Dar kutuma wabunge makini Afrika Mashariki

TANZANIA itapeleka timu ya wabunge makini katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Aprili mwaka huu, Raia Mwema limeambiwa.

Bunge la tatu la Afrika Mashariki linamaliza muda wake Juni mwaka huu na tayari mabunge ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yamepewa taarifa kuhusu kutakiwa kufanya uchaguzi wa wabunge kabla ya Juni mwaka huu.

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, ameliambia gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa wamekwisha kupokea barua ya kuwataka waanze mchakato wa kupata wabunge na tayari vyama vya siasa vimearifiwa.

“Sisi, kama mambo yote yataenda kama yalivyopangwa, tunatarajia kufanya uchaguzi wa wabunge wa EALA Aprili mwaka huu wakati wa Bunge la Bajeti.

“Muda si mrefu tutakutana kwa ajili ya kufanya makubaliano ili kujua idadi ya wabunge kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa kutoka Upinzani. Tanzania ina nafasi tisa na zinatakiwa kuzingatia vyama, jinsia na Muungano.

“ Kwenye Bunge lililopita, CCM ilikuwa na nafasi saba na Upinzani ulikuwa na wabunge wawili. Itabidi tukae chini na kutengeneza utaratibu wa kujua idadi itakavyokuwa. Tutatoa taarifa wakati ukifika,” alisema Ndugai.

Timu ya ushindi

Gazeti hili limeambiwa kwamba Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli, amedhamiria kuhakikisha kuwa safari hii Tanzania inapeleka watu makini kuiwakilisha kwenye EALA.

Sababu kubwa inayoelezwa kusababisha mwelekeo huo mpya wa Rais na chama chake kwa ujumla ni ukweli kwamba Bunge linalokuja linaweza kuwa ndilo lenye kukamilisha suala la kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki (East Africa Federation).

Raia Mwema limeambiwa na vyanzo vya kuaminika ndani ya CCM na Ikulu kwamba huenda safari hii chama hicho kikabadili utaratibu wake na kuchuja chenyewe majina kabla ya kuyapeleka bungeni kupigiwa kura na wabunge.

Katika utaratibu wa nyuma, wagombea ubunge walikuwa wakichukua fomu na kupigiwa kura na wabunge pasipo kujali idadi yao lakini sasa kuna uwezekano Bunge likapelekewa majina ya idadi kamili ya wabunge wanaohitajika.

“Nimeambiwa waombaji watapewa fomuna CCM na halafu watazijaza na zitajadiliwa na Kamati Kuu (CCM). Kama CCM itatakiwa kupeleka majina sita, basi CC itapeleka majina sita yanayofaa zaidi bungeni.

“Hii maana yake ni kwamba wabunge watapigia kura majina ambayo yameletwa na Kamati Kuu. Hatua hii itasaidia chama kupata watu wazuri hata kama si wanasiasa maarufu,” Raia Mwema limeelezwa.

Hata hivyo,  Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (Itikadi na Uenezi), Humphrey Polepole, alisema wanasubiri kwanza maelekezo kutoka bungeni kabla ya kuzungumza chochote.

“ Kama unavyojua haya mambo huwa yanaanzia bungeni kwa Spika. Wao watatupa maelekezo na sasa kuanzia hapo ndipo chama kitaweza kuzungumza na kutoa mwelekeo wake,” alisema Polepole.

Hata hivyo, mmoja wa wabunge wa EALA wanaomaliza muda wao mwaka huu, ameliambia gazeti hili kwamba endapo chama kitatumia utaratibu huo, wagombea watakuwa na nafuu.

“Kwanza niseme kwamba hata hivi sasa ile pitapita tuliyokuwa tumeizoea zamani haipo. Kwa mfano, kwenye huu Mkutano wa Bunge uliomalizika Dodoma, ungeona wanaotaka nafasi wakijipitisha.

“Lakini naona kama kuna ganzi hivi. Hakuna watu wanaopita waziwazi na wabunge pia hawalazimishi ‘kuonwa’ kama ilivyokuwa zamani. CCM ikifanya hivi itakuwa imefanya uamuzi wa maana,” alisema mbunge huyo ambaye hata hivyo hakutaka kutajwa jina.

Hali ikoje Upinzani?

Raia Mwema limeambiwa kwamba tayari kuna mchakato ndani ya vyama vya Upinzani kuhakikisha vinapata pia watu makini wa kuviwakilisha.

Ingawa hizi ni hatua za awali, majina mawili yanayotajwa zaidi katika duru za upinzani ni Profesa Kitila Mkumbo wa chama cha ACT-Wazalendo na Julius Mtatiro kutoka Chama cha Wananchi (CUF).

Hata hivyo, bado kuna utata kuhusu idadi hasa ya wabunge wa Upinzani watakaopatikana kupitia uchaguzi wa safari hii.

Idadi ya wabunge saba kwa CCM na wawili kwa Upinzani ilitokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, lakini mwaka 2015 Upinzani umepata kura nyingi zaidi kuliko uchaguzi uliopita.

Kuna uwezekano mkubwa kwamba Upinzani unaweza kupata nafasi moja zaidi na hivyo; vyama vya Chadema, CUF na ACT Wazalendo vinaweza kupata nafasi moja kila kimoja.

Katika uchaguzi wa EALA mwaka 2012, Chadema haikupata mbunge, ingawa chenyewe ndicho kilikuwa chama kikuu cha Upinzani na ndicho kilichokuwa kimeunda Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Baada ya kukosa fursahiyo, kwa sababu wabunge wa CCM walitumia wingi wao kumnyima mbunge wa Upinzani wasiyemtaka, aliyekuwa mgombea wa Chadema, Anthony Komu, alikwenda mahakamani kupinga matokeo hayo.

Katika kesi iliyofunguliwa katika Mahakama ya Afrika Mashariki mwaka 2012, pamoja na mambo mengine, Komu alihoji utaratibu unaotumika kupata wabunge wa EALA nchini, ambao ni kinyume cha utaratibu unaotumiwa na nchi nyingine.

Kwa mfano, Komu alisema ibara ya 50 ya Katiba ya EALA inataka nafasi za ubunge zigawanywe kutokana na uwiano wa nguvu za vyama katika mabunge ya nchi wanachama lakini hali ni tofauti Tanzania.

Komu pia alihoji kama ni halali kwa chama kinachounda kambi rasmi ya Upinzani bungeni kutokuwa na mbunge kwenye EALA na badala yake chama kidogo kupewa nafasi hiyo.

Ingawa Komu alishinda katika kesi hiyo, Mahakama ilisema kwamba kesi hiyo haikupaswa kufunguliwa na mtu binafsi bali taasisi; na hadi leo marekebisho aliyokuwa akiyalilia mbunge huyo wa sasa wa Moshi Vijijini bado hayajafanyiwa kazi.

Gazeti hili limeambiwa kwamba Ukawa itabidi iamue kuhusu nani ataenda EALA, kwa kutazama uwakilishi wa vyama, Zanzibar na nguvu na ushawishi wa wabunge wanaotakiwa kuwakilisha nchi kwenye Bunge hilo.

Katiba ya EALA inataka wabunge wake wawe wanatokana na vyama vilivyo bungeni na gazeti hili limeambiwa chama cha ACT-Wazalendo kinajipanga kushiriki katika uchaguzi huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *