Mahojiano
Dk. Ndalichako: Naumizwa sana kuwafutia wanafunzi matokeo, lakini hakuna namna
John Daniel
Toleo la 226
15 Feb 2012
  • Asema uchunguzi kuhusu watahiniwa kuandika bongo fleva, matusi, kuchora wachezaji unaendelea
  • Wanafuzi wa darasa la saba kutumia karatasi maalumu kuanzia mwaka huu
  • Aweka wazi mfumo mzima wa usahihishaji mitihani hadi kutolewa matokeo

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) ni miongoni mwa taasisi za umma zinazokabiliwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa makumu yake hasa yanapotolewa matokeo ya mitihani yanayozua miguno ndani ya jamii. Wiki hii Mwandishi Wetu JOHN DANIEL, amefanya mahojiano maalumu na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dk. Joyce Ndalichako, pamoja na mambo mengine, kuelezea ufumbuzi wa miguno hiyo.

Raia Mwema: Baadhi ya watu wamekuwa wakiirushia lawama NECTA kuwa haitendi haki katika kusasahisha mitihani, ni mfumo upi mnaotumia kuanzia kutunga, kusahihisha hadi kutoa matokeo?

Dk. Ndalichako: Kwanza nawashukuru sana kwa uamuzi wa kutafuta ukweli pale mnapopata taarifa kama hizo na kutaka kuelimisha jamii kuhusu hali halisi. Kusema kweli tumepiga hatua kubwa sana katika utungaji, usambazaji, usimamaizi, usahihishaji wa mitihani hadi kutoa matokeo.

Nataka niwahakikishie na Watanzania wote, kuwa baraza linatenda haki katika kutimiza wajibu wake. Hakuna mtu yeyote anayeonewa wala hakuna upendeleo. Sisi kazi yetu kubwa ni kupima uwezo wa mwanafunzi kwa kuzingatia yale anayotakiwa kujifunza, ili mwisho wa siku tuwe na Taifa lenye wataalamu walioiva katika fani zao.

Tumeboresha sana utungaji wetu wa mitihani. Ni jambo ambalo limeyavutia hata mataifa ya nje kuja kujifunza kwetu tumefanyaje, na wametuomba tuwalekeze ni jinsi gani tumeweza kufikia hatua tuliyo nayo sasa.

Wale wanaohusika na utungaji mitihani hawafanyi hivyo katika hatua zote. Tunawapa kazi wakishatuletea tunakaa tena kama baraza kupitia kisha kuboresha kwa njia kadhaa, lengo kuu la kufanya hivyo ni kutoruhusu mwanya wa kuvunja kwa mitihani.

Raia Mwema: Ina maana hata watungaji mitahani pia si waaminifu?

Dk. Ndalichako: Hapana wahusika ni watu tunaowamini sana. Hadi kufikia hatua hiyo kuna mchakato mrefu, si jambo la mchezo. Ni watu wanaoaminika, lakini kama unavyojua ni lazima tuchukue tahadhari mapema na ya hali ya juu, hasa kwa kuzingatia kuwa elimu ndiyo ngao. Sasa lazima tuhakikishe mtu akifaulu kweli amefanya kazi kwa akili zake mwenyewe. Hivyo kufanya hivyo ni tahadhari tu, si kwamba watunzi hawaaminiki.

Katika hilo ndiyo maana mtu mmoja hawezi kutunga paper nzima mwenyewe, na hata kama ni topic, mfano, kama ni maswali manane, si rahisi zote zitoke kwa mtunzi mmoja. Ni lazima tuboreshe tunavyojua kwa mbinu mbalimbali za kitaalamu kwa lengo lilelile la kutunza siri zaidi.

Kwa ujumla zipo hatua kuu tatu au nne za usahihishaji. Ya kwanza ni kusahihisha karatasi ya mwanafunzi, pili ni kuhakiki kile kilichosahihishwa, tatu ni kuingiza matokeo katika kompyuta moja kwa moja kutoka kituo cha usahihishaji na kusomwa na baraza na nne ni sisi kuhakiki tena matokeo hayo na kuyaweka katika mfumo rasmi wa kutangwazwa.

Usahihishaji karatasi ya mwanafunzi hufanywa kwa umakini mkubwa sana. Kila msahihishaji husahisha swali moja tu katika kila somo. Kama somo, kwa mfano, lina maswali 10, maana yeka ni kwamba karatasi ya mwanafunzi huyo itasahihishwa na watu 10 pia.

Baada ya msahihishaji kumaliza kazi yake na kuweka alama, mhakiki hupitia swali hilo kuhakiki kama alama alizopewa mwanafunzi ni sahihi, na jibu pia ni sahihi, na kwamba imezingatia maelekezo yote.

Mhakiki pia anaangalia kama jumla ya alama zote kwa somo ni sahihi maana wakati mwingine alama kwa kila swali inaweza kuwa sahihi lakini jumla ikawa si sahihi, yote hayo huangaliwa katika hatu hiyo ya uhakiki.

Pamoja na hayo mhakiki anaangalia kama kila kitu alichoandika mwanafunzi kimeangaliwa kwa umakini mkubwa.

Raia Mwema: Kabla haujaendelea, ni vigezo gani vinavyotumika kuwapata hawa wasahihishaji?

Dk. Ndalichako: Kwanza ni lazima awe mwalimu mwenye uzoefu usiopungua miaka mitatu kazini na mwenye diploma (stashahada) ya ualimu au digrii (shahada).

Awe pia ni mtu ambaye hajapatikana na hatia yoyote ya udanganyifu kazini, na asiye na kesi mahakamani, pia asiwe mkuu wa shule kwa kuwa kazi hiyo inaweza kuchukua muda mrefu, kama mwezi mmoja.

Kwa kawaida kuna fomu maalumu ambazo tunapeleka kwa wakuu wa shule kila mwaka kwa ajili ya kuwapata, lakini kuanzia mwaka 2008 tuliongeza kipengele cha kutaka wasifu wao pia ili tujiridhishe wenyewe kwenye kumbukumbu zetu kuona jinsi walivyofaulu .

Baada ya kupata fomu husika na kupitia taarifa zao zote tunarudisha majina yote kwa Maofisa Elimu wa Mikoa (REO) kuthibitisha taarifa tulizopokea kama ziko sahihi.

Mfumo huo umetusaidia sana kupata taarifa za kina zaidi, kwa mfano, unaweza kukuta mwalimu amejiandika kumbe ni mkuu wa shule, mwingine tunapata taarifa za kuwa ana utovu wa nidhamu au hata ana kesi. REO akishatupatia taarifa hizo tunawaondoa.

Raia Mwema: Baada ya usahihishaji, ulisema mnaingiza matokeo kwenye kompyuta?

Dk. Ndalichako: Ni kweli baada ya kuhakiki na kujiridhisha kama usahihishaji umefanyika kwa sahihi; alama alizowekewa mwanafunzi kwa kila swali ni sahihi; jumla ya alama zake ni sahihi; hatua inayofuata ni kuingiza matokeo kwenye kompyuta moja kwa moja.

Kwa ufafanuzi huo napenda kuweka wazi kuwa sisi baraza tunaridhika sana na jinsi kazi hiyo inavyofanyika na ni ya haki na hakuna upendeleo wowote, na kama nilivyosema wenzetu wa nchi mbalimbali wanakuja kujifunza kwetu.

Kikubwa tujenge tabia ya kujiamini na kujipenda sisi wenyewe. Kama watu wa nje wanatushangaa tumewezaje, iweje sisi wenyewe bado tunashaka? Ni ajabu.

Mataifa hayo yamekuja, na wengine, wanaomba kuja mwaka huu kuifunza na kutuomba tuwaleze sisi tunafanyeje. Wanaridhika sana na mfumo wetu. Kusema kweli, sisi kama Taifa tumefanikiwa sana katika suala la utungaji, usimamizi na usahihishaji wa mitihani yetu licha ya kuwa kuna changamoto kadhaa. Kama kuna mtu analalamika ni kwa sababu tu hajui hatua hizo zinazopitiwa hadi kupatikana matokeo.

Raia Mwema: Vipi kuhusu rufaa za malalamiko?

Dk. Ndalichako: Kama unavyojua Taifa letu linaongozwa kwa sheria na haki. Wazazi au wanafunzi wanaruhusiwa kukata rufaa pale ambapo hajaridhika bila kujali kuwa malalamiko yake ni sahihi au sivyo. Tunachofanya sisi ni kuyafanyia kazi malalamiko hayo kwa mujibu wa taratibu za baraza na sheria.

Lakini kusema kweli sehemu kubwa ya rufaa hizo naweza kusema ni kupoteza muda na fedha za wazazi bila sababu za msingi. Mfano wa karibu ni mwaka 2010 tulipokea rufaa 1,641 kati ya hizo zilizoshinda ni 13 tu.

Mwaka huohuo tulipata rufaa 97 za walimu Daraja A, hakuna iliyoshinda hata moja. Sasa ukiangalia kwa makini utakuta ni matumizi mabaya ya fedha bila sababu. Ningeshauri wazazi watafakari na kufanya utafiti wa kina kuhusu uwezo wa watoto wao, mazingira ya mtihani na usahihishaji kabla ya kukata rufaa, wakifikiri kwamba baraza kuna uonevu au upendeleo.

Raia Mwema: Unashauri wahusika kutokurupuka kukata rufaa na kwamba kufanya hivyo ni sawa na matumizi mabaya ya fedha, mnatoza shilingi ngapi na kwa nini?

Dk. Ndalichako: Ni kweli kuna ada ya kurudia kazi hiyo na ni malipo halali. Tunafanya hivyo kwa kuwa mtu akikata rufaa kutaka kusahihishiwa tena ni lazima tufuate utaratibu uleule kama nilivyotaja. Yaani kuwa na watu si chini ya watatu kwa kila somo, wote hao wanalipwa. Hivyo ni lazima kutakuwa na gharama kidogo. Kwa kila somo mtahiniwa analipia shilingi 20,000.

Raia Mwema: Uvujaji mitihani umeendelea kujitokeza pamoja na kwamba mnafanya jitihada kubwa kuukabili. Tatizo la kuvuja mitihani ni kubwa kiasi gani na linaanzia wapi?

Dk. Ndalichako: Ni kweli bado hali hiyo ipo, japo si kwa kiasi kikubwa sana. Ukiangalia ongezeko la shule na watahiniwa, chanzo cha tatizo hilo ni mmonyoko wa maadili katika jamii yetu.

Tabia hiyo ina madhara makubwa sana kwa Taifa. Unaweza kusikia kelele zote huko serikalini kuhusu utendaji au wataalamu wetu, inawezekana ni sehemu ya matokeo ya tatizo hilo.

Taifa likishakuwa na mmonyoko wa maadili, wazazi wanashiriki, baadhi ya walimu nao wanashiriki. Sasa sisi kazi yetu kubwa ni kuwashughulikia, na katika hilo sitarudi nyuma. Kwa mfano, mwaka huu tumesema wale wote waliogundulika na udanganyifu wa mitihani licha ya kufutiwa matokeo lakini pia hawataruhusiwa kufanya mitihani hadi baada miaka mitatu. Itabaki hivyo hakuna kubadilika.

Binafsi na baraza zima tunaumizwa sana kuona mwanafunzi anafutiwa matokeo yake. Na wala hatupendi kufanya hivyo. Lakini tunalazimika kuchukua hatua hiyo kwa kuwa hatuna namna ya kuwasaidia na kulisaidia Taifa nje ya uamuzi huo.

Lengo la adhabu hiyo ni kutaka wote tuchukie tatizo hilo. Wazazi wauchukie, na wanafunzi wenyewe pia wauchukie, pamoja na walimu wetu kwa ujumla.

Kwa mfano, ni aibu sana kukuta swali moja jibu sahihi ni P lakini darasa zima wanafunzi wamejibu O, swali jingine labda jibu sahihi ni C, lakini darasa zima wamejibu F na ukichunguza zaidi unakuta kuna mchezo mchafu. Hatuwezi kuvumilia hali hiyo iendelee kushamiri.

Kutokana na udanganyifu wa mitihani ndiyo maana hata matokeo ya kidato cha nne mwaka huu yamechelewa kidogo kutangazwa kwa sababu tulikuwa tunafuatilia baadhi ya mambo kujiridhisha kabla ya kutangaza rasmi matokeo.

Raia Mwema: Ni mambo gani hayo mliyokuwa mkifuatilia mpaka kuchelewesha kidogo matokeo?

Dk. Ndalichako: Kwanza baada ya kubaini kuwapo kwa baadhi ya wanafunzi kuandika vitu visivyoeleweka katika makaratasi yao ya mitihani wakati taarifa zao za kila mwaka walikuwa kwenye taarifa za maendeleo ya mwanafunzi wakipata wastani wa 42 hadi 50 tulijiuliza kulikoni?

Kutokana pia na kuwapo kwa udanganyifu kwa baadhi ya maeneo, tulikuwa tunafuatilia kujua mambo kadhaa kuhusu hali ilivyokuwa hasa kwa kuzingatia kuwa nchi yetu ni kubwa na shule zetu nyingi ziko mbali inatuchukua muda kupata taarifa sahihi kwa haraka.

Hata hivyo, niweke wazi kuwa mwaka huu tumeamua kupiga hatua mbele zaidi. Hatutaishia tu hapo kuwa tumetangaza matokeo basi, hapana. Haiwezekani mwanafunzi akawa anapata alama au wastani wa 50 kisha kwenye mtihani wa Taifa aandike matusi, au vitu visivyoeleweka, au kuchora picha ya mchezaji, kisha turidhike. Hapana. Tutazifanyia kazi changamoto hizo.

Raia Mwema: Mtafanyeje kujua kile mnachotaka?

Dk. Ndalichako: Tutawaita walimu, na ikiwezekana tunataka hata tuwaone wanafunzi husika, tuwahoji wenyewe kulikoni. Maana si jambo la kawaida mwanafunzi anakuwa na maendeleo mazuri, lakini siku ya mtihani anaandika matusi au kuchora picha ya mchezaji kwenye karatasi ya kujibia maswali.

Tumeunda kikosi kazi kufuatilia changamoto hizo za mitihani. Lengo kuu likiwa ni kuboresha utendaji wetu na kuwasaidia vijana wetu na wazazi pia ili hali kama hiyo isitokee tena.

Raia Mwema: NECTA haina ofisi mikoani, mnawapata wasimizi wa mitihani huko, huoni kuwa kukosekana kwenu mikoani ni chanzo cha tatizo hilo na mna mkakati gani kufika huko wenyewe?

Dk: Ndalichako: Ni kweli sisi wenyewe kama baraza hatupo mikoani, lakini Serikali ni moja ya wawakilishi wetu wanaokula kiapo cha uaminifu na kupata miongozo yetu.

Tunazo kamati za mitihani za mikoa ambazo Mwenyekiti wake ni Katibu Tawala wa Mkoa na Katibu wake ni Ofisa Elimu wa Mkoa, kamati hiyo ndio inayofanya kazi kwa niaba yetu.

Kamati hiyo imekuwa ikifanya kazi kubwa sana na wanatupa ushirikiano wa kutosha. Hata ikitokea matatizo ya udanganyifu katika mitihani wao wenyewe wanakuwa wa kwanza kutoa taarifa na kuchukua hatua haraka. Kama nilivyosema, mmonyoko wa maadili ndio unaotusumbua sana.

Katika mpango makakati wa baraza tunatarajia kuangalia jinsi ya kuwa na Ofisi za Kanda ili kuhamisha baadhi ya mamlaka kwao, na sisi kama Makao Makuu kuangalia ni mambo gani tuyafanyie kazi moja kwa moja na mengine tuwape. Hii inalenga kuboresha utendaji kazi zetu kutokana na ongezeko la shule na watahiniwa.

Raia Mwema: Dunia inabadilika kwa kasi sana. NECTA imejiandaa vipi kuboresha mitihani na matokeo kwa njia ya teknolijia rahisi zaidi kuendana na wakati?

Dk.Ndalichako: Kwanza kama nilivyosema, kwa sasa matokeo yanawekwa kwenye kompyuta moja kwa moja kutoka katika kituo cha usahihishaji na kusomwa baraza moja kwa moja bila kusubiri hadi watuletee makaratasi kama zamani.

Lakini pia mwaka huu katika mitihani wa darasa la saba tunatarajia wahitimu wataanza kutumia karatasi maalumu za optical mark reader forms zinayosahihishwa kwa kompyuta moja kwa moja. Hii ni hatua kubwa katika maendeleo ya teknolojia kwa baraza. Tumeanza na darasa la saba, kwa upande wa sekondari bado tunajiandaa.

Raia Mwema: Kuna tatizo la mabadiliko ya mitaala na hata vitabu shuleni, hili linawaathiri pia nyinyi kama baraza?

Dk. Ndalichako: Hilo kwetu si tatizo kubwa. Mtaala mpya wa mwaka 2005 mitihani yake ya kwanza ilikuwa mwaka 2008 hivyo tulijiandaa kabla. Na pia mtaala mwingine wa mwaka 2008 mtihani wake wa kwanza ni mwaka huu hivyo si tatizo kubwa kwa baraza hasa kwa kuzingatia pia kuwa tunasoma vitavu vingi sana kujua kile anachotakiwa kujua mwanafunzi.

Raia Mwema: Una wito gani kwa jamii kama Mtendaji Mkuu wa NECTA?

Dk. Ndalichako: Naomba wanajamii wote watambue kuwa jukumu la kuhakikisha wanafunzi wanafanya mtihani na kupata kile wanachostahili kulingana na uwezo wao ni la kila mmoja. Hivyo washirikiane nasi kutoa taarifa zozote za udanganyifu pale watakaposikia au kuona vitendo vyovyote visivyofaa.

Tunawaomba sana walimu kuendelea kutimiza wajibu wao kwa kufundisha wanafunzi wao vizuri na kwa kuzingatia mtaala kwa kinachotakiwa mwanafunzi akipate bila kutegemea msaada wa aina yoyote tofauti na jinsi walivyowafundisha.

Kwa wanafunzi pia tunawaomba sana wazingatie masomo. Waache kujiingiza katika mambo yanayoweza kusababisha wakaharibikiwa na kushindwa masomo.

Wasimamizi wa mitihani wazingatie taaluma na miiko yao ya kikazi na kuhakikisha kuwa wanaheshimu na kusimamia taratibu.

Nawaomba sana Watanzania kwa ujumla watupigie simu zifuatazo pale wanapobaini udanganyifu au mwenendo usio wa kawaida katika taratibu zetu za baraza: 0768-229010 na 0684-103677.

 

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi

Maoni ya Wasomaji

Huyo Mama yupo makinu kwakweli, wanafunzi mjipange na muache kuibia huu ndio mpango madhubuti wa kufuta mafisadi na vifisadi...Mungu akubariki mama.

Toa maoni yako

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.