Makala
Gaddafi: Shujaa wa maisha bora
Mayage S. Mayage
Toleo la 209
26 Oct 2011
Kanali Gaddafi

NIANZE makala yangu hii kwa kuungana na wote wanaolia na kuomboleza kifo cha Mwanamapinduzi mahiri, Mwana wa Afrika halisi na atakayeendelea kukumbukwa katika historia ya bara hili la Afrika na duniani kote kwa miaka mingi ijayo, Muamar Gaddafi, aliyeuawa kinyama na majahili wenye uchu wa madaraka.

Mapema mwaka huu, alipoanza kukabiliana na uasi wa majahili hao walioitoa roho yake kinyama na kikatili katika tukio la wiki iliyopita, Gaddafi aliapa kuipigania nchi yake hadi tone lake la mwisho la damu.

Ametimiza kiapo chake hicho. Amefia ndani ya ardhi ya mababu zake na damu yake imemwagika ndani ya ardhi ya babu na bibi zake katika shambulizi la mwisho kabisa la kuuteka mji wake wa asili wa Sirte ambao alilazimika kukimbilia baada ya mji mkuu wa Tripoli na makazi yake kutekwa, Agosti, mwaka huu na majeshi ya waasi waliojipachika jina la Baraza la Mpito (NTC).

Kwangu mimi, Gaddafi bado nitaendelea kumkumbuka kama shujaa na kiongozi ambaye alihakikisha kwamba rasilimali za nchi yake zinamilikiwa na kuwanufaisha wananchi. Alikataa kwa nguvu zote ubeberu na unyonyaji wa Marekani na washirika wake, nchi za Magharibi.

Pamoja na utajiri wao na nguvu zao za kijeshi, lakini Gaddafi aliwashinda kwa kuweza kuhimili na kuijenga Libya ndani ya vikwazo vya kiuchumi alivyokuwa amewekewa na Umoja wa Mataifa kwa miongo karibu mitatu.

Aliweza kuigeuza Libya, ambayo karibu nchi nzima ni jangwa tupu, lakini ikawa nchi ya kijani. Mfumo wake wa utawala wa Kijamahiriya, ulimfanya kila Mlibya ajione ni sehemu ya uongozi kwa kushiriki katika Kamati za Uongozi wa Umma zinazoanzia katika ngazi ya kata hadi taifa.

Kwa kujua kwamba siasa inaweza kuwa kikwazo cha kukua kwa kasi kwa uchumi, Gaddafi alipiga marufuku mfumo wa Bunge, akabaki na utawala wa umma pamoja na mahakama za dini.

Wakati nchi nyingi za Kiafrika zikiathiriwa kwa kiasi kikubwa na ukoloni, kwa mfano kutukuza lugha za wakoloni na kutelekeza lugha zao za asili, Libya ilijitangaza kuwa nchi ya Kiarabu na lugha yake ni Kiarabu. Ndani ya Libya, nchi ambayo iliwahi kuwa koloni la Waitaliano, mtu hashangai kukutana na Profesa ambaye hajui lugha nyingine yoyote zaidi ya Kiarabu.

Kwetu sisi msomi wetu hawezi kuheshimika kwa kuwa Profesa anayezungumza Kiswahili pekee. Ataheshimika akijua zaidi Kiingereza au Kifaransa kuliko Kiswahili, lugha ya Taifa ya nchi yake. Ukoloni mtupu!

Naisikitikia Libya, nawasikitikia Walibya. Gharama za demokrasia zimegharimu kifo cha Gaddafi. Wabaya wake walimpachika jina la Dikteta kwa kuwa tu hakuruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini mwake wala kutoa fursa kwa wananchi wake kujadili siasa.

Kwa namna majeshi ya Umoja wa Kujihami wa nchi za Ulaya (NATO) ulivyorusha makombora katika miji ya Tripoli na Sirte na idadi kubwa ya vifo vilivyotokea, itawachukua siku nyingi wananchi na serikali yao mpya kuirejesha Libya katika hali ilivyokuwa chini ya Gaddafi. Hicho ndicho kinachonisikitisha!

Naweza kujiona ni mwenye bahati miongoni mwa wenye bahati katika dunia, kwa Mwenyezi Mungu kunijalia kuikanyaga ardhi ya Libya na kuishi walau kwa wiki nne ndani ya nchi hiyo. Masomo yangu ya wiki nne ya kujifunza mfumo wa utawala wa Libya na itikadi ya Kijamahiriya, viliniingia na kutamani nchi yangu Tanzania kuiga mfumo huo na itikadi ya ujamaa wa Gaddafi.

Libya ni nchi pekee barani Afrika ambayo jukumu la mzazi kwa mtoto wake, linakoma mtoto anapofikisha umri wa kujitegemea, kwa maana ya miaka 18 na kuendelea. Kila kijana wa Kilibya, akishafikisha umri huo awe anaendelea na masomo ya elimu ya juu au yuko nyumbani ilikuwa ni jukumu la Serikali ya Gaddafi kumtambua na kumpatia mahitaji yake yote ya msingi kwa maana ya nyumba bora ya kuishi.

Ni kweli Gaddafi alikuwa Dikteta kwa kutoruhusu utawala wa kidemokrasia ndani ya nchi yake na kutoruhusu uhuru wa mawazo katika dunia hii ya utandawazi, lakini mengi mazuri aliyoifanyia nchi hiyo hayawezi kuyeyuka ghafla na kwenda na kifo chake.

Kila binadamu ataonja kifo, kwa hiyo hata Gaddafi ingefika zamu yake akaondoka duniani tu. Msimamo wangu wa siku zote ni kwamba katika dunia ya sasa na siasa ambazo mabadiliko ni lazima, ni muhimu kwa jamii na wanasiasa kwa ujumla kuchukua tahadhari katika kuyafikia mabadiliko yaliyo sahihi.

Mabadiliko yana pande mbili za hasi na chanya. Katika mabadiliko ya vurugu kama yaliyotokea Libya, na mengine yaliyotokea Tunisia na Misri, ni vigumu kupata mabadiliko yenye matokeo chanya. Binadamu anapotamani mabadiliko bila fomula sahihi ya kuyafikia mabadiliko hayo, matokeo atakayopata yatakuwa ni maangamizi tu kwa binadamu wenzake na Taifa lake.

Nimalizie kumlilia Gaddafi kwa kusema waliomuondoa madarakani kwa nguvu na hatimaye kumuua kinyama ni majambazi wa kisiasa kama walivyo majambazi wengine wanaohujumu uchumi na usalama wa nchi zao.

Aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye alishasema kwamba mwanasiasa anayewaua wanasiasa wenzake kwa kutumia kalamu (magazeti), siku akipata risasi hatashindwa kuzitumia kuwamaliza mahasimu wake wa kisiasa. Hata maandiko matakatifu yanasema anayeua kwa upanga atauawa kwa upanga. Yetu macho, tusubiri tuwaone hao wakombozi wapya wa Libya!

Lakini wiki iliyopita, kulikuwa na matukio mawili makubwa yaliyovuta hisia za Watanzania wenzangu. Moja ni hilo la Kifo cha Gaddafi ambalo nimelielezea hapa na la pili ni lile la Waziri Mkuu wa Kwanza katika Serikali hii ya Awamu ya Nne, Edward Lowassa, kuvunja kimya chake cha muda mrefu na kuamua kuitisha mkutano wa waandishi wa habari nyumbani kwake Monduli kuzungumza aliyoyazungumza.

Kwa bahati nzuri sana, nchi yetu hii imejaaliwa kuwa na wanasiasa wazuri na mahiri, lakini wanaoharibiwa na washauri wao. Tuna wanasiasa wazuri wengi wenye washauri wabaya katika masuala yanayohusu mchezo wa siasa. Kama ningekuwa Lowassa, ningeendelea na kimya changu bila kusema chochote, ikiwezekana hata bungeni anakowakilisha wananchi wake. Ningekaa kimya hadi utawala huu uondoke mwaka 2015, halafu ndo ningeanza kusema hatua kwa hatua mambo ambayo sikuwa nafurahia nayo katika utawala huu.

Najua pia wakati huo ambao ningeamua kuvunja ukimya, wapo baadhi ambao wangesema mbona hukusema wakati huo, bali leo. Nisingekosa sababu za kuelezea ni kwa nini nimeamua leo badala ya jana. Nasema hivyo kwa sababu kwa hadhi ya Lowassa na mazingira aliyonayo kisiasa, kila kitokacho mdomoni mwake hadharani kinakuwa na tafsiri tofauti kutokana na mazingira ya sasa ya kisiasa. Ni katika tafsiri hizo tofauti, badala ya kauli hizo kumjenga na kumrejeshea heshima yake ndani ya jamii, huzidi kumdidimiza kilomita nyingi kisiasa.

Kwa mfano, anaposema kwamba hawezi kuzungumzia tuhuma zinazomkabili kuhusu kampuni ya Richmond, wala kwamba hawezi kuzungumzia falsafa mpya ya chama chake ya kujivua gamba mbele ya waandishi hao aliowaita, lakini akasema yuko tayari kuyazungumza mawili hayo ndani ya vikao vya chama chake, anakuwa anataka kutuma ujumbe gani kwa wajumbe wa vikao hivyo, kwa maana ya NEC?

Kwamba Mwenyekiti wa kikao cha NEC ijayo ya CCM ajiandae kujibu hoja zake ndani ya kikao hicho kuhusu mawili hayo au vipi? Kwa maana Mwenezi Mkuu wa CCM, Nape Nnauye katika mikutano yake anayoendelea nayo hadi leo, amesisitiza kwa mapana sana kwamba wote wanaotajwatajwa kwa tuhuma za ufisadi ndani ya chama chake hawatapata sehemu ya kutokea kwa sababu chama kimeshaamua hivyo!

Sasa Lowassa anapoita mkutano wa waandishi na kukwepa kujibu swali la msingi kabisa ambalo ndilo muhimu kwake kwa sasa katika hatima yake ya kisiasa ndani ya chama chake na Tanzania kwa ujumla, anadhani ni nani atamjibia?

Nasema kama mwanzo angejadiliana na washauri wake na akawaambia ukweli kutoka moyoni mwake kwamba hatajibu swali lolote linalohusu Richmond wala kujivua gamba, busara ya mshauri au washauri wake hao ingewaelekeza kuufuta kabisa mkutano huo na waandishi na kumwambia asubiri muda mwafaka atakaokuwa tayari kutoa majibu dhidi ya tuhuma hizo.

Watuhumiwa wakuu wa kujivua gamba waliotajwa na Nape na John Chiligati, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu (Bara) mara tu baada kikao cha NEC cha Aprili mwaka huu, ni Edward Lowassa, Rostam Azizi na Andrew Chenge. Watatu hao hawakutajwa na vyombo vya habari, bali wajumbe wa NEC ya CCM, akiwamo Makongoro Julius Nyerere alipokuwa anawambia wajumbe na mwenyekiti wao Jakaya Kikwete jinsi kule ‘site’ wanavyosema kuhusu watatu hao.

Lowassa ni mjumbe wa NEC na alikuwamo kikaoni wakati maazimio ya chama chake yanatolewa. Kama Nape na Chiligati wanawapotosha wana CCM wenzao na umma wa Watanzania kwa ujumla, ilikuwa ni faraja kwa Lowassa kutumia nafasi hiyo ya kuvunja kimya chake kueleza ukweli halisi ni upi.

Nihitimishe makala hii kwa kumshukuru Lowassa kwa kuvunja kimya nusunusu. Nimshukuru pia Rostam kwa kuvunja ukimya wa moja kwa moja wa kuachana na siasa uchwara za ndani ya chama chake. Bado tulio wengi tunamsubiri Chenge naye avunje ukimya ili tumshukuru pia.

Ni kwa kusema mtu yaliyomo ndani ya moyo wake ndipo jamii inavyoweza kumtambua zaidi. Ujumbe wa Lowassa umefika. Hatajivua gamba, atapigana ndani ya NEC hadi tone la mwisho la damu. Tunasubiri kusikia msimamo wa Chenge kabla ya NEC ijayo! Naomba kuwasilisha!

Inaendelea

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Mayage S. Mayage
mayages@yahoo.com
+255-713670110

Maoni ya Wasomaji

Bwana Mayage mimi nimesoma hayo maoni yako,ni kweli Walibya watamkumbuka kiongozi huyo wa maana si kwa Walibya bali ni wa mfano wa kuigwa dunianikote , Wanaojiita baraza la mpito watajuta wao wenyewe baadaye nani kawaloga, lakini hata hapa kwangu kuko mrama kutokana na utawala wa mh. wa safari nyingi za matumaini na mwenye haiba kwelikweli hata kwenye mazishi yeye tabasamu la poa mbele ya kadamnasi, watu wana teseka na njaa yeye chakula kaweka SGR,ajira za walimu na waganga hakuna yeye tabasamu , mimi namuunga mkono kijana wngu mpendwa mwenye uchungu na uzalendo kwa taifa na wananchi na kufikiria kuchapa viboko viongozi hajanidanganya. tungeanza na aliyetungiza EPA ale viboko 25 na jela halafu na wenzi wake wote jela na kazi ngumu hawa viongozi wana uzi sana kutokana kushindwa kusimamia uchumi wa nchi na mali za nchi kuporwa kupitia wawekezaji,mchanga kusmbwa na kupelekwa ng'ambo kwa maana ipi?

Toa maoni yako