Umma Party mwaka 1963.

Juu ya kuwepo hali hiyo ilibidi pia wakati ule pawepo na aina ya ushirikiano kati yao katika kukabiliana na wapinzani wao yaani vyama vya Zanzibar Nationalist Party na Zanzibar and Pemba Peoples’ Party.

Haja hiyo ndiyo iliyopelekea pawepo umoja uliovishirikisha vyama vya ASP na Umma, vyama vya wafanyakazi pamoja na Jumuiya ya Wanafunzi.

Kiini cha kuwepo hali hiyo ya kutoaminiana ni ule msimamo wa itikadi ya kikabila wa takriban viongozi wote wa ASP wa kuwaepuka kisiasa Wazanzibari wenye asili ya kiarabu sembuse waliotokana na damu ya Hizbu. Mtazamo huu wa aina ya ‘kikaburu’ ndio uliokuwa msimamo na unaendelea hivyo hadi leo kwa upande wa wahafidhina wa iliyokuwa ASP.

Wabara wasioitakia kheri Zanzibar wamekuwa wakiipalilia moto hali hii iliwaweze kuidhibiti Zanzibar kwa maslahi yao. Kwa hiyo dhana ya Umma Party ya kuyasuka Mapinduzi ili yawe na mtazamo wa kitabaka pekee badala ya ‘ugozi’ (ubaguzi wa kikabila na wa rangi) ilisambaratishwa muda wote tangu kuanzia miaka ya mwanzo ya mwongo wa 1960 na akina Othman Sharif, Jamal Ramadhan Nasib na Mdungi Usi.

Baadaye usambaratishaji huo uliendelezwa na wanapinduzi kina Seif Bakari, Abdalla Said Natepe na kaumu yote ya ile ijulikanayo kama ‘Kamati ya Watu 14.’ Hao ndio waliomshinikiza Sheikh Karume kutowashirikisha Makomredi kwenye uongozi wa nchi.

Siku zote walikuwa wakimtisha Mzee Karume kuwa Makomredi walikuwa na njama na jamaa zao Wakiarabu za kuutokomeza utawala wa Waafrika. Hatimaye walifaulu pale Karume alipowatimua kutoka kwenye serikali kina Badawi Qullateinna Ali Sultan na kubwa lao Babu kudondoshwa na Julius Nyerere.

Kuna siku ambapo Brigadia Yusuf Himidi aliwasikitia baadhi ya wafuasi wa Umma Party waliokuwa naye kwa kuwaambia: “Eh jamaa fitna nyingi zimepita kutugombanisha.” Hakumtaja mtu lakini ilikuwa wazi kwamba mafatani walikuwa baadhi ya wahafidhina wa ASP.

Tatizo kubwa la Zanzibar ni kwa Wazanzibari kukubali kuhadaiwa na wanasiasa uchwara kuendelea kuwa wafungwa wa historia ya kisiasa iliyoigawa jamii katika makundi ya kikabila na kinasaba.  

Jukumu linalotukabili sasa ni namna ya kutafuta njia za kuuyayusha urathi huu muovu unaoigawa jamii ya Wazanzibari na unaoutia sumu ufahamu au utambuzi wa pamoja wa Wazanzibari.

Okello alifurushwa Zanzibar kwa sababu alikuwa akileta matatizo. Alikuwa ni adha lakini hakuwa kitisho cha kisiasa. Angelikuwa ni  kitisho cha kisiasa basi isingekuwa rahisi kumng’oa nchini kama alivyotolewa.

Wala si peke yake kati ya wageni waliokuwa wakifanya fujo aliyefukuzwa Zanzibar. Mwengine alikuwa Engine kutoka Kenya.  Naye pia alitimuliwa baada ya kukamatwa huko Maruhubi, kwa amri ya Sheikh Karume, na kikundi cha Makomredi wakiongozwa na Ali Mshangama.

Mwengine aliyekuwa akiitwa Mfarinyaki alikamatwa Chwaka na Komredi Hamed Hilal aliyempeleka gerezani Kiinua Miguu.  Amri za kukamatwa Mfarinyaki aliitoa Yusuf Himidi akiwa mkuu wa jeshi.  Kwa nini hajawahusisha wanajeshi wengine na wapinduzi wa ASP, haijulikani.  Labda Yusuf Himidi alikwishang’amua kwamba wenzake walikosa nidhamu, wakijihusisha zaidi na wizi wa ngawira, wakati Makomredi walikuwa na nidhamu ya hali ya juu.

Hatujui pia kwa nini Karume alihiyari kuwatumia Makomredi kuwatimua akina Okello, Engine na wapinduzi wengine waliokuwa si wenyeji wa Zanzibar.

Yumkini Karume aliamua kuwatumia Makomredi kumfukuza Okello badala ya kuwahusisha akina Said Washoto, Mohamed Abdalla Kaujore, Seif Bakari, Khamis Darwesh na wengine wa Kamati ya Watu 14 kwa sababu alihisi wangelisitasita na pengine kuibua mgogoro. Said Abdallah Natepe aliwahi kuhadithia kwamba waliwahi kumjadili Okello miongoni mwao na hata pakatolewa wazo la kumuua. 

Sheikh Aboud Jumbe amekiri kwenye kitabu chake ‘The Part-nership’ kuwa alikuwa hawajui na hakupata kuwaona baadhi ya waliokuwemo kwenye  Kamati ya Watu 14, wakiwa pamoja na Okello.

Nakiri kwamba ni taabu kuamini ya kuwa Okello aliibuka ghafla Raha Leo kutoka halaiki ya watu waliokuwa wamekusanyika hapo.  Lakini pia tuna uhakika kwamba  Okello hakuwa na uwezo wala heshima anayobandikwa nayo na Mihangwa. 

Hatusemi hivi kwa sababu Okello hakuwa Mzanzibari.  Tunasema hivi kwa sababu huo ni ukweli huku tukikubali kwamba kuna haja ya kuiangalia upya nafasi yake Okello katika mchakato mzima wa maandalizi ya Mapinduzi.

Nimalizie kwa kukumbusha jingine.  Nalo ni kwamba kadhia niliyoieleza ya kutimuliwa Okello kutoka Zanzibar haikuwa ya mwanzo ya kufukuzwa Okello.  Mara ya kwanza alifukuziwa kutoka uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na kusindikizwa hadi Nairobi na Oscar Kambona, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanganyika.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Ahmed Rajab
ahmed@ahmedrajab.com

Maoni ya Wasomaji

Kaka yangu Ahmed,
Ahsante sana kwa maelezo yako ya makala ya kuhusu John Okello.
Mimi sitaki kuingia katika mjadala wa huyo Okello lakini ninataka kueleza ya kile nilichokisikia kwa wale akina wanamapinduzi walioshiriki kikamilifu. Ninachotaka kuzungumzia hapa ni kuwa nimewasikia hao wana mapinduzi wakisema kuwa Okello hasa sie yule tuliyemjua na kumsikia na tuliyepewa habari zake. Nimesikia kuwa Okello hasa aliuliwa katika mapinduzi siku ya tarehe 12/01/1964 Hollis Road - wakati wa majibizano ya risasi kutoka kwa wanamapinduzi waliokuwa wanataka kuteka kituo cha polisi cha Malindi. Polisi kwa kutumia matundu ya ubavuni mwa kituo chao waliwapa taabu sana wana mapinduzi kukiteka kituo chao  na katika kutupiana risasi nimesikia ikampiga huyo Okello na kufa. Kutoka hapo tena huyo Okello anayezungumzwa akachukua yeye jina hili na kuendekeleza hayo mpaka hapo alipofukuzwa.
Nia na madhumuni ni kueleza tu yale niliyoyasikia kama ni kweli au si kweli lakini hivi ndivyo nilivyohadithiwa.
Wasalam 

Kama ulikusudia kumjibu Mihangwa basi hujafaulu! Hoja za Mihangwa zina base ktk facts na zako pia vile vile zina base ktk simulizi! Mapenzi yako kwa Hizbu ndio umeyaweka mbele!

Kinyume na wewe. Nimeridhika sana na jawabu ya kiungwana aliyopewa Mihangwa. Soma kwa utulivu na utatambua katika jawabu kuwa hamna tusi kama unavyofanya wewe kumshutumu muandishi eti kuwa ana mapenzi na hichi au kile. Nakupa ushauri wa bure katika mambo ya kihistoria jikinge kutumia maneno ya aina "facts". Nimevutiwa sana na Muandishi kuitambua jitihada aliyofanya Mihangwa tangu siku za nyuma kuelezea yale yanayolaanika kama "Mara kadha wa kadha kabla ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa huko Zanzibar alikuwa akiwavua nguo watawala wa Visiwani kwa kufuata kisiri siri sera za kibaguzi zilizopitishwa na Mkutano Mkuu wa ASP mwaka 1973 kule Pemba." Lakini hili halimfanyi kuelewa yote ya wa Zenji. Naamini na yeye mwenyewe Mihangwa akiwa muandishi wakutafakari anatambua hili. Nakumbuka miaka ya nyuma nilisoma kuwa  Mwanamapinduzi Said Natepe alinukuliwa akisema historia ya Mapinduzi keshaiandika au ataiandika lakini haitatolewa mpaka yeye atakapoiwaga dunia. Hilo ndio lishatokea. Nimefahamishwa mwanawe yupo hapo Ikulu ya Zanzibar akishughulikia Diaspora/Wahajiruna/Wazenji. Akiulizwa huwenda akatoa muangaza kwa hili. Si semi hayo yake kama yapo ndio "facts" bali kidirisha chengine kitafunguka kuyachungulia ya akina Okello.

Ni kweli kabisa bwana Ahmed maandiko yako yako hayana rekodi za kurejea, kwa watu waliosoma shule na kufundishwa kuandika, ni kwamba huwezi kuwepo mahali pote na hivyo lazima kuwe na facts za kujenga hoja zako, ila hoja zako Ahmed ni kama za muuza kahawa bara barani...ni ngumu kuziamini kwani mtu yeyeote mwenye kutaka sifa hata zisizo zake anaweza kutunga na kusimulia. Na hapa ndo tofauti yetu na watu wa magharibi, unaposimulia kitu fulani lazima kiwe na records (kumbukumbu). Wewe hautupi records kama za Mihangwa!

tunakushukuru sana Mzee Ahmed kwa kutujuvya ukweli kuhusu Zanzibar yetu
Tunachuma mengi kutoka kwenu, inatusaidia kupata ukweli kutoka upande wa pili wa shilingi kwani wakati tunasoma skuli tulikuwa tukisomeshwa hiyo historia tuliyotengenezewa na akina Okelo na wenzake

OK, Okello alikuwa mamluki, lakini kwanini mkamnyima ujira wake? kama mlikuwa mnaweza kwanini hamkupindua wenyewe?? zaidi kwanini mnatumia muda mrefu na nguvu nyingi kumchafua?? mimi nadhani Okello amedhulumiwa jasho lake. Period.

HAPO NDIPO NAPOONA WEAKNESS KUBWA YA HUYO AHMED RAJAB. ANAVYOSEMA KUWA WABARA WASIOITAKIA MEMA ZANZIBAR ANA MAANA GANI? HISTORIA NI HISTORIA INAWEZA KUWA MBAYA AU NZURI LAKINI HUWEZI KUFOJI HISTORIA, ZAIDI YA KUKUBALIANA NAYO. KAMA HAPA USA HUWEZI KUSEMA KUWA USA HAIKUTAWALIWA NA BRITAIN UTAONEKANA TAAHIRA. USIBISHANE KWA SABABU TU YA UZALENDO.....ANGALIA FACTS BWANA RAJAB LA SIVYO UTADHARAULIKA KAMA UNAVYOFANYA SASA. NIMESOMA HISTORIA ILIYOANDIKWA NA MRUSSIA KITABU CHENYEWE KINAITWA RUSSIA IN AFRICA AU AFRICAN IN RUSSIA, MWANDISHI HUYU ALIKUWAPO ZNZ KABLA YA MAPINDUZI NA BAADA YA MAPINDUZI KILA KITU KIMEELEZWA VIZURI. SUALA LA MAPINDUZI YA ZANZIBAR NA JINSI ORGANAIZESHENI YA MAPINDUZI IMEELEZWA VIZURI. DUNIA NZIMA INAELEWA FIELD MARSHALL  OKELLO ( SIDHANI KAMA ALIKUWA NA CHEO HICHO) NDIYO ALIKUWA KIONGOZI WA MAPINDUZI. HAO MNAOWAITA VIONGOZI WENU WA MAPINDUZI WALIKUWA WAMEJIFICHA HUKO DAR ES SALAAM NA WENGINE HUKO ZNZ. PROPAGANDA HAIJENGI SEMENI UKWELI HAMTADHARAULIKA! NI HISTORIA TU.

@ Mandera 
 mamluki wakishafanya kazi ya kupindua basi hupewa walichokubalina na huondoka tizama mfaransa maarufu kwa kuipindua Komoro ni Bob Denard ,hakutaka kuwa rais wa Komoro au nchi nyengine alosaidia kupindua utawala wake.
Tumia ubongo kufikiri na sio jazba

bwana mwamba,
lakini Bob Denard aliozwa mwanamke wa Kikomoro. Nyinyi wazanzibari mmemfanyia nini Okello? Ujira wake mmemnyima, na mchango wake nao muufiche?? Kwanini lakini?? Mtalaaniwa nyinyi kwa dhuluma zenu. The fact kwamba makala chungu nzima zinaandikwa kuhusu Okello, na siyo Natepe, Nyuni,Himidi,Hanga, na wengineo, inadhihirisha kwamba Okello alikuwa na nafasi kubwa na tena ya kipekee ktk mapinduzi ya zanzibar. Okello alikosea kama binadamu yeyote yule, lakini sidhani kama hiyo inahalalisha kunyimwa ujira wake, na historia ya mchango wake ipotoshwe.

Kuna  Ndugu mmoja hapo ameandika " na hapa ndipo napoona Weakness,"
katika maandishi yake  anasema hamuelewe  Ahmed Rajab anaposema  wabara wasioitakia mema Zanzibar, ndugu yangu  soma kiswahili ukifahamu  hapo hakuwachanganya wabara  wote bali wale tu  ambao hawaitakii mema  Zanzibar kwa kujaribu makusudi kuipotosha historia. Kasoro za  Mwandishi Mhangwa alizozitaja  Ahmed  Rajab kama kusema Amin Alikuwa kutoka kabila la Lango ni ushahidi  wa dhahiri kwamba akipiga juujuu tu bila kujua ukweli. Amin alikuwa Mnubi. Mwandishi Rajab pia ametaja kasoro nyengine. Tatizo ni kwamba kuna wengi anaoandika kuhusu Zanzibar kwa hisia na muelekeo wa kisiasa . Siku moja nilikuwa natazama kipindi cha Hamza Kasongo kuhusu Zanzibar na nilisikitika kwamba Kwanza  walioalikwa wote ni kutoka bara na pili alikuwa hajuwi  juu ya historia ya Zanzibar. Vipi muongozaji kipindi utakuwa na kipindi kuhusu  jambo fulani bila ya kuweka balance. Nilitegemea  badala ya kuwa na  wasomi kina Mukandara pekee angekuweko mtu kutoka Zanzibar kwenyewe. Matokeo yak walikuwa wakipiga tu hapa na pale na kupotosha ukweli mbali na kukandia kwa misingi ya  rangi na kadhalika. Msomi mmoja alifika kusema HIZBU ni itikadi wakati HIZBU  ni neno la kiarabu lililomaanisha Naitonalist  na kitambulisho cha Zanzibar Nationalist Party. Siasa za chama hiki zilikuwa ni za kimaendeleo. Kuna wanaoifananisha Hizbu na  usultani  bila kujuwa kwamba Hizbu  na hasa iongozi wakeAli Muhsn ambaye pia alikuwa na damu ya Kimanyema ikipinga usultani. ZNP ikivutiwa sana na siasa za kimapinduzi za  Kiongozi wa Misri jamal Abdul Nasser. Ninapozungumza hili  nataka nikumbushe kwamba Uzalendo ni imani sio rangi. Afrika kusini  kuna wazungu walioungana na waafrika kupambana na sera ya ubaguzi sio kwa sababu nyengine yoyote bali kuamini kuwa binaadamu wote ni sawa na kuna waafrika kina matanzima na Mangope walioungana na wazungu kuwakandamiza waafrika wenzao. Tatizo langu kubwa ni kuwa wengi Bara hawaijuwi vilivyo siasa ya Zanzibar na wanaamini yakusikia au yanayowapendeza tu kwa kuzingatia misingi  ya dini ,rangi na ukabila.bahati mbaya  hili la dini na ukabila sasa limeanza kuuma  hata bara kwenyewe. kwa kumaliza  Mihangwa aliandika alichokifanyia utafiti, lakini utafiti huo ulikuwa wakupotosha ukweli , Alichofanya Mwaandishi Ahmed Rajab ni kumsahihisha. Kazi kwako . Mimi nasema Hongera  Bw Rajab

Bwana Ahmed anajenga hoja kuwa Makomredi walikuwa na ubaguzi wa kirangi na ndiyo inaonekana walikuwa wanampotosha Marehemu Karume. Lakini ukisoma vema katika mistari yake utabaini na yeye ana zambi hiyo hiyo ya ubaguzi wa rangi.
 
Hakueleza chochote kuhusu ama Okello alishiriki kupanga hadi kutekeleza mapinduzi au hakushiriki kabisa. Anakwepa hoja ya msingi ambayo ni je, alishiriki au hakushiriki. Na nafasi yake ni ipi.
 
Kueleza kuwa Okello aliwauwa Wazanzibari hasa wa rangi ya kiarabu tu nadhani ni kupotosha. Wakati wa mapambano kuna makundi mawili. Wakati wa mapinduzi kulikuwa na polisi wa rangi zote ambao walikuwa katika utawala uliokuwa unapinduliwa. Sasa Je, polisi waliokuwa na rangi ya kibara ambao walikuwa kwenye serikali iliyopinduliwa wao hawakuuwawa!!
 
Bwana Ahmed andika fact acha tafsiri yako ambayo nayo inamlengo wa ubaguzi wa rangi.

KATIKA MAKALA ZAKE MIHANGWA ALITOA FACTS NA UCHAMBUZI WA KINA.KATIKA MAKALA YAKO ILIKUA SIMULIZI.NIMATUMAINI YANGU YA KWAMBA MAKALA ZA MIHANGWA UMEWEZA KUPATA SHULE YA KUTOSHA KUHUSU MAPINDUZI.WACHA USHABIKI UKWELI HAUFUTWI KWA KUKANA UKWELI BALI KWA FACTS MAKALA YAKO HAIKUA NA FACTS BALI SIMULIZI.

Bwana Ahmed ni makosa kusema wapo Watanzania waioitakia Zbar kheri. Huu ni mwendelezo wako wa chuki dhidi ya Wabara. Kama yupo mwandishi basi ni mtu na haina mantiki kumwita Mtanzania. Mwandishi anaweza kuwa na mtizamo wake usiowakilisha Utanzania bara
Pili, neno HIZBU pamoja na maana zake limeletwa katika siasa na Wazanzibar hasa alipogombea Dr Salim. Huyu aliitwa HIZBU kutokana na rangi yake. Kama Hizbu maana yake ni 'nationalist' basi neno hilo lisingetumika kumhujumu Salim. Wabara wanagfuata wanachokisema wzbar wanaoujua uhizbu kuliko wao. Na hadi leo HIZBU linabaki kuwa Usultani na Uarabu kama tulivyoaminishwa na Wzbar
Tatu, Mihangwa kutokuwepo Zbar hakumuondolei haki yake ya kuandika kile anachokijua kuhusu Zbar. Ahmed siyo Mcuba na sijui kama anajua ipo wapi. Hii haizuii yeye kuandika kuhusu Castro na He Guevara.
Mihangwa aliwahi kuleta historia nzuri sana ya Wzbar waliopo Afrika ya kusini. Ninauhakika Wzbar asilimia 99 hawakujua hilo pamoja na kuwa wanaishi Zanzibar
Historia ya Zbar itabaki kuwa ya kubabaisha kwasababu hakuna anayeandika vitabu miongoni mwa washiriki. Lau kana tungekuwa na kitabu cha Jumbe, Thabiti Kombo, Mwinyi n.k tungeweza kulinganisha na kupata ukweli. Ni hatari sana Ahmed anaposema huo ni 'ukweli'. Yaani alichosimuliwa yeye ni kweli na walichosimuliwa wengine ni uongo.
Hii ndiyo inayosababisha Ahmed amkane Mohamed Said ambaye naye pia anasema  aliyoyaandika ni ukweli tena wa kufundishia darasani.
Ahmed, andika maoni yako bila kutanguliza mbegu za chuki, utauwa mwandishi mzuri

Bwana Ahmad huwa ninasoma sana makala zako kinachonifurahisha ni uandishi wako, lakini katika suala hili la Okello kidogo Mihangwa ameandika zaidi facts kitu ambacho wewe umeshindwa kukifanya  zaidi ya kutumia misamiati ya vijembe, mimi ni mbara na nimeweza kufanya kazi zanzibar kwa wakati fulani kuna hali ya unafiki na fitna katika jamii ya kizanzibari na kutokubali watu wa mrima kupata sifa hilo ndilo tatizo unalojaribu kupambana nalo. Okello aliongoza mapinduzi hawa wengine walikuwa wafuasi na hata uibuaji wa wa mkutano wa kutaka kumuua Okello ulioubainisha katika makala hii inaonyesha ni jinsi gani unafiki ulioko na fitina, mtu aliyekubali kuhatarisha maisha yake kwa ajili ya zanzibar leo mnataka kumuua, ni ukweli usiofichika kama Okelo asingekuwa lolote wala si chochote ilikuwaje akawa kwenye Radio muda wote. Ahmad kumchafua Okello.

 
Matatizo si jamii ya Kizanzibari, kwa namna hiyo unavyodai, kutokubali watu wa mrima kupata sifa bali dharau ya baadhi ya hao wa Mrima kumpandisha Okello hadhi ambayo tafsiri yake si ingine isipokuwa kuonyesha kuwa Wazanzibari bila ya Okello wasingeweza kufanya Mapinduzi. Bora tungetumia nguvu zetu kuwaomba Bwana Ahmad pamoja na Mihangwa kutusaidia kudai tume kama ile ya Afrika Kusini yaani Truth Commission iliyoongozwa na Desmond Tutu. Bahati mbaya uongozi wa kisiasa hauna maadili yakulingana na ANC ya wakati ule chini ya Mzee Mandela. Kwa hivyo madam tumekosa utafiti rasmi tutaendelea na daraja ya namna hii yakujadiliana. 

Achana na ubaguzi wako wa kumpendlea Sultan!

Toa maoni yako