Makala
Rai ya Jenerali
Chembechembe za uhai zinazidi kuvia, za mauti zinazidi kujizalisha
Jenerali Ulimwengu
Toleo la 229
7 Mar 2012
  • Siasa zetu soko la mitumba, chagua ule unaonukia zaidi ya mingine

INAWEZA kuwa rahisi kwa mtu anayesoma makala hizi kudhani kwamba ninachosema ni kwamba kupotea kwetu kumeanza hivi majuzi, chini ya awamu hii inayoitwa ya nne na chini ya kiongozi wake Jakaya Kikwete. Mwingine anaweza kudhani kwamba mtazamo wangu ni kwamba tulianza kupotea chini ya awamu inayoitwa ya tatu na chini ya kiongozi wake, Benjamin Mkapa, au chini ya awamu inayoitwa ya pili chini ya kiongozi wake, Ali Hassan Mwinyi.

Sivyo. Kupotea tulikopotea hakuwezi kupimwa kwa kuangalia kiongozi mkuu wa kipindi fulani. Kupotea ninakokujadili hakutokani na matukio machache au uamuzi uliopata kufanyika katika kipindi fulani. Kupotea kwetu ni mchakato (process) wa kitambo, ni mwendelezo wa mienendo iliyotutoa katika msitari tuliokuwa tumelenga na kutupeleka porini taratibu hadi tumejikuta hatujui tunakoelekea na wala tunakotoka hatukuelewi vyema.

Hatutaweza kuelewa vyema jinsi tulivyopotea iwapo hatuko tayari kudurusu kwa umakini mkubwa jinsi tulivyoanza katika harakati za kujikomboa na tulivyoenenda katika miaka ya kwanza ya Uhuru wetu, na jinsi tulivyojenga matarajio yetu, na jinsi tulivyoanza kuyavuruga kidogo kidogo, tukipuuza misingi ya Uhuru wetu, hadi hapa tulipofikia ambapo hata dhana ya Uhuru inakuwa tata.

Hatari iliyotusonga ni kwamba hatujajenga taifa la kutaka kujua, na badala yake tumejenga taifa la watu wengi wanaodhani kupiga kelele kwa sauti kubwa huku ukieneza hisia kali ndiyo ishara ya weledi. Hatutaki kusoma historia yetu, hatutaki kujua ni nini kilifanyika huko nyuma, kilifanywa na nani, kilifanywa kwa ajili gani, manufaa yake yalikuwa yapi na hasara zake zilikuwa zipi.

Tunao watu wanaojiita wanasiasa leo hii ambao hawana hata fununu kuhusu mambo ya msingi kabisa ya taifa hili, ambao kwao historia ni simulizi za wafu na ambao wanaamini kwamba wanaweza kushika madaraka ya nchi bila kutaka kujua nchi yenyewe imeanza vipi, imepitia mabadiliko gani, na imekuwaje hadi ikawa hivi ilivyo leo. Uchakavu (kitaaluma) wa shule zetu bila shaka utazaa “wanasiasa” wengine wengi wa aina hii. Jinsi hii hatuendi kokote, isipokuwa nyuma.

Hatuna budi kuisoma historia yetu, na tukiisoma vyema tutaelewa kwamba tulianza kupotea tangu tulipoanza. Wale wanaoelewa mantiki ya dialektiki (dialectics) wanajua kwamba kila chembechembe ya dhana ina chembechembe ya dhana pinzani, na kwamba katika misuguano baina ya chembechembe hizi ndiko dhana inapata kusonga mbele au kurudi nyuma, na hata kutoweka.

Mtoto anayezaliwa leo anaanza mara moja safari yake ya maisha kuelekea kifo, na ataweza kuishi tu kwa muda atakaoruhusiwa kuishi kutokana na jinsi chembechembe kinzani za maisha na kifo zitakavyosuguana. Iwapo chembechembe za maisha zitakuwa na nguvu zaidi, mtoto atakua, atakomaa, atakuwa mwenye siha njema, atapevuka hadi kifo kimkute akiwa na umri mkubwa. Ikiwa ni chembechembe za mauti zenye nguvu zaidi, atakufa kabla ya kutimiza hata mwaka mmoja. Iwapo matokeo ya mpambano kati ya mauti na maisha ni sare, mtoto atakua, atafikia umri wa kati kabla ya kifo, lakini atasumbuliwa kutokana na afya mbovu ambayo itaondoa furaha katika maisha yake. Na hapa sijazungumzia ajali ya kugongwa na nyoka au kuliwa na simba.

Sasa tuangalie utoto wetu, ukuaji wetu na mpambano kati ya chembe za uhai na chembechembe za mauti. Chembechembe za maisha katika utoto wetu ziliwakilishwa na ile nguvu ya matarajio ya maisha bora katika Uhuru baada ya kuwa tumekandamizwa na dhuluma ya ukoloni, utumwa, unyanyasaji na unyonyaji.

Tulisema kwamba tulikuwa tumeonewa, tumenyonywa na tumenyanyaswa kiasi cha kutosha na kwamba haya yote yalitokana na unyonge wetu; na tukaapa kufanya mapinduzi ili tusionewe tena, tusinyonywe tena, na tusinyanyaswe tena. Wakati huo tulikwisha kuitangazia dunia kwamba tulikuwa tumedhamiria kuwasha mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro ili “umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini ….”

Pia tulikwisha kutamka kwamba binadamu wote ni ndugu zetu na Afrika ni moja; tukatamka pia kwamba rushwa ni adui wa haki, hatutapokea wala kutoa rushwa; aidha tuliapa kwamba cheo ni dhamana, na hatutatumia vyeo vyetu kwa maslahi yetu binafsi….

Yote haya, na mengine mengi yalitokana na uangavu wa fikra za Julius Nyerere na maswahiba zake walioanzisha vuguvugu la ukombozi. Maadili yaliyobebwa na  matamko hayo ni ya kihistoria; yalikaririwa na watu walioijua historia ya ulimwengu na waliosukumwa na utashi wa kujikomboa na kuwakomboa wanadamu wote, nchini na kwingineko. Huu ulikuwa utashi mtakatifu, na haya yalikuwa ni maadili yaliyotukuka.

Ni haya maadili yaliyowafanya waasisi wa nchi hii kutangaza Azimio la Arusha, ambalo najua wengi wa “wanasiasa” wetu wanadhani limepitwa na wakati. Hili ndilo tamko rasmi lililotutanabahisha na utegemezi wa kiuchumi na jinsi unavyoweza kutupora uhuru wa kuamua mambo yetu, na ndilo tamko rasmi lililokataa kujenga nchi yenye matabaka yanayopishana mno kiuchumi kwa sababu ni hatari kwa usalama na amani nchini.

Kutokana na msingi huo wa kimaadili ndani ya nchi, Tanzania ikawa ni ngome ya kupigania uhuru na ukombozi barani Afrika na duniani kote, kimbilio la kila aliyeonewa na kunyanyaswa nchini kwake. Hii ikawa ndiyo sura ya Tanzania; nchi ya watu makini, waongofu, waadilifu, watetezi wa haki; wasiomuogopa mzungu wala mama yake; nchi ya kujivunia kokote ulikokwenda duniani.

Narejea tena katika zile chembechembe kinzani nilizoziainisha hapo juu. Wakati wote wa matamko na maazimio haya; wakati wote wa harakati za ukombozi wa ndani ya nchi na nje; wakati wote tukipigania usawa wa binadamu na umoja wa Afrika, chembechembe za mauti zilikuwa nazo ziko kazini, zikiguguna mithili ya panya wagugunao nafaka isiyolindwa vyema. Wapinga maendeleo tumekuwa nao siku zote, na baadhi yao ni wale waliofanya kazi kwa karibu sana na Mwalimu Nyerere. Baadhi yao aliwaamini mno na kuwakweza katika nafasi mbalimbali.

Hapa ndipo tunakutana na ile safari niliyoitaja ya mtoto anayeanza maisha kuelekea mauti au maisha ya adha kutokana na afya mbovu. Zile chembechembe za mauti alizoshindwa kuziona Mwalimu, au alizoziona lakini akadhani hazitakuwa na nguvu mbele ya safari, hatimaye zilijijenga, zikakomaa, na taratibu zikaanza kubomoa kila alichokuwa amekijenga kwa miaka mingi. Leo zinatawala.

Zinatawala kila idara ya maisha yetu. Zimeshika asasi za uchumi, hasa baada ya kubinafsisha kila kiwanda muhimu alichokijenga Nyerere. Imekuwa mpaka ni kichekesho kichungu, kwamba tunaweza kutangaza “Kilimo Kwanza” wakati hatutengenezi hata panga nchini. Viwanda vya nguo vimefungwa, tunaingiza mitumba (halafu eti tunatafuta vazi la taifa, bila kuwa na nguo). Viwanda vya kutengeneza mashine (Mang’ula na Kili Machine Tools) tumevifunga. Tumekuwa taifa lisilojua kuunda kitu.

Chembechembe hizo zimekamata medani ya siasa kwa kununua michakato yote ya uchaguzi na kuweka mawakala wake katika nafasi au ngazi za uamuzi. Leo nafasi za uwakilishi zinanunuliwa na kuuzwa sokoni, mchana kweupe.

Tunasikia kelele nyingi kutoka kwa watu wanaojiita na kuitwa “wapambanaji dhidi ya ufisadi” ambao tunajua majuzi tu walikuwa sokoni wakiuza na kununua nafasi za uwakilishi. Hata hiyo, dhana ya mapambnao dhidi ya ufisadi imepoteza maana, imezaa kebehi. Siasa zetu sasa, tukubali, ni soko la mitumba: chagua ule unaonukia vizuri zaidi ya mingine.

Chembechembe hizo zimemiliki elimu ya watoto wetu, kwa maana kwamba watoto wa walalahoi wanasoma shule zao, na watoto wa wakubwa wanasoma shule zao. Hivi punde tutakuwa na mataifa kadhaa ndani ya nchi moja kutokana na elimu wanayopewa watoto wa matabaka tofauti. Shule za walalahoi ndiko limejengeka soko jingine, lile la mitihani inayouzwa kama ile mitumba. Wanaonunua ni wale wale walionunua uwakilishi na utawala, wale wale waliokamata uchumi, chembechembe za mauti zilizomea tangu enzi za Mwalimu. 

Niliwahi kuandika kwamba jambo la mwisho linalomzuia binadamu aliyechanganyikiwa asivue nguo na kuingia mtaani akiwa uchi ni haya, au soni. Tone la mwisho la haya likikauka, nguo ya kwanza inavuliwa. Sasa tunayaona: Mara “watumishi wa umma” wamegawana nyumba za umma; mara rais kajimilikisha mgodi wa taifa;  mara wameingia Benki Kuu na kuchota fedha zilizoelezwa na waziri kuwa hazina mwenyewe; mara waliokwapua hizo fedha wamezirejesha, halafu basi; mara  wabunge wanataka posho ili kuziba mapengo ya madeni yanayotokana na mikopo mikubwa waliyochukua bila hesabu; mara spika ajisemee maneno ya ajabu… haya (soni) imekauka, tunaanza kuchojoa. 

Napenda nieleweke. Ninachosema ni kwamba kupotea kwetu kumeanzia mbali, tangu enzi za Mwalimu. Ni kwamba tu kila utawala mpya umekuwa ukiimarisha zile chembechembe za mauti badala ya kuimarisha chembechembe za uhai, na ndiyo maana afya yetu ni ya ovyo mno, tu hoi, hata kama hatujafa. 

 

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Jenerali Ulimwengu
ulimwengu@jenerali.com
www.jenerali.com

Jenerali  Ulimwengu ni Mwanajopo la Wataalam la Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Maoni ya Wasomaji

Naamini mgongano huu unapelekea kuwa na mawasiliano kama ya ujenzi wa mnara wa babeli! wanaopambana na ulafi wa wenzao nao ni walafi wa kesho au wa jana.Na ukitaka kujua ni usanii tu ndo uliobaki basi waambie hao wanaojiita wapambanaji wajitoe kwenye hilo kapu lililooza na waache nyadhifa zao zote,watakumeza kama sio kukutafuna! Hongera jenerali wetu naomba utueleze tufanye nini ili jinamizi hili tulishinde.

Point taken  Jenerali, ni Watanzania wachache wanaelewa haya.

Naona umeleza vizuri kabisa.Unatia matumaini kwamba uozo tulionao tunaweza kukabidi!
Je mchakato wa katiba utasaidia kupunguza uozo huu?

Kwa Kweli ndugu Ulimwengu hizi makala unaziandika kwa mantiki ya hali ya juu ...kwa mtu asiye na maono huenda akadhani unakosoa utawala wa awamu fulani na si kama unavyosema mchakato wa uongozi wa taifa. Nakupongeza

Nimeipenda sana hii Jenerali..."Kilimo Kwanza wakati hatutengenezi hata panga nchi!" Ni bahati mbaya kuwa tumekuwa taifa la watu wanaolaumu bila kuangalia chanzo cha tatizo. Tumekata tamaa mpaka tunasikitisha. Asante kwa kutufungua macho. Naamini utaendeleza makala hii katika toleo lijalo. Ubarikiwe sana!

Toa maoni yako