Makala
Rai ya Jenerali
Tukifanya upuuzi juu ya Katiba, tutakuwa tunarudia upuuzi juu ya ‘kuhamia Dodoma’
Jenerali Ulimwengu
Toleo la 232
28 Mar 2012

HADI sasa, ujumbe ambao nimekuwa nikijaribu kuwasilisha ni kwamba nchi yetu imekumbwa na mitafaruku ya kutoelewana miongoni mwa watu wake, na kwamba mitafaruku hii, ikiangaliwa kwa makini, inatuashiria kwamba tumepotea, tena tumepotea sana.

Nimetoa mifano kadhaa inayoonyesha jinsi tulivyopotea, lakini mingine mingi inaweza kuongezwa. Kadri nitakavyoendelea kutoa maoni yangu ndivyo nitakavyokuwa nikitoa mifano mingine, mingi ikiwa ni ile ambayo msomaji mwenyewe anaijua lakini ambayo inastahili kurejewa na kudurusiwa hadi ufumbuzi upatikane.

Lakini kwa sasa napenda kurejea msimamo wangu kuhusu mchakato wa kuandika katiba mpya au kufanya marekebisho ya katiba. Ninavyoona mimi, hatujafikia mwafaka juu ya nini tunataka kukifanya, baina ya kuandika katiba mpya na kufanya marekebisho ya katiba iliyopo. Haya ni mambo mawili tofauti kabisa, lakini sipati kusikia mjadala makini kuhusu ni nini hasa tunataka kufanya.

Malumbano yamekuwa juu ya masuala ambayo, pamoja na umuhimu wake, yangesubiri hadi pale tunapokubaliana ni nini hasa tunataka kufanya. Kama tunachotaka ni kuandika katiba mpya, hatuna budi kujipanga kwa shughuli nzito, ya kina, na yenye mtazamo wa mbali. Tutakuwa tumejua kwamba nia yetu ni kuandika waraka ambao unaliangalia Taifa hili kwa miwani inayotazama mwaka 2112 na mbele yake.

Lakini kama tunachotaka ni kuchomoa vifungu na kuchomeka vingine – kunyofoa na kunyofeka – hatuna sababu ya kupoteza muda na fedha kwa shughuli nyepesi hivyo.

Kazi hiyo wanaweza wakakabidhiwa wataalamu wachache wenye weledi wa kisheria na wasikivu wa hoja za kisiasa ambao watanyofoa na kunyofeka kadri wanavyosikia kelele za wanasiasa, na tukapata viraka vya kutosha kutusogeza mbele kwa miaka kadhaa, labda mwaka 2015au 2020, hadi hapo itakapoibuka mandhari mpya ya kisiasa itakayoruhusu shughuli ya kuandika katiba mpya ianze kwa dhati.

Nasema hatuna budi kuamua kwa dhati tunataka kufanya nini, la sivyo tutajikuta hatujafanya hata kimoja katika haya mawili. Nchi hii imejaa mifano ya hali hiyo, ambayo sote tunaitambua. Mfano mmoja ni riwaya ya makao makuu ya nchi kuwa Dodoma, baada ya ‘uamuzi’ uliofanyika miaka takriban 40 iliyopita. Hadi leo, baada ya miaka 40, hii imebaki ni riwaya: Makao makuu hayako Dodoma, wala wakuu hawakai Dar es Salaam. Wamo safarini siku zote kati ya Dodoma na Dar es Salaam.

Ungeniuliza leo ya wapi makao makuu ya serikali ya Tanzania, ningesema yamo njiani kati ya Dodoma na Dar es Salaam.

Haiwezekani kwamba wakuu wa serikali hawalioni hili, au kwamba hawatambui uzito wa gharama zinazosababishwa na safari za kila siku, hususan katika mazingira yetu ambamo posho limekuwa ni suala la kifalsafa.  Je, inawezekana kwamba mpangilio huu unaendelezwa ili watumishi wanaohusika waweze kulipwa posho na masurufu ya safari? Nitarudia ule msemo wa Kihaya: Ka kitandugaho!

Fursa ya kuwa na mpangilio wa makao makuu yanayodumu safarini ilipatikana kwa sababu ya kutokubaliana (miongoni mwa viongozi wa wakati ule) makao makuu yawe wapi. Rais Julius Nyerere alitaka sana kuhamisha makao makuu na kuyapeleka Dodoma. Alitoa sababu zake hadharani, zikajadiliwa kidogo, na Mwalimu akatangaza kwamba hoja imekubaliwa.

Lakini hoja hiyo haikuwa imekubaliwa kwa dhati. Maoni ya wananchi yalitafutwa kwa kupitia uratibu wa maoni ya wanachama wa chama-tawala, TANU wakati huo. Hata uratibu huo ulifanyika kwa namna ambayo ilihakikisha ‘ushindi’ wa hoja ya Mwenyekiti. Ndani ya uongozi wa juu wakati ule, nakumbuka, walikuwamo watu ambao hawakukubali hata kidogo hoja ya kuhamia Dodoma, lakini hawakuthubutu kusema hivyo mbele ya Nyerere.

Matokeo yake ni kwamba shughuli za kujenga makao makuu mapya zilianza, shughuli nzito chini ya C. George Kahama na CDA. Mapesa chungu nzima yalitumika kufanya uchambuzi yakinifu, kuajiri wataalamu, kusafiri kwenda duniani kuona nchi zilizojenga makao makuu mapya (Brazil, Australia, nk). Ikulu ikajengewa makazi kijijini Chamwino, na Mwalimu akaonekana akienda kukaa huko na kupokea wageni wa dola.

Wizara mbili au tatu zikahamia Dodoma na zikawa zinafanyia kazi huko kwa muda. Viwanja vikatengwa kwa ajili ya makazi ya wafanyakazi wa serikali na mashirika yake. Watumishi wengi wa serikali wakaomba na kupewa viwanja ili waweze kujenga nyumba zao za kuishi watakapohamia “makao makuu” kikazi. Balozi za kigeni nazo zikapewa viwanja ili zijenge na zihamie Dodoma kuifuata serikali mwenyeji.

Kisha, kimya! Wizara zile mbili au tatu zilizokwisha ‘kuhamia’ Dodoma zikarudi Dar es Salaam. Watumishi waliokuwa wameomba na kupata viwanja wakavitelekeza, na kuanza kutafuta viwanja Dar es Salaam. Hata Mwalimu, mwenye wazo lake, akabaki Ikulu ya Magogoni na nyumbani kwake Msasani, na Chamwino pakawa ni mahali pa mapumziko.

Kuona hivyo, mabalozi wakaachana na viwanja vya Dodoma, na wale waliohitaji majengo mapya wakayajenga Dar es Salaam ( mfano Umoja House, majengo mapya ya balozi za Marekani, Nigeria, Brazil, Uturuki, Kenya, Sahara Magharibi, Rwanda, Saudia na kadhalika).

Bila shaka, mabalozi hawa walikwisha kutung’amua kuwa watu tunaopenda upuuzi kiasi kwamba tumeufanya upuuzi kama nyenzo kuu ya utendaji wetu.

Waliiona mapema kabisa hasara watakayopata iwapo wangeendekeza upuuzi wetu, nao wakafanya maamuzi yaliyopasa. 

Sasa tumo njiani kati ya Dodoma na Dar es Salaam (na mabalozi wanatufuata kila likizinduliwa Bunge), na shughuli pekee inayonufaika hapa ni kulipana posho miongoni mwa watumishi. Taifa halijapata faida yo yote, bali hasara linazoingizwa ni kubwa, na mikanganyiko inayotokana na upuuzi huu mwingine si haba.

Kumbuka, mwanzo mwa simulizi hii nimesema kwamba hapakuwa na makubaliano ya dhati juu ya kuhamia Dodoma, ukiacha wimbo maridadi kabisa wa King Kiki, “Oh, Dodoma, Dodoma Capitale”). Wanasiasa hawakukubaliana, lakini hawakuthubutu kumwambia Nyerere hatuendi. Walijua atazeeka, ataondoka kwa njia moja au nyingine, na wazo lake litaondoka naye.

Sasa, dhahiri, Mwalimu hayupo tena, na wazo lake limekufa, lakini limefufuka upya kama mradi wa ‘walaposho’.

Huo ni uzoefu uliotokana na ‘uamuzi’ ambao haukuwa uamuzi, na matunda yake ndiyo hayo. Sasa tunaingia katika ‘uamuzi’ mwingine, ambao kwangu mimi ni dhahiri kwamba si uamuzi lakini watu wengi hawathubutu kusema wazi kwamba hakuna uamuzi.

Iwapo watawala wetu na wanasiasa kwa ujumla hawatafanya uamuzi wa dhati kuhusu hili, tutabakia hivi tulivyo, bila uamuzi, halafu tutatangaza kwamba tunafanya kitu fulani kuhusu katiba (ama kuiandika upya ama kumyofoa na kunyofeka) lakini matokeo yake hayatahalalisha matumizi makubwa ya fedha yatakayokuwa yamefanyika. Utakuwa ni mradi mwingine wa ‘ulaji.’ kama Dodoma tu.

Nitaonyesha kwa nini nasema kwamba, kama ilivyokuwa kuhusu “kuhamia Dodoma”, hakuna uamuzi ulio bayana kuhusu kuandika katiba.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Jenerali Ulimwengu
ulimwengu@jenerali.com
www.jenerali.com

Jenerali  Ulimwengu ni Mwanajopo la Wataalam la Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Maoni ya Wasomaji

Asante kwa hayo unayotabainisha. lakini nchi hii viongzi wetu wote ni wanafiki wchumia tumbo hawana nia ya dhati kuendeleza nchi hii bali kushibisha matumbo yao angalau kwa leo bila kujali kesho wajuku wao watishi vipi.
Nitoe mfano wa elimu. Kuna kiongozi gani asiyejua kwamba watoto walio wengi wanamaliza shule za msingi sekondari bila kujua chochote tatizo hili lipo muda mrefu lakini hakuna anaye chukua hatua za thati kurekebisha.

This was nyerere, your father of the nation, What I know he did nothing except upuuzi

Kwanza naomba nikupongeze ndugu Ulimwengu kwa kuthubutu ,ambapo waandishi wenzio hawawezi, siyo kwa kutofahamu bali WAOGA>
  Kwa ndugu Sherly, Our father of the nation, hakuwa mupuuzi. huko ni kukosa kuangalia mambo kwa upana itoshe tu kusema Kidole kimoja hakivunji chawa.
Kwa wale walengwa wa maada hii hasa serikali na hasa JK hatupaswi kurudia makosa ya Dodoma kuwa makao makuu ambayo hayajawa hadi kesho au mwisho wa dunia kama upo.
Historia itakuhukumu JK kama utafanya KATIBA iwe kiini macho, Watanzania tunataka Katiba ya kweli inayofanana na umri wa Taifa letu  na inayoyuwezesha kufikia malengo ya maendeleo tunayohitaji.

Kwanza naomba nikupongeze ndugu Ulimwengu kwa kuthubutu ,ambapo waandishi wenzio hawawezi, siyo kwa kutofahamu bali WAOGA>
  Kwa ndugu Sherly, Our father of the nation, hakuwa mupuuzi. huko ni kukosa kuangalia mambo kwa upana itoshe tu kusema Kidole kimoja hakivunji chawa.
Kwa wale walengwa wa maada hii hasa serikali na hasa JK hatupaswi kurudia makosa ya Dodoma kuwa makao makuu ambayo hayajawa hadi kesho au mwisho wa dunia kama upo.
Historia itakuhukumu JK kama utafanya KATIBA iwe kiini macho, Watanzania tunataka Katiba ya kweli inayofanana na umri wa Taifa letu  na inayoyuwezesha kufikia malengo ya maendeleo tunayohitaji.

Toa maoni yako