Makala
Fikra za aliye ndani ya boksi zinategemea ukubwa wa boksi alilomo
Joseph Migunda
Toleo la 202
7 Sep 2011

MIMI ni mpenzi na msomaji wa gazeti la Raia Mwema kutoka mkoani Tabora. Nimesukumwa kukuandikia kwa mara ya kwanza katika gazeti hili ili kutoa mrejesho wa makala iliyoandikwa na Ndugu Nassir Mshanga katika toleo la wiki iliyopita la Agosti 31-Septemba 6, 2011.  Makala hiyo ilibeba kichwa kilichosomeka hivi; “CHADEMA jazeni ombwe la uongozi mnalodai lipo.”

Naomba nianze kwa kuomba samahani kama huu utaendelea kuwa muendelezo wa habari yenyewe ambayo, kwa jinsi alivyoeleza Ndugu Nassir, ni kuwa hata yeye alijitokeza kutoa ufafanuzi juu ya kile kilichoandikwa katika gazeti la Tanzania Daima.

Mimi naomba nianzie hapo katika utangulizi wa mwandishi huyu ambaye kimsingi alijitambulisha kuwa anataka kutoa ufafanuzi wa neno “ombwe la uongozi” lililopo nchini mwetu. Naanza kwa kusema kwa tafsiri yupo sawa kabisa. Ila nina mashaka na maana ambayo kimsingi yeye amechukua maana moja tu aliyoiona inafaa kuandikia habari yake na hakutaka kwenda mbali na kufikiri nini hasa kinawasukuma watu aliowataja kama wanahabari, wasomi na wanasiasa kuendelea kutumia neno hilo.

Inasikitisha kuona tafsiri yake inampeleka mpaka kwenye maeneo ambayo kwa kweli hayakuwa kusudio la habari yake. Nilichokiona kwa mwandishi ni kuwa yeye yumo ndani ya boksi na anafikiri kwa upeo wa ukubwa wa boksi alilomo, lakini kama mwandishi aliyebobea au hata msomi na mchambuzi lazima uchukue muda wa kufikiri ndani na nje ya boksi ili uweze kulinganisha maana na ukweli wa jambo lenyewe.

Mfano kwa akili ya kawaida, sidhani kama msomi akisema kuna ombwe la uongozi, basi, anasema Rais Kikwete hayupo Ikulu au watendaji wa serikali hawapo kazini. Kila mtu anatambua Rais yupo na watu tofauti hupata nafasi ya kuonana nae, kubadilishana nae mawazo na kutia stori nyingi tu za kwao Bagamoyo na kwingineko duniani. Kinachomaanishwa na wasomi, wanahabari na wanasiasa hawa ni kuwa, Rais, kama mkuu wa ofisi kuu na taasisi mama katika nchi, haonekani akitumia nafasi hiyo kama alivyoaminiwa na Watanzania wengi waliomchagua katika kutoa maamuzi.

Nilichokiona kwa mwandishi ni kama vile yeye alivaa jukumu la kumsafisha Jakaya Mrisho Kikwete na sio taasisi anayoiongoza. Wanaharakati hawa hawamtaki Kikwete atoe maamuzi kama raia mwingine yeyote; bali kama mtu mwenye madaraka na nguvu za kimaamuzi, kiulinzi, kifedha na kiushauri ambazo amezipata kwa kuwa kiongozi wa juu wa taasisi hiyo ya urais. Hali ilivyo sasa ndani ya nchi yetu sio lazima mtu awe mchambuzi au mtafiti ili aweze kugundua kama serikali imeelemewa na mambo.

Ukiwa unaishi kwa kujitafutia pesa kwa jasho na sio kupewapewa asante na pongezi toka kwa wezi wa mali za nchi kwa kuwasifu katika habari kama huyu jamaa, utaguswa moja kwa moja na ukweli kuwa serikali ya CCM imepotea katika jamii na imebaki tu CHIMWAGA, BUNGENI na kwenye ziara za nje ambazo huwa tunaoneshwa kwenye TV. Ukirudi katika maisha ya kawaida yanayohitaji uwepo na maamuzi ya kiserikali, jamaa hawapo kabisa.

Mara zote utawaona wanaonekana eti wakizindua hospitali, barabara na shule na kujisifia kwa kutaja idadi ya ujumla ili kuwafumba wanyonge ambao kwa kweli hata muda wa kujadiliana uhalisia na mantiki ya ripoti kama hizo hawana. Ninachofahamu mimi ni kuwa haya ni majukumu ya kawaida ya serikali yoyote na isipofanya hivyo kwa wakati, basi, inapofikia kufanya badala ya kuomba ipigiwe makofi, basi, inabidi iombe kusamehewa kwa kuchelewesha huduma hizo. Sisi tunatimiza miaka 50 ya Uhuru lakini bado CCM wanatumia Kilomita za barabara kama kigezo cha kuomba kura, zahanati walizojenga, kilowati za umeme wanazozalisha na uzushi mwingine mwingi.

Mimi ningemwona mwandishi kuwa na uweledi kama angeainisha maeneo ambayo Rais kaonekana yupo na amefanya maamuzi ili tujiridhishe kwa kuyalinganisha kiuzito na maeneo ambayo hajayatolea maamuzi. Hapo tungekuwa na pa kuanzia na pengine angeweza kuirudisha mioyo ya Watanzania wengi kuendelea kumpenda Rais wao kwa maana aliyoyafanya yangewasuta na kuwafanya wamuongezee uimara kwa kumsapoti.

Haitoshi kuona uozo uliopo CHADEMA, CUF na NCCR-MAGEUZI na mwisho ukajiona eti wewe wa CCM upo salama kwa kuwa umeshikilia dola na ukasahau mapungufu yako. Tusome alama za nyakati; Watanzania wa sasa sio kwamba hawatambui kuwa Prof. Lipumba, James Mbatia na hata Augustino Mrema ni viongozi wajuu katika vyama vyao kwa muda mrefu la hasha! Tunajua ila tunaheshimu kwa kuwa wao ni machaguo ya kidemokrasia kutoka kwa wafuasi wa vyama vyao na wakutoa hoja yenye mashiko inayoonesha kukerwa na hali hiyo inabidi wawe hawa wanachama na sio waandishi waliotumwa au wanaosukumwa na tamaa zao kama huyu.

Itakapofika muda itawabidi viongozi hawa kuondoka na wakiendelea kung’ang’ania, basi, hata yeye mwandishi ataona muitikio wa wanachama wa vyama vyao. Lakini labda niseme tu kwamba si lazima ubaki hata kama wewe ni mzuri sana na muanzilishi wa chama hicho eti kwa sababu una uwezo wa kuongoza.

Kimsingi wakati huu tunamkosa Mwl. Nyerere aliyetuzoesha kuona maamuzi yakitolewa kwa wakati pamoja na mapungufu ambayo yangeweza kutokea, bado yeye ni muhimu kwetu na alikuwa muhimu kwetu lakini aliona ni vizuri awapishe wengine nao waiendeshe Tanzania kwa kuwa hii ni nchi ya watu zaidi ya 40 milioni na sio familia yao ambayo angeweza kuiongoza mpaka afariki. Akafanya hivyo na dunia inaendelea kumuenzi kwa busara za aina hiyo.

Wakati umefika wa CCM kufahamu kuwa watu wameichoka lakini pia imeishiwa mvuto mbele ya jamii, na hivyo si lazima yatokee ya Misri, Libya, Syria, Yemen au Tunisia hapa kwetu; bali busara itumike kuona kuwa wakati umefika na wao wakajiangalie vizuri wakiwa pembeni na sio wajiangalie wakiwa ndani ya serikali “kujivua gamba”.

Kama ni CCM ndiyo iliyotuongoza tokea Uhuru, basi, kukiri kwamba kuna wakati ilikuwa inatengeneza magamba kwa maana ya kuruhusu rushwa, utapeli wa ardhi, ufisadi na uchu wa madaraka, basi, kwa upande mwingine inakiri kuwa imechafuka na haiwezi kujisafisha ikiwa ndani lazima itoke ikae sehemu safi na hapo wataweza kuangaza vizuri maeneo ambayo magamba yao yameota au kuoteshwa.

Kupuuza Wikileaks na kujiridhisha kwa tafsiri eti mwandishi fulani wa Kitanzania ndio kaweka hiyo habari huko ili aitumie kuikosoa CCM, ni uzembe ambao namuomba mwandishi asiuruhusu katika maisha yake ya kila siku kwa kuwa badala ya kujifunza atakuwa anasubiri aanzishiwe story tu ndio atoke na makala yake gazetini.

Mtoto akimwambia baba yake kuwa nyuma ya suruali kumechanika, hata kama huo ni utani itampasa baba mwenye busara kutafuta mahali pa siri ili ajikague na kujiridhisha kama kweli anachoambiwa na mototo wake ni kweli au sio kweli. Kupuuza kabisa kuna gharama kubwa zaidi. Mfano ni mimi nilivyomuona mwandishi huyu kuwa ni mamluki tu na hakuna chochote alichotetea zaidi ya maslahi yake binafsi na ya chama au bosi wake.

Mungu atusaidie viongozi wetu wa upinzani wawe wanaongozwa na shida na mataabiko ya Watanzania katika kupanga mikakati ya kuiongoza nchi hii. Tunajua wanayo nafuu ya maisha ila dhamira zao na za vyama vyao ni kuwasaidia watanzania basi na hilo walisimamie hata kama wao wanakuwa wamevaa tai katikati ya maskini waliovaa viraka. Sisi tutawaelewa tu na imani yetu inaongezeka kwamba mwanzo wa mwisho wa minong’ono ya CCM kuachia madaraka umeanza kuonekana na utatimia.

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Joseph Migunda
mijaceez@gmail.com
+255-752711364

Mwandishi ni msomaji wa gazeti hili.

Toa maoni yako