Makala
Elimu kwa vitendo shuleni iko wapi?
Prosper Minja
Toleo la 239
16 May 2012

KATIKA moja ya hotuba za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kuna baadhi ya mambo hapa nchini ukitaka kuyahoji lazima uwe na moyo mgumu kama wa mwendawazimu hivi. Kwa sasa moja ya mambo hayo ni elimu, kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari na hata elimu ya vyuo. Zamani ili shule ihesabike na hata kusajiliwa rasmi mambo mengi yalizingatiwa ikiwa ni pamoja na uwanja wa michezo na shamba la shule. Siku hizi ni dhambi ya mauti kuzungumzia shamba la shule tena mzazi akikusikia achilia mbali mwalimu. Mwanafunzi ndiyo kabisa, atatamani umwagiwe tindikali.

Siku hizi mtoto anafanyiwa kila kitu awapo shuleni. Kuna watu wa kufanya usafi ndani na nje ya vyumba vya madarasa, kupika, basi la kumbeba na kumrudisha nyumbani, akifika nyumbani kuna msaidizi au mfanyakazi wa nyumbani wa kumfulia hadi nguo za ndani, kumpikia, kumtandikia kitanda na kumnyooshea nguo. Shuleni shamba darasa tena hakuna. Zamani katika orodha ya vifaa vya kwenda navyo shuleni jembe kilikuwa kifaa kimojawapo. Siku hizi dhubutu! Kiwanja cha michezo si sharti muhimu tena. Hali hii iko tangu shule za awali hadi vyuo vikuu. Ni dhahiri maandiko haya hayatabadilisha chochote kwa wakati huu lakini yataonekana ya maana Wachina watakapoanza kuchangamkia hata kazi za majumbani hapa Tanzania kwani wao wamefundishwa maana ya kazi kwa vitendo.

Serikali, wazazi, wadau wako wapi kudai na kuhimiza kazi za mikono katika shule zetu? Shule yoyote kabla ya kusajiliwa ioneshe japo shamba darasa mahali wanafunzi watajifunza kwa vitendo kupanda na kuvuna mchicha. Wanafunzi wafundishwe kufanya usafi kwa vitendo kwa mfano kufagia darasa, kuokota takataka, kukata kucha, kuosha sahani zao wanapomaliza kula,  kutoa buibui na nyinginezo. Wakiwa majumbani wajifulie nguo zao wenyewe, wafanye usafi, wajifunze kupika, wanyooshe nguo zao wenyewe, watengeneze bustani na kuzimwagilia inapobidi, wahimizwe masuala ya kiroho, kwa kifupi wafundishwe kuwajibika.

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ndilo lilikuwa limesalia ili kuziba ombwe hili. Jeshi hili ni tofauti kwa sasa. Majukumu yake si sawa nay ale ya awali, enzi zile za operesheni miaka 30 (waliopita jeshini wanaelewa operesheni).   Ole wetu! Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk. Joyce Ndalichako alinukuliwa akilalamika kwamba wanafunzi waliandika mashairi ya Bongo flavor kwenye mitihani! Kumbe waandike nini? Nyimbo za makuzi shuleni siku hizi hakuna tena. Nyimbo za kizalendo na ukakamavu ni historia shuleni! Kibaya zaidi hata wimbo wa taifa umebaki kuchezwa mkanda tu uliorekodiwa halafu wanafunzi wanasikiliza! Mustakabali wa taifa uko wapi! Tusipojenga msingi imara tusishangae nyumba kuporomoka kwani Walatini wanasema volenti non fit injuria! (lakujitakia halina madhara). Tumeyataka wenyewe!

Tuna wakaguzi waliosoma. Hivi hawa wanakagua nini? Mwandiko mzuri? Mwalimu kumaliza silabasi? Wadau nisaidieni. Mada ni pana. Mtoto huyu akimaliza shule (darasa la saba, kidato cha nne, kidato cha sita, shahada ya kwanza) anakuwa ni mzigo usiobebeka pande zote. Si kwa wazazi, si kwa serikali! Hawezi kufanya kitu chochote! Hajafundishwa kufanya hivyo! Hajalelewa katika mazingira hayo! Hana pa kuanzia. Dhana ya kilimo kwanza kwake ni msamiati usio na mashiko. Likitokea la kutokea kwamba mzazi amefariki dunia huu unakuwa ni mwanzo wa mwisho wa mtoto huyu! Ataanza kujioanisha na mazingira  yatakayomfaa (to search for identity). Atayapata mazingira hayo au kwa watumia dawa za kulevya, kwa wavulana au kwa kufanya ukahaba kwa wasichana. Hapa tusiulizane madhara yake nini.

Laiti mtoto huyu angelikuwa anajua kujitegemea japo kidogo tu angeyamudu maisha. Angekuwa mnyenyekevu. Kwa bahati mbaya kila mtoto anaota kwenda Ulaya tena kwa gharama yoyote ile. Mzazi atafanya kila linalowezekana na lisilowezekana, mtoto atahonga hata visivyohongeka ili mradi aende Ulaya! Kufanya nini? Sina jibu.

Sera ya elimu iangaliwe upya. Shule zote (binafsi na serikali) ziwekewe vigezo. Tusiogope kujifunza kutoka mahali pengine. Kwa mfano shule za seminari zinaongoza kwa kufanya vizuri. Lakini hapa ni mahali wanafunzi wanafanya kazi zote peke yao. Wana mashamba yao wanayolima na kuvuna wenyewe, wanafanya usafi wa mazingira na vyumba vya madarasa yao, kwa kifupi wanajitegemea wakiongozwa na nidhamu ya hali ya juu. Haijawahi kutokea mtoto aliyemaliza masomo katika shule hizi akawa tegemezi kiasi cha kutobebeka. (kwa ujasiri naruhusu changamoto kwa hili kutoka wa mtu yeyote). Huu ni ushahidi kwamba inawezekana. Tujenge msingi imara ili kuwa na taifa imara.

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Prosper Minja
paminja@yahoo.com
+255-713123254
www.prince-minja.blogspot.com

Toa maoni yako