
- Wapendekeza kuanzishwa Baraza la Seneti na Bunge lenye mfumo mpya
- Kikwete apigia debe urais kuhojiwa mahakamani
KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi iliyokutana mjini Dodoma mapema wiki hii imependekeza, pamoja na mambo mengine, kufumuliwa kwa muundo wa sasa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Raia Mwema limeelezwa.
Muundo wa sasa ni wa wabunge wa aina tatu: wa majimboni, vitimaalumu na wanaoteuliwa na Rais kwa mujibu wa madaraka yake ya kikatiba.
Badala yake, yameibuliwa mapendekezo kwamba lianzishwe Baraza la Seneti ambalo litaundwa na wajumbe wa aina mbili; ya kwanza ikiwa ni ya marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar..
Aina nyingine ya wajumbe wawe ni watakaopatikana kwa njia ya kuchaguliwa, wakiwa ni mjumbe mmoja kutoka kila mkoa.
Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika vya gazeti hili vilivyoshiriki vikao vya majadiliano katika Kamati Kuu, mjini Dodoma mwanzoni mwa wiki hii, utaratibu huo wa kuanzishwa kwa Baraza la Seneti unalenga kuwatumia marais wastaafu kwa maslahi ya nchi.
“Tunakoelekea tunaweza kuwa na marais wastaafu wengi iwe kutoka CCM au kutoka vyama vingine vya siasa kama vitaweza kuchaguliwa na wananchi kuingia Ikulu. Busara inaelekeza kwamba marais hawa wastaafu ni vizuri kuwatumia katika kushauri namna ya kuongoza nchi. Hii ndiyo mantiki kubwa ya kupendekeza kuwapo kwa Baraza la Seneti,” kilieleza chanzo chetu cha habari.
Nchi mbalimbali zimekuwa na mabaraza ya maseneta, ikiwamo Marekani, Uingereza na hata Sri-Lanka iliwahi kuwa na Baraza la Seneti. Uzoefu katika nchi hizo unaonyesha kuwa mara nyingi unapokuwapo mfumo wa Baraza la Seneti ni lazima kuwapo na Baraza la Wawakilishi (Bunge) ambalo wajumbe wake hupatikana kwa kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi, tofauti na ilivyo kwa Baraza la Seneti.
Katika baadhi ya nchi, Baraza la Seneti linaundwa na wakongwe na wabobezi katika masuala mbalimbali ya utawala na utumishi wa umma lakini pia wajumbe wengine huteuliwa kuingia kwenye Baraza hilo kutoka katika Bunge au Baraza la Wawakilishi.
Nchini Uingereza, kwa mfano, Baraza la Wawakilishi limekuwa likitambulika kama House of Lords (Bunge la Mabwanyenye) na Bunge la kawaida ambalo wabunge wake huchaguliwa, limekuwa likiitwa House of Commons (Bunge la Makabwela). Marekani pia imekuwa na Baraza la Seneti, sambamba na Baraza la Wawakilishi.
Tofauti ya vyombo hivyo ni kwamba, Baraza la Seneti linategemewa mno katika kutoa misimamo mizito inayokidhi maslahi ya umma kwa kuzingatia kigezo cha uzoefu wa wajumbe wake. Lakini Bunge au Baraza la Wawakilishi jukumu lake ni kuwasilisha maslahi ya wananchi moja kwa moja kutoka katika majimbo.
Kamati Kuu ya CCM pia imependekeza kwamba Katiba mpya ya Jamhuri Muungano wa Tanzania itamke idadi ya wabunge au wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ili kufuta michakato wa kuanzishwa kwa majimbo mapya ya uchaguzi mara kwa mara bila hata baadhi ya majimbo kukidhi vigezo vilivyopata kuanishwa.
Katika suala la vitimaalumu imependekezwa kuwa kila chama kipate wabunge wa vitimaalumu kwa kuzingatia asilimia ya majimbo ya uchaguzi waliyoshinda.
Matokeo ya urais kuhojiwa kortini
Katika kikao hicho, taarifa zaidi zinaeleza kuwa Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti CCM na ndiye aliyekuwa akiongoza vikao vya chama hicho, alikuwa mstari wa mbele kuwashawishi wajumbe kuridhia kwamba, Katiba mpya itambue na kuruhusu mchakato wa kuhoji matokeo ya kura za urais mahakamani.
Azimio hilo pia linatajwa kupitishwa na Kamati Kuu na kusisitizwa kuwa ni lazima uwekwe muda maalumu kwa wanaotaka kuhoji matokeo ya urais mahakamani ili kesi husika ziweze kumalizwa na Mahakama katika muda mfupi
Lakini kwa upande mwingine, gazeti hili limeelezwa kuwa yapo mambo ambayo Kamati Kuu imependekeza yaendelee kuwapo katika Katiba mpya kama yalivyo katika Katiba ya sasa, ikiwa ni pamoja na haki ya kupiga kura na kuwapo kwa mihula ya uongozi wa kuchaguliwa na kwamba, wananchi ndiyo waachwe waamue muhula uwe wa miaka mingapi.
Kwa sasa muhula wa uongozi wa kuchaguliwa ni miaka mitano katika nchi nyingine mihula ya kukaa madarakani inapishana kati ya miaka mine hadi saba.
Tume ya Maadili
Kwa mujibu wa habari hizo, CCM kupitia Kamati Kuu yake imependekeza pia kwamba Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma itambuliwe katika Katiba mpya na kwamba ijengewe mifumo huru ya kufanya kazi bila woga.
Kwa sasa tume hiyo imekuwa ikiripoti kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na imekuwa chini ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utawala Bora kama ilivyo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Utaratibu wa sasa kwa muda mrefu umekuwa ukilalamikiwa kwamba hautoi fursa kwa tume kuwa huru katika kuwashughulikia viongozi wa umma wanaokiuka sheria ya maadili na wengine wamekuwa wakishinikiza kuwapo kwa uwazi wa kisheria katika utendaji kazi wa tume hiyo.
Ni mapendekezo ya CCM
Hata hivyo, hayo na mengine yanatajwa kuwa ni mapendekezo tu ya CCM kama taasisi na chama tawala na kwamba, hayazuii Watanzania kwa ujumla wao kuwa na maoni mengine tofauti.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, CCM kinatarajiwa kuwaelimisha wanachama wake kuhusu masuala ya msingi wanayodhani ni muhimu kuwamo katika Katiba mpya ili kupata uungwaji mkono kutoka kwa umma na hatimaye masuala hayo yawe sehemu ya Katiba mpya.
Kudhibiti mfumuko wa bei
Katika hatua nyingie, jana Jumanne, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM-Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu vimeitaka Serikali kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa muhimu nchini, na hasa chakula.
“Kutokana na kuwapo kwa hali ya kupanda mno kwa bei za bidhaa nchini ambako kunasababishwa na mambo mbalimbali, ikiwamo mavuno duni na kupanda kwa bei za nishati ya mafuta duniani, Halmashauri Kuu imeamua pamoja na Serikali kuendelea kuchukua hatua za muda mrefu na wa kati kukabiliana na tatizo hili, CCM inaiagiza Serikali kuchukua hatua za haraka za muda mfupi ikiwamo kuangalia upya baadhi ya kodi katika vyakula pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika sukari,” alisema Nape naye katika mazungumzo yake hayo na waandishi wa habari mjini Dodoma.
Maoni ya Wasomaji
Wakati mwingi naona ccm
Wakati mwingi naona ccm inafanya maamuzi/mapendekezo ya kiujanja kukwepa hatari inayoweza kuwabana viongozi wake. Swala la Senate ni kweli liko katika nchi nyingi, wajumbe wake ni watu mashuhuri katika maendeleo ya jamiii. Sasa TZ ukiweka marais wastaafu hawa ambao tayari wananchi wanajua wamejilimbikizia mali kutokana na kutumia fedha na rasilimali za taifa, itakuwaje sasa kama siyo mbinu ya kujilinda kwao? Nilitarajia ccm wazungumzie maswala muhimu ya maendeleo kama umeme, barabara, maji, reli, afya, elimu, uwezeshaji wa kimaendeleo wa mikoa mbali mbali, nk. "These people when they meet they enjoy and talk things that does not help the people except for their benefits. Not being an adiition only, what TZian gne benefit from such words from them. It's a shame for a once respected and model country". On matokeo ya uraisi kuhojiwa mahakamani, sioni mantiki ya hoja hii. Napendekeza pia baada ya kipindi cha kufikia 2015 kuisha, na kuanzia hapo raisi akohojiwe mahakamani kuthibitisha kuwa ali"deliver" katika kipindi chake sawa sawa kama alivyoapa mbele ya kadamunasi, ili aweze kuwa "cleared as clean, otherwise he or she should be taken to task. Na hii iingizwe katika katiba mpya. Hii ni kwa sababu tunaona mtu alikuwa hana kitu lakini akipata madaraka ankuwa na utajiri wa kutupa in no time, misnagement of the economy, kutowajibika, na matamko yanayodhalilisha wananchi, kutofuatwa katiba katika maamuzi mbali mbali, and much more. Sijaona faida ya tume ya maadiri. KATIBA MPYA LAZIMA IWE WAZI KATIKA MAMBO MBALI MBALI NA HASA RAIS BAADA YA KUMALIZA NGWE YAKE AKATHIBITSWE NA JOPO LA MAJAJI KAMA ALITIMIZA ALICHOTAKIWA KUKIFANYA KWA AWALI KATIKA MTINDO KAMA ULE WA MSHITAKIWA. AKIONEKANA HAKUTIMIZA MAJUKUMU YAKE BASI ASHITAKIWE KABISA. HII ITAONDOA OPPORTUNITISTS WANOFIKIRI URAIS NI KWENDA KUTANUA NA KUJILIMBIKIZIA MALI.
CCM wamechanganyikiwa. Majuzi
CCM wamechanganyikiwa. Majuzi waliwaondoa maraisi na mawaziri wakuu wastaafu ktk toka kuwa wajumbe wa kamati kuu pamoja na nec. Hiki wanachopendekeza ni upuuzi mtupu. kama raisi anahitaji ushauri wa viongozi wastaafu anaweza kuwaita ikulu na kupata ushauri.
Nadhani lililo muhimu
Nadhani lililo muhimu Tanzania ni kuweka sheria inayoruhusu Rais ashitakiwe baada ya kumaliza muda wake madarakani kama alivunja sheria katika kutekeleza majukumu yake
Nimeshituka sana kuingiza
Nimeshituka sana kuingiza marais wastaafu kwenye seneti. Uongozi wowote ule unaohusu sera katika kuwatumukia wananchi ni sharti utokane na kura za wananchi tu ili kuwafanywa waliochaguliwa kuwajibika moja kwa moja kwa wananchi.
Hii picha wanayotaka cheza ni
Hii picha wanayotaka cheza ni namna ya kujilinda na kuendelea kulipa mzigo taifa ambalo wao wamelifikisha hapa wakati wakiwa madarakani, na sidhani kama ni busara kutumia mawazo ya watu waliosaidia kilihujumu taifa hili
Hivi maana ya kustaafu nini
Hivi maana ya kustaafu nini sasa? Eti Rais amestaafu halafu bado ana majukumu mengine makubwa ya kuongoza nchi.Sasa huko ni kustaafu ni kubadilishiwa majukumu tu. I think this is another type of clinging to power, and a trick to avoid being put accountable by the public.
Habarini za asubuhi ndugu
Habarini za asubuhi ndugu jamaa na marafiki, maoni yetu yanaonesha jinsi sasa serikali yetu ilivyochokwa na ambavyo haiaminiwi na wananchi wake kitu ambacho ni kibaya sana.
Pengine ubaya huu si kwa wananchi ila ni kwa CCM na Serikali yake imetufikisha hapa tulipofika ndiyo maana hata kama ikija na mipango na sera nzuri inaonekana ni yale yale...
Mbona sheria ziko nyingi tena nzuri? Mbona katiba ipo na iko wazi pamoja na udhaifu wake? Lakini mbona kuna watu wanajilimbikizia mali halafu bado hawachukuliwi hatua zozote? Ila wewe kaibe kuku we! Kwahiyo CCM isimtafute mchawi itakataliwa maana inaonesha hata hayo yatakuwa hayana maana.
Hata mimi pamoja na utamu wa hoja na mapendekezo ya CCM juu ya kuundwa upya kwa katiba napata shida kidogo kuamini hilo..na ni kwasababu nilizotoa hapo juu.
Miaka ya nyuma (wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa) wakati ule kuna njaa sana na matatizo chungu nzima lakini bado watu waliishi kwa furaha na kwa kupendanda sana maana waliiamini serikali yao na waliamini kuwa ipo siku itatutoa kwenye shida hizi, lakini si sasa.
Hata hivyo niseme kwamba, tuwape nafasi tuone kama watafanya hayo ili tuwahukumu kutokana na kufanya ama kutofanya kile walichoahidi kwa mbwembwe na madaha. Kwa sasa upande wangu naona sitajitendea haki nikianza kuhukumu pamoja na kwamba kibinaadam napata shida sana kukubali kuwa kutakuwa na mabadiliko kwenye hilo.
CCM na Serikali yake katika hili mmejitahidi sana. Pamoja na kwamba maneno matupu hayavunji mfupa, wakati huo huo mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.
Katika kupanua demokrasia
Katika kupanua demokrasia kweli kuna haja ya kuwa na vyombo kadha. Baraza na seneti lipo nchi nyingi hasa za wenzetu, maseneta huchaguliwa na wananchi wao na siyo mtu au kikundi fulani.
Matatizo yanayoikabili nchi yetu ni kuwa na watumishi wa umma wasiotumikia umma bali wananmtumikia aliye waweka madarakani. Vyeo na viongozi wengi huteuliwa aidha na rais au kikundi fulani mtu aliyewekwa na rais au kundi fulani atakachofanya na anachofanya nikufulahisha kundi lilomweka huku akilinda masilahi yake hilo ndo tatizo lilotufikisha hapa.
Nimekuwa nikifuatilia baadhi ya nchi za wenzetu ambazo mahakimu, wakuu wa polisi, wanasheria wa serikali hupigiwa kura na wananchi ambao mhusika anataka kuwatumikia. Kwa nchi kama yetu na hasa kwa wananchi ambao hatujawahi kuliona hili litakuwa ni la ajabu, kwani tumezoea kuletewa viongozi k.m mkuu wa wilaya, OCD, Hakimu wa wilaya n.k. Hao watu wilayani si watumishi wa umma ni waajiriwa na wawakilishi wa wale waliowaleta hapo .
Sasa kama baraza la seneti ni mwafaka lifike wakati tumeisha kuwa na katiba inayomruhusu mwananchi yeyote kugombea nafasi yoyote hata ikiwa ni nafasi ya urais. La sivyo seneti yetu itakuwa ya walewale waliotufikisha hapa tulipo.
Tumeona jinsi Rais anavyoteua watu ambao hata vigezo vya kuwachagua vinatatanishaa ,lakini kwa vile hakuna mtu wa kumuhoji anafanya apendavyo. Ipo mifano hai ya watu wasio faa hata kidogo lakini kama wana mahusiano na wakubwa wanapewa dhamana kubwa kubwa wasizoziweza.
Hivyo basi wazo la CCM ni jema lakini kwa sasa halitatufaa kwani litawanifaisha walegwa wachache.
NADHANI YOTE HAYA NI KWA
NADHANI YOTE HAYA NI KWA AJILI YA KUTAPATAPA KWA CCM, WAMEJUA KABISA 2015 NI NJE TU KWA VYOVYOTE, NDIYO MAANA WANAANZA KUJITENGENEZEA MAZINGIRA FULANI YA KUJIHAMI. HEBU NYIE WANA CCM NAWAOMBENI MUWE WATULIVU, SISI TUTAUNDA SERIKALI IMARA WALA MSIWE NA HOFU, TULIENI JAMANI MUDA WENU UMEKWISHA
incase hao wastaafu hawaishi
incase hao wastaafu hawaishi hii inakuwaje? hilo halipo katika akili za CCM.
kwanza, wakuu wa wilaya waondoke na wakuu wa mikoa waombe kula kutoka kwa wananchi na wawe kama wawakilishi watakao kuwa na hoja zaidi za kutumikia wananchi badala kurig kula kwa rais aliyewateua.
pili,katiba ilenge kuwalinda waliowengi, Ni wazi chama kilichoshinda siyo kimeshinda kwa wingi wa wananchi wanao wanasupport bali ni idadi iliyo jitokeza kujiandikisha na kupiga kura. hivyo basi kama raia bado hawajapoteza haki ya uwakilishi...katiba inayotakiwa iangalie uwezekano wa uwakilishi wa haki kwa ajili ya nchi badala kutoa mawazo ya muda mfupi.