NCHI inapitia kipindi tete, kipindi ambacho kinashuhudia maswali mengi yakiruka kutoka kila upande huku kukiwa hakuna majibu yanayoeleweka. Halitakuwa kosa kuieleza hali hii kama hali ya mkanganyiko wa kitaifa.
Hivi majuzi niliandika makala katika mlolongo wa safu hii iliyosema kwamba “kupotea tulikopotea ni kupotea kukubwa.” Hali tuliyo nayo leo hainipi sababu ya kudhani kwamba hali yetu ya upotevu imebadilika sana, isipokuwa tu kwamba watu wengi zaidi wametambua kupotea kwetu ama wameamua kukupigia ukunga, kusema kwamba hata wao wameuona upotevu huo.
Hivi majuzi Rais Jakaya Kiwete ameiapisha tume yake aliyoiteua kuratibu maoni ya wananchi kuhusu katiba mpya. Napenda kuwapa pole wote walioteuliwa kwa kubebeshwa mzigo usiobebeka, kwa sababu ambazo nitazieleza leo na katika makala nyingine zijazo.
Kimsingi, ninachokiona mimi ( na wala siko peke yangu katika hili) ni kwamba tuko katika hali ya wananchi kufurukuta wakitaka mabadiliko makubwa yafanyike na yaonekane yakifanyika, lakini wakikabiliana na utawala uliokufa ganzi na kuduwaa, usijue la kufanya. Wananchi wanaumia, wanahenya, wanalalama, wanatafuta majibu, lakini wanakutana na maswali zaidi.
Kila mtu anajua kwamba hali ya maisha kiuchumi imekuwa ngumu sana, hususan katika maisha ya watu wa kawaida ambao wanaathirika vibaya kutokana na gharama za maisha kuzidi kupanda kutokana na bei za mafuta na chakula kupanda kila uchao. Hawaoni jitihada zo zote za serikali yao kupambana na hali hiyo, na badala yake wanashuhudia wakubwa ndani ya serikali wakizidi kujijengea ukwasi usiokuwa na maelezo.
Taratibu, wananchi wameanza kutambua kwamba ufukara wao katika mazingira ya nchi tajiri sana unahusiana moja kwa moja na utajiri mkubwa wa watawala wao ambao wamekuwa wakitumia ofisi zao kujikusanyia mali haramu. Ofisi za serikali sasa zinajulikana kuwa ni mali binafsi za wale waliowekwa mle eti kuwatumikia wananchi. Kila anayepata nafasi hiyo ameiona kama ‘kihamba’ chake binafsi bila kujali maslahi ya nchi.
Jambo moja linajidhihirisha kila mwaka, nalo ni kwamba kila siku uozo wa watawala wetu unazidi kujidhihirisha kwa kiasi kile kile ambacho tunadhihirisha udhaifu wa jamii yetu kukabiliana nao.
Kwa mfano, ofisi ya CAG ina maana gani kama kila mwaka inatoa taarifa inayoonyesha ubadhirifu katika idara za serikali lakini hakuna hatua yo yote inayochukuliwa kutokana na taarifa hizo?
Hakuna shaka kwamba ofisi ya CAG inaendeshwa kwa gharama kubwa na ziara za uchunguzi zinazofanywa na ofisi hiyo ndani na nje ya nchi ni mzigo mkubwa kwa bajeti ya nchi, na gharama hizi hatimaye zinabebwa na mlipa kodi. Kama tunajua kwamba taarifa za CAG hazina umuhimu kwa sababu hakuna dhamira ya kuzifanyia kazi, ni kwa nini ofisi hiyo isifungwe ili, angalau, tupunguze matumizi katika eneo hilo finyu?
Ofisi ya CAG ni kielelezo cha undumilakuwili wa utawala wetu. Sipati neon toshelezi la kuielezea hali hii, hivyo nalazimika kutumia neno la Kiingereza ‘schizophrenia,’ kwa maana ya kuwa na hulka mbili kwa wakati mmoja.
Kwa upande mmoja, tumerithi kutoka kwa wakoloni vyombo vya udhibiti ambavyo kazi yake ni kuhakikisha kwamba fedha za serikali hazitumiki hovyo, na kwamba pale zinapothibitika kutumika hovyo, wahusika wanachukuliwa hatua.
Lakini kwa upuuzi wetu hatuna dhamira ya kuchukua hatua pale inapobidi kwa sababu, kimsingi, ni kama tumekubaliana kwamba kila mtu atajinufaisha na ofisi yake, na kwa hiyo hakuna wa kumsema mwenzie.
Kwa maana hiyo, ingekuwa hatua ya mantiki kuifutilia mbali ofisi ya CAG, lakini hiyo ingetusababishia matatizo na wafadhili ambao wangetusuta kwa kufuta ofisi muhimu kama hiyo.
Hivyo, basi, tunayo ofisi ya CAG ambayo inatoa taarifa za kila mwaka ambazo hazifanyiwi kazi lakini hatuifuti kwa sababu wafadhili watatusuta. Watu wa ajabu!
Kuna jambo ambalo inawezekana watawala wetu wamekosa kuliona kutokana na ulafi wao na uwezo mdogo wa kufikiri unaotokana na ulafi huo. Kuruhusu ofisi ya CAG kutoa taarifa hizi kila mwaka zikionyesha wizi mkubwa wa fedha za wananchi bila kuzichukulia hatua ni njia mojawapo ya kujenga chuki ya wananchi dhidi ya serikali. Serikali inayofikiri ingechagua moja: ama kuzifanyia kazi taarifa hizo, ama kuzipiga marufuku kabisa na kuifuta ofisi ya CAG. Kwa sasa serikali yetu ni ‘schizophrenic.’
Kwangu mimi ni dhahiri kwamba siku wananchi watakapochukua hatua ya kuwaadabisha watawala wao, hoja mojawapo itakayowasukuma itakuwa ni taarifa za CAG zisizofanyiwa kazi.
Wiki iliyopita, bungeni, tumepata ushahidi mwingine kwamba watawala wetu wameshindwa kufanya kazi wanayotakiwa kuifanya. Baadhi yao wamebanwa na wabunge ambao bila shaka wamesukumwa na hasira za wananchi dhidi ya utawala wa ubadhirifu, wizi, kutokujali, na upuuzi. Katika sakata tulilolishuhudia bungeni, mojawapo ya sababu za malumbano yale ni taarifa za ubadhirifu serikalini (kutoka kwa CAG na kwingineko) ambazo serikali inaonekana kutokuwa na uwezo wa kuzishughulikia.
Kusema kweli, sura iliyojitokeza wiki hii iliyopita ni kwamba hatuna serikali inayofanya kazi kama serikali, bali tuna mkusanyiko wa maofisa waliokabidhiwa ofisi mbalimbali ambazo wanazitumia kadri wanavyojua wao na wala hawana udhibiti wa kati (central control).
Kila mmoja anasema anavyotaka, na katika kusema huko tunagundua kwamba katika ofisi yake anatenda anavyotaka pia, na hana ofisa mwandamizi wa kumwelekeza.
Walichotuonyesha watawala wetu wiki iliyopita ni taswira ya mkanganyiko mkubwa na wa kutia wasiwasi kwa ye yote anayethubutu kufikiri kidogo. Nchi hii haijakabiliwa na janga kubwa la ghafla katika miaka ya karibuni. Hatujakabiliwa na vita, mafuriko makubwa wala milipuko mikubwa ya magonjwa ya kutisha. Tuthubutu kujiuliza, je, iwapo tungekabiliwa na mojawapo ya majanga kama hayo, wale tuliowaona na kuwasikia bungeni Dodoma ndio tungewaamini kwamba wangetuongoza kuishinda dharura hiyo? Wale?
Nasema hapana. Tulichokishuhudia ni msamabaratiko ambao haujawahi kutokea katika historia ya nchi hii, serikali iliyoparaganyika, mawaziri wenye kauli za kitoto, wakuu wa serikali wasiokuwa na maamuzi, waziri mkuu kivuli asiyekuwa waziri mkuu, na mkuu wa nchi mtoro.
Hapo juu nimewapa pole wale walioteuliwa katika tume ya kuratibu maoni ya wananchi kuhusu katiba mpya. Hii ni kwa sababu namheshimu sana Joseph Warioba, kama ninavyowaheshimu baadhi ya wajumbe wa tume yake. Ningependa Warioba, ambaye tunajua sote ni mtu makini, afanikiwe nasi tupate manufaa.
Katika wiki zijazo nitaieleza ‘pole’ yangu, lakini nianze tu kwa kusema kwamba, katika kazi ambazo zinaweza kufanywa na tume hiyo katika muda mfupi iliyopewa ni kuangalia nafasi ya waziri mkuu asiye waziri mkuu, anayefanya kazi chini ya mkuu wa nchi asiyekuwapo, na anayewasimamia mawaziri asiowasimamia na wanaofanya shughuli zao binafsi.
Hivi tunaelezaje kwamba inafikia hatua ya wabunge (bila kujali vyama) wanachukua uamuzi wa kufanya jambo ambalo halijawahi kufanyika katika historia yetu, kama kusukuma hoja ya kutokuwa na imani na serikali kwa sababu mawaziri wachache wanaoonekana wameboronga hawataki kuondoka hata pale wanapotakiwa kufanya hivyo na chama chao bungeni, halafu waziri mkuu hana kauli na bosi wake yuko ughaibuni?
Kama nilivyosema kuhusu ofisi ya CAG asiye CAG, hivi kuna haja gani ya kuwa na waziri mkuu asiye waziri mkuu? Niliwahi kuijadili mada hii katika safu hii yapata miaka miwili iliyopita, nikieleza ‘schizophrenia’ ya ofisi hii.
Nilieleza kwamba katika mojawapo ya mazoezi ya kuunda serikali katika miaka ya sabini, Mwalimu Nyerere alimteua Edward Sokoine kuwa waziri mkuu, na akaulizwa na waandishi wa habari kwa nini anamteua waziri mkuu wakati Katiba haitaji ofisi hiyo.
Jibu la Mwalimu lilikuwa ni kwamba, kweli, Katiba haikusema kwamba kutakuwa na waziri mkuu, lakini pia Katiba haikutamka kwamba hakutakuwa na waziri mkuu, na kwamba waziri mkuu ni waziri kama mawaziri wengine isipokuwa yeye yuko kidogo juu ya wenziwe. ‘Schizophrenia.’
Baadaye ikaandikwa kwenye Katiba kwamba tutakuwa na waziri mkuu atakayekuwa kiongozi mkuu wa “shughuli za serikali bungeni” lakini tunashuhudia ukweli kwamba tunaye waziri mkuu asiye waziri mkuu.
Ndiyo maana hawezi kuwaambia mawaziri wanaotoa kauli za kijinga “Shut up!,” hawezi kumwambia bosi wake awaondoe, na imedhihirika kwamba huko maofisini mwao wanafanya wanavyotaka. Waziri anaweza akasema hadharani kwamba naibu wake anafanya mambo bila kumwambia, anakwenda kutafuta wakandarasi wake bila kumpa taarifa, na kadhalika, hali inayodhihirisha ubinafsishaji wa ofisi za serikali yetu.
Maoni ya Wasomaji
Ama kwa hakika hali ni tete.
Ama kwa hakika hali ni tete. Kama nilivyosema awali - ufalme umefitinika! Mparaganyiko huu ni hatari mno. Na kutegemea miujiza itokee katika mazingira haya ni kumdharau Mungu aliyetupa akili tuzitumie vyema. Tunahitaji kuamka sasa. Taifa linaangamia. Naomba nikushukuru tena Generali kwa kipande hiki murua! Wenye masikio watakuwa wamesikia.
Kwa Udhaifu huu wa Kikwete
Kwa Udhaifu huu wa Kikwete ndo Maana Dr Slaa anaamin CCM haikushinda kwa vile haionyeshi nia ya kuongoza bali ni wapangaji wanaojitafutia rizki
Kamwe JK sio Tobwe.Sisi
Kamwe JK sio Tobwe.Sisi tuliozaliwa kabla ya Uhuru
tulishayaona Madudu zaidi ya haya toka awamu ya kwanza. Je,Wezi wa enzi za Vyama vya Ushirika,Mashirika ya Umma na Serikali, Ni nani alijiuzuru? nakukumbushia tu Mheshimiwa Ulimwengu.
kwa mtazamo wa watawala,naona
kwa mtazamo wa watawala,naona wanatulazimisha kutumaini kisichotumainika,ila kinachotia moyo ni kuona kuwa sasa,wananchi wameunana mwanga wa kuwafikisha waendako
Umeandika hoja ya msingi
Umeandika hoja ya msingi zaidi kuhusu hali ambayo taifa letu kwa sasa inakabiliwa nayo. Taswira inayoonekana serikali kwa sasa, inatia mashaka kama kweli dhamira ya kuwakomboa watanzania na umaskini na maisha magumu iko. Serikali imeshindwa kutembea, imesimama sehemu moja na kushudia viongozi wakifanya wanavyotaka kwa maslahi yao wenyewe badala ya wananchi. Ni rahisi kwangu kusema, serikali haitembei, kwani kama ingekuwa inatembea ni wazi tungeona mabadiliko. Kuna mabadiliko gani unaweza kuyategemea kwa chombo ambacho hakiwajibiki? Serikali imeshindwa kuwajibika, na madhara yake ni wananchi kutaabika kwa sababu ambazo zingeweza kukwepeka. Rais Kikwete (binafsi nampenda kama yeye na siyo kama rais) anasemwa sana, sishawsihika kuamini kama yote anayosemwa yeye moja kwa moja na serikali yake kwa maana ya watendaji hayana ukweli! Cha ajabu ni kwamba amekaa kimya na kushindwa kuchukua hatua. Serikali yake inalaumiwa sana, tena bahati mbaya hata wengine wanaoilaumu ni watu kwenye serikali hiyo hiyo yake, lakini ameshindwa kuchukua kufanya maamuzi magumu. Ametuacha wananchi wa Tanzania kuwa na maswali mengi ya kujiuliza kuliko majibu, wapi tunakwenda? Ni aina gani ya upole wa rais Kikwete dhidi ya watu wanaosababisha yeye kuchukiwa na kusema vibaya kiasi hicho?
Kikwete ametolewa mbuzi wa
Kikwete ametolewa mbuzi wa Muhanga ,kila mtu anajuwa toka enzi za Julius Nyerere kama Nchi haiendi mbele kila siku inarudi nyuma.
Nani alievunja mashamba ya mkonge , viwanda vya chuma ,urafiki,kiltex,mwatex,sunguratex ,bora shoes ,Kikwete ?
Viko wapi leo viwanda vyote kule Tanga na Dar,? Nani kauwa Sukita ? Jee kuna Waziri yoyote alijiuzulu kwa kuuwa uchumi wa Tanzania tangu tupate Uhuru ? Kuna mtu yoyote aliejuwa Almasi na Dhahabu iliokuwa ikipatikana wakati wa Mwalimu? TANI NGAPI ZILIPATIKANA KWA MUDA WOTE ALIOKAA MADARAKANI ?
Kikwete pole baba kamba imekatikia pabovu kwa hiyo lawama zote unapewa wewe. Lakini wote hao watajibu jinsi wanavyo kukandia siku ya hukumu ya kweli ikifika.
Tunaweza kuutumia vizuri
Tunaweza kuutumia vizuri wakati uliopita kujifunza na kurekebisha makosa pale tu tunapoona tulikosea! Lakini vile vile tukumbuke kuwa wakati uliopita si mara zote unaweza kutusaidia kujifunza na kurekebisha makosa. Inategemea tunautumiaje wakati uliopita ktk kujijenga kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa kuelewa na kukubali kurekebisha pale tulipokosea na kusonga mbele!!
Suala la nani aliiba mwaka gani na uchumi ulikuwaje enzi zile ndo mambo ambayo tunapaswa tuyafanyie kazi hivi sasa. Si vyema tukabweteka eti kisa mbona mwaka 1965 fulani aliiba na hatukusema au hawakusema kwa hiyo conclusion ni kumwacha mwizi na mbadhirifu aendelee kuitafuna nchi hii kisa eti mbona hata babu yake alikuwa hivyo hivyo!!
Mambo yanabadilika na nyakati sio zile za "kidumu chama cha mapinduzi" au "zidumu fikra sahihi za mwenyekiti!! Hii ni dunia tofauti kabisa na ile ya juzi, fanya ufisadi leo kesho tutakuanika na jina lako tunalihifadhi kwenye notebook zetu hutatudanganya tena!!
Tukubali kufanya mabadiliko ya ki mtazamo vinginevyo mabadiliko yatatukabili sisi wenyewe!! Tusiwe wavivu wa kimawazo na kuona kila kitu ni kudra za mungu..
Sidhani kama mtanzania wa kawaida anahitaji diploma au degree kusoma alama za nyakati!!
The past is the past!! nobody is going to let the past rule our beloved country future!!
Think!!
May God bless Tanzania.
Mimi ningeliona kwamba mambo
Mimi ningeliona kwamba mambo ambayo wananchi wanalalamikia
serikali yanayafanyiwa kazi.Basi utawala hauoni kama kuna matatizo na inaendelea kukaa kimya.Watu wanalalama kuhusu utawala mbaya na hawaoni ufumbuzi wowote.Sasa inakuwa kama watawala wamenyimwa kauli mbele ya watu na Mungu ili mradi waonekane hawafai.Amini usiamini ukatae, udharau Mungu anaweza kuupiga stop utawala wowote hapa duniani kwamba hutatawala hawa watu wangu tena.Inakuwakuwaje watu wanazungumza kwamba hatukuwa tunapigania uhuru wa watu wengi bali wa watu wachache tu? Bahati mbaya viongozi wengi hawajui kwamba Mungu anafuatilia watawala wabovu na ikifika saa ya kuwaondoa hakuna wa kumzuia na anayeshindana na kusudi lake anaumizwa zaidi.Jenerali Ulimwengu katika uandishi wake ameshauri mambo mengi tena na mengine amerudiarudia.Sasa ndiyo tuseme sikio la kufa halisikii dawa.
mi naona umekosea kidogo
mi naona umekosea kidogo ulipoandika SCHIZOPHRENIA ...baada ya kauli ya nyerere KIMSINGI HUKUMUELEWA .... ...alimaanisha kwamba katiba haijamwambia aunde wizara gani na awateue mawaziri gani ......ni kama aliamua kuteua waziri mkuu kama alivyoteua mawaziri wengine but waziri mkuu ni waziri katika wizara inayodeal na mambo yote juu ya wizara zote .......
Kuhusu schizo ...nadhani pia unachanganya na MPD (multiple personality disorder) ..ambayo ni tabia mojawapo tu au sio uti wa mgongo wa ugonjwa wote kwa ujumla ..............
Lakini Schizo hua mara nyingi wanatabia ya ku-blackmail ..manipulatiors .......a sense of high ego etc.... over ambitious ....so check these well ....
OTHERWISE MAKALA YAKO NI NZURI ILA WE KAMA MHARIRI MWAMBIE MIHANGWA A CHANGE MADA TOKA NIKIWA MDOGO ENZI HIZO RAI .....amekua akiandika habari zile zile ila kwa lugha tofauti za KARUME, KATIBA, MAPINDUZI na ukoloni mkongwe.......
Tunapochagua viongozi
Tunapochagua viongozi hovyohovyo lazima tujiandae kuona mambo yakienda hovyohovyo, na hatupaswi tena kulalamika hovyohovyo. Tujilaumu sisi na kujipanga tena upya kwa chaguzi zijazo.