Tanzia
Dudley Thompson: Taa iliyochochea uhuru Afrika Karibeani
Ahmed Kiwanuka
Toleo la 226
15 Feb 2012
Dudley Thompson
  • Alikuwa mwasisi wa TANU asiyekuwa rasmi
  • Kenyatta alimshukuru kwa kuokoa roho yake

KWA Watanzania wengi wa leo, marehemu Dudley Thompson anaweza kuwa mgeni kwao. Na hiyo ni haki yao kwa kuzingatia mabadiliko ya kisiasa yaliyosheheni nchini mwetu.

Na kwa Afrika Mashariki, marehemu Thompson ndiyo kafunika kabisa. Alipofariki dunia hivi karibuni, ni gazeti moja tu hapa nchini lililotoa taarifa ya kifo chake. Nchini Kenya nako ni gazeti moja tu lililoandika habari hiyo. Tabia hii si ajabu kwa waafrika.

Si karne nyingi tulikuwa watumwa, tukiuzwa kama maembe sokoni. Leo hii tunajiona kama kwamba tumefika. Wapi na wapi kama si ulofa, kutojua tulikotoka, tuliko na tuendako?

Marehemu Dudley Thompson alizaliwa Panama Januari 1, 1917 mwaka yalipotokea mapinduzi makubwa nchini Urusi. Na amefariki New York, Marekani, akiwa na umri wa miaka 95. Magazeti mengi ya Marekani na Karebiani yalitangaza kifo chake.

Kwa Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, Thompson alikuwa ni mwenzetu, na miongoni mwetu. Historia ya Afrika sahihi haiwezi kumpuuza. Alipohitimu elimu yake ya Chuo Kikuu cha Mico, Jamaica, alifanya kazi ya ualimu. Wakati wa Vita kuu ya pili alijiunga na Jeshi la Anga la Uingereza akiwa rubani wa ndege za kivita.

Mara baada ya vita, alijiunga na Chuo, Oxford ambako alitunukiwa shahada ya uzamili ya MA na nyingine ya sheria. Baadaye alijiunga na Taasisi ya Gray’s Inn kwa mafunzo ya uanasheria.

Wakati wote akiwa Uingereza, alijitambulisha kama mpigania uhuru na mtetezi wa Afrika na Karibeani. Alihudhuria mkutano wa tano wa jumuiya ya Afrika mjini Manchester, Uingereza mwaka 1945 ambao pia ulihudhuriwa na William Dubois, Kwame Nkrumah, Geroge Padmore, Jomo Kenyatta n.k.

Baadaye alihamia Tanganyika alikoishi kati ya mwaka 1951 hadi 1956, akiwa mwanasheria wa kujitegemea. Akiwa hapa kwetu alijenga urafiki na mahusiano na watu wengi, waswahili.

Alisimamia matatizo ya kisheria. Na kubwa zaidi ni mshikamano na udugu wake na viongozi wetu wapigania uhuru, hususan Mwalimu Nyerere walifahamiana huko Uingereza.

Marehemu Thompson daima atakumbukwa kwa mambo mawili. Kwanza, yeye akiwa hapa, alikuwa ni muasisi asiye rasmi wa chama cha TANU, Julai 1954.

Alikuwa mara kwa mara akitoa ushauri wa kisiasa na kisheria kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Pili, Thompson ndiye aliyekuwa wakili mtetezi wa Mzee Jomo Kenyatta alivyoshitakiwa kuhusiana na na harakati za Maumau nchini humo.

Siku moja, mara baada ya uhuru wa Kenya 1963, Mzee Kenyatta alisema: “Huyu bwana aliniokoa nisinyongwe na Waingereza.”

Mchango wa Thompson kwa harakati za uhuru hapa kwetu ulikuwa mkubwa, tuna kila sababu ya kumkumbuka na kumuenzi.

Baada ya kurejea Jamaica, aliendelea na kazi ya uwakili na kupewa daraja la QC (Queens Councillor) mwaka 1963. Na wakati huo alikuwa mwanachama mwandamizi wa chama cha Peoples National Party (PNP) kikiongozwa na Norman Manley na baadaye Michael Manley.

PNP, kama TANU, na baadaye CCM ya mwanzo, kilikuwa ni kimbilio na sauti ya wanyonge- wakulima na wafanyakazi. Vile vile kilipigania uhuru na umoja Karibeani na Afrika. Jamaica inasherehekea miaka 50 ya uhuru wake mwaka huu kama sisi tulivyofanya mwaka jana.

Maisha yake ya kisiasa yalikuwa na majukumu mengi. Alikuwa mbunge wa PNP kuanzia mwaka 1964 Hadi 1980. Alikuwa kiongozi wa upinzani bungeni kati ya 1965 hadi 1974.

Na kati ya mwaka 1975 hadi 1978 alikuwa ni mnadhimu wa Serikali bungeni. Kati ya mwaka 1975 hadi 1980 alikuwa Wazirti wa Mambo ya Nchi za Nje, Waziri wa Madini na Maliasili na Waziri wa Ulinzi na Usalama wa Taifa.

Pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa PNP hatimaye kuwa mwenyekiti wa taifa wa PNP. Taifa la Jamaica kwa kutambua utumishi wake uliotukuka, ulimtunukia Nishani ya Jamaica yenye hadhi ya kipekee.

Marehemu atakumbukwa pia kwa utumishi wake wa kimataifa. Hakuwa mgeni kwenye vikao vya Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Madola, Umoja wa Nchi za Afrika, Nchi zisizofungamana na upande wowote na Umoja wa Nchi za Karibeani. Kote huko ushauri na fikra zake vilithaminiwa.

Kwa kushirikiana hasa na Michael Manley, Waziri Mkuu wa zamani wa Jamaica, nchi hiyo ilijijengea heshima kubwa kimataifa na ikaaminiwa.

Sisi Afrika tulishirikiana na Jamaica katika mapambano yetu dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi kusini mwa Afrika hadi ushindi ulipopatikana. Marehemu Thompson alienziwa na Umoja wa Afrika kwa kutambuliwa kama ‘Raia wa Afrika’ mwaka jana.

Katika kuimarisha udugu wa Jamaica na nchi za Karibeani na bara letu, marehemu aliteuliwa kuwa Balozi wa nchi yake huko Nigeria, Ghana, Sierra Leone na Namibia katika miaka ya 1990 hadi alipostaafu.

Wakati wa uhai wake alikuwa ni mwenyekiti wa Umoja wa Watu Weusi walioko Nje ya Afrika (World African Diaspora Union).

Marehemu Thompson aliongozwa maishani na imani ya usawa wa binadamu. Aliamini ya kuwa watu wote- wake kwa waume wameumbwa kwa sura ya Mungu. Kwa hiyo kama mwanasiasa, mwanasheria, balozi na kiongozi, aliwaheshimu watu wote kwa usawa na utu wao.

Hakuwa na chembe ya ubaguzi wala dharau. Hakuwa na tamaa ya mali wala ulua. Muda wote alipenda kuwa mtumishi, hasa wa wanyonge na makabwela. Maisha yake hayakulewa fahari au kiburi. Alikuwa ni mtu wa watu.

Waziri mkuu wa sasa wa Jamaica, Bi Portia Simpson Miller alilieleza Bunge la Jamaica ya kuwa marehemu Thompson alikuwa ni binadamu wa aina yake, raia mwema wa dunia, mwanajumvi wa Afrika na Karibeani, mpigania uhuru, balozi mahiri na kiongozi mtukuka.

Hadhi na nafasi yake nchini Jamaica imefananishwa na marehemu Marcus Garvey, mwanajumvi mkuu wa Afrika wa karne ya 19 mwanzoni.

Tumempoteza kiongozi hodari na mweledi wa Jamaica, Karibeani na Afrika. Jambo jema ni kwamba maisha yake yalifaulu kwa maana ya kuona mengi aliyoyapigania yakifanikiwa kwa kiasi cha kuridhisha.

Katika miaka yake 95 ya maisha yake, Jamaica, Karibeani na Afrika kwa ujumla tumefanikiwa kuwa huru zaidi na kupata heshima.

Ni kweli bado hali si nzuri kama ambavyo angelipenda. Lakini mapambano bado yapo, na yanaendelea.

Maisha na mchango wake ni hazina kwa watu wa Karibeani na Afrika kuitumia ili kudumisha, kulinda na kuendeleza umoja, uhuru, usawa na haki katika nchi zetu. Mola aiweke pema roho ya marerhemu Dudley Thompson. Amina.

 

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi

Toa maoni yako

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.