Diplomasia ya Uchumi itazame DR Congo

KUNA dalili za kuamini kwamba hali inaweza kuchafuka na kuwa mbaya zaidi katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Tatizo lililopo ni kwamba taifa hilo lilitakiwa kufanya uchaguzi wake kwa mujibu wa Katiba yake mwaka huu, lakini kwa sababu ya kile ambacho wapinzani wa Rais Joseph Kabila wanakiita figisufigisu, uchaguzi huo uliahirishwa.

Kinachoendelea sasa nchini DRC ni pigo lingine kwa demokrasia ya bara la Afrika. Kama kuna kitu kibaya ambacho kinarejea Afrika kwa kasi siku hizi, ni ile tabia ya watawala kung’ang’ania madaraka.

La kwanza ambalo tunapenda kulisisitiza ni kwamba wananchi wa DRC wana haki ya kujiamlia hatma ya nchi yao pasipo kuingiliwa na nchi yoyote ya kigeni.

Hata hivyo, ukweli ulio wazi ni kwamba wananchi wa Congo hawataachwa na mabeberu waamue hatma yao –kama ambavyo imekuwa kwa takribani miaka 50 iliyopita.

Ndiyo sababu, kwa namna ya kipekee kabisa, tunaiomba serikali yetu isikubali kuachwa nyuma au kupitwa na mambo yanayoendelea ndani ya taifa hilo.

Kiuchumi, DRC ni miongoni mwa wabia muhimu wa kibiashara wa Tanzania. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka jana, DRC na Zambia peke yao, wanachangia mizigo inayopitishwa kwa kutumia bandari ya Dar es Salaam kwa zaidi ya asilimia 70.

Wakati hali ikiwa hivyo, tunafahamu pia kwamba watumiaji wengine wakubwa wa bandari yetu, Burundi, nao wako kwenye machafuko; jambo ambalo limeathiri ufanyikaji wa kibiashara.

Kwa sababu sasa tumeamua kufuata kinachoitwa Diplomasia ya Uchumi, tunadhani Tanzania haiwezi kukubali kuachwa nyuma wakati wengine wakitafuta suluhisho la kipindi kifupi, cha kati na cha muda mrefu kuhusu DRC.

Tusikubali kuonekana watu wenye upande kwenye yanayoendelea nchini humo kwa sasa (ingawa huo nao ni upande kwa namna fulani), kwa sababu mwisho wa siku, mteja wetu anatakiwa kuwa taifa la DRC.

Kwa vyovyote vile, tunawajibika –kwa sababu ya maslahi yetu ya kiuchumi kwa DRC, na ukweli kwamba matatizo yakiwa makubwa wimbi la wakimbizi litakuja kwetu, kuhakikisha tunashiriki kwenye kuhakikisha mambo hayaharibiki.

Hii ni kwa sababu, kwa jirani kukiungua, kwako si salama.

One thought on “Diplomasia ya Uchumi itazame DR Congo”

  1. Osman says:

    Mmmmhimu. ..DRC ni jirani Wa haja zote,..  Is a strategic neighbor,.. Kujitenga na mambo ya DRC ni kujidogosha../ natamani tuambae kadri umbali na zaidi ya ule aliotufikisha mwalimu kidiplomasia..  Africans have to feel our positive presence kama zamani jamani,.. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *