Habari
Dk.Slaa asema nchi inalipuka
Mwandishi Wetu
Toleo la 148
25 Aug 2010
  • Asema viongozi wanakurupuka kutafuta sifa
  • Aelezea alivyopambana na wakepa kodi Kanisani

MGOMBEA Urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema nchi inalipuka katika kufanya uamuzi magumu bila utafiti na hiyo imekuwa ikiligharimu Taifa mabilioni ya fedha za umma.

Katika mahojiano yake maalumu na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Dk. Slaa alisema kulipuka huko kumekuwa kukifanywa na viongozi wa serikali wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete, katika maamuzi ambayo amesema yamekuwa yakifanywa kutafuta umaarufu usio na maslahi kwa umma.

“Kwa kweli nchi inalipuka kila kukicha.... mambo yanafanywa bila kufanyiwa utafiti. Mambo yanafanywa kwa populism (umaarufu bila sababu),” alisema Dk. Slaa akitoa mifano ya maamuzi kadhaa ikiwamo suala la mabilioni ya Kikwete, fedha ambazo anasema zimetumika bila kufanyiwa utafiti.

Alisema mabilioni yaliyotengwa na kugawanywa yanaelezwa kuwanufaisha watu 44,000 kati ya Watanzania milioni 40, fedha ambazo zingeweza kutumika kujenga zahanati ama barabara.

“Awali serikali ilipanga kugawa Sh milioni 500 nchi nzima kama mikopo kwa wafanyabiashara wadogo kabla ya kuziongeza na kufikia Sh bilioni 21 ambazo ziligawanywa mikoani. Fedha hizo zingeweza kujenga shule zahanati ama hata barabara lakini wamepewa watu 44,000 tu, ambao nao hazikuwatosha kutatua matatizo yao ya kifedha,” alisema Dk. Slaa katika sehemu ya mahojiano hayo yaliyochapishwa kwa kirefu katika kurasa za kati za toleo hili.

Akitoa mifano mwingine wa kitu alichosema ni ‘ulipukaji’ ambao Serikali imeufanya ni kuagiza matrekta madogo (power tiller) ambayo yameonyesha kushindwa kukidhi matarajio ya wakulima kuzalisha chakula cha ziada.

“Huo wote ni ulipukaji. Hakukua na utafiti wa kutosha kuagiza yale matrekta, maana maeneo mengi hayawezi kuchimbua ardhi kama inavyopaswa, lakini yameagizwa kwa mabilioni ya shilingi na sasa mengi yameegeshwa bila kufanya kazi,” alisema.

Amesema pia kwamba nchi inaendeshwa bila bajeti akitoa mfano zaidi ya shilingi trilioni 1.7 zilizotengwa kusaidia wafanyabiashara wa mazao waliodaiwa kuathiriwa na mtikisiko wa uchumi, fedha zinazojulikana kama stimulus package , ambazo amesema hadi sasa zina utata mkubwa kutokana na kutolewa bila kuidhinishwa na Bunge na hakukuwa na uwazi katika uidhinishwaji wa wafanyabiashara wanaostahili.

Akizungumzia mipango miji, Dk. Slaa alibeza kauli ya Rais Kikwete kwamba foleni za Dar es Salaam zinatokana na neema, na badala yake amesema tatizo kubwa ni udhaifu katika kufanya utafiti na kufanya maamuzi katika kupanga miji ikiwamo jiji la Dar es Salaam ambalo alisema linapaswa kupangwa sasa.

“Tunahitaji programu ya miji yetu. Dar es Salaam hakuna miundombinu ya umma inayojengwa kwa viwango vinavyolingana na ukiaji wake. Hakuna ubunifu. Eti Rais anasema foleni ni ishara ya maendeleo. Haoni kila kukicha kunajengwa show room za magari na hakuna miundombinu mipya,” alisema.

Alisema ni lazima serikali ifanye uamuzi sasa wa kujenga miundombinu mipya kwa gharama zozote maana itafika wakati itakuwa ni vigumu kulipa fidia kutokana na mabadiliko yanayotokea kwa kasi katika miji mbalimbali ikiwamo jiji la Dar es Salaam.

‘Ulipukaji’ mwingine ambao Dk. Slaa ameutolea mfano ni uamuzi wa Serikali wa kutoa mtandao wa reli kwa kampuni ya Rites ya India, kwa maelezo kwamba kampuni hiyo haikuja na fedha nchini bali ilikopa fedha katika taasisi moja ya kimataifa kwa kudhaminiwa na Serikali, jambo ambalo lingeweza kufanywa na Serikali yenyewe na ikatafuta menejimenti ya kuajiri.

Dk. Slaa amezungumzia pia dhamira yake katika kupambana na ufisadi na kutoa mifano ya jinsi alivyoweza kukamata mali zilizokuwa zikiingizwa kwa kutumia kanisa kukwepa ushuru na kwamba alikuwa akisimamia minada ya mali hizo ili serikali iweze kukusanya kodi inayokusudiwa.

“Aliyekuwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI)  Mwaitenda (Arthur) anajua Dk. Slaa ni nani. Mimi mara kwa mara nikiwa Katibu wa TEC nimekuwa nikizuia na kuita vyombo vya dola kukamata mali zilizoingizwa nchini kwa muhuri wa makanisa lakini si za makanisa na wanafanya hivyo ili kukwepa kodi.

“Kontena ilikuwa ikiingizwa nchini kama si halali niliwaita polisi na kukamata mara moja. Kwa hiyo nilikuwa naiwaita polisi na kontena hiyo inapigwa mnada moja kwa moja hadharani,” alisema.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Toa maoni yako