Makala
Dk Hosea na kauli tata za EPA
Chesi Mpilipili
Toleo la 057
26 Nov 2008

WIKI iliyopita, tumesikia tena yale maneno yanayoashiria kuwa nchi yetu inaelekea kuwa ni pepo ya wahalifu ambamo uhalifu unalipa ili mradi tu uhalifu wenyewe uwe mkubwa wa kutosha na si ule wa kumuibia jirani kuku.

Yale maneno ambayo sasa yana muelekeo wa kutaka kuwaaminisha Watanzania kuwa mafisadi sio watu wa kawaida na hatua zinazopaswa kuchukuliwa dhidi yao lazima ziwe tofauti na hatua zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya wezi wengine wa fedha zetu.

Kwanza tulisikia Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hosea, akikaririwa na vyombo vya habari akirudia maneno tuliyokwisha ambiwa huko nyuma kuhusu mafisadi kuwa na nguvu na uwezo wa kuyumbisha nchi.

Akitoa mada kwenye semina iliyohusisha wajumbe wa kamati za maadili za vyuo vikuu tisa nchini, Dk. Hosea alisema kuwa watuhumiwa wa ufisadi wa EPA ni watu wenyewe nguvu na wakipelekwa wote mahakamani kwa pamoja nchi inaweza kuyumba.

Tukumbuke kuwa aina hii ya kauli ilipata pia kutolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; tena bungeni pale alipotamka kuwa mafisadi walikuwa ni watu hatari kwa usalama wa nchi yetu na walipaswa kushughulikiwa kwa tahadhari ili wasije wakaiangusha nchi.

Ni wazi kuwa maneno haya yanayorudiwa rudiwa kutamkwa na wakubwa wetu yana hatari ya kujenga usugu kwenye fahamu za Watanzania kuhusu mafisadi kuwa watu wasiowezekana.

Hata hivyo, katika kilichoonekana kama ni 'kuihariri' kauli aliyotoa, siku mbili tu baadaye kwenye kongamano la wadau wa mapambano dhidi ya rushwa kwenye ukumbi wa Karimjee, Dk. Hosea alinukuliwa akisema serikali haiogopi mtu na kwamba kiama cha mafisadi vigogo ni mwezi ujao; kwa maana ya mwezi Desemba.

Tukumbushane tu hapa kwamba mwezi Desemba ndio mwezi ambao huko nyuma Mkurugenzi huyu alipata kutoa nafuu kwa waliotuhumiwa ufisadi kula Krismasi yao kwa amani kabla zahama haijawashukia. Labda safari hii kutakuwa na tofauti na mafisadi watalia krisimasi zao wakijisaidia kwenye mitondoo huko rumande!

Kauli ya Dk. Hosea ya kwamba serikali haiogopi mtu na kututaka tusubiri mwezi ujao ili kuona kiama cha watuhumiwa mapapa wa ufisadi pia inatupa picha kuwa hawa tunaowaona wakipelekeshwa kati ya Kisutu na magereza yetu ni vidagaa tu, na kama tunataka kuyaona mapapa yenyewe ya ufisadi, basi, tusubiri mwezi ujao serikali itakapofanya vitu vyake.

Ni vyema Mkurugenzi huyu wa TAKUKURU ametoa kauli hii ya kututaka tusubiri Desemba ili kuona mambo, iwe imemtoka kwa bahati mbaya ama kwa kudhamiria, maana tangia hapo wengi wetu tuliishanza kuwa na wasiwasi kama kweli hawa tunaowaona wakisimamishwa kizimbani ndio waliokuwa wakisemekana kuwa wana uwezo wa kuifanya nchi iyumbe.

Kumekuwa na taarifa kadhaa juu ya watuhumiwa wa EPA kutenganishwa na watuhumiwa wa makosa mengine walioko rumande wakisubiri uchunguzi wa kesi zao kukamilika. Imefanywa hivi, tunaambiwa, ili kuepusha uwezekano wa watuhumiwa hao kushambuliwa na wafungwa wengine wenye hasira dhidi yao kutokana na tuhuma zao za ufisadi.

Hawa watuhumiwa wengine wanajumlisha watuhumiwa wa ujambazi wa kutumia silaha, wabakaji na hata waliopoteza uhai wa wananchi wenzao, iwe kwa bahati mbaya ama makusudi. Wote hawa tunaaminishwa kuwa wanaweza kuwashambulia watuhumiwa wa ufisadi wa EPA. Kama hili ni kweli, basi ni jambo la kushangaza.

Kwa mujibu wa taarifa za mitandao mbali mbali, magereza mengi ya nchi zilizoendelea yana utaratibu maalumu wa kuwaweka mbali na wafungwa wengine watuhumiwa wa ubakaji wa watoto ambao hujulikana zaidi kwa jina la pedophiles na akina mama.

Hii inatokana na kanuni isiyo rasmi ya wahalifu wengi wa nchi hizo kuwa tayari kufungwa na mhalifu mwenzao mwingine yoyote, lakini sio aliyefanya uhalifu dhidi ya watoto na akina mama.

Mfano mzuri ambao, hata hivyo, hauna mwisho mwema ni wa mfungwa Peter Andrew Budjoso wa jimbo la New South Wales, Australia ambaye mwaka 1990 alihukumiwa kifungo cha miaka miwili na nusu kutokana na kosa la kubaka watoto watatu wa kiume kwa nyakati tofauti.

Mwaka 1991 mfungwa huyo alihamishiwa gereza la Silverwater ili kumalizia kifungu chake, gereza ambalo lilikuwa na utaratibu wa kuruhusu baadhi ya wafungwa kuajiriwa kwa sharti la kurudi kulala gerezani usiku.

Inaelezwa kuwa usiku mmoja katika mwaka huo mfungwa huyo aliingiliwa kwenye chumba chake na wafungwa wenzake wanne waliojifunika sura ambao walimpiga kwa nondo, mateke na ngumi hadi akapoteza fahamu kutokana na tu na yeye kuwa pedophile.

Pengine habari hii ingeishia hapo hapo ingeleta maana fulani lakini inaelezwa kuwa baada ya kutoka jela Peter Andrew Budjoso alifungua mashitaka dhidi ya serikali ya jimbo la New South Wales kwa kushindwa kumlinda akiwa chini ya himaya ya magereza huku ikielewa kuwa kwake pedophile kulikuwa kunamuweka kwenye hatari ya kushambuliwa na wafungwa wenzake, kama ilivyotokea. Alishinda kesi.

Pamoja na serikali ya jimbo la NSW kukata rufaa mahakama ya rufaa hadi mahakama kuu dhidi ya uamuzi huo, bado hukumu hiyo ilisimama na mnamo Machi, 2007 jopo la majaji wa mahakama kuu, David Hodgson, David Ipp na John Basten liliiamuru serikali ya jimbo la New South Wales kumlipa Peter Budjoso fidia ya paundi 175,000 - karibu Shilingi milioni 350.

Hii ni hukumu iliyowagawa wananchi wa jimbo hilo kutokana na ukweli kwamba mwaka 1990 wakati mshitakiwa huyo alipokiri kosa na kutiwa hatiani, aliamuriwa kumlipa mmoja wa wahanga wa upuuzi wake paundi 14,000 tu, sawa na shilingi milioni 28 tu, kama fidia ya upuuzi aliofanyiwa!

Pengine ni 'vichekesho' kama hivi katika masuala ya sheria vilimvyomfanya muandishi wa riwaya wa zamani wa Kiingereza, Charles Dickens kumtumia Mr. Bumble, mmoja wa wahusika kwenye kitabu chake mashuhuri cha mwaka 1838 cha 'Oliver Twist' kumaka 'The Law is an …'  neno la mwisho likikupa uhuru wa kulitafsiri kama 'punda kihongwe' ama tafsiri mbaya zaidi isiyostahili kuandikwa hapa!

Nia yetu hapa sio 'kusherehekea' uhalifu; bali kuonyesha kuwa kwa wenzetu wahalifu pekee wanaostahili kutengwa na wahalifu wenzao ni wale wanaotuhumiwa kuharibu maisha ya watoto wanaojulikana kama pedophiles ili kuwakinga na hasira za wahalifu wenzao wengine.

Hapa kwetu, kama tunayosoma kwenye baadhi ya magazeti ni kweli, hali ni tofauti maana tunaaminishwa kwamba wahalifu wengine wote kuanzia majambazi wa kutumia silaha, wauaji, wakabaji na wabakaji wa watoto na akina mama wanaweza wakawekwa mahabusi moja na 'wakaishi kwa amani' lakini watuhumiwa wa EPA wakalazimika kutengwa katika kinachoelezwa kuwa ni 'kwa ajili ya usalama wao'!

Inaniwia vigumu kuamini kwamba wafungwa wetu huko ndani waliko wanaweza kuwa na hasira zaidi na wanaotuhumiwa kukwapua fedha za EPA kuliko walivyo na hasira na wanaotuhumiwa kubaka watoto wao, kiasi cha kuhitaji watuhumiwa hao wa EPA kutengwa mbali nao!

Hivi nchi yetu hii kuna anayeweza kuwa na hasira na anayedhaniwa kuiba fuko la fedha wakati tuna hata utamaduni wa kuwasifia wanaotumia ofisi za umma kujitajirisha; huku tukiwadharau wale wanaofikia hatua ya kustaafu wakiwa na maisha ya kawaida tu?

Tuna wasiwasi kwamba kama hawa ambao wanaelekea kuwa ni vidagaa, kama maneno ya Dk. Hosea ya kututaka tusubiri mwezi Desemba kuwaona mapapa wa ufisadi ni kigezo, wanaweza kupewa upendeleo wa kutengwa na mahabusu wenzao, je watakapokamatwa mapapa wenyewe?

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Chesi Mpilipili
chesimpilipili@gmail.com

Toa maoni yako