Makala
Kwa nini mkulima Mwamwindi alimpiga risasi RC Dk. Kleruu? V
Maggid Mjengwa
Toleo la 220
4 Jan 2012

UKIMWONA kwenye mitaa ya Iringa bado anatembea  kwa hatua za kijeshi. Ni Mzee David Butinini. Alipata kuwa askari polisi na alishuhudia kwa macho yake, siku Mkulima Said Mwamwindi alipofika kituo cha Polisi Iringa akiwa na mwili wa marehemu Dk. Kleruu kwenye gari aliloendesha.

Dk. Kleruu alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliyeuawa na Mwamwindi kwa kupigwa risasi. Mzee David Butinini alikuwa pia mmoja wa mashahidi kwenye kesi ya mauaji iliyomkabili marehemu Mwamwindi.

Mzee David Butinini ni rafiki yangu wa muda mrefu. Jioni ya Jumapili moja tunakutana Soko Kuu Iringa. Namuuliza juu ya kumbukumbu zake ya kilichotokea miaka 40 iliyopita.

Tunazungumza huku kwa pamoja tukikiangalia kituo cha polisi kilicho mbele yetu na ambapo Mzee David Polisi alifanya kazi kama Polisi miaka 40 iliyopita.

“Unasikia Maggid, nilishuhudia kwa macho yangu. Nilikuwa bado kijana enzi hizo. Nilikuwa mwanamichezo pia. Nilikuwa kwenye kikosi cha polisi cha mpira wa miguu. Nakumbuka ilikuwa jioni ya Jumapili ya Krismasi . Ni kwenye saa kumi na moja hivi.

Tulikuwa kama askari watatu hivi tumevalia kiraia na tulisimama pale nje ya kituo,”  Mzee David ananieleza huku akionionyesha kwa mkono mahali hapo.

Kelele za makuli wabeba mizigo sokoni zinatufanya mimi na Mzee Butinini tusisikilazane vema. Wote, kutokana na utamu wa simulizi hii tunajikuta tunasogea mbele kidogo na kusimama kando ya kibanda cha rafiki yangu Mwarami. Kijana  anayeuza matunda Soko Kuu la Iringa.

“Unajua Maggid, Iringa ya wakati huo ilikuwa na watu wachache sana hapa katikati ya mji. Na magari nayo yalikuwa ya kuhesabika. Na Jumapili ile ya Krismasi ilikuwa tulivu kupita kiasi. Ghafla tukasikia muungurumo wa motokaa kama tulivyokuwa tukiyaita magari enzi hizo.

“Mita mia tano mbele yetu tukaliona gari likitokea kwenye mtaa huu tuliosimama. Ni Mtaa wa Jamatini wengine wanauita Uhindini. Na kama ilivyo sasa, na enzi hizo pia barabara hii ni one way.  Gari zinakwenda njia moja tu.

Zinashuka kusini, hazipandi kaskazini.

Je, ni wakati gani mlibaini kuwa ni gari la mkuu wa mkoa? Namwuliza Mzee Butinini.

“Kwanza kama askari tukabaki tukijiuliza; kwa nini dereva wa gari linalokuja anavunja taratibu za barabarani? Lakini, gari lilipokaribia tukabaini haraka kuwa ni Peugeot 404 rangi ya buluu. Ni gari la mkuu wa mkoa. Na pembeni lilikuwa na maandishi ’ RC-Iringa’. Sikumbuki namba za usajili wa gari lile. Tukahisi kuwa mkuu wa mkoa amekuwa na dharura iliyomfanya avunje taratibu za barabarani,” anasema Mzee Butinini anayeonekana kuwa na kumbukumbu nzuri ya tukio kana kwamba lilitokea juzi tu.

Unasema mlihisi mkuu wa mkoa alikuwa na dharura fulani. Je,  gari lilikuwa likiendeshwa kwa mwendo gani na dereva wa gari alifunga wapi breki ya kwanza? Mbele ya kituo? Nyuma ya kituo au kando ya kituo? Namuuliza Mzee Butinini.

“Kwa kweli hata mwendo haukuwa wa kasi sana. Ni wa kawaida tu. Dereva alipunguza mwendo baada ya kupita kituo cha polisi. Akakata kulia na kufunga breki kando ya kituo pale kwenye ule mnara wa kumbukumbu ya askari waliopigana Vita Kuu ya Dunia,” anajibu.

Nini kikatokea? Namuuliza tena Mzee Butinini ambaye wakati huo alikuwa askari kijana sana.

“Tukamuona mtu ambaye hakuwa mkuu wa mkoa akifungua mlango na kuelekea mlango wa mapokezi. Alikuwa mtu mrefu, mnene kiasi na  nakumbuka alikuwa na sharubu kiasi.”

Namkatisha Mzee Butinini kwa kumwuliza;  kwa vile mlifahamu kuwa gari lilikuwa la mkuu wa mkoa na dereva hakuwa mkuu wa mkoa wala dereva wake, hamkuona kuwa ni jambo la kushangaza? Mlichukua hatua gani kabla dereva huyo hajafika ‘kaunta’ ya mapokezi pale polisi?

“Bwana Maggid, kila kitu kilikuwa cha kushangaza na kilikwenda haraka sana. Maana, yule Bwana Mwamwindi  alikwenda moja kwa moja kaunta na pale alikutana na afande Mbete, nakumbuka alikuwa kijana wa Zanzibar. Mara tukamwona akitoka tena na kurudi kwenye gari. Akachukua bunduki na kuja nayo tena kaunta ya polisi. Alikwenda ‘kuisarenda’ kwa maana ya kuikabidhi,” anasema Mzee Butinini.

Je, nyinyi  askari mliokuwa nje mlibaki hapo hapo na umesema mlivaa kiraia. Je, mlikuwa makachero?

“Kazi ya uaskari ni kazi ya ukachero pia, lakini kwamba tulivaa kiraia siku ile ni kwa vile ilikuwa Jumapili na tena siku ya Krisimas. Na kwa kweli  hatukuwa na pa kwenda. Tulikuwa tukijiandaa kusafiri kwenda Moshi kesho yake. Nilikuwa kwenye kikosi cha mpira na tulikuwa na mashindano ya polisi kule Moshi.

Kwa sisi askari vijana kituo cha polisi ilikuwa ni kama kijiwe pia cha kukutania na kupiga stori tukiwa nje. Si unaona hata sasa hivi kuna askari vijana pale kituoni wamevalia kiraia wanapiga gumzo. Na sisi ilikuwa hivyo hivyo enzi zetu,” anasema Mzee Butinini huku akinionyesha askari wale vijana nje ya Kituo cha Polisi Iringa, siku ile ya Jumapili jioni.

Namrudisha tena Mzee Butunini kwenye reli ya mazungumzo kwa kumkumbushia swali langu; Je, mlifanya nini baada ya kumwona Mwamwindi akiwapita na bunduki kwenda kukabidhi kituoni?

“Ahaa! Tuliingiwa na shauku ya kipolisi ya kutaka kwenda kuichunguza gari ya mkuu wa mkoa. Nakumbuka wakati Mwamwindi akiandikisha maelezo yake tuliizunguka gari ile ya mkuu wa mkoa kugagua kilicho ndani.

“Mimi nilikuwa wa kwanza kumtambua Mkuu wa Mkoa, Dk. Kleruu aliyekuwa amelazwa kiti cha nyuma akiwa amevalia overall nyeusi na miwani machoni. Nikasema jamani huyu ni RC Kleruu!” Mzee David anaelezea picha yake ya kwanza ya kifo cha Dk. Kleruu. Namwuliza ni kipi kikatokea baada ya hapo.

Anajibu; “Kwa kweli mambo yalikwenda haraka sana. Nakumbuka kulikuwa na pilikapilika nyingi pale kituoni. Mimi nilikuwa mtaalamu wa chumba cha mawasiliano tukiita signals. Taarifa zilianza kusambazwa kupitia chumba cha signals nilikofanyia kazi.

Ilikuwa mshikemshike. Tarumbeta la polisi likapulizwa. Askari wakakusanyika. Tukatangaziwa rasmi kifo cha mkuu wa mkoa. Kuna askari waliotumwa hospitalini kwenda kuchukua kitanda cha magurudumu cha kumlaza Dk. Kleruu na kumpeleka kumuhifadhi chumba cha maiti.

“Gari la mkuu wa mkoa likazungushwa na kuingizwa uani kwenye kituo cha polisi.

Wanamichezo tuliokuwa tukijiandaa na safari ya Moshi kesho yake tukaambiwa tuendelee na mipango ya safari. Tuliondoka asubuhi yake na basi la Relwe.

“Nyuma yetu tuliacha vumbi kubwa. Msako mkali wa kipolisi ulianza usiku ule ule wa kuamkia safari yetu ya Moshi. Iringa ilitikisika na ikaendelea kutisikika kwa wiki kadhaa.

“Kuna jamaa wa mjini na ambao walikuwa ni wakulima na walimchukia sana Dk. Kleruu. Baadhi nawakumbuka kwa majina. Jamaa hawa walipopata habari ya kifo cha Dk. Kleruu, basi, mmoja wao alinunua kreti za bia na kuanza kunywa na wenzake kusheherekea. Kati ya watu wa kwanza kunaswa kwenye msako wa kipolisi ni jamaa hawa.

Maswali kwa askari huyo wa zamani yanaendelea, namuuliza; Je, Dk. Kleruu alikuwa ni mtu wa namna gani?

“Bwana Maggid, na kwa bahati nilimfahamu sana Dk. Kleruu,  maana kabla ya kuhamishiwa Iringa alitokea Mtwara. Na mimi nilifanya kazi Polisi Mtwara wakati Kleruu akiwa Mkuu wa Mkoa. Naweza kusema namfahamu Dk. Kleruu. Na ninayo ya kumwelezea hata sasa. ”

Inaendelea

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Maggid Mjengwa
mjengwamaggid@gmail.com
+255-754678252, +255-712956131
http://mjengwa.blogspot.com

Maggid Mjengwa pia ni Mwandishi wa Kitabu; "Maisha Ya Barack Obama, alikotoka, aliko na anakokwenda". Kinapatikana mitaani.

Maoni ya Wasomaji

maggid hamna haja ya kukirefusha kisa hiki kionekane kirefu kwa kurudia rudia mambo ambayo umeshayazungumza. katika hili najua hutokubali lakin huo ndo ukwel. una prolong the story iwe ndefu every week uendelee kusimulia.why? mi nlidhan ungeisimulia iishe then ungetafuta jambo lingine tusonge mbele.imekuwa sasa ina bore( sijui kwa kiswahili kubore ni nin- nadhan niseme inachusha not chosha) hii hadith haikuwa ndefu kias hicho kaka.

Mwendelezo unachanganya!!
Mwendelezo wa makala hii unaleta ugumu wa kuelewa mwandishi anahitimishi vipi kila aliyefanya naye mahojiano kuhusu tukio hili ambalo kibinadamu ni tukio la kuhuzunisha na kuogopesha.
Katika sehemu ya pili au ya tatu ya makala hii, mwandishi alieleza mahojiano na mtoto wa Marehemu Mwamwindi. Na akaahidi kuwa ataendeleza maelezo ya mtoto wa Marehemu Mwamwindi sehemu inayofuata.
Sehemu iliyofuata, haikuendelezaa maelezo ya mtoto wa Marehemu Mwamwindi bali yakatokea maelezo ya Maheremu Hongele. Huyu alikuwa mwandishi wa habari wakati tukio la kuuwawa Klyeluu linatokea. Na tukaahidiwa kupata maelezo zaidi ya Hongole sehemu inayofuata. Ambayo ndiyo hii ya tano. Hata hivyo, badala yake yameibuka mahojiano na mtu mwingine, yaani Mzee David. Na tumeahidiwa pia maelezo yake yataendelezwa sehemu inayofuata.
Kama ni mbinu ya kiuandishi kwamba maelezo ya waliohojia yanaguswa tu na kuahidiwa kuendelezwa baadaye lakini hatua inayofuata yanakosekana nadhani si uandishi mzuri.
Na kinachonipa shida nyingine ni kuwa kila aliyehojiwa aneonesha kuwa tukio lile la kuhudhunisha amebaini kuwa watu walilishangilia. Hakuna aliyeonesha kuwa ni tukio la kuhudhunisha na kusononesha.
Ubinadamu ni ustarabu. Ndiyo maana sisi tunatofautiana na wanyama kwamba ustarabu wetu unawekewa sheria ya kuusimamia ambazo tunatunga sisi wenyewe. Klyeluu kama binadamu anaweza kuwa alikuwa na upungufu na makosa. Sheria zingetumika. Lakini, si kuonesha kwamba kuuwawa kwake watu wameshangilia.
TUNAJIFUNZA NINI HAPA!!

Nimeipenda story ya Mzee Butinini ,niliwahi sikia nikiwa mdogo sana nikaifurahia sana,leo Butinini ananipa ukweli wake,nakumbuka mwalimu wetu wa sheria MUCCOBIS-kizumbi 1990, MR Urio alituonjesha kidogo darasani kutupa mfano wa kesi hii ya Mwamwindi.Eti mwamwindi alifikiri Dr Kreluu ni nguruwe pori! aneharibu mahindi yake,nae Dr Kreluu alifuata ninin shambani kwa Mwamwindi?
    Big up Butinini! wazee kama nyie bado mnatakiwa katika kizazi hiki,watoto wa siku hizi wanakosa vitu kama hivi.hivi huyu mwamwindi alikuwa mzima kweli? au Mkuu wa mkoa Kreluu alimfanya nini? hayo maswali yamebaki kichwani mwangu.
    Aksante pia kwako Maggid kwa kuleta uhondo wa story hii,huu ndio uzalendo wa kweli kuelimisha wananchi wachanga kuelewa nchi yao ilikotoka.
              Naisubiri kwa hamu,
                                                Asumpta,
                                                                    Ulinzi & JKT.
                                                                         9th Jan 2012.
 
 
 
 
 

KUMBUKA KUELEZA YOTE BILA KUFICHA KWAMBA KWANINI RC ALIKWENDA SHAMBANI KWA MWAMWINDI BILA ULINZI NA BILA DREVA WAKE? UKIFICHA MIMI NITASEMA

Bwana wee hebu tuambie ukweli. Mimi nilikuwa mdogo sana mwaka alipouawa Kleruu ila nakumbuka hayo makasheshe tu kwa umbali.
IMEKUWAJE KLERUU AKAWACHA KULA KUKU WAKE WA KRISMASI NA KWENDA KUPAMBANA NA AKINA MWAMWINDI? AU NDIYO MALAIKA ZIRAILI ALIKUWA ANAMWITA?
RIP KLERUU KUNA MASUALII HAYAJIBIKI MPAKA KIAMA.
 

Dr Wilbat Kleruu niliyehata mwimba shule ya mwingi hawezi kuwa na story iso isha. Aliuwawa na makes ni mfupi tu, ingawa nilitaka jua has a kiini, this is boring na naw Hama nayo sass goodbye

Majid hata mimi sioni unachokifanya mpaka sasa. Hadithi ilikuwa nzuri ila umeshaiharbu kwa kuendeleza jambo lisilo endelezeka. Kila wiki unarukia mtu mwingine mpya. Huu ni upuuzi kama huna vya kuandika waachie wengine wana mambo ya kutuhabarisha.

Majid unatuudhi sasa acha hizo!

Toa maoni yako