Mahojiano
Dk. Bana: Wanasiasa wanavuruga mwenendo wa kitaaluma kwa wanafunzi vyuoni
John Daniel
Toleo la 222
18 Jan 2012
  • Ashauri wahadhiri wapewe fursa kutekeleza wajibu wao kwanza, siasa baadaye
  • Apendekeza mfumo wa Serikali moja ili kulinda Jamhuri ya Muungano
  • Asema mashambulizi kwa Magufuli ni mwendelezo wa siasa za kuvua gamba

JANUARI 4, mwaka huu, Mwandishi Wetu, JOHN DANIEL, alifanya mahojiano na Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dk. Benson Bana, kuhusu masuala mbalimbali yanayoendelea nchini. Ili kufahamu zaidi yaliyojiri, endelea kusoma.

Raia Mwema: Nini mwelekeo wa nchi kisiasa na hasa kwa kuzingatia mwenendo wa baadhi ya vyama vya siasa kuwafukuza uanachama baadhi ya wanachama wake, wakiwamo wabunge?

Dk. Bana: Kusema kweli kwetu sisi kama wanataaluma katika masuala ya kisiasa kwa sasa hali si nzuri nchini na hata tukisema ni nzuri tunajifariji tu ila si kweli.

Tukianza na vyama vya siasa kwa maana ya vyama pinzani kuna tatizo la kutokomaa kwa viongozi wa vyama hivi japo kwa upande mmoja wanafanya kazi vizuri.

Raia Mwema: Unaposema viongozi hao wa vyama vya siasa hawajakomaa una mantiki gani?

Dk. Bana: Naweza kusema hivyo kwa kuwa ukomavu wa kisiasa ni pamoja viongozi kuwa na uvumilivu na kujua jinsi ya kutatua matatizo bila kusababisha malumbano zaidi au mpasuko katika masuala magumu ikiwa ni pamoja na anapoguswa wewe binafsi (kiongozi) na chama chako.

Watanzania walio wengi ni mashahidi kwa yaliyotokea kwa NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF), kwa kuwavua uanachama wabunge wao eti kwa kosa la kwenda kinyume cha taratibu za chama.

Ukiangalia kwa undani utabaini kuwa wabunge wote wawili waliovuliwa uanachama aidha walikosana na viongozi wa juu wa vyama hivyo au waliwasema vibaya, sasa inapotokea hali hiyo ikawa chanzo cha kiongozi mkubwa kama mbunge kufukuzwa kwa sababu kama hizo, ni tatizo kwa siasa za Tanzania hivyo ni wazi kuwa hali ya kisiasa si nzuri.

Hoja ya msingi hapa na jambo muhimu zaidi kujiuliza ni je, wanaoazimia kufukuza mbunge kwenye chama na kusababisha apoteze sifa ya kuwa mbunge ni wangapi? Je, wanafikia hata robo ya waliomchangua mbunge husika kwa kumpigia kura jimboni? Je, wamepata maoni ya wananchi (wa jimbo husika) kuhusu uamuzi wao?

Pia sijasikia vyama husika vikitangaza hadharani kwa umma makosa halisi ya wabunge hao, nasikia tu makosa ya kinidhamu, kutoa siri za chama, kuzungumza kwenye vyombo vya habari, mbona hawasemi ametoa siri hii, amekosa nidhamu kwa hili, alionywa na kikao cha tarehe fulani kwa barua hizi tatu….hatusikii haya, mbona hawaelezi haya kwa wananchi?

Binafsi nafananisha kitendo cha kumfukuza mbunge kwenye chama na kusababisha apoteze sifa ya kuendelea kuwa mbunge kikatiba na adhabu ya kifo ambacho kimsingi haifai kutolewa kwa mtu yeyote.

Kitendo hicho ni sawa na kuua demokrasia ya kweli nchini. Tunawafunga mdomo wabunge kutohoji mwenendo wa mwenyekitia au katibu mkuu wa chama, hata kama amefanya makosa maana akifanya hivyo atafukuzwa.

Kitendo hiki kinanikumbusha Kabwe Zitto (Mbunge wa Kigoma Kaskazini - CHADEMA) alivyopata misukosuko alipotaka kugombea nafasi ya uenyekiti wa taifa ndani ya CHADEMA.

Wenye kumbukumbu nzuri watakumbuka kuwa ilifikia hatua akaitwa na watu waliotajwa kuwa ni wazee wa chama hicho. Wazee hao wakamuomba aachane na wazo hilo la kugombea uenyekiti kwa kushindana na mwenyekiti aliyepo ambaye naye alikuwa akigombea kurejea katika nafasi hiyo.

Kama vyama vya siasa ambavyo tunatarajia vilete changamoto kubwa na ya wazi kidemokrasia ndivyo vinakuwa chanzo cha kukandamiza demokrasia, ni wazi kuwa hali ya kisiasa si nzuri na viongozi wa vyama hivyo hawajafikia kiwango cha juu cha ukomavu kisiasa.

Raia Mwema: Unadhamani nini chanzo cha hali hiyo?

Dk. Bana: Chanzo cha tatizo ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 71 (f ) kinachotoa nafasi kwa chama cha siasa kumfanya mbunge apoteze nafasi yake pale wanapomfuta uanachama.

Kifungu hicho cha Katiba kinataja mambo kadhaa yanayoweza kumfanya mbunge apoteze nafasi hiyo, ikiwemo kuvuliwa uanachama na chama chake.

Raia Mwema: Kutokana na Katiba kutoa mwanya huo unaoelekea kuua demokrasia ndani ya vyama vya siasa na nchi kwa ujumla, je, nini kifanyike?

Dk. Bana: Kwanza kabisa nawaomba Watanzania wote tukatae kifungu hiki katika mchakato wa kupata Katiba mpya. Hii ndio njia rahisi na nafasi kwa wananchi kuiambia Serikali kuwa tunachotaka ni hiki na si kile.

Lakini pia vyama vya siasa vitafute utaratibu mwingine mzuri zaidi kuwaadhibu wabunge wake pale inapothibitika kuwa wametenda kosa.

Njia mojawapo ni kuchapisha makosa ya mbunge na kuyasambaza jimboni kwake ili wananchi waliomchagua wajue alichofanya mwakilishi wao.

Pia baada ya chama husika kukutana na kupendekeza, adhabu ichapishwe na kusambazwa kwa wananchi jimboni ili wapime kama adhabu hiyo inaendana na kosa na pia kama inawaridhisha. Wananchi ndio wawe watu wa mwisho kumwadhibu mbunge wao maana ndio waliompa nafasi hiyo na si chama.

Raia Mwema: Mbali na mapendekezo hayo, kuna njia nyingine inayoweza kutumika kuepuka hali hii ya kufukuza wabunge ndani ya vyama vya siasa?

Dk. Bana: Ndio, njia nyingine ni chama husika kupewa mamlaka kisheria kuteua mtu mwingine kuwa mbunge iwapo aliyekuwepo ataondolewa kwa sababu za kuridhisha ambazo pia zimeridhiwa na wananchi wa jimbo husika la ubunge.

Pia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iwe na mamlaka kisheria kumtangaza aliyechukua nafasi ya pili (kutoka chama chochote) kwa mujibu wa matokeo ya kura za ubunge wakati wa Uchaguzi Mkuu, iwapo mbunge aliyekuwepo atakuwa ameondolewa kwa sababu zozote ikiwemo kufariki dunia au kufukuzwa.

Lakini pia vyama vya siasa visiogope inapotokea kutoelewana kati yao na mbunge wao waombe ushauri kwa wanazuoni waliobobea katika masuala ya kisiasa. Tuko tayari kuwasaidia bila kufukuzana, hiyo ndio kazi ya wataalamu kutoa ushauri kuhusu fani zao.

Nasikitika sana eti mbunge akikosana na mwenyekiti tu basi anafukuzwa, hana nidhamu. Hatuwezi kuendesha siasa za namna hiyo tukajidai eti demokrasia imekuwa nchini.

Utafiti umeonesha kuwa wabunge wengi hawachaguliwi kwa sababu ya vyama vyao bali ni haiba yao na umaarufu wao, kwa hiyo, ushindi wao kwa sehemu kubwa unatokana na namna wananchi wanavyowapenda wao wenyewe, kwa majina yao na si vyama vyao.

Mtu hawezi kuwaambia Watanzania kuwa Kafulila alichaguliwa kuwa Mbunge pale Kigoma kwa kuwa NCCR-Mageuzi inapendwa na ina wanachama wengi pale. Ni kweli wale wananchi wanampenda Kafulila na inawezekana uchaguzi mdogo wa ubunge ukirudiwa pale chama hicho kisipate tena hiyo nafasi.

Maana ya demokrasia ni kuwa wananchi ndio wawe na sauti ya mwisho na si kundi fulani dhidi ya wananchi. Uchaguzi mdogo pia ni gharama kwa taifa, unachukua muda mwingi ambao ungetumika kuzalisha.

Nashauri vyama vya siasa vijenge utaratibu wa kumfanya mtu ajiondoe mwenyewe, aambiwe makosa yake au tuhuma zake, ajipime na kufikia uamuzi yeye mwenyewe si kufukuzwa, huo ndio utaratibu wa demokrasia ya kweli.

Kutokana na hali hii nadiriki kuweka wazi kuwa CCM imepiga hatua kubwa katika hili, wao licha ya kulumbana na mpasuko lakini hawajafikia hatua ya kufukuzana. Rostam (Azizi aliyekuwa mbunge wa Igunga) alijiondoa mwenyewe baada ya kupima, lakini tunakumbuka jinsi uchaguzi wa kuziba nafasi yake ulivyotugharimu muda na fedha nyingi.

Raia Mwema: Pamoja na ushauri wako, wewe kama Mwenyekiti Mwenza wa REDET (Mpango wa Utafiti wa Elimu ya Demokrasia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam), mnafanya nini kuwezesha vyama hivi kukomaa kidemokrasia?

Dk. Bana: Kwanza tumekuwa tukiwapa mafunzo ya aina mbalimbali, lakini kwa sasa tunajiandaa kufanya utafiti kujua chanzo cha tatizo hili na kutoa mapendekezo kitaalamu zaidi.

Raia Mwema: Huu ni mwaka wa kuanza rasmi kwa mchakato wa Katiba mpya baada ya Rais Jakaya Kikwete kusaini sheria ya kusimamia mchakato huo. Nini mtazamo wako kuhusu hatua hii?

Dk. Bana: Kwanza namwonea sana huruma Rais Kikwete kwa mchakato huo, anapaswa kuwa makini kuliko wakati wowote tangu aingie madarakani.

Suala la Muungano linapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa sana, turuhusu mijadala na watu kutoa mawazo yao bila kuwazuia lakini tuchambue sana uamuzi wa mwisho.

Kama mtu mmoja tu alichana hadharani karatasi ya muswada kule Zanzibar wakati wa mchakato wa kukusanya maoni ya wadau kuhusu sheria ya kuundwa kwa tume, hali itakuwaje tutakapoanza kujadili Muungano wenyewe kwa ujumla katika Katiba mpya?

Ni lazima Rais Kikwete ajiandae kukabiliana na hali hiyo na kutuliza jazba kama hizo. Lakini kikubwa ni lazima tuhakikishe Katiba mpya inaleta Serikali moja ya Muungano kama kweli tunataka kudumisha Muungano wetu kwani mfumo wa sasa unadhoofisha Muungano na dawa yake ni Serikali moja tu.

Raia Mwema: Kushamiri kwa migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na mambo mengine lakini pia inahusishwa na siasa, kuna ukweli wowote kuhusu maelezo haya?

Dk. Bana: Ni kweli vyama vya siasa vimeshiriki kwa namna moja au nyingine kuchangia migomo kwa wanafunzi wetu wa elimu ya juu.

Ombi langu kwa wanasiasa ni kutuachia hawa vijana wetu tuwapike kwanza ili baadaye wapate watu waliokomaa na wanaojua mambo kwa undani kuendeshsa vyama hivyo, kuwaingiza sasa katika vurugu ni kutowatakia mema huko mbele.

Kuwatafuta wanachama wasomi ni jambo jema sana lakini wasubiri wakati wa likizo wawape sera zao, wasituingilie kisha wanawapa uelekeo mbaya ya kugoma na kuona kila kitu kuwa ni tatizo.

Tuna mfano hai, hata baadhi ya wanasiasa katika vyama hivyo walifanya hivyo wakafukuzwa leo wanahangaika kweli kwenda kusoma mara Ulaya mara wapi kwa kuwa waliingia katika siasa kwa wakati usiofaa, wakaanza malumbano na uongozi wa chuo badala ya kusoma.

Raia Mwema: Katika kipindi cha mwaka 2011 Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umetikishwa kwa kauli mbalimbali za baadhi ya wanasiasa, ambazo ni pamoja na hoja ya kutaka rais ajaye atoke Zanzibar. Unazungumziaje hali hii?

Dk. Bana: Kwanza nasikitika sana jinsi wanasiasa wenyewe wanavyoshiriki kudumaza Muungano wetu, hata leo nikiulizwa ni mfumo upi kwanza unaofaa kudumisha umoja wetu, nitasema kwa haraka ni Serikali moja na hili ni vizuri liingizwe katika Katiba mpya kama kweli tunataka kudumisha Muungano, ila kama tunataka kuuvunja tuendelee na mifumo mingine.

Katiba inaweka wazi kuwa Rais akitoka upande mmoja makamu wake atoke upande wa pili basi. Tukianza kuchokonoa kwamba huyu katoka huku awamu ijayo atoke kule tunataka kuvunja Muungano.

Tukianza hivyo itafika siku tutaanza; yule alitoka Unguja safari hii atoke Pemba, baadaye tutaanza kuulizana huyu alitoka mkoa upi, wilaya ipi na kisha tutaanza kuulizana kabila.

Wanasiasa wawe wawazi kuwaelekeza wananchi njia sahihi ya kudumisha Muungano wetu, wasiwe wanafiki kwa manufaa yao na vyama vyao kisha kuwa chanzo cha kero za Muungano zisizo na tija.

Kama ASP na TANU vilivyokubaliana kuacha mambo yao na kuunda CCM na taifa moja la Tanzania, ndivyo tunavyotakiwa kuwa, nawashangaa wanasiasa wetu kushindwa kuwa wakweli kama alivyofanya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Raia Mwema: Tunapoanza mwaka 2012 unazungumziaje mwenendo wa siasa ndani ya CCM, kama chama tawala pamoja na mkakati wake wa kujivua gamba?

Dk. Bana: Kwa ujumla hali ya siasa ndani ya CCM si nzuri, ndio maana nilisema hali ya siasa nchini kwa ujumla si nzuri, CCM bado wanalumbana hadharani, hii ni dalili ya kuwapo kwa mpasuko mkubwa na vita vya chini-chini vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya chama.

Mkakati wa kujivua gamba haijawasaidia, nadhani imezidi kuwavuruga tu, nataka nitoe mfano hai. Hivi karibuni Waziri Magufuli (Waziri wa Ujenzi) alitangaza bei mpya ya kivuko cha Kigamboni, jambo ambalo ni la kawaida lakini wabunge wa CCM na baadaye Mwenyekiti wa CCM Dar es Salaam, walitoa tamko la kumkosoa na kibaya zaidi, wanatumia kauli mbaya kutaka wananchi wamwone Magufuli kuwa ni mtu mbaya wakati sivyo.

Hii ni mojawapo ya dalili mbaya sana kwa CCM kama Waziri wa Serikali yao anaweza kupingwa hadharani na mwenyekiti wa chama hicho ambaye angeweza kutofautiana naye ndani ya vikao. Kuna tatizo kubwa ndani ya chama hicho.

Lakini pia Waziri Mkuu wa zamani, Sumaye (Frederick) alizungumza hivi karibuni akikosoa Serikali. Kati ya aliyoyasema ya kweli ni moja tu kuhusu posho za wabunge.

Lakini mengine yote angeweza kusema ndani ya vikao vya CCM ambako ni mjumbe lakini pia angeweza kuwasilisha mawazo yake moja kwa moja kwa kiongozi yeyote bila kuyasema kama alivyofanya, kitendo kile ni kubomoa.

Yapo mambo mengi lakini mifano hiyo miwili ni dalili ya dhana ya kujivua gamba kutoisaidia CCM bado kuna mgawanyiko mkubwa zaidi, ila nadhani Wilson Mukama (Katibu Mkuu wa CCM) ameshajua hilo, naamini atalifanyia kazi ni mtu mwenye uelewa na uwezo wake ni mkubwa.

Raia Mwema: Nini ushauri wako wenye lengo la kukisaidia chama hicho?

Dk. Bana: Ieleweke kuwa CCM ndio chama pekee chenye itikadi, vyama vyote vina sera, kanuni na taratibu nyingine. Lakini ukiuliza itikadi ni CCM pekee na itikadi yenyewe ni kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi.

Dawa ni kurudi kwanza kwenye itikadi yake, wakulima na wafanyakazi wakipewa nafasi kila kitu kitarudi katika hali ya kawaida, hivi sasa CCM ni mali ya wafanyabiashara wakubwa, tena wengine hata asili ya utajiri wao hauelezeki.

Pili warejeshe mshikamano wao, na hapa narudia hivi wale wabunge wa CCM na Mwenyekliti wa chama hicho Dar es Salaam waliojidai kuwatetea wananchi mbona hatujawasikia wakiwatetea wakati wabunge walipojipandishia posho kubwa huku wananchi wakiwa na hali mbaya?

Mbona hatujawasikia wakishughulikia msongamano katika Jiji la Dar es Salaam? Hatujawasikia wakitetea rasilimali za nchi zinazokwapuliwa na wachache? Mbona hatujawasikia wakiwatetea wananchi wa maeneo mbalimbali wanaolipa nauli ya Sh. 500, hapa Dar es Salaam kutokana na ubovu wa barabara?

Hivi sasa kiongozi wa Serikali au CCM ana hisa katika kampuni zaidi ya moja, ni mwenyekiti wa bodi ya kampuni fulani. Je, watakuwa na uwezo wa kuhoji vipi utendaji wa kampuni hizo kwa ukweli wakati wao ni sehemu ya tatizo?

Ningependa CCM itambue kuwa ina mradi mmoja tu wa kusimamia nchi kwa maana ya rasilimali, wananchi, uchumi na kila kitu. Viongozi wake wanatakiwa kutambua hilo na warejee kwenye itikadi yao ya kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi.

Dalili nyingine inayoonesha hali mbaya ndani ya CCM ni kukosekana kwa maandalizi ya wazi ya rais ajaye, wakati Mkapa anaondoka madarakani kulikuwa na majina yaliyojulikana kuwa mmoja wao atarithi nafasi hiyo ndivyo ilivyotokea.

Leo tukiulizwa ndani ya CCM ni nani hakuna jibu, ni lazima kazi hiyo ifanyike kuanzia mwaka huu ili kujenga maslahi ya chama hicho katika siasa huwezi kukwepa hilo.

Lakini hilo si kwa CCM pekee hata vyama vingine vya siasa ni hivyo hivyo, hakuna maandalizi tena wao ni mbaya zaidi mtu akitaka kuwa maarufu kuzidi mwenyekiti anapigwa vita, anatungiwa hata tuhuma kumdhoofisha, hii ni hatari kwa siasa za Tanzania.

Raia Mwema: Unazungumziaje hatua ya Tanzania kuelekea shirikisho la kisiasa kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki?

Dk. Bana: Kwanza umoja wa kisiasa kwa nchi za Afrika Mashariki ni safari ndefu na haihitaji haraka kama baadhi ya watu au nchi wanavyotaka.

Ni Tanzania pekee kati ya nchi tano za jumuiya hiyo iliyojenga msingi wa utaifa, nchi zilizobaki bado zina matatizo makubwa ambayo yasiporekebishwa kwanza yanaweza kuwa hatari kubwa kwa mustakabili wa ushirikiano huo baadaye.

Kila raia wa Tanzania anajua neno moja tu ‘mimi ni Mtanzania’ lakini ukienda Kenya kuna mkikuyu, mjaluo, mkalenjini na mengine.

Ukienda Uganda hali ni hiyo hiyo, Rwanda kuna ukabila kama ilivyo Burundi ambako bado hawajatulia, kwa hiyo, safari yetu kufika katika hatua hiyo bado sana.

Tunachotakiwa kufanya kama nchi kwa sasa ni maandalizi makubwa katika sekta mbalimbali ambazo tuko nyuma, hususan biashara na utalii.

Wakati tukisubiri wenzetu kujenga utaifa na kufuta ukabila kwanza ni vema Serikali ikaangalia kwa ukaribu sana kuwajengea wananchi uwezo wa kibiashara za ushindani hususan katika sekta ya utalii, walimu wazuri walioko nchi wanachama tuwachukue waje watufundishe huku katika vyuo vyetu na si kupelekea tu wanafunzi wetu kwao.

Nashukuru Serikali kuruhusu ajira ya walimu hususan katika masomo ya sayansi kutoka nchi wanachama wa Jumuiya japo tumechelewa sana kufanya hivyo, hatua hiyo ikisimamiwa vizuri na kwa uzalendo itatusaidia.

Raia Mwema: Nini ujumbe wako katika masuala siasa kwa Watanzania katika mwaka huu wa 2012?

Dk. Bana: Nawaomba kwanza wanasiasa waache kuwapotosha wananchi, hususan vijana kwa maslahi yao na vyama vyao. Wawe wakweli na waeleze itikadi na sera zao vizuri kwa maslahi ya nchi yetu.

Pia waache kuingiza siasa katika masuala ya utendaji na sheria kwa maslahi ya nchi, waache viongozi wa Serikali watimize wajibu wao, vijana wasome, wananchi wazalishe.

Viongozi wa vyama vya siasa waache kuongoza vyama kwa maslahi yao na familia zao, ni aibu kusikia ndani ya chama cha siasa kiongozi mmoja ni babu, baba, mtoto, shemeji au dada, masuala kama haya hayaendelezi demokrasia bali yanaendeleza mtu mmoja tu au kikundi fulani.

Mshikamano kwa wananchi wote kutetea na kuthamini Tanzania ni muhimu kuliko jambo lolote, lakini pia tuepuke lugha za kuvunja umoja wetu hususan Muungano.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi

Maoni ya Wasomaji

Hivi jamani huyu Dr Bana anawalipa kutoa hoja zake? Huyu jamaa ni kilaza mno wala hastahili kusikilizwa. Na kama muhaya mwenzie walioko wote REDET asingekuwa anambeba hata uhadhiri UDSM angeshatoka. Muulizeni ame-publish lini kwenye international journals. Muulize ame-present lini kwenye international conferences. Muulizeni amechapisha kitabu kipi? Kama yote hayafanyi anastahili vipi kuwa muhadhiri muandamizi? Nchi hii inaangamia kwasababu vilaza wameshika hatamu. Si ata JK rais pekee aliyekuwa na degree yenye just pass (gentleman) alisema uongozi hauitaji elimu? What a pathetic country Tanzania has become!

Comment ya namna hii haisaidii kuelimisha wasomaji na inaonyesha ni namna gani ndugu yetu huyu abel alivyo maskini wa fikra. kukomenti juu ya jambo fulani ni kuonyesha mtazamo wako juu hicho kilichozungumzwa na muhusika/wahusika na si hivi kama alivyofanya.
Kwa mtazamo wangu  ninadiriki kusema kazi nzuri za kutuelimisha zinazofanywa na wanazuoni wetu hapa nchini akiwemo Dr. Bana hazipaswi kubezwa hata kidogo. Kwanza napenda kumshauri ndugu yangu abel na wenzake wanaofanana naye wawe wafuatiliaji wa karibu wa matukio ya kisiasa na kiuchumi yanayotokea hapa nchini na kisha ndiyo waweze kutafakari mawazo mazuri ya Dr. Bana.
Aidha, napenda kuwapongeza wanazuoni wetu kwa kazi yao nzuri ya kuielimisha jamii ya watanzania juu ya mustakabali wa maisha yao kiuchumi, kisiasa na kijamii. Pongezi za pekee pia kwa waaandishi wetu wa Gazeti letu kipenzi la Raia mwema kwa kweli  wanastahili kupongezwa kwa kazi yao nzuri!

Toa maoni yako