WAZIRI Mkuu mstaafu Joseph Warioba ameiambia Raia Mwema wiki hii kwamba dhamiri yake ni safi na hatishwi na tetesi kwamba atakamatwa wakati wowote kujibu tuhuma za ubadhirifu.
Akizungumza na baadhi ya wanahabari wiki hii, Warioba alisema amesikia kwamba tuhuma hizo ni za ubadhirifu wa dola za Marekani milioni tano (Shilingi bilioni tano) anazodaiwa kufuja katika kampuni ya usafishaji dhahabu ya Mwananchi Gold.
“Yapo madai nimetumia madaraka yangu vibaya na kujichotea dola milioni tano zilizotolewa na Benki Kuu kwenda katika kampuni ya Mwananchi Gold Ltd.
“Sasa kuna uvumi kwamba nitakamatwa. Siku moja kuna mkubwa (kiongozi wa juu serikalini) mmoja alinifuata akaniambia nina ujumbe wako. PCCB haina mpango wa kukukamata.
“ Lakini kuna mkubwa mwingine siku nyingine alinufuata akaniambia kuna mpango wa kukukamata, lakini PCCB hawajui. Hawa wote nawaamini…mimi sijui lakini let them come (waache waje). My conscious is clean (dhamiri yangu ni safi),” alisema Jaji Warioba.
Katika kuonyesha kwamba tuhuma dhidi yake hazina nguvu, Warioba alionyesha baadhi ya nyaraka za Mwananchi Gold ambazo ni pamoja na zila za kuundwa kwake.
Hizo ni pamoja na Mkataba wa Maridhiano (MoU) kati ya wabia wa mradi huo na namna matumizi ya fedha yalivyofanyika.
Mkataba huo wa maridhiano unahusisha wabia wa mradi huo, ambao ni Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni ya Ma-CE s.r.I ya nchini Italia.
Katika maelezo yake, Jaji Warioba anasema jambo la kuzingatia wakati wote ni ukweli kwamba mradi huo ni wa Serikali na wenye manufaa makubwa kwa Taifa, japokuwa umeanza kutibuliwa na upepo wa kisiasa.
Anasema mara baada ya mchakato wa kuanzisha kampuni ya kusafisha dhahabu kukamilika na kuridhiwa na wabia, dola milioni 1.875 za Marekani zilitolewa, ambazo zilihusisha gharama ya kiwanja chenye ukubwa wa zaidi ya eka 30, kodi ya ongezeko la thamani, ushuru wa forodha na malipo kwa ajili ya huduma za kampuni ya uwakili ya Nyalali, Warioba, Mahalu & Law Associates.
Anatilia shaka kuwa inawezekana mradi huo wenye manufaa makubwa kwa Taifa kwa kuwa kusafisha dhahabu nchini kuna faida kubwa kuliko kusafirisha dhahabu ghafi, umezongwa na wingu la kisiasa zaidi.
“Kwanza Mwananchi Gold ni kampuni iliyotokana na uamuzi wa Serikali kwa lengo la kutekeleza sera ya Taifa inayosisitiza kutosafirisha bidhaa ghafi. Lakini Serikali ikaendesha mchakato wa mradi huu kupitia BoT na NDC.
“Serikali ilikuwa na hisa 35, kati ya hizo hisa 20 ni za BoT, hisa 15 ni za NDC na mwekezaji wa nje ana hisa asilimia 20 na hisa zilizobaki ziwe chini ya kampuni mwavuli, itakayokusanya kampuni nyingine ndogondogo.
“Kutokana na kuhitajika kwa kampuni moja itakayojumuisha hisa za kampuni ndogondogo, ikaanzishwa kampuni ya Mwananchi Trust Ltd., alisema Warioba katika mahojiano yatakayochapishwa kwa kina katika toleo lijalo la Raia Mwema.
Anasema kampuni hiyo ya Mwananchi Trust Ltd inajumuisha hisa 30 za kampuni ndogo ambazo ni Umoja Entertainment yenye hisa asilimia 5, VMB yenye hisa asilimia 5, YM Holdings yenye asilimia 5 za hisa pia na CCM Trust Company yenye asilimia 15 ya hisa.
Kampuni hizo ndogo kupitia kampuni ya Mwananchi Trust Ltd zinamiliki asilimia 30 ya hisa ndani ya Kampuni ya Mwananchi Gold Ltd, wakati BoT ikiwa na hisa 20, NDC hisa 15, mwekezaji wa kigeni hisa 20 na Mwananchi Trust Co. Ltd husa 30. Hisa zilizosalia bado hazijagawiwa.
Akionyesha kusikitishwa na hatua ya BoT kujitoa katika mradi huo wa kusafisha dhahabu, Jaji Warioba anasema inawezekana Serikali imeishinikiza BoT kujitoa.
“Sijui kwa nini wamejitoa…wanasema hawapaswi kufanya biashara lakini ni jukumu la Benki Kuu nchini kushughulika na dhahabu na hiyo si hapa tu, bali hufanyika katika nchi nyingi duniani. Dhahabu husaidia hata kuimarisha sarafu nchi husika inapoyumba,”
Baada ya kujitoa kwa BoT, kwa sasa uongozi wa Mwananchi Gold Ltd unasaka mbia atakayenunua hisa za BoT pamoja na kulipa madeni ambayo ni fedha zilizotolewa na benki hiyo kwa ajili ya kufanikisha mradi huo.
Baada ya mbia huyo mpya kupatikana na kulipa madeni Mwananchi Gold katika BoT, benki kuu inatarajiwa kuachia hati ya kiwanja ili iwe mikononi mwa Mwananchi Gold.
Toa maoni yako