Falsafa miaka 3000, Ukristo miaka 2000, sayansi miaka 1000, na uchawi Afrika: Tatizo sio Plato pekee

NAPENDEKEZA kukosoa mtazamo wa Padre John S. Mbiti na wafuasi wake kuhusu jambo moja muhimu katika vita ya kuporomosha ushirikina pamoja na mateso yake katika Bara la Afrika.

Katika kitabu chake:  “African Philosophy and Religion,” kilichochapishiwa Nairobi, mwaka 1969, kupitia kampuni ya Heinemann Kenya Ltd, Profesa Mbiti anaonekana kutetea uhai wa kiontolojia (ontological existence) wa “ulimwengu wa roho.”

Anaandika: “Whatever science may do to prove the existence or non-existence of the spirits, one thing is undeniable, namely that for African peoples the spirits are a reality and a reality which must be reckoned with, whether it is clear, blurred, or confused reality (uk.91).”

Ni maoni yangu kuwa, huu ni mtazamo wenye msingi wake katika kosmolojia ya Plato, kosmolojia ambayo ni kikwazo kikubwa katika vita ya kuporomosha ushirikina barani Afrika.

Ushahidi mwingi wa kisayansi unaonyesha kuwa, tofauti na mafundisho ya Plato, na tofauti na picha ya dunia waliyo nayo Waafrika, kuhusu ulimwengu wa roho (spirit-world), ulimwengu huu hauna uhai wa kiontolojia (ontological existence). Hivyo, sehemu kubwa ya picha ya dunia waliyo nayo Waafrika kuhusu ulimwengu wa roho inaweza kubadilishwa na kuwa ya kisayansi.

Makala hii inalenga kuutetea msimamo huu kwa hoja. Nitayachambua maandiko ya Plato, ili kuonyesha kuwa picha ya ulimwengu wa roho anayoiongelea ni hekaya za Wagriki (Greek mythology), zisizo na msingi wowote wa kisayansi, wala kifalsafa.

Hoja 10 za Plato. Mhariri John Cooper, ameyakusanya maandiko yote ya Plato katika kurasa zisizozidi 1,500 ndani ya kitabu kimoja: “Plato, Complete Works (Indianapolis: Hecket Publishing Company Ltd, 1997).” 

Baada ya kusoma kitabu hiki, pamoja na maandiko kadhaa yenye kukitafsiri, ninaona kwamba, kosmolojia ya Plato inajumuisha hoja kubwa 10.

Kuna hoja kuhusu kiranja mkuu wa ulimwengu aitwaye Demiurige (supremacy of Demiurge thesis);  hoja juu ya kanuni za mabadiliko katika ulimwengu wa mwili (spatio-temporal causality thesis); na hoja kuhusu namna fomati za mbingu zinavyofanya kazi ya kuhuisha kumbukumbu za binadamu aliye duniani (ensoulment and recollection thesis).

Kuna hoja kuhusu chimbuko la uovu ulimwenguni (an errant cause thesis); hoja juu ya mizunguko ya nyota kama kipimo cha muda (star-centric time reckoning thesis); na hoja kuhusu maudhui ya vitu vyenye mwili (material composition thesis).

Aidha, kuna hoja juu ya udhaifu wa milango ya maarifa (fallibility of human senses thesis); hoja kuhusu aina mbili za ulimwengu (dual world thesis); hoja juu ya fomati-za-mbinguni kama vitu halisi visivyo na mwili unaopatikana katika vitu vilivyoko duniani (immaterial-material divide between universals and particulars thesis); na hoja kuhusu mfumo wa nasaba uliopo kati ya fomati za mbinguni taswira za duniani (metaphysical structure of participation thesis).

Kwa sababu ya lengo lake, lakini pia kutokana na ufinyu wa nafasi, makala hii itajadili, japo kwa ufupi kabisa, yaliyomo katika hoja nne za mwisho, kama zilivyotajwa hapo juu.

Plato na udhaifu wa milango ya maarifa

Hoja ya Plato juu ya udhaifu wa milango ya maarifa (fallibility of human senses thesis) inasema kuwa, kuna maarifa ambayo hayawezi kupatikana kwa kutumia milango mitano ya fahamu, isipokuwa kwa njia ya ufunuo kutoka mbinguni. Katika hoja hii Plato anasema:

Maarifa ya kweli hayapaswi kubadilika kulingana na muda au mahali alipo mwenye maarifa hayo. Lakini, tunafahamu kuwa, maarifa yetu juu ya ulimwengu unaotuzunguka yanabadilika kila mara kulingana na muda au mahali alipo mwenye maarifa husika.

Kwa mfano, asubuhi mvua inanyesha, mchana mvua hainyeshi, bali kuna jua kali. Hivyo, muda aliomo mwenye maarifa kwa sasa unabadilisha maarifa yake ya awali.

Unaweza pia kumtazama tembo kwa mbali akaonekana kama mbuzi mdogo. Ukimsogelea karibu unakuta si mbuzi mdogo tena, bali ni tembo mkubwa. Hivyo, mahali aliposimama mwenye maarifa kwa sasa panabadilisha maarifa yake ya awali.

Kwa hiyo, Plato anasema, tunapoutumia mlango wa maarifa kukitambua kitu, picha tunayoipata kichwani, si maarifa, bali maoni binafsi yanayobadilika juu ya kitu kile, japo kitu chenyewe hakibadiliki. Maoni yanategemea muda na mahali alipo mwenye maoni.

Lakini, bado Plato anaamini kuwa, maarifa ya kweli yanawezekana. Anadai kuwa maarifa ya kweli yanahusisha utambuzi wa sifa za msingi za kitu husika. Hizi ni sifa zisizobadilika kulingana na muda au mahali alipo mwenye maarifa.

Hapa, Plato anaongelea sifa mtambuka (universal or essential properties), yaani sifa “zinazotambuka” mabadiliko ya muda na mahali. Hivyo, anaona kuwa, sifa hizi lazima ziwe nje ya ulimwengu wa mabadiliko.

Inaeleweka kuwa, anga lote ni tufe linalotawaliwa na kanuni za muda na mahali, kwa maana kwamba ni uwanja wa matukio na mabadiliko yanayotokana na matukio hayo. Hivyo, Plato anapendekeza kuwa, ulimwengu wa sifa zisizobadilika lazima uwe ni ulimwengu ulio nje ya anga hili (spatio-temporal exteriority). Anauita ulimwengu ulio nje ya muda na mahali “mbingu.”

Kwa hiyo, Plato anafikiri, vitu “tunavyoviona” kwa kutumia milango mitano ya maarifa, vitakuwa ni taswira-za-duniani (world of sensible objects), ambazo ni nakala za fomati-ya-mbinguni (heavenly world of forms). Wakati fomati-ya-mbinguni ni ya kudumu, taswira-ya-duniani inabadilika kulingana na muda na mahali, anasema.

Namna hii, Plato anahitimisha kuwa, tunapopata maarifa ya kweli, si maarifa juu ya kitu chenye mwili, ambacho ni taswira-ya-duniani, bali ni maarifa juu fomati-ya-mbinguni, yenye kudumu na iliyoko uwinguni.

Hivyo basi, kutoka na hoja hii, tunaona kuwa, harakati za Plato katika kutofautisha maarifa yasiyobadilika, kwa upande mmoja, na maoni yanayobadilika, kwa upande mwingine, zilimlazimisha kubuni wazo kwamba “ulimwengu wa mwili” wenye kubadilika ni taswira ya “ulimwengu wa roho” usiobadilika. 

Kimsingi, anachosema Plato hapa ni kwamba, pamoja na tofauti zilizopo kati ya kondoo wote dunaini, huko mbinguni, kuna fomati-ya-ukondoo isiyobadilika, na ambayo “inapigwa fotokopi” ili kupata taswira-ya-duniani ya kila kondoo tunayemwona. Ni vivyo hivyo, kwa kila seti ya vitu iliyopo hapa duniani.

Yaani, seti ya wanadamu ni kusanyiko la mwanadamu mmoja mmoja ambaye ni “fotokopi” ya fomati-ya-ubinadamu iliyoko mbinguni; seti ya mbuzi ni kusanyiko la mbuzi mmoja mmoja ambaye ni “fotokopi” ya fomati-ya-umbuzi iliyoko mbinguni, seti ya maaskofu ni kusanyiko la askofu mmoja mmoja ambaye ni “fotokopi” ya fomati-ya-uaskofu iliyoko mbinguni; na orodha inaendelea.

Vitambuka na vitambukwa vya Plato

Kusudi tuweze kuikosoa hoja hii ya Plato, ni muhimu tuelimishane kidogo kuhusu kauli yake kwamba, fomati-za-mbinguni ni sifa-mtambuka (universal properties) yenye jina moja linalotumika kuvirejea vitu anuai, ambavyo ni “fotokopi” yake.  

Sifa-mtambuka (universal property) ni sifa inayopatikana kwa wakati mmoja, katika vitu viwili, au zaidi, vilivyo katika maeneo mawili tofauti, na hivyo kuvifanya vitu hivyo kufanana kwa sababu ya kuonyesha sifa hiyo kwa pamoja.

Yaani, kama “kitu x” kinayo “sifa-F,” na “kitu y” kinayo “sifa-F,” basi, kuna “sifa-F,” ambayo inapatikana katika “kitu x” na inapatikana katika “kitu y” kwa wakati mmoja.

Kwa mfano, kama “shati lako” ulilolivaa sasa hivi lina “rangi nyeupe,” na “viatu vyako” ulivyovivaa sasa hivi vina “rangi nyeupe,” basi, kuna “sifa-ya-weupe,” ambayo imelizingira “shati lako” na imevizingira “viatu vyako” kwa wakati mmoja.

Na hapo kuna mambo matatu, ambayo lazima kuyafahamu, lakini makubwa ni mawili. Kwanza, kuna rangi nyeupe kama sifa inayozingira shati na viatu vyako kwa mpigo. Kwa hiyo, rangi nyeupe ni sifa mtambuka (cross-cutting property). Katika makala hii, sifa ya aina hii tuiite “kitambuka” (universal) katika umoja, au “vitambuka” (universals) katika wingi.

Na pili, kuna shati na viatu vyako kama vitu viwili vinavyozingirwa au kutambukwa na sifa mtambuka moja, yaani “sifa-ya-weupe.” Kwa hiyo, shati na viatu, kila kimoja, ni “kitambukwa” (particular), na vyote viwili kwa pamoja, tuviite “vitambukwa” (particulars).

Kwa hapa itoshe kusema kuwa, kuna mifano mingi ya vitambuka (universals). Kuna ualimu, ubaba, umama, upadre, uaskofu, ubunge, ukaka, na udada. Pia kuna vitambuka kama vile weusi, wekundu, ubinadamu, unyani, usungura, ukondoo, ukuku, ubata, umbuzi, uanauke, uanaume, ujana, uzee, ulemavu, urembo, weupe,  na kadhalika. Kuna vitambukwa (particulars) kwa kila kitambuka (universal) kilichotajwa.

Kwa ujumla, Plato alifundisha kuwa, wakati vitambuka (universals) vinaishi katika ulimwengu wa roho, kama fomati-za-mbinguni, vitambukwa (particulars) vinaishi katika ulimwengu wa mwili, kama fotokopi-za-duniani.

Hivyo, utaona kuwa, hoja ya Plato inazua maswali kadhaa ya kidadisi. Mwandishi mmoja amefupisha maswali hayo vizuri kama ifuatavyo:

“The problem of one universal and many particulars relates to the deep questions concerning the ontological status of particulars and universals. These questions are: (1) what is the difference between particulars and universals? (2) do universals exist extra-mentally or they are only mental concepts? (3) if they exist extra-mentally, are they material or immaterial entities? (4) if they are immaterial entities residing in heaven, how do they communicate with material entities residing on earth?”

Plato alijitahidi kujibu baadhi ya maswali haya. Lakini, kwa mujibu wa utafiti wangu, hakutoa jibu sahihi kwa swali la kwanza. Kuhusu swali la pili, Plato anasema vitambuka (universals) vinayo makazi yake nje ya akili, kwa maana kwamba, vitambukwa ni zaidi ya taswira zilizo vichwani mwetu.

Kuhusu swali la tatu, Plato anasema kuwa, vitambuka (universals) ni vitu visivyo na mwili, lakini vyenye uhai kamili wa kiontolojia, kama ilivyo kwa vitambukwa (particulars). Na kuhusu swali la nne, Plato anasema kuwa, mawasiliano kati ya vitambuka na vitambukwa ni kupitia mchakato anaouita “participation,” yaani, “particulars participate in universals.”

Majibu mengi ya Plato ni dhaifu sana kiasi kwamba, yalikataliwa na Aristotle, na kutupiliwa mbali na Thomas Aquinas.  Kwa ufupi, tuone majibu yake kwa swali la tatu na swali la nne hapo juu.

Plato anadai vitambuka havina mwili

Plato anadai kuwa vitambuka, na fomati-za-mbinguni zikiwemo, ni vitu halisi visivyo na mwili (universals as immaterial entities thesis). Kusudi tuweze kuelewa anachokisema, tutumie mfano kwamba, sasa hivi wewe msomaji umevaa suruali nyeusi, kofia nyekundu na viatu vyekundu, ili kuonyesha hoja ya Plato. Kuhusu jambo hili, Plato alijenga hoja ifuatayo:

Kama “kofia yako” uliyolivaa sasa hivi ina “rangi nyekundu,” na “viatu vyako” ulivyovivaa vina “rangi nywekundu,” basi, kuna “sifa-ya-wekundu,” ambayo inapatikana katika “kofia yako” na inapatikana katika “viatu vyako” kwa wakati mmoja.

Hii maana yake ni kwamba, japo “kofia yako” na “viatu vyako” viko katika maeneo mawili tofauti ya mwili wako, bado, vitu hivi viwili vinashirikiana kitu kimoja, yaani “sifa-ya-wekundu.”

Lakini, tunafahamu kuwa, hakuna kitu chenye mwili kinachoweza kuwa katika maeneo mawili kwa wakati mmoja. Kofia haiwezi kuwa miguu na kichwani kwa mpigo. Na viatu haviwezi kuwa miguuni na kichwani kwa mpigo pia.

Hivyo, Plato anahitimisha kuwa, kitambuka kiitwacho “rangi nyekundu” ni kitu chenye uhai wa kiontolojia unaojitegemea, lakini kisicho na mwili (abstract object).

Kwa maoni yake, hii ndiyo sababu “rangi nyekundu” inaweza kuwa katika sehemu mbili kwa wakati mmoja. Kwa mujibu wa Plato, makazi ya kitambuka hiki, kiitwacho rangi nyekundu, pamoja na vitambuka vingine vyote, yako mbinguni. Yaani, kwa hapa duniani, “rangi nyekundu” ni mpita njia tu.

Anachosema Plato ni kwamba, vitambuka (universals) vifuatavyo vinayo makazi yake mbinguni: ualimu, ubaba, umama, upadre, uaskofu, ubunge, ukaka, na udada. Pia kuna weupe, weusi, wekundu, ubinadamu, unyani, usungura, ukondoo, ukuku, ubata, umbuzi, uanauke, uanaume, ujana, uzee, ulemavu, urembo na kadhalika.

Kwa kuzingatia mantiki hii ya Plato, huko mbinguni, kuna vitambuka ambayo havijazingira kitu chochote hapa duniani, lakini viko vikisubiri wakati wake ufike. Yaani, shati lako jekundu likichomwa moto tunapata majivu meusi. Hii maana yake ni kwamba, rangi nyekundu iliyokuwemo imetoweka na kurudi mbinguni, na inasubiri kurudi duniani ili ikizingire kitu kingine katika wakati mwafaka.  

Anayoyasema Plato juu ya vitambuka hiki kiitwacho “rangi nyekundu,” ndiyo aliyoyasema juu ya uhusiano uliopo kati ya fomati-ya-mbinguni (kitambuka) na fotokopi-za-duniani (vitambukwa).

Yaani, kwa mujibu wa Plato, kuna uhusiano wa kitambuka-na-vitambukwa (universal-to-particulars relation) kati ya fomati-za-mbinguni na fotokopi-za-duniani. Anapendekeza “uhusiano wa umoja-na-wingi” (one-to-many relation) kati ya fomati-ya-mbinguni na fotokopi-za-duniani.

Katika falsafa, uhusiano wa aina hii huzaa kitendawili kiitwacho “the one and the many problem,” au “the unity in diversity problem,” au “the unity and multiplicity problem,” au “the sameness in difference problem.”

Bahati mabaya, jawabu la Plato kuhusu kitendawili hiki, linakosa nguvu pale anapotakiwa aseme kuna “biashara” gani inayoweza kufanyika kati ya miili ya duniani na roho za mbinguni. Yaani, swali: “how do material entities participate in immaterial entities?”

Hili ni swali kuhusu mfumo wa nasaba ya kimetafizikia iliyopo kati ya vitu vyenye mwili na vitu visivyo na mwili. Tuone majibu ya Plato kuhusu swali hili pia, kabla ya kuhitimisha hoja.

Plato na unasaba kati ya mwili na roho

Hoja ya Plato kuhusu mti wa nasaba ya kimetafizikia iliyopo kati ya fomati-za-mbinguni fotokopi-za-duniani (metaphysical structure of participation) inasema kuwa, vitu vyenye mwili, ambavyo ni vitambukwa (particulars), hupokea sifa za msingi kutoka katika fomati za mbinguni, ambazo ni vitambuka (universals).

Hata hivyo, pendekezo hili halikubaliki hata kidogo. Uzoefu wangu kama mhadhiri wa somo liitwalo, “object oriented philosophy in computer programming,” utanisaidia kuonyesha kwa nini Plato alipendekeza wazo lisilo na mashiko kifalsafa.

Katika mfumo wa nasaba ya kimetafizikia kati ya “seti kuu, seti ya kawaida, na seti ndogo” (yaani, super-set, set, and sub-set); au tuseme, nasaba ya kimetafizikia kati ya “tabaka kuu, tabaka la kawaida, na tabaka dogo” (yaani, super-class, class, and subclass);  sifa zinapokelewa kutoka ngazi ya juu kwenda ngazi ya chini. Yaani kutoka “seti kuu, kupitia seti ya kawaida, mpaka seti ndogo,” au tuseme, kutoka “tabaka kuu, kupitia tabaka la kawaida, mpaka tabaka dogo.”

Katika mfumo huu, mwanachama wa seti anayepatikana katika seti zaidi ya moja ni kitambuka (universal) cha seti hizo mbili, wakati seti hizo ni vitambukwa (particulars).

Na kifaslafa, tunasema kwamba, vitambukwa vinaweza kupokea sifa za vitambuka, kwa kuzirithi (inheritance) kupitia tendo la kuzidurufu (instantiation). Yaani, “particulars can participate in universals either through acts of inheritance via instatiation of properties.” Tuone mfano halisi.

Hapa tutumie seti ya vitu visivyoonekana (A), seti ya vitu vinavyoonekana (B), seti ya vitu hai (C), seti ya wanyama (D), na seti ya wanadamu (E). Katika kila seti kutakuwa na wanachama kulingana na sifa maalum, kama ifuatavyo:  

Kwanza, kila kitu kilicho katika seti ya vitu visivyoonekana, kina sifa kuu moja ya kufikirika (conceivability), ambapo mfano kitu kisichoonekana ni ndoto. Pili, kila kitu kilicho katika seti ya vitu vinavyoonekana, kina sifa kuu nne: uzito, ujazo, umbo, na kuhisika kwa njia ya milango ya maarifa (perceptibility).

Tatu, kila kitu kilicho katika seti ya viumbe hai, kina sifa nane, yaani: kujongea, kujisaidia, kuzaa, kupumua, kufa, kuhisi, kula, na kukua. Yaani, “movement, excretion, reproduction, respiration, yoke of death, irritability, nutrition and growth.”

Nne, kila kitu kilicho katika seti ya wanyama, tofauti na ilivyo kwa mimea, kina sifa kuu moja: kusikia maumivu (sentience). Na tano, kila kitu kilichomo katika seti ya wanadamu kina sifa kuu mbili, yaani: mawazo na maamuzi.

Hatimaye, mfumo wa nasaba ya kimetafizikia unaojitokeza kati ya seti hizi tano, kwa njia ya urithi, ni kama ifuatavyo:

Seti E inarithi sifa zote za seti D, seti C, seti B na seti A; seti D inarithi sifa za seti C, seti B na seti A; seti C inarithi sifa za seti B, na seti A; na seti B inarithi sifa za seti A. Kwa Kiingereza tunasema: “set E inherits properties from set D,” na kadhalika. Hii ni sawa na kusema, “set E participates in set D via inheritance,” na kuendelea.

Kwa kifupi, katika mfumo huu, kila mrithi anapokea sifa mpya kutoka katika ngazi zote za juu yake katika mti wa nasaba ya kimetafizikia. Hizi ni sifa zinazoshuka kutoka ngazi za juu (transcendental propeties). Mbali na sifa zinazoshuka kutoka ngazi za juu, kila mrithi anakuwa na sifa zake za kipekee. Hizi ni sifa zinazopatikana katika ngazi za chini kwenye mti wa nasaba ya kimetafizikia (immanent properties).

Hivyo, katika mti wetu wa nasaba ya kimetafizikia, mambo yafuatayo ni kweli: seti A inayo sifa moja, seti B inazo sifa tano, seti C inazo sifa 13, seti D inazo sifa 14, na seti E inazo sifa 16.

Hata hivyo, utaratibu wa kurithi sifa kutoka seti moja kwenda seti nyingine, ni tofauti kidogo na utaratibu wa kurithishana mali tuliouzoea. Katika utaratibu tuliouzoea, kurithi ni kuchukua mali jumla, baada ya mmiliki wa awali kufa.

Lakini, katika utaratibu unaoongelewa hapa, mambo ni tofauti. Katika mti wa nasaba ya kimetafizikia, tendo la kurithi linafanyika kupitia utaratibu wa kudurufu sifa husika. Kwa hiyo, pamoja na kuwa, seti E inazo sifa 16, hilo halimaanishi kuwa zimehamia katika seti hii kutoka ngazi za juu, kiasi kwamba katika ngazi za juu hakuna kitu tena.

Sifa hizo zimedurufiwa tu, kiasi kwamba, ngazi za chini zinapata “fotokopi” ya sifa husika kwenye gnazi za juu, wakati nakala asilia inabaki kwa mmiliki wake ambaye bado yuko hai.

Kwa Kingereza, kitendo hiki kinaitwa “property instantiation” au “property exemplification.”  Hii ndiyo sababu, katika falsafa tunasema kuwa, “participation transforms transcendental properties immanent properties.

Mchakato wa kutengeneza mti wa nasaba ya kimetafizikia, na hivyo kutofautisha kati ya “transcendental properties” dhidi ya “immanent propertieskutoka ngazi mmoja hadi ngazi nyingine, ni zoezi linalohusisha mchujo wa akili.  Hizi “transcendental properties” ndio zinaitwa “universal properties,” yaani vitambuka. Kwa hiyo, vintambuka, haviko mbinguni, bali vichwani mwetu.

Huu ndio msimamo wa Aristotle na Aquinas, na ndiyo maana walizikataa hoja za Plato kuhusu uwepo wa fomati-za-mbinguni. 

Kwa mfano, Msimamo wa Aquinas ni huu: “Participation: Its Latin roots mean literally ‘to take a part of,’ and this points him to an ontological view: ‘to receive partially what belongs to another in a universal way,’ that is, to receive only part of what belongs to another fully, and so merely to share in it without exhausting it.”

Anachosema Aquinas ni kwamba, katika mti wa nasaba ya kimetafizikia, sifa zilizo katika ngazi za juu zinarithiwa kuelekea ngazi za chini. Kwa hiyo, kama fomati-za-mbinguni ni roho, kama anavyosema Plato; kwa maana kwamba, hivi ni vitu visivyo na uzito, ujazo wala umbo; basi fotokopi-za-duniani, ambazo ni vitu vyenye uzito, ujazo na umbo; hazina sifa hata moja zinayoweza kuirithi kutoka mbinguni! Kwa sababu hii, hoja zote za Plato zinaporomoka na kuwa kifusi.

Hitimisho na mapendekezo

Kutokana na yote yaliyojadiliwa hapo juu, majumuisho kadhaa pamoja na mapendekezo husika yanafuata:

Kwanza, “metaphysical realism, the doctrine according to which, universals exist extra-mentally in spatiotemporal exteriority as perfect counterparts of imperfect particulars existing extra-mentally in spatiotemporal interiority, is false.”

Pili, “scientific-realism, the doctrine according to which, universals exist intra-mentally in spatiotemporal interiority as counterparts of particulars existing extra-mentally in spatiotemporal interiority, where the latter can be conceptualized in the same way and be labeled by the same term, is true.”

Tatu, kuendelea kuongelea uhai wa kiontolijia wa ulimwengu wa roho (spirit-world) ulioko nje ya vichwa vyetu, ni kushindwa kuona kwamba, kosmolojia ya Plato inao msingi wake katika visasili (mythologies). Hizi ni hekaya zenye lengo la kufunza wanadamu kwa kutumia lugha ya picha juu ya matukio yaliyo kwenye ulimwengu wa kufikirika.

Nne, ushirikina utaporomoka haraka tukiutambua ukweli kwamba, “ulimwengu wa roho”uko vichwani mwetu. Hii inamaanisha kuwa, mizimu, wachawi, mapepo, shetani na majini yako vichwani mwetu. Serikali ikiutambua ukweli huu na kuendesha propaganda endelevu kwa miaka 20 uchawi utaporomoka. Hii ndiyo sababu sikubaliani na mtazamo wa Padre Mbiti.

Kwa hiyo napendekeza mambo kadhaa, kama sehemu ya mkakati wa kuporomosha ushirikina katika Afrika.

Kwanza, napendekeza kuwa, mitaala “physics” katika ngazi ya vyuo vikuu iongeze somo liitwalo “Spacetime Physics.” Nafahamu kuwa kwa sasa halipo. Pili, mitaala ya “falsafa” katika ngazi ya vyuo vikuu iongeze somo liitwalo “Metaphysics of spacetime physics.” Pia, nafahamu kuwa kwa sasa halipo.

Tatu, napendekeza kuwa, somo la Elimu ya Maendeleo (Development Studies) vyuoni, sasa lifundishwa kwa wale wanaotaka, na badala yake, lilirithiwe na Elimu ya Falsafa (Philosophical Studies).

Najua kuwa, hapo awali somo la Elimu ya Maendeleo lilianzishwa kama tiba ya ombwe la maarifa juu ya sera za kitaifa kuhusu maendeleo miongoni mwa vijana wa vyuo vikuu, hasa baada ya baadhi yao kuandamana kwenda Ikulu kumpinga Nyerere. Sasa hivi kuna kitivo cha Elimu ya Maendeleo na kinatoa vyeti mpaka shahada ya uzamivu. Ombwe la maarifa linalotishia usalama wa Taifa kwa sasa ni ombwe la Elimu ya Falsafa.

Nne, napendekeza kuwa viongozi wa dini waifanyie kazi hoja ya Mwanateolojia Rudolf Bultiman, juu ya “Demythologizing the New Testament.” Kwa kufanya hivi, watakuwa wameitakatisha dini dhidi ya visasili vinavyokoleza ushirikina katika Afrika.

Wao wanalielewa vizuri jambo hili kuliko mimi. Kinachokosekana ni utashi wa kiteolojia na kifalsa. Nawaomba watofautiane kidogo na Askofu Tertullian wa kale, aliyehoji: “What has Athens got to do with Jerusalem?” Kupitia swali hili, Tertullian alitaka kusema kuwa, Wanafalsafa wa Athens hawana msaada wowote kwa Wanateilojia wa Yerusalem. Alikosea.

Na tano, napendekeza kuwa, serikali iweke utaratibu wa kutekeleza mapendekezo ya Dk. Simeoni Mesaki, kupitia tasnifu yake ya uzamivu (1993). Mapendekezo ya Dk. Mesaki nitayanukuu kwa ukamilifu hapa chini:

“As expected of all responsible governments, the state in Tanzania is interested in eradicating witchcraft or at least to control its violent repercussions.

“This is so because the goals of the state and ambitions for modernization are frustrated… There are many causes of the problem but no simple solutions… One would have expected witchcraft matters to be dealt with by agencies concerned with culture in the country.

“It has been documented that since independence culture has not been taken seriously… This anomaly needs to be corrected and cultural aspects like witchcraft given due attention in the form of serious study and action.

“The Tanzanian government managed to accomplish many campaigns in agriculture, heath and education through highly profiled mass media campaigns like "Kilimo cha Kufa na Kupona," "Mtu ni Afya," and "Chakula ni Uhai."

“There is no reason why similar campaigns cannot be implemented with regard to witchcraft…‘It is an affront to treat falsehood with complacency,’ Thomas Paine once said (Mesaki: 142-143).”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *