MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa ametangaza kwamba wananchi wakimpatia ridhaa ya kuiongoza Tanzania, elimu itatolewa bure kuanzia shule za chekechea hadi kidato cha sita.
Wakati Slaa akiahidi hivyo, mgombea wa urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amekwenda mbali zaidi. Yeye amesema akiikamata dola, elimu itakuwa bure hadi chuo kikuu.
Lakini, mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Mrisho Kikwete hajazungumzia suala hilo la kutoa elimu bure akipewa miaka mingine mitano ya kuwapo Ikulu, isipokuwa amekuwa akisisitiza juu ya azma yake ya kuendeleza kile alichokianzisha katika miaka yake mitano ya kwanza kwa kuboresha elimu inayotolewa.
Kwa mfano, katika moja ya mikutano yake ya kampeni, Rais Kikwete alisema ya kuwa zaidi ya walimu 16,000 wanatarajia kumaliza mafunzo yao kutoka vyuo mbalimbali nchini ili kupunguza pengo la uhaba wa wataalamu hao katika sekondari za kata.
Alisema kumalizika kwa tatizo hilo kutaboresha elimu ya sekondari za kata nchini.
Baadhi ya wakuu wa CCM wanabeza hoja ya elimu kutolewa bure kwamba jambo hilo katika Tanzania haliwezekani.
Mwenyekiti wa timu ya kampeni ya CCM, Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba na Spika anayewania kuchaguliwa tena kuwa mbunge wa Urambo, Samwel Sitta, ndiyo waliojitokeza kuwapinga Slaa na Lipumba kwamba ni ndoto kutoa elimu bure.
Slaa na Lipumba wanasema elimu kutolewa bure ni jambo linalowezekana iwapo serikali itajipanga sawasawa kwa maana ya kukusanya kodi zote zinazostahili kulipwa na kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha za serikali.
Kwa kifupi wanachosema ni kuwa serikali kuwa makini kuhakikisha kwamba inaziba mianya yote ya ufisadi ili fedha ambazo zingewanufaisha watu wachache zielekezwe katika masuala yenye maslahi na wananchi ikiwemo elimu. Pia Serikali ipunguze matumizi ya anasa kama vile kununua magari ya kifahari ili fedha hizo zielekezwe katika elimu, afya na mambo mengine muhimu kwa wananchi.
Lakini ni kweli kwamba elimu inaweza ikatolewa bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu? Wapo wanaoamini kabisa kwamba hilo linawezekana na wanatoa mfano wa enzi za uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere kwamba elimu ilitolewa bure hadi chuo kikuu na wagombea wote watatu wa nafasi za urais (Slaa, Lipumba na Kikwete) walinufaika na mpango huo.
Wanaopinga wanasema kwamba enzi za Mwalimu na sasa ni tofauti. Enzi hizo idadi ya watu haikuwa kubwa kama ilivyo sasa; hivyo Serikali ilimudu kuwa na jeuri hiyo, tofauti na sasa ambapo idadi ya watu wakiwemo wanafunzi ni kubwa mno.
Hebu turudi tena kwenye swali letu la msingi: Kweli elimu inaweza kutolewa tena bure kama ilivyokuwa enzi za Mwalimu?
Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa nchini, Lameck Mfalila ni miongoni mwa wale wanaoamini kwamba elimu kutolewa bure Tanzania ni jambo linawezekana; tena anawataka Watanzania wamwone mtu anayetoa ahadi hiyo kuwa ni mtu makini anayewafaa.
"Huyu ni shujaa, sio ghilba bali amethubutu kusema anaweza kufanya mabadiliko hayo, mchagueni," alisema jaji huyo katika mkutano wa wanaharakati kuhusiana na Uchaguzi Mkuu, mjini Dar es Salaam, hivi karibuni.
“Kuna mgombea mmoja kutoka kwenye vyama vya upinzani, naona anaitia changamoto Serikali, yeye alithubutu kusema ikiwa atachaguliwa kuingia Ikulu, atasomesha wanafunzi na kutoa huduma ya afya bure. Huyu ni shujaa, sio ghilba; bali amethubutu kusema anaweza kufanya mabadiliko hayo, mchagueni,” alisisitiza.
Jaji Mfalila alisema Tanzania ina makampuni makubwa ya madini yakiwamo ya dhahabu na almasi na makampuni hayo yanaingiza kiasi kikubwa cha fedha, lakini kutokana na ujanja uliopo makampuni hayo yanalipa kiasi kidogo cha kodi hivyo kuwanufaisha wachache.
Jaji Mfalila aliichambua Tanzania ilikotoka, ilipo hivi sasa na inakokwenda akisema ya kuwa rasilimali zake zinatumika kiujanja ujanja jambo lililosababisha nchi kutegemea misaada kutoka kwa wahisani na nchi rafiki.
Katika mkutano huo huo, Profesa Chris Peter Maina wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam naye alisisitiza ya kuwa elimu kutolewa bure ni jambo linalowezekana.
“Nimesoma bure kuanzia darasa la kwanza hadi nilipopata shahada yangu ya uzamili. Sharti kuu lililokuwapo ni kwamba nilihitajika kujaza fomu kuazimia kuwa nitalitumikia taifa langu baada ya kuhitimu masomo yangu,” alisema Profesa huyo.
Serikali ya Awamu ya Nne, chini ya Rais Kikwete, inajivunia ujenzi wa shule za kata ambzo zimeongeza idadi ya watoto wanaopata fursa za elimu ya sekondari. Hadi kufikia mwaka 2005, shule za sekondari zilizo chini ya serikali zilikuwa 1,745 na idadi ya shule hizo kutokana na ujenzi wa shule za kata ikapanda hadi kufikia shule 4,102 mwaka 2000.
Idadi ya wanafunzi nayo ikaongezeka kutoka 524,325 mwaka 2005 hadi 1,466,402 mwaka 2009; hivyo wanafunzi wengi zaidi walipatiwa fursa ya elimu ya sekondari ambao wasingeipata kama mpango huo usingetekelezwa.
Sawa, shule za kata zimejitokeza kama uyoga na wanafunzi wengi wamepelekwa katika shule hizo, lakini elimu wanayopata kweli inakidhi? Serikali inawajibika ipasavyo?
Profesa Maina alitoa mwanga kidogo kuhusu tatizo lililopo katika shule hizo za serikali katika mkutano wa wanaharakati.
Alisema tatizo la Tanzania ni viongozi waliopo serikalini ambao wanajijali wao tu na akatoa mfano wa wakaguzi wa elimu kupewa magari ya Sh. milioni 150 yaliyo na viyoyozi na kazi yao ikiwa ni kukagua madarasa yasiyo na madawati na yenye wanafunzi wanaoketi sakafuni!
Kwa wale waliosoma enzi za Mwalimu mkoani Dar es Salaam katika miaka ya 1960 na 1970 watakubaliana na Profesa Maina kwamba hilo nalo neno. Enzi hizo kulikuwa na mkaguzi mmoja maarufu kwa jina la Kibira ambaye alikuwa makini mno na kazi yake na kufanya shule za Dar es Salaam zisisinzie hata kidogo katika kutoa elimu bora na alifanya kazi hiyo bila ya kupewa gari la kifahari.
Ndiyo, kukosa umakini, ukosefu wa uwanjibikaji ndiyo tatizo kubwa katika sekta yetu ya elimu kiasi kwamba sasa tunatoa ‘wahitimu’ wa kila ngazi wenye viwango vya ajabu mno.
Lakini, hivi watoto wetu wanajifunza? Hili ndilo swali ambalo mradi wa miaka minne unaoitwa UWEZO unaolenga kuboresha stadi za kujua kusoma na kuandika na hisabati kwa wanafunzi wenye umri wa miaka 5-16 nchini Kenya, Tanzania na Uganda, unajaribu kulijibu.
Ifuatayo ni ripoti ya UWEZO kuhusu utafiti uliofanywa nchini Tanzania kwa wanafunzi wenye umri wa miaka mitano hadi 16 kama ilivyotolewa kwa wadau wa elimu, hivi karibuni, mjini Dar es Salaam.
Utangulizi
Kote nchini, maendeleo makubwa yamefikiwa kwenye elimu ya msingi ndani ya muongo (miaka 10) uliopita. Uandikishaji umepanda maradufu kote elimu ya msingi na sekondari, na mamilioni ya watoto wameweza kwenda shule. Tanzania iko mbele ya muda wa kutekeleza na kuyafikia malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) yanayohusu upatikanaji wa elimu na usawa wa kijinsia katika elimu.
Madarasa maelfu yamejengwa na maelfu ya walimu wameajiriwa. Bajeti ya elimu imeongezeka mara tatu zaidi kwa kipindi hiki; Serikali sasa inatumia dola za kimarekani zaidi ya bilioni moja kila mwaka au karibu Sh. 1 kwa kila Sh. 5 ya bajeti ya elimu.
Mafanikio haya siyo hatua rahisi; yalihitaji dhamira kubwa ya kisiasa na mgawo mkubwa wa fedha za umma. Wazazi pia wamejitahidi kugharamia sehemu yao, maana hata ile elimu ya bure kiuhalisia sio bure, maana kuna gharama za sare za shule, vitabu, kalamu, masomo ya ziada, usafiri na mengineyo.
Swali la msingi hapa ni: Je, jitihada na uwekezaji huu mkubwa umezaa matunda gani? Je, watoto wetu wanauwezo wa kusoma na kufanya mahesabu? Mantiki ya elimu ni kumsaidia kila mtoto kukuza maarifa ili aweze kuishi maisha yenye ustawi ndani ya dunia – kwa kuanza kujua kusoma na kufanya mahesabu stadi ambazo zinaweka msingi wa uwezo wa kudadisi, kufikiri, kusikiliza, kuuliza maswali, kuchambua, kupambanua na kuwasiliana kwa kujiamini. Je, shule zetu zinafanikiwa kwenye jukumu hili? Watoto wetu wanajifunza?
Matokeo muhimu
Mhitimu mmoja kati ya wahitimu watano hawezi kusoma Kiswahili cha ngazi ya darasa la pili.
Japo Kiswahili ni lugha inayozungumzwa kwa upana zaidi nchini, idadi kubwa ya watoto hawawezi kusoma Kiswahili bila shida. Kwenye sampuli zetu, chini ya nusu (42.2%) ya watoto waliofanyiwa uchunguzi waliweza kusoma kwa hatua ya hadithi.
Wakati watoto wote katika darasa la tatu wanapaswa kuweza kusoma hadithi ya ngazi ya darasa la pili, watoto chini ya mmoja kati ya 3 (32.7%) ndio wanaweza. Watoto wengi hawajifunzi kusoma hadithi rahisi hadi wafikie darasa la tano au la sita Hata hivyo, hadi wanamaliza shule ya msingi, mtoto mmoja kati ya watano hawezi kusoma hadithi ya ngazi ya darasa la pili.
Licha ya kumaliza miaka saba ya elimu ya msingi, watoto hao wanaelekea kubaki mbumbumbu (hawajui kusoma na kuandika) maishani mwao.
Nusu ya wanafunzi hawawezi kusoma Kiingereza cha ngazi ya darasa la pili.
Kiingereza ni somo gumu zaidi kwa wanafunzi. Ingawa wanafunzi wote wa darasa la tatu wanapaswa kuweza kusoma Kiingereza cha ngazi ya darasa la pili, chini ya mwanafunzi mmoja kati ya 10 (7.7%) ndio anaweza.
Maendeleo kwenye somo la Kiingereza ni ya taratibu sana; kwa darasa la tano, ni mtoto mmoja tu kati ya watoto wanne anaweza kusoma hadithi. Karibu nusu ya wanafunzi hawawezi kusoma hata maneno mafupi ya Kiingereza.
Watoto wengi wanafika darasa la saba bila kuwa na stadi zozote za Kiingereza. Hadi wanamaliza shule ya msingi, nusu ya wanafunzi (49.1%) bado hawawezi kusoma hadithi ya kiwango cha darasa la pili ya Kiingereza, na bila shaka wanafunzi wachache sana wana uwezo wa kusoma kwenye ngazi ya darasa la saba.
Hii ina maana kuwa idadi kubwa ya wanafunzi wanaoingia sekondari hawawezi kusoma kwa lugha ya Kiingereza ambayo ni lugha ya kufundishia elimu ya sekondari.
Wahitimu saba tu kati ya 10 wanaweza kufanya hesabu za ngazi ya darasa la pili
Ingawa stadi za kuzidisha ziko kwenye mtaala wa darasa la pili, wanafunzi wachache tu wa darasa la pili waliweza kuzidisha bila shida. Zaidi ya nusu ya wanafunzi hawawezi hata kujumlisha. Hadi kipindi wanafika darasa la 5, watoto wengi wanaweza kutoa na kujumlisha, lakini wengi bado hawawezi kuzidisha.
Watoto wengi wanapata stadi za Hisabati mwishoni mwa shule ya msingi. Hata hivyo, watoto watatu kati 10 (31.5%) wa darasa la saba bado hawawezi kufanya hesabu za kuzidisha za ngazi ya darasa la pili.
Na mtoto mmoja kati ya 10 anamaliza shule ya msingi bila kuwa na stadi za Hisabati kabisa; hawezi hata kujumlisha hesabu ndogo. Hii inaweza kumaanisha kuwa watoto wengi wanaojiunga na shule za sekondari hawana msingi imara kwenye Hisabati ambao ni muhimu kwenye kujifunza na uchambuzi, hasa katika masomo ya sayansi na biashara.
Watoto wa mijini hufanya vizuri zaidi kuliko wa vijijini
Watoto wa mijini hupata asilimia kati ya 7 na 10 zaidi kuliko watoto wa vijijini katika masomo yote. Tofauti ni kubwa zaidi hususani katika madarasa ya pili hadi nne, wakati watoto wa mijini huanza kupata stadi za msingi ilhali wenzao wa vijijini wanaachwa nyuma.
Inaelekea kuwa watoto wa vijijini hatimaye huanza kupata stadi hizo za darasa la pili wafikapo madarasa ya sita na saba; lakini kuna uwezo mkubwa kuwa wanazidi kuporomoka zaidi kwenye stadi ya kusoma katika ngazi yao.
Wasichana hufanya vizuri kuliko wavulana
Wasichana walifanya vizuri zaidi katika masomo yote waliyopimwa, ingawa tofauti ni ndogo sana. Kati ya watoto wote waliopimwa, 43.5% ya wasichana waliweza kusoma hadithi katika Kiswahili ikilinganishwa na 40.7% ya wavulana.
Katika masomo ya Kiingereza na Hisabati tofauti ilikuwa ni ndogo mno, kama inavyooneshwa katika jedwali hapo chini. Hata hivyo matokeo haya yanapingana na ile
dhana ya muda mrefu kuwa wasichana hawafanyi vizuri kama wavulana, na inaibua maswali kuhusu kwa nini kunakuwa na tofauti kubwa katika matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ambapo wavulana hung’ara zaidi.
Hata hivyo, tofauti hizi ndogo zisifiche ule ukweli mkubwa zaidi kuwa watoto wengi mno wasichana na wavulana hawana uwezo wa kimsingi katika masomo ya lugha zote mbili na Hisabati.
Watoto wenye mama waliosoma hufanya vizuri zaidi
Watoto ambao mama zao wamesoma hadi elimu ya sekondari hufanya vizuri sana kuliko watoto wengine. Kwa mfano, katika darasa la 3 na 4 watoto hawa wana uwezekano wa mara tano zaidi kuweza kusoma hadithi ya Kiingereza na wana uwezekano wa mara mbili zaidi kufanya Hisabati na kusoma hadithi ya Kiswahili.
Hata watoto ambao mama zao wamemaliza elimu ya msingi tu wanafanya vizuri kiasi kuliko wale ambao mama zao hawajasoma kabisa. Tofauti katika matokeo huanza kujionesha kuanzia darasa la kwanza hadi darasa la saba; ikiashiria kwamba elimu ya mama ni muhimu katika ngazi zote za shule.
Hitimisho
Matokeo ya tathmini ya Uwezo iliyohusisha kaya zaidi ya 20,000 na watoto zaidi ya 40,000 yanaonesha kuwa kuna tatizo kubwa katika elimu nchini Tanzania. Hadi wanapoingia darasa la tatu, watoto asilimia 100 wanapaswa kuwa na stadi za kusoma na kuhesabu.
Lakini ukweli ni kuwa hadi darasa la tatu, watoto saba kati ya 10 hawawezi kusoma Kiswahili cha msingi; watoto tisa kati ya 10 hawawezi kusoma Kiingereza cha msingi, na watoto wanane kati ya 10 hawawezi kufanya Hisabati za msingi.
Hata wanapofikia hatua ya kumaliza elimu ya msingi idadi kubwa mno ya watoto huwa hawawezi kufanya kile ambacho walipaswa kuwa wanakijua miaka mitano iliyotangulia wakati wakiwa katika darasa la pili. Mgawanyo kiwilaya unaonesha tofauti kubwa kati yao, na ambapo baadhi ya wilaya ziko chini sana ya wastani wa kitaifa.
Ukweli ulio bayana ni kuwa, licha ya maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika elimu yaliyowezekana kutokana na kuwekezwa kwa matrilioni ya shilingi kila mwaka, idadi kubwa sana ya watoto nchini Tanzania hawajifunzi.
Je, nini kifanyike kuhusu hali hii? Kwanza, tunahitaji kutulia na kutafakari matokeo haya na kuchunguza yanamaanisha nini. Kukimbilia kuyapuuza au kutunga masuluhisho ya haraka haraka pengine haitasaidia, kwani inaweza kusababisha kushindwa kutambua kiini cha tatizo na hivyo kuchukua hatua zisizofaa.
Kushangilia majengo mapya na idadi kubwa ya watoto wanaoandikishwa shule inaweza kuwa hatari kama matokeo yake ni kufunika ukweli kwamba idadi kubwa ya watoto wanamaliza elimu ya msingi bila kujua kusoma na kuhesabu.
Pili, ingawa changamoto lazima ziwepo pale ambapo mfumo wa elimu unapopanuliwa ghafla, bado tunaweza kuuliza: Je, mikakati ya kisera na malengo ya kisiasa yanalenga mambo sahihi?
Hivi sasa, nchini Tanzania na kwingineko, mkazo zaidi umewekwa katika kupatikana kwa vitendeakazi kama vile madarasa, maabara, vitabu na walimu, badala ya matokeo ya ujifunzaji. Mathalani, stadi za kusoma, kuhesabu, kuandika udadisi na ubunifu.
Kwa vile ushahidi unaonesha kuwa vitendeakazi havijaleta stadi hizi, kuna umuhimu wa kupanga mfumo mzima wa elimu kulenga zaidi uwezo na stadi za mwanafunzi, kuanzia ndani ya wizara zinazohusika na elimu, taasisi za elimu, watunga mitaala, mitihani, tathmini ya walimu na shule, vipimo vya maendeleo na vipaumbele vya kisiasa.
Tatu, kuna haja ya kuangalia zaidi nini kinachotokea shuleni kuliko kutazama takwimu za kitaifa pekee. Tafiti zilizofanyika katika nchi nyingi zinaonesha kuwa mchakato wa kufundisha na kujifunza unaweza kuwa na hitilafu kubwa.
Mawili kati ya matatizo ambayo hujitokeza mara kwa mara ni kuwa shule hazipati fedha za kutosha (yaani bajeti za elimu zinazoongezeka zinatumika kwa mambo mengine badala ya kuboresha shule) na kwamba walimu hawana motisha ya kutosha na hawafundishi (yaani muda wanaotumia kufundisha darasani ni mdogo mno).
Pengine itasaidia kuchambua mambo hayo mawili kwa kina, na kutafuta namna ya kuyaboresha. Pia kuna haja ya kuangalia kwa makini uhusiano kati ya rasilimali za kutosha kufika shuleni na walimu kuwapo kazini kwa upande mmoja, na uwezo na stadi za mwanafunzi anapohitimu kwa upande mwingine.
Nne, uwazi zaidi unaweza kuwawezesha watunga sera na watu wengine kutafakari na kuchukua hatua. UWEZO imedhamiria kusambaza matokeo ya tafiti zake ili kusaidia kulifikia lengo hili.
Lakini Serikali inaweza kwenda mbele zaidi ili kuwezesha data za kila shule kupatikana kwenye mtandao, na katika vyombo vya habari kila afisa wa serikali ya mtaa, mwalimu, mzazi na mwanafunzi alinganishe hali na utendaji wake na wa wengine.
Maendeleo ya teknolojia hasa usambazaji wa simu za mkononi vimewezesha ubadilishanaji habari katika kiwango kikubwa na kufungua fursa mpya nyingi.
Tano, badala ya kuendelea kufanya kile ambacho kimeshafanyika kwa jitihada zaidi, pengine umefika wakati wa kufanya kitu tofauti. Utafiti wa Uwezo na tafiti zilizofanyika duniani zinaashiria kuwa kiini cha kitendawili hiki ni kuangalia upya suala la motisha ili wadau muhimu katika sekta hii watambuliwe kwa kuhamasisha kujifunza.
Wazo moja ambalo linafaa kufikiriwa, na ambalo Rais Jakaya Kikwete keshalipokea, linaitwa ‘cash on delivery’ au malipo baada ya matokeo. Msingi wake mkuu ni kuwa kupatikana kwa fedha zaidi kwa kazi ya elimu kutategemea kufikiwa kwa malengo (yaliyokaguliwa na shirika huru), kama vile kusoma na kuhesabu (kwa mfano kwa kila mtoto anayemaliza elimu ya msingi akiwa na stadi zilizokubalika, zitatolewa Sh. 300,000).
Wazo hili linaweza kupanuliwa ili hizo Sh. 300,000 zigawiwe kwa viongozi wa eneo ilipo shule, walimu, na pengine hata wazazi. Lengo ni kuwashawishi wadau wahusika kuzingatia na kutambua mafanikio katika kujifunza. Hakuna hakikisho kuwa wazo hili litafanikiwa.
Lakini katika hali ya kuwepo kwa tatizo kubwa linaloikabili sekta ya elimu Tanzania kwa sasa, hasa pale ambapo njia za kawaida zimeshindwa kuleta mafanikio ya maana, kufanya majaribio mbadala.
Toa maoni yako