Makala
Hoja yangu
Lowassa anasema nini kuhusu usalama nchini?
Lula wa Ndali Mwananzela
Toleo la 248
11 Jul 2012

SIKU hizi chache zilizopita zimetuacha baadhi yetu tukiwa na maswali mengi zaidi kuliko majibu kuhusiana na hali ya usalama nchini.

Matukio mbalimbali yanatufanya tuhoji uwezo wa Serikali yetu kuhakikisha usalama wa raia na mali zao na usalama wa Taifa na rasilimali zake. Kuna mambo ambayo yanatokea yanatulazimisha tuhoji kama tulipo ni pabaya zaidi na kwamba yawezekana hatuwezi kutoka isipokuwa kwa wananchi wa Tanzania kuamua kuwaondoa viongozi walioko madarakani kwa njia za kidemokrasia.

Tukio la kutekwa na jaribio la kuuawa la Dk. Steven Ulimboka na madai yaliyotolewa na uongozi wa juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kunalazimisha mtu yeyote mwenye akili timamu kujiuliza ni nini kinaendelea.

Dk. Ulimboka na viongozi kadhaa wa Chaddema na hata wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wameonekana kudai kuwa kuna michezo ya hatari inayofanywa na watu wanaohisiwa ni watu wa Usalama wa Taifa; michezo ambayo inatia maisha ya viongozi mbalimbali na kama tukio la Ulimboka linavyodokeza, inatishia vile vile usalama wa wananchi wa kawaida.

Katika haya yote ni ukimya wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama na Mambo ya Nje, Edward Lowassa ndio unanishtua zaidi. Lowassa ndiye anayesimamia kimsingi wizara zinazoshughulika na masuala haya ya ulinzi na usalama na ana madaraka ya kufuatilia mambo mbalimbali yanayohusiana na usalama nchini. Kinachonishangaza mimi zaidi na naweza kusema kunishtua ni ukimya wake katika masuala haya ambayo yanatusumbua kama Taifa.

Suala la utoroshwaji wanyama kwa ndege ya kijeshi kutoka Qatar

Baada ya tukio hili la kushangaza na kuaibisha, wengine tulitarajia Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama angekuwa wa kwanza kutaka kujua ni nini kimetokea na ilikuwakuwaje wanyama wa thamani kubwa tena wazima wakaweza kuchukuliwa kama magunia ya maembe.

Tulitarajia kamati yake ingefuatilia kwa undani kwa sababu pia inahusisha mambo ya nje; inakuwaje watu wenye pasi za kidiplomasia wanaweza kuingia nchini usiku na kuondoka na wanyama na hadi sasa wanyama hao hawajarudishwa? Tulitarajia Lowassa angeonyesha hasira ya hili; lakini hakufanya hivyo. Hajahoji wala kuitisha mkutano au kuanzisha uchunguzi ili kuwajulisha wananchi ni nini kimetokea.

Kupigwa kwa wabunge wa CHADEMA na kuuawa kwa kijana wa CDM Igunga

Mojawapo ya matukio ya ajabu na ya kushitua ni lile la kutekwa kwa kijana mwanaharakati kule Igunga na ambaye mwili wake ulikutwa siku chache baada ya uchaguzi wa Igunga; mwili ukiwa na dalili zote za kuteswa vibaya sana. Tulitarajia Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama angalau kuonyesha kujali. Hakufanya hivyo.

Tukio la kupigwa kwa wabunge wenzake ambao walidai wamepigwa mbele ya Polisi tulitarajia Mbunge huyo mkongwe na ambaye amewahi kuwa waziri mkuu angeonyesha uharaka wa kutaka kujua ni nini hiki. Hakufanya hivyo.

Matukio ya Tarime, Songea na Arusha

Matukio mengine ambayo yalihusisha vyombo vya usalama ni yale ya Tarime, Songea na Arusha. Sehemu hizi zote tumeweza kuona viongozi na wanachama wa CHADEMA na wananchi wa kawaida wakiwekwa katika hali ya machungu baada ya vyombo vya dola kutumia madaraka yake vibaya na kusababisha maumivu.

Tumeona jinsi miili ya wafu ilivyofukuriwa kule Nyamongo na tumeona jinsi Polisi walivyofanya unyama kule Songea na Arusha. Tuliona vile vile jinsi Polisi walivyokuwa wanatumia nguvu zao kule Tukuyu kwenye uchaguzi wa udiwani. Kote huku Mwenyekiti Lowassa akiongoza bila ya shaka Kamati yenye nguvu zaidi nchini hakusema lolote. Hakuna uchunguzi, hakuna mikutano na wananchi, hakuna lolote. Tunabakia na maswali.

Tukio la Dk. Ulimboka na madai ya CHADEMA

Tukio la kutekwa nyara kwa Dk. Ulimboka na madai yaliyotolewa juzi na uongozi wa CHADEMA vingepasa kumfanya Lowassa hata kuonana na viongozi hao na hata madaktari kujua nini kinaendelea.

Juzi madaktari wameamua kuandika barua Umoja wa Mataifa wakielezea hofu ya maisha yao. Hili lingemfanya Lowassa na wajumbe wa kamati yake kushtushwa. Jamani, mambo yanayotokea si ya kawaida japo tunafikiri ni ya kawaida. Matukio yanayotokea sasa hayawajahi kutokea wakati wa Nyerere – ambaye wapo wanaofikiria alikuwa dikteta!

Kwa nini Lowassa ameamua kuacha vyombo vya usalama viende vinavyokwenda kama vile hakuna usimamizi wa kisiasa? Ni kwa nini Lowassa inaonekana hashtushwi na matukio haya na hata kuitisha mikutano na wananchi au kufuatilia kwa karibu ili wananchi na viongozi wao wasiishi katika hofu ya kudumu?

Kwanini Lowassa ameacha ‘usalama wa taifa’ uanze kuwa ni ‘uhasama wa taifa’? Hakuna anayeweza kumjibia isipokuwa yeye mwenyewe.

Naweza kufikiria baadhi ya majibu- yawezekana ni kwa sababu yanaowakuta ni wapinzani! Labda kwa vile mambo haya karibu yote yanawakuta watu wanaoonekana kuiumbua Serikali ya chama chake; yawezekana ni kwa sababu watu karibu wote waliokutwa na majanga haya ni wale ambao wamekuwa ni mwiba kwa Serikali.

Yawezekana kwa sababu hiyo Mwenyekiti huyu ameamua kukaa pembeni ili hao wote wakione cha moto. Hana sababu ya kuzuia Polisi, hana sababu ya kuwajibisha Usalama wa Taifa, wala hana sababu ya kumuita IGP Mwema kutaka maelezo au uongozi wa Polisi kukutana naye.

Hili linanitisha. Linanitisha kwa sababu kama leo ameamua kukaa pembeni kwa sababu vyombo vya dola vinawakomoa wananchi wa kawaida na amekuwa kimya kwa sababu wapinzani ndio wanamwaga damu yao, itakuwaje kama atakuja kushika madaraka ya nchi yetu kama Rais. Hilo wazo linanitisha.

Lakini zaidi kinachonitisha ni kuwa kama Bunge (chini ya kamati yake) inaonekana hawawezi kujadili na kufuatilia masuala ya Usalama wa Taifa, nani mwingine anaweza kuwasimamia hawa wanausalama ambao wameamua kwenda kombo? Kweli kuna mtu anaweza kuwa salama nchini? Kama walinzi (kina Lowassa) wameamua kukaa kimya, tukivamiwa na watawala nani atatutetea?

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Lula wa Ndali Mwananzela
lulawanzela@yahoo.co.uk

Maoni ya Wasomaji

Lowasa yuko Ulaya akitanua wakati bunge la bajeti likiendelea. Huyu hana habari na masuala yenye masilahi ya nchi hii. Nitashangaa sana kama atagombea uraisi mwaka 2015.

Lowasa alihutumiwa, bado ana nguvu serikalini, bado analipwa pesa. Alitaka kuwa rais anajua haitawezekana. Amekwenda London na Rais bila kutoa hoja yoyote ya matatizo yanayotukabili. Kwa nini bado ana cheo? kwa nini bADO ANA SAUTI? KWA NINI BADO YUPO HURU?  Tanzania haiwezi kuendelea na viongozi kama hawa. Tanzania Haitaendelea kama maghaidi hawa bado wapo Huru. Ilibidi pia Rais wetu atangazie wananchi wake aeleze haya matatizo na kuwatumainisha wananchi usalama upo, na kuwahakikishia. Kushindwa kutoa hotuba hii na kukaa kimya anakubali na mambo yaendavyo, na hajali matatizo makuu ya nhi. Anaacha watu na viongozi wengine washtumiane wao kwa wao ambapo ni hatari kwa wananchi. Kwa nini wananchi wasimuulize moja kwa moja? kwa nini asitumie vyombo vya habari?

Toa maoni yako