Gidabuday ushamaliza maneno tuonyeshe vitendo

“HAKUNA jipya linaloweza kutokea huko London kwa wanariadha wetu kurudi na medali ya namna yoyote ile. Kama ikitokea wamerudi na medali nitaenda kwenye masanduku yangu nyumbani na kuvitafuta vyeti vyangu vyote vilipo na kuwaita waandishi wa habari na kuvichoma moto hadharani” Wilhelm Gidabuday.

Hii ni kauli ya kishujaa iliyotolewa na Gidabuday, mwaka 2012 baada ya wanariadha wa Tanzania kwenda nchini Uingereza kushiriki michuano ya Olympiki, huku wakati huo akiwa si kiongozi.

Hapa Gidabuday aliamini kutofanya vizuri kwa wakimbiaji wa Tanzania kunatokana na maandalizi dhaifu yanayofanyika kila inapokuja ratiba ya michuano hiyo na michuano mbalimbali.

Wakati unapoweka umakini kulisoma andiko hili, fahamu kuwa mwishoni mwa wiki iliyopita, Chama cha Riadha Tanzania (RT) kilifanya uchaguzi wake mkuu wa kuwapata viongozi wapya na Gidabuday alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa RT.

Katibu Mkuu ndiye mtendaji mkuu wa ofisi. Hapa tunasema upele umepata mkunaji. Matumaini yangu ni kuwa  Gidabuday kile alichokuwa anakililia kila leo na kutishia kuchoma moto vyeti vyake juu ya wanariadha wetu, hivi sasa yeye atakuwa mtu wa kwanza kumtazama ikitokea tumefanya vibaya katika michuano tutakayoenda kushiriki.

Gidabuday ana mipango mingi ambayo aliamini siku moja akiwa sehemu ya viongozi wa RT atakuja kuileta mbele ya Watanzania na nchi kurejea katika zama za wakimbiaji mahiri kama Seleman Nyambui na Filbert Bayi.

Hapana shaka huu ni muda wa Gidabuday kutuonyesha kile alichokuwa anakifikiri kama mtu wa kawaida nje ya RT na sasa aje na jicho la tatu kukiongoza kile alichokuwa akililia siku zote.

Sijawahi kuwa mshabiki wa riadha kama nilivyo mshabiki wa ngumi na soka, lakini maneno ya Gidabuday yamenivuta kuupenda mchezo huu na sasa nitakuwa nikisimama nyuma yake kutazama kile anachokwenda kukisimamia kama kiongozi.

Sijui Gidabuday atatoa kauli gani ikitokea mambo yamekwenda kombo kwenye miaka yake minne ndani ya RT. Sijui kwa kweli. Maana kama kuzungumza ameshazungumza sana mpaka kutoa viapo na tunachohitaji kutoka kwake ni matendo tena na si kurudia maneno ambayo alishayasema tangu mwaka 2012.

Nafahamu ugumu anaoenda kukutana nao rafiki yangu Gidabuday kutokana na RT kutokuwa hata na ofisi moja kwenye mikoa 26, lakini Gidabuday anayajua haya ndio maana mara zote alikuwa akipiga kelele.

Kama akishindwa kutupa hata medali moja si vibaya akituachia misingi ambayo inaweza kuja kusaidia Tanzania kurejesha heshima yake iliyopotea kwenye mchezo huo.

Riadha ina changamoto nyingi kuliko mchezo wa soka ambao una aina fulani ya mwanga, lakini wakuu wa mchezo huo wakishindwa kuwa na mipango iliyo nyoofu.

Lakini kwa Gidabuday kuwa sehemu ya vongozi wa sasa wa RT, mpaka kumalizika kwa miaka minne naamini kuna kitu cha tofauti kitakuja kutokea tofauti na hali ya mambo ilivyokuwa huko nyuma.

Licha ya Gidabuday kuwa sehemu ya uongozi mpya wa sasa, viongozi wengine walioteuliwa ni Anthony Mtaka (Rais), William Kalaghe (Makamu wa Rais – Utawala), Dk Ahmed Ndee (Makamu wa Rais – Ufundi), Ombeni Zavala (Katibu Mkuu Msaidizi) na Gabriel Liginyani (Mweka Hazina).

Wengine ni Wajumbe wa Kamati ya Utendaji Lwiza Msyani, Meta Bare, Rehema Killo, Dk Nassor Matuzya, Robert Kalyahe, Zakaria Buru, Mwinga Sote, Tullo Chambo, Christian Matumbo na Yohana Mesese.

Yote kwa yote nasimama nyuma ya rafiki yangu Gidabuday, nikiamini riadha imepata Katibu Mkuu mwenye usongo wa kulipa mafanikio taifa na kulipeleka mbali.

Kila la kheri Gidabuday.


0746-594360

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *