Tanzia
Dk. Vedasto Kyarakishaija Nshunju Kyaruzi
Ahmed Kiwanuka
Toleo la 241
30 May 2012

WIKI iliyopita, Mei 20, 2012, Dk. Vedasto K.N. Kyaruzi aliaga dunia kwenye Hospitali ya Mkoa wa Kagera, mjini Bukoba akiwa na umri wa miaka 91. kwa kifo hiki, Tanzania imeondokewa na mmoja wa watumishi wake waliotukuka, daktari bingwa na muasisi na mwanasiasa mahiri.

Mchango na utumishi wake kwa maendeleo ya taifa letu hauna kifani. Ni miongoni mwa watu wachache waliolitumikia taifa letu kwa moyo, uaminifu na uadilifu mkubwa.

Marehemu Dk. Kyaruzi alizaliwa Februari 20, mwaka 1921 huko kijijini Kigarama-Kanyigo, tarafa ya Kiziba. Alianza elimu ya msingi Kashasha mwaka 1930 hadi 1933. Akaendelea na masomo hayo Shule ya Mugana kati ya mwaka 1933 hadi 1934. Baada ya hapo alijiunga na Shule ya Kajunguti-Rubya kuanzia mwaka 1934 hadi 1939.

Alipohitimu alichaguliwa kujiunga na Shule ya Mtakatifu Maria (sasa Milambo) kuanzia mwaka 1939 hadi 1941. Kisha akajiunga na Chuo Kikuu cha Makerere kwa masomo ya udaktari hadi mwaka 1948 alipohitimu. Akiwa Makerere na Tabora, alijuana na wasomi wenzake kwa mfano marehemu Mwalimu Julius Nyerere, marehemu Balozi Andrea Tibandebage, marehemu Hamza Kibwana Mwapachu na Mzee Aboud Jumbe.

Alipohitimu, alipangiwa kazi Hospitali ya Sewa Haji, jijini Dar es Salaam alikofanya kazi kati ya mwaka 1949 hadi 1951. Pamoja na kazi zake alijihusisha na kazi za siasa ndani ya chama cha TAA, ambacho baadaye kilizaa chama cha TANU mwaka 1954.

Kwa uwezo na uzalendo wake, alichaguliwa kuwa Rais wa TAA mwaka 1950 hadi 1951. Katibu Mkuu wake alikuwa marehemu Abdulwahid Sykes. Inasemekana kwamba Gavana hakufurahishwa na harakati za Dk. Kyaruzi na hivyo akaagiza ahamishiwe Gereza la Kingolowira kuwatibu wafungwa. Alikaa hapo hadi mwaka 1952.

Baadaye alifanya kazi hospitali za Nzega, Biharamulo na Bukoba. Na kati ya mwaka 1954 na 1959, alikuwa Chuo Kikuu cha Edinburgh kwa masomo ya juu kuhusu fani yake.

Tulivyokaribia kupata uhuru mwaka 1961, alikuwa ni miongoni mwa walioandaliwa kupewa madaraka serikalini. Walipelekwa Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza kwa mafunzo ya diplomasia na utawala.

Mwaka 1961, marehemu Kyaruzi aliteuliwa kuwa Balozi wa kwanza wa Kudumu kwenye Umoja wa Mataifa, New York. Nchi yetu ilipokuwa Jamhuri mwaka 1962, marehemu alirejea nchini maana aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ulinzi, iliyokuwa chini ya Rais.

Baadaye, wizara hiyo ikaongozwa na marehemu Oscar Kambona, Katibu Mkuu akiwa ni Dk. Kyaruzi. Kwa sababu ya uadilifu na nidhamu yake ya kazi na maisha, Dk. Kyaruzi hakukaa sana na Waziri wake! Na hivyo, akapata kazi UNICEF, kama mwakilishi wa nchi za Afrika Kusini mwa Sahara, ofisi zake zikiwa Lagos, Nigeria.

Alifanya kazi kuanzia 1963 hadi 1968. Na kuanzia mwaka 1968 hadi 1976, alifanya kazi makao makuu ya Jumuiya ya Madola, London, kama mtaalamu wa Afya. Na kuanzia mwaka 1976 hadi 1980, alikuwa ni Mtendaji Mkuu wa Afisi ya Afya ya nchi za Afrika Mashariki na Kusini, yenye makao yake makuu jijini Arusha.

Tangu mwaka 1980 alipostaafu, alirejea mjini Bukoba. Hapo alifungua hospitali ndogo na akaendelea kuwahudumia watu mpaka mwisho wa uhai wake. Wote tuliomjua Dk. Kyaruzi tulitambua upendo wake kwa watu, uzalendo wake na ucha Mungu wake.

Hakuwa na majivuno, kiburi au makeke. Alikuwa ni mtu wa kawaida, akishirikiana na kila mtu, akichekeana na wote. Maisha yake hayakuwa na ufahari wowote. Wanaomjua zaidi, hakuwa na tamaa ya kujilimbikizia mali. Maisha yake yaliongozwa na nidhamu ya hali ya juu katika kazi zake. Alikuwa ni mtu wa ibada. Kwa kweli, nchi yetu imeondokewa na kiongozi mweledi na adili.

Marehemu Kyaruzi amezikwa Mei 26, 2012 kijijini Nyabianga, Kyaka, wilayani Misenyi, mazishi yaliyohudhuriwa na maelfu ya watu! Ameacha mke na watoto watatu na kitukuu. Bwana alitoa, na ametwaa! Mola ailaze peponi roho ya marehemu Dk. Kyaruzi-Amina.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi

Toa maoni yako